Friday, April 24, 2015

Tutaishije bila Falsafa Mpya ya Kifo?

Tutaishije bila Falsafa Mpya ya Kifo?

(*Buriani Esther Lameck Mwamukonda*)

Chambi Chachage

Ninaogopa kufa. Kifo kweli hakina huruma! Lakini mbona kinaonekana kana kwamba kina upendeleo wa wazi kabisa?

Kifo kimeuandama mtaa niliokulia. Nikiutazama uwanja wetu wa mpira wa utotoni pale Ubungo Flats ninamwona golikipa mahiri Angelo, mshambuliaji hatari Abdallah na kiungo mshereheshaji Juma. Wote hawa wametutoka katika kipindi cha hii miaka mitatu.

Wote walikuwa hata hawajitimiza miaka 40. Bado walikuwa vijana. Pia uwanjani namwona Bugwema aliyekuwa mmoja wa vinara wetu darasani. Namwona na Masanja aliyekuwa mjasiriamali toka akiwa shuleni. Hali kadhalika namwona Eric aliyekuwa na kipaji cha ufurahishaji toka utotoni. Hao nao wametutoka hivi karibuni. Wengine 7 niwakumbukao walitangulia zamani. Jumla: Watu 13. 

Inakuwaje katika nchi ambayo tunaambiwa na wanatakwimu kwamba kwa wastani tunategemewa kuishi zaidi ya miaka 40 mtaa mmoja upoteze watu wote hao uliowakuza mapema hivyo ili walitumikie taifa wanapokuwa wakubwa. Wanasiasa wa aina mpya wanatusisitizia kwamba sisi ni Taifa la vijana sasa inakuwaja shule moja iliyowapa msingi ipoteze vijana wabichi wote hao na zaidi?

Je, Mungu ndiye ametaka iwe hivyo? Kama anajua nani atakufa lini, je, ndiye anapanga nani afe lini? Ndiye anaamua watu wa mtaa au kijiji fulani wafe zaidi? Ama ndiye huamua vifo vya ajali za mabasi vitokee zaidi nchi fulani? Wapi alisema kwamba wakati wa kujifungua mama wajawazito na watoto wachanga wafe zaidi katika bara fulani? Ndiko kutimizwa kwa mapenzi yake huko?

Gautama Siddartha (Buddha) aliyekuwa mwanafalsafa maarufu huko barani Asia (inasemekana) aliwahi kumpa funzo mtu mmoja aliyejiona kama yeye peke yake ndiye amefiwa. Alimwambia aende katika kila nyumba ambayo haijawahi kufiwa na kuomba kitu kama mchicha hivi ambacho hupatikana katika kila kaya. Hakufanikiwa kukipata na hivyo akajifunza kwamba kumbe kifo hutugusa sote.

Vivyo hivyo nasi tunapaswa kujifunza kwamba japo kifo huwajia watu wote, hiyo haimaanishi tubweteke tu na kutofanya jitihada za makusudi kabisa za kupunguza na kuzuia vifo hasa pale inapokuwa ndani ya uwezo wetu kama wanadamu. Mbona wenzetu wengi wameweza? Kama ushindi dhidi ya kifo ulishaanzishwa kwa nini tusubiri tu siku ya kuimba “Uko wapi Ewe mauti uchungu wako?”

Mwanafasihi na ‘Mwanafalsafa’ Ngugi wa Thiong’o analalama kwa huzuni kuu kwamba thamani ya maisha ya Mwafrika duniani ‘imedogoshwa’ ukilinganisha na ya wengine. Vifo vitokanavyo na mashambulizi ya Ki-Xenophobia huko Afrika Kusini, kuzama kwa wahamiaji huko Afrika Kaskazini, vita vya kigaidi huko Afrika Magharibi pamoja na kupigwa risasi huko kwenye Diaspora ya Afrika ni ushahidi tosha kwamba hakika kufa ‘kunaafrikishwa.’
 Cha kusikitisha mno na kuusononesha moyo ni kwamba Watanzania tunaenda mbali zaidi, sasa ‘tunatanzanisha’ kifo. Ni kama vile tunataka kuionesha dunia kwamba kufa ni kawaida zaidi hapa kwetu kiasi cha kwamba leo kuna aina ya vifo vinapatikana Tanzania tu kama ilivyo Tanzanite. Hivi albino wa Tasmania au Tajikstan akiaambiwa aje ‘kuishi’ hapa Tanzania atakubali kweli?
 Yule Mwanahabari na ‘Mwanafalsafa’ Ayub Rioba aliwahi kujaribu kuchambua baadhi ya misemo na methali zetu ambazo alisisitiza zinahitajika kuangaliwa upya kwa kuwa zinajenga falsafa zinazoathiri maendeleo yetu kama jamii. Pengine sasa ni muhimu tuanze kuziangalia kwa kina zile ambazo zinaongelea kifo maana labda zinachangia kwa kiasi kikubwa sana ‘kukikawaidisha’ kifo.

Tuanze kwanza na hili la ‘kufa kufaana’ na ‘kifo cha wengi harusi.’  Maana ya ndani ambayo imelengwa inaonekana ina mantiki nzuri sana ambayo, kitafsida, wala haizungumzii kifo kama kifo. Lakini ukiitazama maana ya nje unakuta inajenga falsafa ya kwamba kifo kinaweza kutufaa na hasa kifo kinapokuwa kimetamalaki. Na kwa kawaida falsafa ya maisha ndiyo hutuongoza kivitendo maishani.

Lakini tunapokufa wengi kwenye ajali za mabasi hayo ni matanga, siyo harusi. Na tunapowaua ndugu zetu albino na ajuza hatuwafai, hivyo, hatufaani nao. Kufa kutofaana. Kifo cha wengi matanga.
Halafu kuna ‘hujafa hujaumbika.’ Mama mjamzito anapopoteza himila kwenye tumbo la uzazi hospitalini au mimba changa kabisa inapotolewa ni kweli mtoto anakuwa bado hajaumbika kikamilifu. Kilicho muhimu ni kuhakikisha kwamba tunazuia upotezaji holela wa maisha wakati mgumu wa ujauzito na ajali zingine ili tusiwe na kisingizio/sababu ya kutumia falsafa hiyo kujifariji na kuwafariji waliokumbwa na majanga. Maafa mengi tunayaumba wenyewe.

Je, kweli ‘kufa ni wajibu’? Ni wajibu wangu kufa kwa malaria au ni wajibu wangu ‘kuwaua’ hawa mbu wengi wanaoning’ata ninapoandika haya na kununua chandarua hasa chenye dawa? Hivi ni wajibu wangu kufa tu kwa UKIMWI ama ni wajibu wangu kujikinga na maambukizi ya VVU au kutumia dawa za kurefusha maisha na kuhakikisha napata matibabu ya magonjwa nyemelezi?

Sam Cooke aliwahi kuimba wimbo wenye maneno haya ya simanzi: “Nimechoka kuishi lakini naogopa kufa.” Kuna wakati tunachoka kabisa kuishi kutoka na sababu mbalimbali zinazoyafanya maisha (matamu) yawe machungu – umaskini/ufukara, maradhi/magonjwa na kadhalika. Lakini kwa kawaida binadamu anaogopa sana kufa. Dwight Nelson yeye anasisitiza kwamba mbinu ya kukabiliana na kifo chako bila hofu na kwa kukiongelea kijasiri kabla hakijatokea.

Remmy Ongala, yule Mwanamziki na ‘Mwanafalsafa’, naye aliwahi kuimba wimbo maarufu wenye falsafa yake tata ya kifo. Unasema “Kifo hakina huruma.” Mtenda(ji) ni kifo na mtendwa(ji) ni mtu. Mama Mjamzito anakufa mtoto akiwa tumboni, wimbo unakilaumu kitendo cha kifo na siyo kitu ambacho mtu huyu, huyo ama yule alikifanya au kutokifanya na hivyo kusababisha kifo.
 Alichosahau Remmy au ambacho hakukiona wakati ule ni kwamba wale waliojiandaa kukabiliana nacho hawaishi tu kwa kutegemea rehema/huruma ya kifo na kuinungunikia kudra ya Mungu. Kama jamii wao hupunguza kasi ya kufa na wengine hufanikiwa kabisa kutokomeza vifo vinavyozuilika. Na ndiyo maana kuna nchi ambazo zimefanikiwa kutokomeza magonjwa kama malaria. 

Ongezeko la jitihada za kulinda maisha ni moja ya sababu kuu ya kwa nini takwimu zinaonesha kwamba kiujumla kuna nchi/jamii zinaishi maisha marefu kuliko zingine. Kwa mfano, huko Marekani tafiti zinaonesha kwamba, kwa wastani, Waadventista Wasabato (wengi) huishi muda mrefu zaidi kutokana na kuzingatia kanuni jumuishi za kutunza afya. Kanuni hiyo imejikita kwenye neno NEWSTART lenye maana ya ‘Mwanzo Mpya’, ambapo kila herufi inawakilisha hitaji fulani ambalo mtu anatakiwa ahakikishe analipata vya kutosha kiuwiano, yaani Nutrition (Lishe), Exercise (Mazoezi), Water (Maji), Sunshine (Mwangaza), Temperance (Kiasi), Air (Hewa), Rest (Mapumziko) na Trust (Imani).

Uchambuzi wa matabaka/madaraja pia unahitajika tunapotafuta falsafa ya kukabiliana na kifo. Sidhani kwamba ni jambo la kawaida tu kwa mtaa wa Ubungo Flats katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupoteza vijana wake 13+ ilhali kuna mitaa mingine katika Chuo hicho haijapoteza hata mmoja. Haijatokea tu kibahati bahati, inaonekana kuna sayansi fulani au siri ya kitabaka/kidaraja.

Daraja/Tabaka na tofauti zake ilikuwa ni moja ya misingi mikuu katika ubunifu na ujenzi wa Chuo Kikuu hicho. Na kama kuna mtaa ambao ulidhihirisha hilo ulikuwa ni Ubungo Flats. Wakati tunakua mitaa ya Kileleni na Kilimahewa ndiyo ilikuwa ‘Oysterbay’ na ‘Masaki’ ya chuoni ikifuatiwa na mitaa mingine kama Koroshoni, Darajani, Lamboni, Miembeni na Ng’ambo.
 Zamani zile Ubungo Flats ndiyo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imekusanya matabaka yote makuu ya Chuo Kikuu. Jengo la mapolisi halikuwa lilivyo sasa – lilikuwa linaongoza kwa kubanana na uchafu, huku ikisemekana familia mbili tofauti zilikuwa zinaishi kwenye nyumba ndogo ya vyumba viwili. Pia kulikuwa na majengo ya wafanyakazi wa kawaida na upande mwingine kulikuwa na majengo ya wahadhiri ambao wengi wao walikuwa kwenye michakato ya kuomba wahamishiwe mitaa ya ‘uzunguni’/‘unaizesheni’ ya humo chuoni Mlimani.

Baada ya miaka mingi jirani yangu wa utotoni aliniambia kila jioni taa zikiwashwa walikuwa wanaangalia upande majengo yetu yalipo na kutuona sisi ndiyo tumefanikiwa sana na kutamani kuhamia kwetu na kuwa kama sisi. Nasi tulikuwa tunatamani kuhamia walipokuwa wanaishi zaidi vingunge wa chuo na wahadhiri wageni kutoka nje ya nchi. Jirani yangu huyo yeye alifanikiwa kuhama.

Pamoja na hayo Ubungo Flats ya enzi hizo za miaka ya 80 haikupoteza watoto wake wengi kama ilivyowapoteza sasa baada ya kuwakuza. Msiba mkubwa wa kwanza wakati huo ulikuwa wa mdogo wangu, Atuhalile, aliyeumwa Degedege na kupoteza maisha njiani wakati jirani yetu Dokta Minja anajitahidi kadri ya uwezo wake wote kumwahisha hospitalini Muhimbili baada ya jitihada zingine kushindikana. Ilikuwa siku ya majuto na majonzi mtaani.

Enzi hizo kifo hakikuonekana ni kitu cha kawaida. Hata utamaduni wa kuomboleza misibani unaonekana ulikuwa tofauti na wa siku hizi. Majuzi Bibi yangu, Mkunde, alikubaliana na hoja tete kwamba zama hizi misiba mingi mijini imekuwa ni kama sherehe – ni kana kwamba sasa tumekizoea kifo kwa kuwa kipo karibu mno; kinatokea kila kukicha hapa, hapo, pale na si kule tu. Kama hili ni kweli, je, linatokea kwa sababu falsafa yetu ya kifo imebadilika?

Falsafa yetu ya kifo ni ya kusubiri tu siku zetu za kufa kwa kuwa eti zimeshapangwa/zimeshaandikwa kabla hatujazaliwa? Au ni ya kuzuia vifo vinavyozuilika? Hata misahau si inasema kwa nini tufe kabla ya siku zetu? Si inasema tunaweza kuongeza siku za kuishi?

1 comments:

Anonymous April 26, 2015 at 3:52 PM  

Pole sana kwa misiba hii mingi ya watu wa karibu. Na kama mambo yanaendelea hivyo, hali itaendelea kuwa mbaya zaidi. La msingi ni kujiweka kwa Mungu na kukumbuka tumaini lenye baraka kwamba siku moja Yesu atakuja kutuchukua atupeleke katika nchi ile aliyotuandalia mahali amabako hakutakuwa na vifo, wala vilio, wala machozi, wala maombolezo.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP