Tuesday, July 7, 2015

Jinamizi la Urais wa Lowassa

CCM katika ncha ya Mpasuko: Jinamizi la Urais wa Lowassa 2015

Richard Mbunda

Idara ya Sayansi ya Siasa (UDSM)

Siasa za Tanzania ni za pekee?
Siasa za Tanzania zimekuwa na upekee katika mambo kadha wa kadha. Ni upekee huu unazozifanya siasa za Tanzania kutokutabirika na kuwavutia wachambuzi wengi sana. Kwa mfano, huko duniani, umaarufu katika siasa ni chachu kubwa ya mgombea kuchaguliwa katika uchaguzi. Lakini hapa Tanzania hali inaweza kuwa tofauti. Mwaka 1985 wakati Mwalimu Nyerere anang’atuka, hakuna aliyetarajia kuwa Mzee Mwinyi angemrithi. Macho ya watu yalikuwa kwa mwanadiplomasia mahiri Afrika Salim Ahmed Salim, ambaye inasadikiwa pia alikuwa chaguo la Mwalimu Nyerere. Walakini haikuwa hivyo.

Mwaka 1995 wakati Mzee Mwinyi anamaliza muda wake, kuna sura kadhaa zilizobeba umaarufu mkubwa sana ndani ya Chama cha Mapinduzi. Kiumaarufu, mtakubaliana na mimi kuwa John Samwel Malecela, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Edward Lowassa na Jakaya Kikwete walikuwa maarufu zaidi ya Rais Benjamin Mkapa. Kuna baadhi ya maandiko yanamkariri Mwalimu Nyerere akisema kuwa tusiangalie umaarufu ‘…. Kama umempenda kwa kuwa ni mtu maarufu nenda kanywe naye chai…’ Hii inasaidia kutuonyesha kuwa watu maarufu walikuwepo, lakini kutokana na mfumo uliokuwepo hawakuweza kuchagulika.

Upekee mwingine unatokana na nafasi ya Rais na Mwenyekiti wa chama anayemaliza muda wake kumteua anayempendekeza kuwa mrithi wake madarakani. Katika historia ya nchi, tangu Baba wa Taifa mwenyewe hakuna Rais aliyeweza kumweka mgombea wa pendekezo lake madarakani. Simulizi za kisiasa zinaonyesha kuwa Mwalimu Nyerere alishindwa kumweka Dkt. Salim A. Salim madarakani mwaka 1985. Mzee Mwinyi naye alikosa fursa hii adhimu mwaka 1995 pale ambapo Mwalimu Nyerere kama Baba wa Taifa alipotumia nafasi yake kuhakikisha chaguo lake, Ben Mkapa anaingia madarakani. Pamoja na uwezo, heshima aliyojijengea na ushawishi Mzee Mkapa pia, hakuweza kushawishi ataeuliwa mgombea aliyemtaka ili awe Rais pale alipomaliza muda wake 2005.
 Kuna sababu kuu mbili zinazoelezea hali hii ya Rais anayemaliza muda wake kushindwa kumweka mrithi. Mosi, Rais anapomaliza muda wake anakuwa hana mamlaka ya kidola ya kushurutisha watu. Kuna kiongozi mmoja mwandamizi aliwahi kuniambia kuwa, mwaka mmoja kabla ya tarehe ya uchaguzi, Rais huwa hapewi usikivu kwa asilimia mia moja. Hivyo ni vigumu kushurutisha watu waenende kulingana na matakwa yake. Lakini la pili ni kuwa, watu tayari wanakuwa wameshajipanga na kuunda mitandao ya ushindi. Mara nyingi Rais anayemaliza muda wake anajaribu kukwepa mitandao hii kwa kuwa kama isipofanikiwa anahatarisha kuingia katika mgogoro na Rais atakayemrithi.

Hata hivyo, binadamu wanatofautiana na mara nyingi hawatabiriki. Siasa ni kamari, na wacheza kamari hawaogopi madhara bali husukumwa na faida. Kwa kuzingatia historia ya nchi yetu, viongozi wakuu wa nchi katika awamu zote nne unaweza kuwaweka katika makundi mawili. Kuna wale ambao walizingatia utawala wa dola tu. Mzee Mkapa na Mzee Mwinyi wanaangukia katika kundi hili. Kwa upande wa Mzee Mwinyi, sababu mojawapo ilikuwa ni Mwalimu kuendelea kuwa Mwenyekiti wa chama kwa miaka kadhaa baada ya kung’atuka urais. Na hata alipopewa kofia ya chama, bado hakuonyesha hamasa ya kukitumia chama ili kufanikisha malengo yake. Mzee Mkapa, angetamani hata huo uenyekiti wa chama angepewa mwingine ili yeye abaki na serikali.

Mwalimu Nyerere na Rais wa sasa Jakaya Kikwete ni watu waliopenda kuzitumia kofia zote mbili. Ikumbukwe kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi kujiuzulu Uwaziri Mkuu mara tu baada ya Uhuru ili akakijenge chama. Mwalimu alikitumia chama kama nguzo kuu ya maamuzi. Wakati wa mfumo wa chama kimoja maamuzi mengi muhimu yalitoka kwenye chama, ambako alikuwa mwenyekiti. Rais Kikwete pia, ni mtu aliyekulia kwenye chama na anajua umuhimu wa chama na siasa ndani ya chama. Pia kwa hulka yake, Rais Kikwete ni mwanasiasa asiyekubali kushindwa. Kwa mantiki hiyo basi, ni vigumu kusema hataweza kuelekeza mchakato wa kumteua mrithi wake. Ana nafasi kubwa sana ya kufanya hivyo, na ni matumaini yangu kuwa atapenda afanikiwe katika hili.

Kwa wale wanaobeza uwezo wa Rais anayemaliza muda wake kuelekeza mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ningependa kuwasihi wamwangalie Rais Kikwete katika jicho tofauti. Ningependa kuwakumbusha mambo machache: mosi, mgogoro wa kurithishana madaraka Zanzibar, ambapo Mh. Gharib Bilali aliona kuwa sasa ilikuwa zamu yake. Kikwete alifanikiwa kumweka Dr. Shein Zanzibar. Pia, mwaka 2010 katika mchakato wa kumchagua Spika wa Bunge, Rais Kikwete aliwashtua watu na chaguo lake. Kuna baadhi ya wanasiasa hawajui walipigwa na kitu gani. Lakini Mh. Anne Makinda aliibuka kuwa Spika hata sasa.
  
Mwenyekiti yupo Kambi ipi?
Swali ambalo lilikuwa rahisi miaka 10 iliyopita sasa linaonekana gumu sana. Wachambuzi wa Kitanzania watakumbuka mtandao madhubuti ulioundwa na Timu iliyomhusisha Edward Lowassa na wapambe wake kuhakikisha Rais Kikwete anaingia Ikulu. Mtandao huu ulimpa Ushindi wa kishindo Rais Kikwete. Hivyo basi, ilitarajiwa kuwa Rais Kikwete awe upande wa Lowassa kwa mantiki ya yeye kulipa fadhila. Lakini hali haipo hivyo. Mimi nilikuwa wa kwanza kukimbilia kitabu cha wasifu cha Rais Kikwete kilipotoka, ili nijue kitu gani kilitokea mpaka waziri wake mkuu akajiuzulu 2008. Sikuridhika na maneno tu kuwa ‘ilikuwa ajali ya kisiasa’. Kwa bahati mbaya, sikuona lolote la maana katika kipengele hicho kwenye kitabu hicho.

Hata hivyo, kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kundi hili, lililojulikana maarufu kama “Boys II Men”, limesambaratika. Waandishi wa habari wamekuwa wakiuliza maswali na wamekuwa hawaridhishwi na majibu wanayopewa. Aliulizwa Lowassa katika mkutano wake na Wahariri kule Dodoma, na kwa kuwa swali lilijirudia mara nyingi likamkasirisha. Vijana wa ‘www.com’ wanamsemo kuwa ‘kusoma hujui na picha huioni?’ Waandishi wa habari wametusaidia kurekodi kauli zinazopingana. Wakati anatangaza nia kule Arusha, Lowassa alibainisha kuwa alimuunga mkono Kikwete 2005 na 2015 ni zamu yake kuungwa mkono. Lakini Rais Kikwete alipoulizwa na Mwanadiplomasia wa Marekani June 9 kama atamuunga mkono Lowassa alisema yeye hana mgombea. Na hata kama anaye kura yake ni moja tu. Ingawa kauli hii inalenga kuonyesha kuwa Mwenyekiti wa chama hapaswi kuwa na mgombea au sehemu ya mtandao, lakini kwa wawili hawa inasadikiwa palikuwa na yamini. Majibu kama haya yanaweza kutupa dondoo tu ya uhusiano wao kwa sasa.
 Mzee Kingunge alitufunua macho pia alipowaasa wawili hawa kupatana wakati akihutubia siku Lowassa alipotangaza nia kule Arusha. Wito wake wa kutaka wawili hao kupatana kutokana na historia yao ya kisiasa unatuonyesha kuwa hali ya uhusiano wao sio shwari. Lakini suala la kuhasimiana katika siasa sio jambo geni. Wananadharia za kihalisia wanasema hakuna urafiki wa kudumu katika siasa bali masilahi ya kudumu. Hata hivyo, wito wa Mzee Kingunge una mantiki kubwa. Kwa sababu ikiwa maswahiba hawa wa zamani sasa wanapambana kwa namna yeyote madhara yake yatakuwa makubwa sana kwao binafsi na hata kwa chama. Makala hii ndefu ina jaribu kubashiri (project) kinachoweza kutokea katika mchakato huu wa uteuzi.

Siasa za Umaarufu
Umaarufu katika siasa ni silaha muhimu sana. Na unatafsiriwa katika uwezo wa kuvuta watu katika mikutano yako, na kuwa midomoni mwa wananchi muda wote. Umaarufu unaanza na mtu. Kwa wanasiasa wajanja zaidi, huupamba umaarufu kwa sera za kuvutia, na ahadi zinazoendana na matakwa ya wananchi. Mwaka 2005 Rais Kikwete alikuwa maarufu kiasi kwamba watu wakadhani ataumaliza kabisa upinzani. Na ahadi yake ya maisha bora kwa kila mtanzania iliwafanya wapiga kura ‘warukwe na wazimu’. Lakini mwisho wa siku ni maneno tu, katika dhana nzima ya umaarufu.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka huu Edward Lowassa ndio habari ya mjini. Jina lake limekuwa midomoni mwa watu kuanzia mijini mpaka vijijini. Prof. Kitila Mkumbo alitanabaisha katika makala yake kuwa Lowassa ana ufuasi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi. Ingawa wapinzani wake wamekuwa wakibeza umaarufu wake kwa vigezo kuwa anawanunua watu, lakini uhalisia wa madai haya una walakini. Ni vigumu kudhani kuwa Lowassa ni trilionea mkubwa sana anayeweza kuwalipa maelfu ya wananchi wanaojitokeza kumuunga mkono kila anapojitokeza! Na kama anaweza kufanya hilo, nitashangaa kuona vyombo husika vikilifumbia macho hili, kwa kuwa ni kansa inayolitafuna taifa. Lakini kuna watu wanaosifu timu yake kwa kuweza kuwaleta karibu na Lowassa watu wote hao. Na kama madai haya ni kweli basi anastahili sifa ya kuwa mhamasishaji mzuri. Ni vyema tukasema pia kuwa, kwa wagombea wote waliojitokeza, hakuna mwanasiasa anayemkaribia Lowassa kwa ‘umaarufu’. Na Lowassa amekuwa akitumia umaarufu huu kama karata yake ya turufu kuwafanya CCM wajue anakubalika. Je, CCM watashawishika?

Siasa za Uteuzi
Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikijinadi kuwa mchakato wake wa uteuzi wa wagombea ni wa kidemokrasia sana. Lakini kuihalisia, hasa katika ngazi ya wagombea wa Urais kamati mbili za awali zinaweza kutoa maelekezo. Kamati ya Usalama na Maadili ndio chombo cha kwanza kuwajadili watia nia. Kamati hii hujadili majina haya kwa kina, kwa kumptia kila mgombea na kisha kutoa mapendekezo kwa Mwenyekiti wa Chama. Kwa mujibu wa mmoja wa makada maarufu wa CCM, ripoti ya Kamati ya Usalama na Maadili huwa ni ya siri. Kiujumla, Kamati hii huundwa na sekretatiati pamoja na wakuu wa Idara mbalimbali kama vile Uenezi, Mambo ya Nje, Oganaizesheni, Uchumi na Fedha, na Uendeshaji. Kila mgombewa hupewa alama (grade).

Kamati ya pili inayopitia majina haya ya wagombea ni Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC). Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Rais wa Jamhuri, Makamu wa Rias, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Spika, Wenyeviti wa Jumuiya na Wajumbe 14 wa kuteuliwa. Kamati hii ina mamlaka ya kuchagua majina matano kati ya majina ya wagombea wote ambao watapelekwa katika kamati ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili yapigiwe kura. Ingawa Kamati ya Usalama na Maadili nayo ina nafasi yake katika kutoa mapendekezo, Kamati Kuu ya Taifa ndiyo kikwazo kikubwa cha harakati za wagombea akiwemo Edward Lowassa kuendeleza safari yake ya matumaini.

Bundi katika Kambi ya Lowassa
Pamoja na umaarufu wake ambao umejidhihirisha katika kila kona ya nchi alikopita kutafuta wadhamini, wachambuzi wameyasema mambo kadhaa ambayo yanaitia dosari safari yake ya matumaini. Kati ya hayo, makubwa ni mawili. Mosi, amekuwa akituhumiwa sana kwa ufisadi. Tangu miaka ya 1990, maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu utajiri wake. Ingawa hakuna takwimu sahihi za utajiri huo [kwa maana sijawahi kuliona jina lake katika gazeti la Forbes Africa] lakini tuhuma hizi zimekuwa sehemu ya maisha yake ya kisiasa. Inasadikiwa kuwa, Mwalimu alimkataa Lowassa kwa sababu ya utajiri huo ambao chanzo chake hakielezeki. Kilele cha tuhuma ilikuwa na kashfa ya kampuni ya kufua umeme maarufu kama Richmond, mwaka 2008. Lowassa akiwa Waziri Mkuu alipinga tuhuma hizo akidai kuwa wapinzani wake walikuwa wanautaka Uwaziri Mkuu. Hivyo basi, aliamua kujiuzulu ili tu awape amani wapinzani hao. Wananadharia za Kihaini (Conspiracy Theorists) walimhusisha pia ‘Mkuu wa Kaya’ katika anguko la ‘Bwana Mkubwa huyu, wakidhahania kuwa, alikuwa ‘akimfunika’ Rais katika utendaji wake, hivyo ilimpasa kuondoka.

Hivi karibuni Lowassa amejitahidi kujibu tuhuma hizo na kuna kauli mbili nzito alizozitoa. Ya kwanza aliitoa kwa waandishi wa habari Dodoma akidai kuwa, Richmond haikuhusisha pesa hata senti tano, na yeye mwenyewe ndiye aliyezuia malipo ya aina yoyote yasifanyike kwa kampuni hiyo mpaka pale ambapo wangekuwa wamejiridhisha. Aliendelea pia kusema kuwa [waandishi wa ripoti hiyo ya kamati teule ya Bunge] wanapaswa kuona aibu kwa kuwa mitambo ya Richmond ilionekana bora zaidi katika kufua umeme na ikathibitishwa na Rais wa Marekani Barack Obama na (aliyekuwa) waziri wake Hillary Clinton walipokuja kuzuru nchini. Kauli ya pili ameitoa hivi karibuni aliposema mtu anayemtuhumu kwa ufisadi na ana ushahidi basi na amtaje. Ukweli  ni kuwa mpaka sasa tuhuma za ufisadi dhidi ya mtia nia huyu hazijawahi kuthibitishwa. Kisheria, mtu huyu anapaswa kudhaniwa kuwa si mkosaji mpaka ithibitishwe. Lakini kisiasa, vipimo tofauti vinatumika. Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, Rais wa nchi hapaswi hata ‘kutuhumiwa’ tu. Kauli hii ya Nyerere inaweza kuwa imepitwa na wakati, kwa kuwa kutuhumiana miaka ya sasa imekuwa mbinu ya kisiasa. Spika wa zamani, Samwel Sitta aliiita mbinu hii ‘siasa za maji taka’. Kuthibitisha hilo, takribani watia nia wote wa CCM wameshawahi kutuhumiwa kwa namna moja au nyingine hasa hasa katika mambo ya ufisadi.

Doa la pili ni lile la afya yake. Wachambuzi wamemuandika Lowassa kuwa ni mdhaifu wa afya.  Kuna baadhi ya wachambuzi wanadhani mtia nia huyu ni mdhaifu. Hata hivyo, Lowassa amejitahidi kuonyesha uimara (u-fit) wake kwa maneno na matendo. Katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari Lowassa alisisitiza yuko ‘fit’ kiafya na akasisitiza yeye na watia nia wenzake wapimwe afya na jopo la madaktari wa ndani nje ya nchi. Walakini, majibu haya hayajawatosheleza wengi na swali juu ya afya ya mtia nia huyu bado lipo kwenye midomo ya Watanzania walio wengi.

Mustakabali wa Lowassa
Ni vyema tuakaanza na mtazamo chanya. Akiteuliwa Lowassa, je, ataweza kuihakikishia CCM ushindi dhidi wa wapinzani wake? Hilo ni swali gumu, hasa pale ambapo upinzani wamekaa kimya wakisikilizia. Hata hivyo, Lowassa anabebwa na kura za maoni zilizoendeshwa na baadhi ya Taasisi za utafiti nchini. Kwa mfano, kabla hata hawajatangaza nia, TWAWEZA walitoa majibu ya maoni yao na walimtangaza Lowassa kama ndiye anayeongoza kwa kukubalika. Inasadikiwa pia kuna utafiti ulifanyika hivi karibuni, ambao unaonyesha pia Lowassa anakubalika zaidi kuliko Dr. Wilbrod Slaa wa UKAWA. Tafiti hizi zinatoa taswira kuwa Lowassa ana mvuto na anachagulika. Hatujui atakubalika kwa kiasi gani kwani atakuwa na tuhuma lukuki za kujibu kutoka kwa wapinzani wakati wa kampeni. Anachoweza kujipa moyo ni kuwa takribani tuhuma zote zimeshatajwa. Yawezekana wapinzani wake hawatakuwa na kashfa mpya ambayo itatikisa kampeni zake. Kwa utabiri wangu akiwa mgombea wa CCM anaweza kupata ushindi usiozidi 70%.

Hata hivyo, pamoja na mvuto wake, Lowassa ana kibarua kigumu kuhakikisha jina lake linapitishwa. Kauli za Mwenyekiti wa CCM akiwa katika maazimisho ya miaka 125 ya KKKT huko Mbuyukenda, yaliyofanyika mnamo Julai 5, 2015 jijini Tanga imezidi kutia shaka kama kweli Lowassa atapenya. Bila kujiumauma Mwenyekiti aliwataka Viongozi wa dini nchini kukemea wanasiasa wanaopenda madaraka na wanaotumia pesa ili kununua ushindi. Mwenyekiti alihitimisha kuwa, watu wa namna hii watalifikisha taifa pabaya. Ingawa watia nia wengi wametumia pesa kusaka ushindi, lakini kauli hii inashabihiana na tuhuma zilizoelekezwa kwa Lowassa na wapinzani wake katika mchakato wa uteuzi. Kimfumo, mwenyekiti wa chama ana ‘kura ya turufu’ katika vikao vya awali vya mchujo ambavyo havihitaji uwingi wa kura. Kama alichokiongea Mwenyekiti ndicho anachokiamini, kuna walakini kwamba jina la mwanasiasa huyu mwenye mvuto litapita katika kamati hizo.

Athari kwa CCM kama jina la Lowassa likikatwa
Mambo makuu matatu yanaweza kutokea kama jina la Lowassa halitapita kwenye mchujo wa wagombea. MOSI, Lowassa mwenyewe amesema hatahama CCM na asiyemtaka CCM aondoke yeye. Kwa kauli hii, tutegemee Lowassa kukubali kuwa ameenguliwa katika mchakato halali wa chama na atangaze kumuunga mkono aliyependekezwa na chama. Dhahania kuu katika mazingira haya ni kuwa viongozi wa chama wamekaa naye wakaongea kwa kina na wakakubaliana kuwa chama kwanza maslahi binafsi yaje baadaye. Katika hali hii, ambapo Lowassa atakuwa amewaomba wafuasi wake kumuunga mkono mteule wa Chama kuna uwezekano chama kitafanya vizuri. Lakini kutokana na mvuto uliofifia kwa hao wagombea wengine, CCM itapata ushindi mwembamba tu katika uchaguzi wa huru na haki.

Suala la kuzingatia katika mazingira haya ni mmpeperusha bendera mteule awe ameshafanya mazungumzo na Lowassa na wameafikiana. Hata hivyo, kuna ugumu sana wa kufikia mazingira hayo kwa sababu kuu mbili: Lowassa na kambi yake wanaamini kuwa wanachagulika, na wanajinadi kuwa ni chaguo la watu na ana uzoefu wa kiuongozi. Na pia, Lowassa alimuunga mkono Mwenyekiti wa sasa miaka kumi iliyopita na sasa anaona ni zamu yake kupeperusha bendera wa CCM.

Mazingira ya PILI ni yale ambapo Lowassa baada ya kukatwa akaamua kukaa kimya kabisa. Asiseme chochote. Kikubwa anachoweza kufanya ni kustaafu siasa maana ni mchezo uliomshinda. Hali hii inaweza kutafsiriwa na wafuasi wake kuwa ameonewa na wakaamua kukisusia chama. Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa alidokeza mazingira kama haya hivi karibuni akidai kuambiwa na vijana wa mkoa huo kuwa, kama CCM ikimkata Lowassa basi vijana ‘wataizingua’ CCM. Kwa maono yangu, hali ikiwa hivi na UKAWA wakawa wamejipanga vizuri, watatoa upinzani mkubwa sana kwa CCM. Hali ya kuchagulika kati ya CCM na UKAWA inaweza ikawa ni 50 kwa 50. Sababu zingine zozote zitaufanya upande wowote kushinda.
 Mazingira ya TATU ni pale ambapo Lowassa hataridhika na mchakato wa uteuzi na akaamua kuondoka CCM.  Kutokana na uzito wa jina lake Lowassa anaweza kutua UKAWA au akaamua tu kwenda katika chama kimojawapo kama vile ACT-Wazalendo. Labda tuanze na uwezekano wa yeye kwenda UKAWA. Kumekuwa na minong’ono mingi kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya mfumo, wakidai kuwa kuna makubaliano yasiyo rasmi kuwa watamkaribisha Lowassa akikatwa. Labda swali la kujiuliza ni, akitua UKAWA Lowassa anaweza kubadilisha hali ya upinzani kuchagulika? UKAWA wanaweza kuwa na kazi nyepesi mno ya kumnadi Lowassa. Kukosekana kwa ushahidi wa wazi katika tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa kunampa nafasi kubwa ya kuonekana kuwa ameonewa katika mikwaruzano ya kugombea madaraka ndani ya CCM kama mwenyewe alivyosema wakati anajiuzulu Uwaziri Mkuu. Hali itakuwa ngumu kwa CCM kama wataamua kumnyooshea Lowassa vidole au kuanza kufukunyua kashfa zake. CCM ndio wamemlea Lowassa mpaka alipofika na wamekuwa wakitetea chama chao ni cha wasafi. Kumnyooshea kidole Lowassa ni sawa na kurusha mawe kwenye nyumba yao wenyewe.

Kutokana na skendo nyingi zilizoendelea kuikumba CCM wapinzani watakuwa wamepandisha idadi ya kura zao kwa asilimia kadhaa. Katika uchaguzi wa mwisho walikuwa na jumla ya asilimia 38. Mwaka huu wanaweza kuwa na angalau 40%. Kwa maono yangu, kiwango hiki kinaweza kucheza kati ya asilimia 30 – 45 kutokana tu na wagombea wa pande zote mbili, mambo mengine yakibaki kama yalivyo. Kwa hali ilivyo basi, Lowassa ana takribani asilimia 20 - 30 [kadirio la chini nusu ya asilimia 60 za CCM] ya wana CCM wanaomuunga mkono kwa hali yeyote. Kama hesabu hii ikaletwa katika muktadha wa sanduku la kura, na Lowassa akafanikiwa kuondoka na wapiga kura wake wote, UKAWA ina nafasi ya kuleta upinzani na kuyafanya matokeo yawe 50-50 au wakafanikiwa kushinda kwa silimia 50.01 – 55. Kuna uwezekano mkubwa pia kwamba wabunge wa CCM watapungua sana, na hivyo kuwanyima uhuru wa kutawala mhimili huo wa dola.

Je, kama Lowassa hakubaliki UKAWA, nini hatima yake?
Kuna tetesi kuwa Lowassa amekuwa akifadhili shughuli za ACT. Ni chama kipya, lakini ilikuwa lazima kiongozi wake Zitto Kabwe azunguke Tanzania nzima kukinadi ili kukifanya kijulikane. Na kwa ujumla, Chama hiki hakiwezi kubezwa kwa jinsi kilivyovuta watu kwenye baadhi ya mikutano yake. Hatuwezi kukwepa ukweli pia, kama ilivyo Kenya, yawezekana Tanzania tunafikia hali ya watu kuwa na vyama na sisi tukawa tunafuata watu na sio vyama. Kama Lowassa akiamua kwenda ACT hali inaweza ikawa kama ifuatavyo: ACT Wazalendo na Zitto Kabwe tayari wameshafanya kauharibifu katika vyama vya upinzani hasa CHADEMA. Wafuasi wa Zitto amehama nao kutoka CHADEMA. Tumeona orodha ya viongozi wa vyama vya siasa wakijitangaza kuhama CHADEMA na CUF. Bila shaka na wanachama wa kawaida wamehamasika pia. Lakini ujio wa Lowassa utatoa mng’ao mpya kwa  ACT-Wazalendo. Kuna uwezekano chama hiki kikaharibu hali ya siasa nchini kwa kuvuta hisia za mashabiki wengi ambao wataondoka UKAWA na CCM.

Kimahesabu, hali inaweza ikawa hivi: tunaweza kusema kuwa ACT wana mtaji wa 2% kama wakisimamisha mgombea leo. Lakini mgombea akiwa na mvuto zaidi wanaweza kufikisha 7%, ambazo watazitoa katika vyama vya upinzani. UKAWA watabaki na 33%. Akiingia Lowassa akaja na 30% kutoka CCM basi ACT itakuwa na idadi ya 37% ya kura zote. CCM kwa upande wao watabakiwa na 30%. Mfumo wetu wa uchaguzi katika katiba ya sasa mshindi hupatikana kwa wingi wa kura tu (simple majority). Katika muktadha huu, ACT na Lowassa wanaweza kuwa washindi. Hata hivyo, kuna vigezo (factors) muhimu vya kuzingatia. Mosi, uchaguzi lazima uwe huru na wa haki. Kutakuwa na mbinu nyingi za kutaka kuiba kura. UKAWA na ACT itabidi wawe macho ili kura zisiibiwe. Lakini wizi wa kura utategemea vipi vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaaje kuiona CCM inatoka madarakani. Wakiridhia hilo au kama wakashindwa kulidhibiti Watanzania watarajie mabadiliko makubwa. Pili, kukubalika kwa mgombea atakayepitishwa na CCM. Kama watapitisha mgombea asiyeaminiwa na watia nia wengine waliobaki na asiyekuwa na uwezo wa kuunganisha makundi  yaliyopo, tutegemee viongozi hawa kuondoka na Lowassa. Hivyo hali ya CCM itazidi kuwa mbaya zaidi.

Hitimisho
Lowassa ni ‘jinamizi’ kwa wote wanaofikiria uchaguzi wa 2015. Jinamizi kama lilivyo katika hadithi za kale, linatisha. Inategemea tu, Lowassa na timu yake wamejipanga vipi kwa ajili ya huo uchaguzi, na kama wana mpango mbadala (plan) B, na C ili kuwaleta UKAWA na ACT kwenye mchezo. Lakini pia inategemea hawa wahusika wengine kama vile CCM, UKAWA na ACT walivyojipanga kulidhibiti au kulitumia jinamizi hili. Ni muhimu pia tukadhahania kuwa CCM inaweza kupasuka mikononi mwa Kikwete. 

6 comments:

ALPHONCE WIKEDZI July 9, 2015 at 9:18 AM  

Mwandishi nikupongeze sana. Umechambua vizuri sana maada hii.

Anonymous September 16, 2015 at 4:21 PM  

Hakika you are a genious, on top of your game! Hii ni September and what you wrote is almost the realite. Uchambuzi wa kisayansi.

Anonymous September 28, 2015 at 5:47 PM  

NIMEAMUA KUIREJEA ARTICLE YAKO. WEWE UNA AKILI NYINGI SANA NA NAKUKUBALI BY 90% NA JUU YA WENGINE WOTE WA AINA YAKO KATIKA JAMBO HILI. ENDELEA KUWA MKWELI NA WAELIMIHE WATANZANIA.

Anonymous October 22, 2015 at 3:17 PM  

Uliyajuaje haya? mbona ni ukweli mtupu?

bilashaka uko jikoni na unajua kinachendelea. Unakula na wakubwa wa pande zote.

hamisi abdallah October 27, 2015 at 4:08 AM  

Mh.Umenifungu kichwa changu mana nilikuwa gizani sitambui niripo simama wala nilipo kaa huwo niukweli mtupu nakupongeza kwakazi nzito uliyoichambua manawengine tumevaliswa miwani yambao mbele atuoni walanyuma ongela sana kwautafiti wako hasante sana

Anonymous October 5, 2016 at 11:50 PM  

WEWE NI GENIOUS, LEVEL YA NCHI ZILIZOENDELEA.

YOU PREDICTED THE FUTURE OF TANZANIA, YOU CARRIED IT IN YOUR HANDS!

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP