Thursday, July 9, 2015

Wagiriki Wametimiza Ndoto ya Nyerere

Wagiriki Wametimiza Ndoto ya Nyerere

*Wapiga kura kuyakataa masharti ya IMF
**Shivji asema tulichoshindwa Waafrika, Wakigiriki wamekiweza

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Jumamosi, Julai 4, 2015, tulikuwa katika mabishano makali kwa njia ya barua-pepe. Wanafunzi wenzangu wa shahada ya uzamivu walikuwa wakitaka walipwe fedha ya kujikimu inayoendana na viwango vya nchi tajiri. Iwapo viwango hivyo vitakubalika, basi mwanafunzi mwenye familia atakuwa akilipwa kiasi cha dola 2,500 (sawa na shilingi milioni tano) kwa mwezi.

Mie nilikataa. Nilisema kuwa kiasi hicho ni kikubwa sana kulinganisha na hali halisi ya nchi za Kiafrika. Hakuna chuo chochote hapa Afrika kinachotoa kiwango hicho cha fedha. Zaidi ya hapo, fedha zote hutegemea ufadhili, na iwapo ufadhili utakatika ndio utakuwa mwisho wa masomo. Kwa vyovyote vile, ili ufadhili uendelee ni lazima tufumbie macho uporaji wa rasilimali za Afrika unaofanywa na nchi za kibeberu. Tukiukataa unyonyaji na uporaji huo, hakuna ufadhili! Nilitoa sababu nyingine: malipo hayo yatazalisha wasomi walafi, ambao, kama walivyo wanasiasa wetu, wataenda kuwakamua wanyonge ili wajilipe mishahara minono na “miposho” mikubwa.

Kwa kuwa wengi walichagua upande wa walafi, nilichofanya ni kujiuzulu nafasi yangu ya ujumbe wa kamati ya uandishi wa sera ya fedha za kujikimu. Nilisema nisingependa historia iniweke katika upande wa walafi. Nikimnukuu Alexis Tsipras, waziri mkuu wa Ugiriki, nilisema siwezi kuwa mwandishi wa “kila tokeo”.

Naam, Tsipras alisema kuwa hawezi kuwa “waziri mkuu wa kila tokeo” (“I cannot be prime minister of every outcome”). Hii ilikuwa ni baada ya “utatu mtaka-vitu” (Troika) unaoundwa na nchi za sarafu ya euro (Eurogroup), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na Benki ya Biashara ya Ulaya (ECB) kuilazimisha Ugiriki kukumbatia sera za uliberali mambo-leo zilizoisababishia Ugiriki dhahama kubwa.

Hivi sasa karibuni asilimia 50 ya vijana wa Ugiriki hawana ajira, huku serikali ikiwa imejiondoa katika utoaji wa huduma za msingi. Na bado Troika wanailazimisha Ugiriki iongeze kodi kwa walalahoi, iondoe pensheni kwa wastaafu pamoja na ruzuku kwa wanyonge. Masharti mengine ni pamoja na kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za kigeni na kubinafsisha kampuni za umma.

Tsipras na serikali yake walikataa. Walisema kuwa sera hizo ni za kijambazi na za kiuaji na zinainyima Ugiriki haki ya kujiamulia mambo yake yenyewe. Serikali inayoongozwa na Tsipras ikajiondoa katika mazungumzo kuhusu mikopo mipya, na ikagoma kuendelea kulipa deni inalodaiwa na Troika. Na ikaitisha kura ya maoni ili wananchi wa Ugiriki waamue kama wanataka kufuata masharti ya “Troika” ama la. Tsipras mwenyewe alitishia kujiuzulu iwapo upande wake ungeshindwa, akisisitiza kuwa hakuwa tayari kutekeleza sera za kiuaji.

Japokuwa mwanzoni niliuunga mkono umamuzi huo wa Tsipras baadaye nilianza kuutilia shaka. Chama cha SYRIZA kiongozwacho na Tsipras kina miezi sita tu madarakani, na hakijapata wakati wa kujidhatiti ili kutekeleza sera zake za kijamaa. Niliwaona SYRIZA wakichezea shilingi katika tundu la choo.

Kingine kilichonipa mashaka ni pale vyama vya kibepari vilipoungana na “Troika” kuihujumu serikali ya SYRIZA. Walitunga mbinu nyingi kuwahadaa wananchi kuwa iwapo upande wa “hapana” ungeshinda basi Ugiriki ingetimuliwa katika ukanda wa sarafu ya Euro na isingepata mikopo, hivyo kungekuwa na ufukara wa kudumu.

Serikali ya Ujerumani ambayo ndiyo “kaka mkubwa” wa ukanda wa Euro, ndiyo hasa iliyoongoza kampeni dhidi ya SYRIZA. Siku moja kabla ya kura ya maoni, mashabiki wa SYRIZA nchini Ujerumani waliukatisha mkutano wa Kansela wa nchi hiyo, Angela Markel, wakiwa wamebeba mabango ya OXI (hapana). Baada ya “wavamizi” hao kuondolewa, Merkel, kwa mbwembwe, akawataka Wagiriki kupiga kura ya NAI (ndiyo).

Mpaka siku moja kabla ya kura ya maoni, vyombo vya habari vya kibwanyenye viliripoti kuwa wananchi wa Ugiriki wamegawanyika sawa kwa sawa kuhusu kura ya maoni, na kulikuwa na uwezekano wa upande wa “ndiyo” kushinda.

Majuma machache kabla ya Serikali ya SYRIZA kujiondoa katika mazungumzo, Tume ya Kuchunguza Uhalali wa Deni la Ugiriki ilitoa taarifa yake ya awali.  Kwa ufupi taarifa ya Kamati hiyo inasema kuwa serikali ya Ugiriki iliyokuwa ikiongozwa na vyama vya kibepari, ilipanga njama za kukopa fedha kwa kushirikiana na “Troika” huku wakijua kabisa kuwa Ugrikiri isingeweza  kulipa madeni hayo. Zaidi ya asilimia 90 ya fedha hizo zilichukuliwa na benki na kampuni za kibepari, huku kiasi kilichoenda serikalini kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa kawaida ni pungufu ya asilimia 10.

Taarifa hiyo inazidi kubainisha kuwa tangu Ugiriki ilipoanza kufuata sera za uliberali-mamboleo miaka ya 1980, deni la serikali lilianza kupaa. Kupaa huko hakukutokana na matumizi makubwa ya serikali, bali kulitokana na riba kubwa zilipwazo kwa wakopeshaji pamoja serikali kutoa ruzuku za mitaji kwa benki na kampuni binafsi. Ukopaji wa fedha hizo ulikiuka taratibu za kisheria na ulienda kinyume na matakwa ya wananchi.

Taarifa hiyo ikaweka msimamo:

“Ushahidi wote tunaouwasilisha katika taarifa hii unaonyesha kuwa Ugiriki haina uwezo wa kulipa deni hili, lakini pia haipaswi kulilipa kwa sababu deni hilo litokanalo na mipango ya ‘utatu mtaka-vitu’ (Troika) ni ukiukwaji wa haki za msingi za watu wa Ugiriki. Kwa hiyo, tumefikia hitimisho kuwa Ugiriki isilipe deni hilo kwa sababu ni la kilaghai, haramu na la kionevu” (tafsiri yangu).

Taarifa hiyo inaungwa mkono na wabunge walio wengi katika Bunge la Ugiriki, pamoja na Chama cha SYRIZA, ambao wote wanaitaka serikali igome kabisa kulipa deni hilo.

Sasa sauti za wananchi wa Ugiriki zimepigilia msumari. Matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa Jumapili, Julai 5, 2015 yamethibitisha matakwa ya wengi. Asilimia 61.3 ya waliopiga kura wamesema “HAPANA”, huku waliosema ndiyo wakiwa ni asilimia 38.7 tu. Wengi wape. Wagiriki wameamua kuzikataa sera za kiuaji za uliberali mambo-leo.

Yalipotangazwa matokeo nilijikuta nikitoka nje kushangilia. Muda mfupi baadaye, nikapokea ujumbe wa simu kutoka kwa Profesa Issa Shivji, ambae hakuficha furaha yake: “Hili ni jambo jema sana. Watu wa Ugiriki wameukataa uendawazimu wa sera za uliberali-mamboleo. Tulichoshindwa kukifanya Afrika kama bara, wamekifanikisha kama nchi” (tafsiri yangu).

Nami nilimjibu: “Huwezi kujua furaha niliyonayo. Nimekuwa nikiufuatilia mjadala wa Ugiriki kwa karibu sana. Wagiriki wameandika historia. Nikitumia maneno ya mwanamapinduzi Lenin, ukuta wa uliberali mamboleo umeoza na unatweta. Tunachotakiwa kufanya ni kuusukuma ili uanguke”.

Wagiriki wametimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere. Kinachotokea Ugiriki hivi sasa hakina tofauti na kilichoikumba Tanzania miaka ya 1980 ambapo IMF kwa kushirikiana na Marekani na Uingereza waliilazimisha Tanzania kuachana na sera za kijamaa ili kukumbatia sera za uliberali mamboleo. Mwalimu aliigomea IMF huku akiuliza, “When did the IMF become an ‘International Ministry of Finance’? When did nations agree to surrender to it their power of decision making?” (Kwa tafsiri isiyo rasmi, “Tangu lini IMF imegeuka kuwa Wizara ya Kimataifa ya Fedha? Tangu lini mataifa yalikubali kusalimisha mamlaka yao ya kujiamulia mambo yao kwa IMF?)

Na hapo ndipo Mwalimu alisisitiza kuhusu msimamo wa Tanzania: “Tanzania haiko tayari kushusha thamani ya fedha yake eti kwa sababu hili ndilo suluhisho la kimapokeo la ‘Soko Huria’ kwa kila kitu bila kujali maslahi yetu. Tanzania haiko tayari kusalimisha haki yake ya kudhibiti bidhaa ziagizwazo toka nje, kwa hatua zilizolenga kuhakikisha kuwa tunaagiza dawa za hospitali badala ya vipodozi, au mabasi badala ya magari ya watu binafsi kwa ajili ya vigogo. Serikali yangu haiko tayari kuachana na jukumu letu la msingi la kutoa elimu ya msingi kwa kila mtoto, huduma za matibabu ya msingi na maji safi na salama kwa ajili ya watu wetu wote”.

Katika hotuba hiyo, iliyotolewa katika hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya 1980 iliyoandaliwa kwa ajili ya mabalozi, Mwalimu alisisitiza: “Na juu ya yote hayo tutaendelea na jukumu letu la kujenga jamii ya kijamaa”.

Mwalimu hakufanikiwa katika harakati zake za kuizima IMF na kuzizika sera za uliberali mamboleo. Ndani ya Chama chake na serikalini kulikuwa na kundi kubwa lililoshirikiana na wahujumu uchumi kuuteketeza ujamaa. Kundi hili lililoungwa mkono na IMF na nchi za kibeberu lilipata nguvu zaidi.

Mwalimu alipoondoka maradakani, serikali ya Mwinyi ilisaini mkataba na IMF, na kisha zikaanza zama mpya za ubinafsishaji wa mashirika ya umma, uporaji wa machimbo na ardhi ya wachimbaji wadogo na wakulima, serikali kujiondoa katika utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi wake, na ufisadi mkubwa wa kutisha.

Duniani kote hivi sasa wanyonge wameunganisha nguvu kuzikataa sera hizi. Katika bara la Amerika ya Kusini, wanyonge wa nchi hizo wamevichagua vyama vya kijamaa kuongoza katika nchi za Cuba, Ecuador, Nicaragua, Venezuela na Bolivia. Nchini Brazil, Argentina na Uruguay vipo vyama vya mrengo wa kati, lakini vyenye kupinga uliberali mamboleo. Huko Ulaya, baada ya SYRIZA kuingia madarakani, vuguvugu la kijamaa limepata nguvu kubwa sana katika nchi za Italia na Hispania.

Vuguvugu hili la kuubomoa ubepari litafanikiwa. Kama alivyopata kusema Mwalimu mwaka 1972, “Mabeberu na wabaguzi wa rangi watatoweka; Vorster na wenzake kama yeye watazuka na watatoweka. Kila beberu na mbaguzi wa rangi ni mnyama wa aina fulani; na aina hizo za unyama hazina nafasi ya kudumu. Hatimaye zitatoweka! Afrika lazima ikatae kusukumwasukumwa na kunyonywa.”
 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP