Saturday, April 11, 2015

Nini Maana ya Dhana ya Chama Dola?

Nini Maana ya Dhana ya Chama Dola?

Chambi Chachage

Nimeshtushwa na tafsiri ya Profesa Kitila Mkumbo kuhusu dhana ya chama dola. Katika makala yake ya Nini maana ya dhana ya kiongozi wa chama cha ACT? anadai kwamba sababu ya msingi ya kuwa na mfumo huo wa uongozi wa chama tofauti na ule wa kuwa tu na Mwenyekiti ni kuepuka kutengeneza chama dola. Lakini chama dola ni nini hasa?

Profesa Mkumbo anatoa mfano huu: “CCM ni chama dola kwa maana kwamba kimejipenyeza serikalini kutokana na muundo wake ambapo mwenyekiti wake ndiyo huyo huyo anakuwa kiongozi wa serikali. Huyu akimaliza kuendesha vikao vya Baraza la Mawaziri anahamia kuendesha vikao vya chama. Ni kwa sababu hii chama kinakuwa hakina uwezo wala mamlaka ya kuhoji utendaji wa serikali yake. 
Matokeo ya muundo huo ndio yanayomfanya sasa Katibu Mkuu wa CCM kufanya kazi ya vyama vya upinzani ya kulalamika na kuikemea serikali yake barabarani kwa sababu anajua kwamba hawezi kuwa na nafasi hiyo ndani ya vikao vya chama kwa sababu huko serikali ndiyo inayoendesha chama.”

Kwa maana nyingine, anachosema ni kwamba sasa hatupo kwenye enzi za Mwalimu Nyerere za ‘chama kushika hatamu’ bali za ‘serikali kushika hatamu.’ Ila kama hivyo ndivyo, basi tulicho nacho siyo ‘chama dola’ bali ni ‘dola chama’.  Na kwa mantiki hiyo anaposema kwamba mfumo “wa chama dola ni hatari kwa demokrasia kwa sababu hulazimisha watumishi wa umma kufanya kazi ya chama tawala badala ya kutumikia serikali kwa mujibu wa taaluma zao,” Profesa Mkumbo anaonekana kujikanganya maana hiyo hali hutokea pale ambapo viongozi wa chama wanakuwa na sauti kubwa kuliko watumishi wa serikali, yaani, hali ya chama kushikilia dola/serikali na si dola/serikali kushikilia chama.

Utata huu kitafsiri unajitokeza na kueleweka zaidi kwenye mfano huu anaoutoa Profesa Mkumbo: “Kwa hiyo, msingi wa kuwa na mfumo wa uongozi wa chama sambamba na uenyekiti ni kuondoa udola katika chama cha siasa. Mfumo huu unatoa nafasi kwa chama kuweza kuhoji na kusimamia utendaji wa serikali yake bila chenyewe kujigeuza kuwa serikali. Hiki ndicho kilichofanyika Afrika Kusini ambapo baada ya kuona Rais Thabo Mbeki ameshindwa kusimamia sera za ANC katika serikali chama kiliamua kumuweka pembeni na hatimaye kumchagua Jacob Zuma kuwa Kiongozi wa Chama na baadaye Rais wa Afrika Kusini. Jambo hili lisingewezekana katika mfumo wa chama dola.”

Lakini hicho kilichotokea Afrika Kusini kilikuwa ni kitendo cha chama tawala, ANC, kujimilikisha dola/serikali kwa ‘kumwita’ na kumtoa/kumjiuzulisha Rais aliyechaguliwa na raia/wananchi wote, yaani wakiwamo hata wale ambao siyo wanachama wa ANC, na kuwawekea Rais wa muda, Kgalema Motlanthe, ili baadaye wamsimamishe Jacob Zuma kwenye Uchaguzi Mkuu ili awe Rais. Inasemekana hata wangetaka wangemweka tu Zuma badala ya Motlanthe. Huo si ndiyo mfumo wa chama dola, yaani, mfumo ambao chama tawala kiko juu ya serikali ya nchi eti kwa kuwa chenyewe ndiyo kimeiunda serikali baada ya kushinda uchaguzi?

Walichofanya ANC si ni sawa tu na CCM iamue kumtoa Rais Jakaya Kikwete leo na kumweka  Philip Mangula awe Rais wa Muda wa Nchi bila hata ya kupigiwa kura na wananchi ili baadaye Edward Lowassa agombee Urais huo? Kuna udola wa chama zaidi ya huo? Si ndiyo maana vyama vya upinzani huko Afrika Kusini havitaki kabisa ANC iwe inapata ushindi wa theluthi mbili wakati wa Uchaguzi Mkuu ili kisisimike zaidi huo uchama dola wao?

Je, historia ya jinsi ANC ilivyoanzisha nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama inatudhihirishia pia kwamba nia hasa ilikuwa ni kuondoa mfumo wa uongozi wa vyama vya siasa kuwa wa kidola? Baada ya Nelson Mandela kutoka jela aliyekuwa Rais wa ANC, Oliver Tambo, alitengenezewa hicho cheo cha Mwenyekiti mwaka 1991 ili kumpisha Urais Mandela. Hiko cheo ‘kilichomekwa’ tu na ikabidi waendelee nacho tu baada ya Tambo kufariki dunia.

Wakuu wa chama waliendelea, kimamlaka, kuwa Rais wa Chama na Makamu wa Rais wa Chama. Mamlaka yao yameelezewa vizuri katika tofuti rasmi ya ANC. Rais wa Chama ndiye “mkuu wa kisiasa na afisa mkuu mtendaji wa ANC na mkuu wa ‘ukumbi’ wakati wa Mkutano Mkuu.” Pia chini ya usimamizi wa jumla wa Kamati Kuu ya Chama, “ndiye  anayeongoza na kuelekeza kazi zote za ANC.” Msaidizi wake ni huyo Makamu wa Rais.

Mwenyekiti wa Chama cha ANC kazi yake kuu inakuwa ni kuwapunguzia mzigo wa majukumu (siyo wa mamlaka/madaraka) hao Marais wa Chama kwa kusimamia/kuendesha shughuli za Chama. Ndiyo maana Mwenyekiti wa Chama akiwa hayupo au akishindwa kutekeleza majukumu yake basi Rais wa Chama mwenyewe ndiye analazimika kutekeleza majukumu hayo.

Inaonekana huu ndiyo aina ya mfumo ambao Profesa Mkumbo anauongelea kwa kujiamini anaposema hivi: “Siku ACT-Wazalendo ikichaguliwa na kuunda serikali jukumu la Kiongozi wa Chama litakuwa ni kusimamia uendeshaji wa serikali na kuhakikisha kwamba serikali inatekeleza sera za chama kikamilifu na atatoa taarifa ya utekelezaji wa sera katika vikao vya chama vitakavyoendeshwa na Mwenyekiti wa chama.” Akishatoa hiyo taarifa chama kikaikataa si ndiyo ataitwa na kutolewa kama Mbeki? Huko ni kuwajibika kwa chama tawala kilichoshikilia dola au kwa wapiga kura wote waliomchagua awe mkuu wa dola/serikali hiyo?

Au hatatolewa kama Mbeki kwa kuwa kwa namna fulani muundo huo umehakikisha kwamba daima Kiongozi wa Chama atakuwa na nguvu, nuru, madaraka na mvuto mkubwa zaidi kuliko Mwenyekiti wa Chama? Si ni Profesa Mkumbo mwenyewe anayetujulisha hivi: “Kwa hiyo, pamoja na kwamba kimuundo Kiongozi wa Chama ndiye mwenye mamlaka zaidi ya kiuongozi ndani ya ACT-Wazalendo, mgawanyo wa nafasi mbili za Kiongozi wa Chama na Mwenyekiti ni wa kimajukumu zaidi kuliko kimamlaka”?

Kama ana mamlaka zaidi si ina maana akiwa Rais atakuwa amevaa kofia mbili pia – ya mamlaka zaidi katika serikali na mamlaka zaidi katika chama? Sasa atakuwa na tofauti gani na yule aliyevaa hivyo enzi zile za chama kimoja kushika hatamu (za dola)?

Yote hayo hayamzuii Profesa Mkumbo kutoa hitimisho hili: “Tunaamini kwamba kwa kuwa na mfumo wa uongozi huu ni hatua muhimu ya kujenga chama cha siasa kisicho chama dola.” Waumini wanaamini hivyo. Labda Uongozi, kama ulivyo Ujamaa, ni imani.

Heri yao waaminio. Ole wao wasioamini. Imani bila matendo hufa. 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP