Thursday, March 26, 2015

Karibuni Kavazini: Kavazi la Mwalimu Nyerere

UZINDUZI WA KAVAZI LA MWALIMU NYERERE 
USULI WA KAVAZI LA MWALIMU NYERERE


Na Profesa Issa Shivji
Mkurugenzi wa Kavazi 


Mhe. Mzee Mkapa, Mhe. Mzee Msuya. 

Dkt. Hassan Mshinda, Mkuu wa Tume ya Sayansi 

 Waheshimiwa Mabibi na Mabwana, marafiki na makamaradi 

Napenda kuungana na Dkt. Mshinda kuwakaribisha kwenye shughuli hii adhimu. Ni kilele cha kazi yetu ya utafiti wa miaka mitatu wa kuandika biografia ya Mwalimu Nyerere. Tumefarijika sana kwamba mmekubali mwaliko wetu na kujumuika nasi. 

Miaka mitatu iliyopita, pamoja na wenzangu wawili, Profesa Saida Yahya‐Othman na Dkt. Ng’wanza Kamata, tuliamua kuandika biografia ya Mwalimu. Ulikuwa uamuzi wa kijasiri kwelikweli lakini mara nyingine lazima uamue kufanya linalotakiwa kufanywa. Bahati nzuri, Dkt. Mshinda alikubali kugharimia mradi wetu. 

Wakati wa utafiti wetu, tuliweza kukusanya nyaraka katika makavazi mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na kuwahoji watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wastaafu wa ndani na nje ya nchi. Tunashukuru kwamba, bila kusita, wengi wenu mlitupokea na kuzungumza nasi kuhusu Mwalimu. 

Ni kweli kwamba kuna mengi katika urithi aliotuachia Mwalimu, ambayo tumeyasahau au kuyapuuza. Lakini kuna jambo moja lililojengeka katika hulka ya viongozi wetu, hasa viongozi wa kizazi cha kwanza baada ya uhuru, ambalo bado lipo, ingawa limeanza kufifia. Hulka hii ni upole na unyeyekevu, bila kuwa na kiburi, jambo ambalo sio kawaida kwa viongozi wengi. Marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, viongozi waandamizi serikalini, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mashirika ya umma, na zaidi, familia ya Mwalimu ‐ wote hao walikaa nasi kwa masaa mengi ya mazungumzo. Wachache walitukatalia, na wachache zaidi waliamua kusema yale tu waliyotaka kuyakumbuka; ingawa hao walikuwa wachache sana.

Baadhi ya wale tuliowahoji walituruhusu hata kuchambua nyaraka zao binafsi. Hii inanipa ujasiri wa kuwaomba viongozi na wananchi wengine walifikirie Kavazi kama mahali pa kuhifadhi nyaraka zao.

Wote tunawashukuru kwa moyo mkunjufu. 

Tulitarajia kwamba utafiti wetu utazaa matokeo mawili. La kwanza, ambalo ni wazi, ni kitabu ambacho tunaendelea kukiandika. La pili, ambalo sio wazi sana, ni KAVAZI LA MWALIMU NYERERE ambalo tunalizindua leo. Lengo kuu la KAVAZI lilikuwa wazi tangu mwanzo, ambalo ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka na taarifa tulizopata wakati wa utafiti wetu. Hii ndio sifa kuu ya makavazi. 

Tukiwa tunaendelea na utafiti lengo la pili lilijitokeza. Tulipokuwa tunasoma na kujadili nyaraka mbalimbali – madokezo ya Mwalimu katika mafaili, barua na makala zake, n.k. – tulifikiri kwamba haitoshi kuhifadhi nyaraka kana kwamba fikra za Mwalimu ni mfu. Fikra zinastahili kuwa hai. Uhai wa fikra ni kuzijadili, kuzidadisi, kuzichambua na kuzikosoa. Mijadala ndio utambulisho wa fikra. Migongano ya fikra ndio huzaa ufahamu na uelewa mpya. 

Ndipo tukaamua kwamba Kavazi liwe na shughuli nyingine muhimu. Kupitia njia mbalimbali – kama mihadhara, makongamano, mazungumzo n.k. – Kavazi litandaa malumbano juu ya fikra za Mwalimu pamoja na masuala mengine muhimu ambayo yalikuwa yanamtatiza. Na bila shaka Tume ya Sayansi ni mahali mwafaka pa kuendeleza mijadala ya aina hii. 

Kadhalika, tuligundua jambo jingine wakati wa mahojiano yetu na viongozi. Wengi wao, hususan wale wa kizazi cha kwanza na cha pili baada ya uhuru, na ambao wamestaafu, wanakereketwa na mengi, wangependa kujadili, kubadilishana mawazo na kushiriki katika mijadala ya kitaifa bila vikwazo vya kiprotokali. Kwa hiyo, tukaona Kavazi linaweza kuwa mahali pa wao kukutana na wenzao, na wasomi na watafiti, na kujadili nao, kuzungumza nao, kubadilishana taarifa na mawazo na kutoa mchango wao. Fikra kama hizi ndio zimechangia, kwa kiasi fulani, katika kuandaa ratiba ya sherehe hizi za uzinduzi. Huu ni mwanzo; fikra zetu zinakua. Tunawategemea nyinyi kutuuunga mkono. 

Bila shaka kutakuwa na mawazo mengi katika mijadala yetu. Kutakuwa na migongano ya mawazo. Tunatarajia kujadili na kudadisi  mawazo na fikra pana – fikra za kimaendeleo, sio fikra mgando. Tunakusudia kuendeleza fikra‐mkakati katika mijadala na masomo yetu. Tunataka kuangalia mbele, sio tu ya kesho au keshokutwa au uchaguzi ujao. Mijadala yetu itakuwa inaangalia mbali na wakati wake utakuwa wa masafa marefu – zaidi ya malumbano ya vyama vya siasa, zaidi ya mifumo iliyopo ya demokrasia na kiuchumi. Tunataka kufikiri na kuwafikirisha wanazuoni wetu kuhusu mifumo mbadala. Binadamu hajafilisika kifikra kiasi cha kukubali kuwa demokrasia ni mchezo wa kubadili sura za watawala kila baada ya miaka mitano. 

Binadamu hajafika kilele chake cha ubunifu kiasi cha kudhani kuwa soko ni mfumo pekee wa uchumi. Tunataka kuvuka mipaka ya ufahamu iliyowekwa na mifumo tawala. 

*** 

Napenda kuhitimisha kwa kugusia mambo mawili, moja ni la msingi, na jingine ni la kawaida. La kawaida linahusu fedha. Tungependa KAVAZI lijitegemee. Ndio maana tumeunda mfuko maalum (endowment fund) ambao utazalisha fedha za kujiendesha. Tunamshukuru sana Dkt. Ramadhani Dau, Mkuu wa NSSF, kwa kuchangia fedha za awali za kuanzisha Mfuko huu. Tunawakaribisha wengine wachangie kuukuza Mfuko wa Kavazi.

Tunashukuru shirika la Rosa Luxemburg waliotupa fedha za kuendesha shughuli za Kavazi kwa mwaka wa kwanza. Jina la Rosa Luxemburg lina umuhimu wa kipekee katika historia ya ujamaa. Rosa alipambana dhidi ya unyonyaji na udhalilishaji wa wavujajasho. Na alijitoa mhanga katika mapambano hayo. Aliwahi kusema kwamba: “Wasiosogea hawatambui kuwa wana minyororo” - “Those who do not move, do not recognise their chains”. 

Naam! Tumeitambua minyororo ya utumwa; tumesogea na tumeivunja. Tumeitambua minyororo ya ukoloni; tumesogea chini ya uongozi wa Mwalimu, na tumeivunja. Sasa tunapaswa kubaini minyororo ya kiitikadi na kizuoni tuliyofungwa na wababe wa mitazamo ya uliberali mamboleo; tunapaswa kusogea ili tuivunje. Ni matarajio yetu kwamba KAVAZI litachangia, ingawa kwa kiwango kidogo, kuchochea kusonga mbele. 

Jambo la pili, ni kuhusu jina la KAVAZI LA MWALIMU NYERERE. Jina hili linatakiwa kufafanuliwa, japo kwa ufupi, kwa sababu limezuwa mjadala. Tafsiri ya Kiswahili ya neno la Kiingereza ‘Archives’ ni Makavazi, kwa maana ya mahali pa kuhifadhi nyaraka za kale na za kihistoria. Kama ilivyo kwa neno la Kiingereza (archives), neno Makavazi halina umoja. Hata hivyo, kwa hisia na dhamira zetu, makavazi yanayotunza nyaraka zinazomhusu Mwalimu yana umuhimu na hadhi maalum. Na sisi tulitaka jambo hili lijitokeze waziwazi katika jina la chombo hiki. Ndio maana tumediriki kubuni neno KAVAZI ambalo ni mzizi wa neno au dhana ya makavazi. Ili kusisitiza upekee wake, tunaliita ‘Kavazi LA’ Mwalimu Nyerere, na sio Kavazi ‘ya’ au Kavazi ‘ka. Kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiingereza ‘Kavazi la’ ni sawa na kusema ‘The Archive’; huwezi ukasema ‘The Archives’ katika wingi.

Tunaamini kwamba hatimaye neno KAVAZI litazoeleka. Tutafarajika ikiwa tutasikia vijana wetu na watafiti wakiambiana: TUNAKWENDA KAVAZINI. 

Karibuni Kavazani.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP