Monday, July 6, 2015

Mapitio ya Kitabu cha Profesa Chachage

KITABU NILICHOKISOMA JUNI 2015

Na Godfrey Eliseus Massay

Mwandishi: Chachage Seithy L. Chachage
Mahali ilipochapishwa: Dar es Salaam
Mwaka: 2014

Muhtasari wa Kitabu
Kitabu hiki kinajumuisha jumla ya makala 21 zilizoandikwa na hayati Profesa Chachage Seithy Chachage kati ya mwaka 2000 hadi kabla ya kifo chake mwezi Julai 2006. Prof. Shivji ambaye ni rafiki wa karibu wa mwandishi ameandika utangulizi wa kitabu. Kitabu kimegawanyika katika sehemu tatu ambazo zinadadisi kwa kuuliza swali kumfikirisha msomaji. Sehemu ya kwanza, Utandawazi au Utandawizi? Ina makala sita (6). Sehemu ya pili, Soko Huria au Soko Holela? Ina makala sita (6). Na sehemu ya tatu, Mwelekeo Bora au Bora Mwelekeo? Ina makala tisa (9). Katika makala zote, Profesa Chachage anachambua madhara ya mfumo wa utandawazi katika jamii ya Watanzania. Binafsi sitaelezea kila makala imesema nini bali nitaelezea dhima kuu zailizojadiliwa katika kila sehemu ya kitabu. Lengo ni kukutia hamasa ya kukisoma kitabu hiki wewe unayesoma makala haya.

Sehemu ya Kwanza
Sehemu hii inaonyesha kwa kina namna ambavyo mfumo wa utandawazi umekuwa ukitumia propaganda za kuhadaa na kidanganyifu katika kufukarisha na kuharibu mifumo ya jamii. Mwandishi anaeleza namna ambavyo mfumo unaikuza lugha ya Kiingereza kama lugha bora ya kidunia hata kuifanya lugha ya Kiswahili ionekane haina nafasi. Anaeleza kwa umahiri mkubwa namna ambavyo utamaduni, lugha na maendeleo ya Nchi yanavyohusiana. Anapinga vikali ukandamizaji wa lugha ya Kiswahili katika maendeleo ya Nchi. Aidha, mwandishi anaeleza namna ambavyo muziki umetumika kueleza madhara ya mfumo wa utandawazi nchini. Vijana kama kundi kubwa ambalo limeathiriwa na mfumo huu wamebuni nyimbo na misamiati kuonyesha namna wanavyoathiriwa na ugumu ya maisha. Madhara makubwa yaliyowapata wananchi na Taifa kutokana na uchimbaji wa madini na mapambano ya Umma dhidi ya mbinu za unyanyasaji na ukandamizaji yanaelezewa kwa kina. Mwandishi anatoa mifano ya mapambano katika sehemu mbalimbali duniani huku akionyesha namna Watanzania walivyopambana kuupinga ukandamizaji tangu kipindi cha vita vya Maji Maji. Mwandishi hakuishia hapo, anaeleza madhila ya wafanyakazi yatokanayo na mfumo wa Utandawazi kwa uwazi na ufasaha mkubwa. Kama namna ya kutafuta njia ya kutafuta mwarobaini wa matatizo yao, Nchi za Afrika zilitengeneza mpango wa ushirika mpya wa maendeleo ya Afrika-NEPAD. Mwandishi anaonyesha kuwa mpango huo si chochote bali  namna nyingine ya kuwanyonya na kuwakandamiza Waafrika. Ni mpango ambao  ulipata kibali na unategemea fedha kutoka kwa mataifa makubwa ya kibeberu na wenye lengo la kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji wa makampuni ya kibeberu barani Afrika.

Sehemu ya Pili
Makala zote za sehemu hii zinaeleza uholela wa soko katika zama za utandawazi. Katika mahojiano, mwandishi anaeleza sababu zilizomsukuma kuandika na upekee wa Riwaya yake ya Makuadi wa Soko Huria. Anasisitiza kuwa ni riwaya ya kweli na yenye kueleza mfumo wa utandawazi katika muktadha wa historia. Mabadiliko yaliyosababisha madhaifu ya bodi za Tumbaku na Korosho ambazo kwa pamoja zilisababisha kuanguka kwa soko na ubetuaji wa wakulima yanaelezwa kwa kina. Chachage anasimulia namna ambavyo takwimu za utalii zinatumika kupotosha ukweli juu ya mchango wa sekta katika pato la taifa. Suala la takwimu linaelezewa katika upana wake kwa kujumuisha changamoto za uwezo wa mamlaka husika, upatikanaji wa taarifa sahihi, na tafsiri ya takwimu. Aidha mwandishi anaeleza mgogoro wa magunia uliosababishwa na wafanyabishara na serikali na hivyo kuathiri biashara ya korosho nchini. Mwandishi anajadili pia tatizo la uandishi na uchapishaji wa vitabu katika zama za utandawazi.  Hoja yake ni kuwa Watanzania hawana tabia ya kusoma vitabu na wengi hupendelea vitabu visivyo vya msingi kama vile vinavyoelezea mapenzi, upelelezi, mapishi, urembo, na namna ya kupata utajiri haraka. Haya ni matokeo ya utandawazi.

Sehemu ya Tatu
Hii ni sehemu yenye makala nyingi zaidi kuliko sehemu zingine. Jumla ya makala tisa zimejadili kuonyesha 'bora mweleko'. Nilivutiwa zaidi na mada mbili, moja juu ya vyama vingi na utamaduni wake na ya pili juu ya biashara ya shahada. Katika hiyo mada ya kwanza mwandishi anaeleza kuwa mfumo wa vyama vingi una utamaduni wake ambao umekuwa ukitumika hasa katika nchi zilizoasisi vyama vingi. Kubwa kuliko vyote ni utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi. Hapa Tanzania katika chaguzi zote, hasa za Zanzibar, kumekuwa na tatizo kubwa la kuuheshimu utamaduni huu. Hata hivyo, mwandishi anadokeza upekee wa siasa za Zanzibar ambazo hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema serikali ya mseto ni njia pekee ya kumaliza mgogoro wa kisiasa kati ya CCM na CUF. Katika mwaka huu wa uchaguzi ni vyema kujikumbusha kuhusu utamaduni wa vyama vingi na kuuheshimu. Mada juu ya biashara ya shahada imejikita zaidi katika vyuo vya Uingereza ambavyo vina matawi nje ya nchi hiyo na namna vinavyotengeza pesa nyingi kutokana na biashara ya shahada. Hii ni biashara ambayo huangalia fedha zaidi kuliko sifa za mwombaji. Chachage anadokeza kuwa nchi za Afrika ndizo zinazoathirika kwani wanafunzi kutoka Afrika ndiyo wanaongoza kununua shahada hizo. Hii inanikumbusha miaka michache iliyopita, kuna mwandishi alitoa kitabu chenye majina ya wanasiasa ambao shahada zako zilikuwa na matatizo. Hakuna mwanasiasa hata moja aliyeenda mahakamani na mwandishi wa kitabu kile alipania kuweka mabango makubwa yenye picha viongozi hao katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. Hakusikika tena kwenye vyombo vya habari!

Somo
Kitabu hiki kimenisaidia kuuelewa utandawazi na ubeberu kwa undani zaidi. Kimenionyesha madhila ambayo wakulima, wafanyakazi na serikali wanayapata na wataendelea kuyapata kutokana na mfumo huu hapa nchini. Kinanifikirisha katika kutafuta namna ya kukabiliana na mfumo huu. Kimenipa ari ya kutafuta na kusoma vitabu vyote alivyoviandika Profesa Chachage. Ili kuelewa zaidi Utandawazi, nashauri usome pia vitabu vilivyoandikwa na David Harvey, Thandika Mkandawire, Issa Shivji, Karim Hirji, Adebayo Olukoshi na Karl Polanyi.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP