Wednesday, August 12, 2015

Nani Atatuokoa Tanzania - Lowassa au Magufuli?


Nani Atatuokoa Watanzania - Lowassa au Magufuli?

"Historia ya vyama vingi Tanzania inatuonyesha kuwa umaarufu wa masiha ni katika uchaguzi mmoja tu" - Sabatho Nyamsenda: Masiha wa Tanzania 2015 ni Nani?

Chambi Chachage

Hali ilikuwa ni mbaya sana nchini Zimbabwe. Ilionekana hakuna dalili zozote zile za mabadiliko. Wapo waliofikia hata kuifananisha nchi hiyo na Tanzania yetu ya miaka ile tete ya 'kujifunga mkanda'.

Nilipomuuliza Mzimbabwe mmoja aliyeikimbia nchi yake kwa nini kuondoka kwa Rais Mugabe madarakani kutakuwa mwarobaini wa matatizo yao, jibu lake lilikuwa fupi: "Kuondoka kwake kutaleta matumaini". Na hayo matumaini, akasisitiza, yanatosha kuikoa Zimbabwe maana ndiyo yatakayowafanya warudi kujenga nchi.

Kipindi hicho hicho nilibahatika kutazama filamu moja kuhusu harakati mapinduzi katika nchi moja katika mabara ya Amerika. Siku chache, kama siyo moja, kabla ya kuyafanikisha, kiongozi wa mapinduzi hayo aliuliwa. Waandishi wa habari wakabembelezwa waweke pembeni maadili yao ya kazi na kuzingatia hitaji kubwa kwa kumpige picha kana kwamba yupo hai ili wananchi wasipoteze matumaini yatakayofanya waweza kuleta mapinduzi kesho yake.

Leo nimeyakumbuka hayo yote hasa baada ya kusoma makala ya Jenerali Ulimwengu inayosema 'Tusipojifunza kutoka historia yetu hatutaweza kuona yajayo.' Katika makala hayo Jenerali anasema yafuatayo baada ya kueleza jinsi wananchi walivyo na "mfadhaiko mkubwa" kutoka na "zahma" nyingi tu walizo nazo: "Wananchi wanataraji kupata viongozi wa kuwaongoza kutoka katika hali hii, lakini hawawaoni. Mara kwa mara wanapewa matumaini hewa, na baada ya muda mfupi wanagundua kwamba wameghilibiwa."
Lakini wananchi, Jenerali anatukumbusha, "hawaachi na wala hawachoki kuwashabikia wanasiasa wengine kila anapojitokeza mwanasiasa mwingine akatamka maneno yanayoashiria uwezekano wa mabadiliko." Hivi ndivyo ilivyokuwa enzi za Mrema, Mtikila na hata Sokoine, anasisitiza. Nami nakubaliana naye hadi hapo.

Ila Jenerali anaenda mbali zaidi na kusema hivi: "Ndivyo ilivyo sasa na Edward Lowassa. Kwa sababu ambazo mimi binafsi sizielewi, watu wengi wanamuona Lowassa kama mkombozi fulani. Nasema sizielewi sababu zake kwa kuwa sijui ni nini Lowassa anaweza kufanya ili kubadilisha hali ya umaskini iwe ya neema, hali ya kukata tamaa iwe ya kujenga matumaini, hali ya udhaifu iwe ya ukakamavu na kujiamini." Kwa nini haelewi?

Yaani Jenerali haelewi kwamba wananchi siyo wajinga kiasi cha kudhani kwamba hakuna masiha/masihi atakayewaokoa na zahma? Haelewi kwamba ushabiki/unazi wa wananchi kwa wanasiasa - hasa wenye pesa - haumaanisha wanaamini kila wanachokiahidi? Hivi wananchi wetu ni mbumbumbu kiasi cha kuamini kila mmoja atapata nyumba, gari, lapitopu na kadhalika pale mwanasiasa fulani atakaposhinda uchaguzi? Au wananchi ni wajanja/werevu kiasi cha kutambua kwamba huu ni wakati wa walau kugawana utajiri ambao wanasiasa wameuchuma bure kwa posho na dili za 'siasa-biashara'?
Hivi wale waendesha bodaboda na bajaji wanaodai walilipiwa mafuta 'fulu tenki' na kupewa posho ya 'elfu kumi kumi' ili kwenda kwenye 'mafuriko' ya Lowassa jijini la Dar es Salaam wanaamini kabisa kwamba akishinda itakuwa rhuksa tu kuingia katikati ya jiji? Au kwao hii ni fursa adimu ya walau kupata 'kitu kidogo' ambayo wenzao wanayo kila wanapokuwa Bungeni Dodoma na kwenye mikutano ya Kamati za Bunge ambako 'wamehalalisha' posho n.k.?

Pamoja na hayo Jenerali anadai yeye amekuwa "mwanafunzi wa historia ya dunia kwa muda mrefu kidogo" na katika "kuidurusu historia" hajawahi "kuona mtu mmoja, na awe hodari kiasi gani, aliyeweza kubadilisha hali ya wananchi wake kwa uwezo wake peke yake." Hivyo basi, anahitimisha kuwa kutarajia "kwamba tunaweza kupata mabadiliko ya haraka kutokana na mtu mmoja ni aina fulani ya ushirikina ambayo" inamtisha kwa sababu alikwishakuibaini ingawa anadhani "kwamba watu wetu walio wengi, na jamii yetu kwa ujumla, hatuitambui." Sidhani.

Ndiyo, sidhani kama wananchi walio wengi hawaitambui. Pengine wasomi/wanazuoni na wateule/manaizi ndiyo hatutambui. Katika kutafuta mantiki - lojiki - katika kila kitu wafanyacho wananchi wenzetu hasa wale wanaowashabikia wanasiasa wakwasi pengine tunaishia kutotambua kwamba hakuna mantiki kuu zaidi ya ile ya 'hapendwi mtu ila pochi' au 'baniani mbaya kiatu chake dawa' ama 'jungu kuu halikosi ukoko' na heri 'moja shika si kumi nenda uje.'

Unapokuwa na chama tawala kibabe ambacho kimekukatisha sana tamaa miaka nenda rudi na vyama vya upinzani uchwara ambavyo havikupi matumaini, una nini cha kupoteza zaidi ya kutafuta faida ya haraka haraka vinaponyukana? Kama umepata fursa inayotokea tu kila baada ya miaka mitano ya kuugeuza msemo wa 'wapiganapo tembo nyasi huumia' kuwa 'wapiganapo panzi neema kwa kunguru', kwa nini usiitumie tu hiyo nafasi ya kuwa kunguru badala ya nyasi?
Mwanazuoni mmoja analihoji hilo kihivi: "Inasemwa hivi eti mtu huyu ni mchafu anatumia pesa kwani wao hawatumii??? Wanasema Mwalimu [Nyerere] hakumpenda kwani yupi alimpenda? Wanasema Mwalimu alisema hafai kwani kipi aliacha kinafaa?"

Nachelea kusema wananchi wanajua kwamba wako kwenye mtanziko wa kuchagua kati ya kuliwa na zimwi walijualo au kuogelea kwenye bahari pana yenye kina kirefu. Hivyo, kwa kuwa 'hakuna namna nyingine' sasa baadhi yao wameamua tu kujiunga - na kufaidika kwa hali na mali - na safari ya matumaini. Kwao chama tawala chenye kiburi ni kama Mugabe tu hivyo hawajali kikiondoka madarakani hata kama ni kwa matumaini hewa.

Asili huchukia ombwe.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP