Monday, August 24, 2015

Lugha ni Hisia?

EB:

Mimi mtazamo wangu wa lugha ya kufundishia unafanana na wale wanaosema Kiswahili kitumike. Pamoja na hoja nyingi walizotumia wenzangu cha kuongezea ni kuwa ni muhimu kuzingatia kuwa ‘LUGHA NI HISIA’. Kwa kutumia lugha na maneno sahihi unaweza kujenga hisia na picha fulani kuonesha au kuelezea hayo maneno na hivyo kuongeza UELEWA wa hilo jambo.

Mfano mdogo ni mtu akikuambia 'UDONGO MFINYANZI' na 'CLAY SOIL’. Kuna hisia tofauti unaipata ukiambiwa na lugha yako mama, kwangu mimi mtu akisema udongo mfinyanzi napata hisia za udongo unaonatanata moja kwa moja bila maelezo mengine, CLAY SOIL itabidi niitafsiri kwanza kwa kiswahili ndio nipate hisia hizo hizo. Sasa katika kujenga UELEWA ni muhimu wanafunzi wetu wapate hizo HISIA wakati wanafundishwa, la sivyo vingi watakuwa WANAKARIRISHWA.

Kuna mifano mingine mingi ya maneno kama mtu akikutukana kwa kiswahili na akikutukana kwa kiingereza au lugha nyingine ambayo sio lugha yako mama, tusi lipi litakuuma zaidi au kukupa hisia kali zaidi?

Kwa upande mwingine ni ukweli usio na shaka pia kuwa, sio watanzania wote wanatumia kiswahili kama lugha mama. Haswa kwenye makabila makubwa kama WAHAYA, WANYAKYUSA na WACHAGA n.k. Lugha zao ndio zinapewa kipaumbele haswa haswa wakiwa vijijini, hivyo kufifisha hoja ya kutumia KISWAHILI kwa kuwa sio lugha mama yao. Ila ni vyema kuangalia pia kutokana na muingiliano wa makabila (inter-mariages) n.k. kuna dalili nyingi kuwa lugha zetu za nyumbani zitafifia, na pengine kiswahili ndio lugha inayoweza kutu-unganisha.

Kwa wale waliokuwa na hoja kuwa kiingereza ni lugha ya kimataifa, hivyo ili kutayarisha vijana wetu vyema kuna tija kama tutawafundishiwa watoto wetu kwa kingereza. Swali langu kwao ni, je, ni idadi gani ya watanzania kweli kwenye kazi zao wanalo hilo hitaji la kuwasiliania kwa kiingereza? Sina takwimu ila nahisi ni chini ya asilimia 2 ya watanzania wanahitaji kiingereza katika taaluma zao. Watanzania walio wengi hawatofika vyuo vikuu, pengine nguvukazi kubwa ya vijana watasomea VETA, hivyo kweli hitaji kubwa la msusi/makenika/barmaid/mwendesha bajaji/mkulima atakayeshughulika kwa asilimia kubwa na watanzania ni kujua kingereza au kuelewa taaluma yake kiufasaha?
Binafsi siamini kama kuna hitaji kubwa la kujua kiingereza kwa watanzania walio wengi kwa sasa, kuliko hitaji la watanzania kuelewa taaluma zao kiufasaha. Mfano binafsi ni kuwa mimi lugha yangu niliyojifunzia katika ngazi zote za masomo ni kiingereza, tangia vidudu, msingi, sekondari n.k. Ila nyumbani, shuleni na wenzangu na kwenye michezo nilikuwa naongea kiswahili kwa kuwa watu niliozungukwa nao ama hawakupendelea au hawakujua kuongea kiingereza muda wote. Ila pamoja na hayo, ‘Newton's law of motion’ niliikariri tu kidato cha pili, ilileta maana tu nilipofika A-level, kabla ya hapo nilikuwa natumia formula tu.

Ingawa ni ukweli usio na shaka, tatizo la elimu Tanzania yetu sio Lugha ya Kufundishia tu, ni vitu vingi ila kufundishia kwa kiswahili ni hatua muhimu kwenye njia sahihi.
BJ:

Katika kuchangia mada ya 'lugha ya kufundishia' [EB] amezungumzia kuhusu hisia mtu anazopata akisoma au akisikia lugha fulani, ikanikumbusha swali nililowahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja. Tulikuwa tunazungumza tu hili na lile akaniuliza, "Hivi BJ, huwa ukiota ndogo unaota kwa lugha gani?" Nadhani swali la rafiki yangu huenda likawa relevant katika huu mjadala kwa sababu, na hapa naungana na [EB], ni rahisi zaidi kwa mtu kuota au kufikiri kwa lugha ambayo inampa hisia. 

Najaribu kufikiria kwa sauti hapa, huenda tunalenga mno kwenye uwezo wa wanafunzi kuifahamu lugha na/au kutofautisha lugha ya kuzungumza na ile ya kufundishia, wakati pengine tatizo liko zaidi katika umahiri wa lugha miongoni mwa wafundishaji wa hizi lugha, pamoja na njia wanazotumia kufundishia. Ikiwa mwalimu wa Kiswahili au wa Kiingereza anashindwa kuzungumza lugha anayoifundisha vizuri, tunategemea wanafunzi wafanyeje? Ndio maana si jambo la kushangaza kukuta Mtangazaji wa redioni au wa runinga au Mwandishi wa habari kwenye magazeti akitamka au kuandika kwa kutumia lugha isiyo sahihi. 
Nikija kwenye mbinu za kufundishia, nilipokuwa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu nilichukua somo la 'LL110' sijui kama bado hilo somo lipo siku hizi. Tulifundishwa Kiingereza Sanifu. Tulikuwa na language labs ambapo unaingia kwenye booth unavaa headphones kisha unasikiliza maelekezo ya mwalimu. Wakati mwingine atakusomea neno na kukuomba ulitamke huku akisikiliza kama umelitamka vizuri na kukupa mrejesho hapo hapo. Kisha atakupa spelling test, atalitamka neno na wewe unaandika kile unachosikia, halafu utapewa paragraph fupi uisome wakati huo mwalimu akiwa anakusikiliza unavyotamka maneno, the tone of voice unayotumia and the expression. We were taught how to read with expression. 

Leo hii unaweza kukuta mtoto wa darasa la 7 anasoma kama mtoto anaejifunza kusoma, as in: "Hi li ni ja mbo la ku sha nga za sa na..." na anapofika mwisho wa sentensi akamalizia kwa kuashiria kwamba sentensi inaendelea badala ya kuweka sauti inayoonesha sentensi imefika mwisho na kutumia tone inayoashiria mshangao huo anaouzungumzia. Ilitufanya tufurahie sana somo la Kiingereza, tupende kujisomea zaidi na kukizungumza. Lakini pia ilitusaidia kujieleza vizuri zaidi katika masomo mengine. Naamini kabisa kwamba essays tulizokuwa tunaandika sisi wana LL110 zilikuwa zinanoga zaidi :) 

Maybe this is asking for too much given our situation today where in most schools and colleges classrooms are overcrowded, teachers overworked and underpaid and have to work with limited materials. Lakini, tukiweza kubadilisha mfumo wa elimu na mitazamo (attitudes) ya waalimu na wamiliki wa shule ikiwemo Serikali na watu binafsi, tunaweza kuleta mabadiliko. 
Kila siku tunapiga kelele "Elimu ipewe kipaumbele" but we need to define what exactly do we mean! If you ask me, I would say we need a total overhaul of the education system in our country and a change in mindset with regard to the teaching profession as a whole. Siku hizi ualimu unachukuliwa kama last resort hata mtu akipangiwa kusomea ualimu kama sio chaguo lake haioni kama fursa anaiona kama adhabu. Tunasahau kwamba waalimu ndio wanaozalisha Waalimu wengine, Madaktari, Wahandisi, Wahasibu, n.k. 

So katika kuchangia nini kifanyike naomba nianze na haya machache:

1. Tukianza hapa tulipo (simple reorganization - minimal cost if any) Wamiliki wa shule/Wakuu wa shule wawapangie waalimu masomo ya kufundisha kulingana na umahiri na uwezo wao wa kufundisha masomo wanayopangiwa. Kama shule haina mwalimu wa somo fulani lakini shule ya jirani inaye basi wafanye utaratibu wa kutumia mwalimu wa shule ya jirani. Some sort of teacher exchange programme. Hili ni jambo ambalo Wakuu wa shule kwa kushirikiana na Wakaguzi wa Elimu na Idara za Elimu katika Halmashauri husika wanaweza kukubaliana jinsi ya kulitekeleza. 

2. Waalimu waanzishe au waendeleze mbinu za kufundishia zinazotia hamasa ya kujifunza. Kwa mfano, mashindano ya kuandika na kusoma ngojera, mashindano ya kuandika insha na makala na mbinu nyingine za kukuza uwezo wa lugha miongoni mwa wanafunzi. Siku hizi tuko kwenye enzi za jiditali - tunaweza kutumia televised classes zilizoandaliwa na waalimu waliobobea kwenye masomo mbalimbali na hizo classes zikawa available kama clip ambayo mwanafunzi anaweza kupakua hata kwenye simu yake ya mkononi. Again maybe this is thinking too far lakini matumizi ya simu za mkononi yanazidi kuenea na baadhi ya taarifa tayari zinatumwa kwa kutumia mitandao ya simu za mkononi. Mfano mzuri ni huo wa kuhakiki taarifa za wapiga kura. Can we not do the same for education-related matters? 

3. Tufanye utafiti kwa kuwauliza wanafunzi "How they would like to learn. We may very well be surprised. I believe if students enjoy the learning process they are more likely to understand what they are being taught. Na hii naweza kutoa ushuhuda mimi mwenyewe. Miaka kadhaa iliyopita niliwasaidia watoto wa rafiki zangu waliokuwa wanahangaika kuwahamisha watoto wao kutoka shule moja kwenda nyingine. Mmoja wao alikuwa na watoto wawili waliosoma English medium fulani (jina kapuni) kwa miaka 3 na bado walikuwa hawawezi kusoma "This is a cat" n.k. Nilitumia mbinu nilizojifunza kwenye language lab niliyoizungumzia hapo juu na ndani ya wiki mbili mabadiliko yakaanza kujionyesha. Those kids wako Chuo kikuu sasa hivi and they always tell me how I made a difference in their learning. Mmoja alikuwa akisikia tu nimebisha hodi alikuwa anajificha uvunguni mwa kitanda. Lakini alipoona kwamba anapata alama za juu zaidi kwenye somo la Kiingereza na Mwalimu wa somo akawa anamtolea mfano kama mwanafunzi bora kwenye somo la Kiingereza akamwomba mama yake aongeze siku za tuition. There is a lot we can do to turn things around starting with the basics.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP