Sunday, September 27, 2015

Kwa nini Wananchi Bado Wana Imani na CCM?


Ndugu Chambi na Wanazuoni Wengine, 

Naomba tujaribu kuwafafanulia wananchi sababu ya kisayansi ya tabia za binadamu ambazo zinawafanya wananchi wetu kuonyesha kuwa bado wana imani na CCM au Magufuli pamoja na ukweli kuwa kuna vigezo vingi ambavyo kwa hali ya kawaida inatakiwa waachane na CCM? Nimekuwa najaribu kujielimisha kwa kusoma majarida na vitabu kujua kwa nini wananchi katika miaka ya nyuma (tangu enzi za Mrema na NCCR Mageuzi) wamekuwa wanajitokeza kwa maelfu kwenye mikutano ya vyama vya upinzani, mara nyingi kuliko wanavyojitokeza kwenye mikutano ya chama tawala, lakini siku ya kupiga kura wanaendelea kukipigia kura chama kilichopo madarakani? Hali hii naona imetia fora mwaka 2015 ambapo maelefu wanajitokeza kwenye mikutano ya CCM na ile ya Ukawa na ACT-Wazalendo. 

Sasa tunaambiwa kama kura ingepigwa wiki ya kwanza ya Septemba mgombea Uraisi wa CCM angezoa asilimia 65 ya kura. Wengi wameshtuka kuona tofauti kubwa hivyo kati ya mgombea wa CCM na wa Ukawa. Nadhani kutoa maelezo ya kisayansi kutasaidia sana kuelewa kisa cha matokeo ya utafiti wa Twaweza, ambayo sina sababu ya kutilia mashaka kutokana na uadilifu wa Aidan Ayekuze, ingawa nami sikutegemea kuwe na pengo kubwa hivyo. 

Katika kuelewa kwa nini wapiga kura wanaonekana kuwa bado na imani na CCM au mgombea uraisi wa CCM, nimesoma na kugundua kuwa kuna dhana ya "mshikamano wa kiuanachama" ("club effect" or "bandwagon effect" (www.redstate.com)). Nimesoma pia "The Guradian" ya Uingereza (www.theguardian.com>science>general election2015>...) ambayo inaelezea dhana ya "Dunning-Kruger Effect" kwenye makala ya tarehe 2 April 2015 "Democracy v. Psychology: why people keep electing idiots" na dhana ya "Incumbency Effect" katika makala ya tarehe 6 Mei 2015. Katika kitabu cha K.Van de Straeten (2010) "The Mechanical and Psychological Effects of Electoral Processes..." na andiko la "factors that influence voters during presidential elections" (soma kwenye http://study.com/academy/lesson/factors-that-influence-voters..) vinaelezea jinsi hulka ya mpiga kura (umri, tabaka la kimapato, ushabiki wa chama, nk) inavyomfanya mpiga kura kuchagua chama kile kile hata kama kwa mtizamo wa kawaida ingefaa kipumzishwe. 

Nilivyoelewa katika kusoma majarida na vitabu hivi ni kuwa asilimia kubwa ya wadau wa chama cha siasa huendelea kuwa waaminifu (loyal) na kukilinda chama chao (ndiyo hiyo dhana za club effect) hata kama kinaonyesha mapungufu, wakitarajia kitajirekebisha huko mbele. Lakini wakati wa kampeni huungana na wapinzani kupiga kelele ya kukikosoa (ndio maana ya mafuriko kwenye mikutano yote) - ingawa mwisho wa siku watakipigia tena kura chama walichokizoea. Kwa hiyo kura ambazo huamua chama kushindwa ni zile za wasio na msimamo, ambao kufuatana na tafiti za USA ni kama asilimia 10-15 hivi (study.com/academy/lesson/..).

 Labda niweke mfano rahisi wa dhana hii ya 'club effect'. Kwenye imani za dini, ukizaliwa kwenye familia ya dhehebu fulani mara nyingi utaendelea kuwa muumini hata kama kuna maudhi ya ubadhirifu wa mapato au kiongozi wa dini kushikwa ugoni. Kwenye michezo, mimi nimekuwa shabiki wa Yanga na niliendelea kuiunga mkono hata ilipomeguka kuwa Yanga Raison na Yanga Kandambili, na hata tunapopata vipigo vya mfululizo na Simba Sports sijawahi kufikiria kuihama. 

Maana yake nini kwenye siasa?  CCM ina mtaji mkubwa wa wanachama ambao wamekulia na kulelewa humo, na hivyo wataendelea kuwa wanachama au mashabiki wake hata pale ambapo ni wazi kimeshindwa kutimiza ahadi za huko nyuma. Mbinu ambazo uongozi wa CCM imekuwa ikitumia ni kuwajengea matumaini wananchi wake kwa kuwaonyesha mafanikio (na ni dhahiri huwa hayakosekani: umeme vijijini, barabara, mashule, nk), kukiri mapungufu (kama kuonyesha kuna viongozi wachache mafisadi na wanashughulikiwa au wameshaenguliwa kwenye safu ya viongozi), na kutoa dira jinsi itakavyoshughulia kero zilizobakia. 

Kwa hiyo, kiongozi wa CCM anapoonekana anakiri mapungufu anakuwa "anatubu dhambi na kuomba msamaha" kwa niaba ya Chama chake. Wanachama wengi husamehe, hata kama kwa shingo upande, na kuendelea kukibeba chama chao, ingawa kuna wachache watakuwa wanapungua kila mwaka, na inakuwa siyo rahisi kupata wanachama wapya wenye mapenzi na chama chao kama wale waliojiunga enzi ambapo chama kilikuwa kinatawala vizuri. 

Ni kwa kutambua hilo ndiyo maana Katibu Mkuu wa CCM alipita nchi nzima kwa madhumuni ya kujaribu kurudisha imani kwa wale ambao wamekata tamaa. Jinsi CCM itakavyoshindwa kurejesha imani kwa wanachama wake na kuwapata wapya, ndivyo jinsi vyama vya upinzani vitakavyoendelea kupata wanachama wapya na hivyo kuizidi CCM mtaji wa wapiga kura. Kufuatana na maoni kwenye mitandao ya kijamii inaonekana wengi wanadhani kuwa mwaka huu upinzani imeshapata mtaji mkubwa wa wapiga kura kuliko CCM. Tunahitimisha hivyo kutokana na wingi wa watu kwenye mikutano ya Ukawa (ingawa tunasahau kuwa hata ACT-Wazalendo na CCM pia huvutia wananchi wengi na hufanya shamrashamra zinazolingana). 

Tukumbuke kuwa pia nadharia ya saikojia wa wapiga kura inatuasa na athari za "bandwagon effect" ambapo watu hufuata tu mkumbo kama vile fashion. Kwa maoni yangu ni kweli kabisa wananchi wote bila kujali chama wanataka mabadiliko. Ni kwa kutambua hilo ndiyo maana vyama vyote vinajinadi kwa kauli mbiu ya "mabadiliko". Kwa hiyo kinachosumbua kwenye akili na nyoyo za watu ni "nani tutamwamini kuongoza haya mabadiliko?"
Lakini pia tukumbuke CCM inanufaika na kile kinachoitwa "incumbency effect" ambapo chama au kiongozi aliyepo madarakani huwa tayari ana kura (asilimia 15-30) zisizoyumbishwa na kampeni. Hawa kwa lugha rahisi wanaamini katika "zimwi likujualo". Ukifuatilia nadharia ya tabia za wapiga kura ya "club effect na incumbency effect", tusishangae kama wapiga kura wengi wa CCM na mashabiki wao wakiamua kuwa wanaamini kuwa Mh.Magufuli (ndani ya CCM) ataweza kuleta hayo mabadiliko. 

Kwa mantiki hiyo si busara sana kukimbilia kwenye hitimisho kuwa matokeo ya utafiti yameghushiwa. Nahisi kama tungepata ripoti kamili ni dhahiri ufuasi mwingi ni kutoka vijijini, ambako kuna wapiga kura zaidi ya asilimia 70. Lakini pia, kama alivyodokeza [mchambuzi mmoja], maoni ya wapiga kura yanaweza kubadilika wiki mbili kabla ya uchaguzi na hivyo tukija kuona chati ya CCM imeshuka tusiwe na sababu ya kulalamika kuwa sio ya kweli maana inawezekana kabisa kuwa wanachama na mashabiki wa mgombea wa vyama vya upinzani (pamoja na wale waliomo CCM) wakawa wameongezeka kuwazidi wale wanaomuunga mkono mgombea wa CCM. 

Nasema hilo linawezekana kama wananchi wameamini kabisa kuwa ahadi za kusafisha tabia za kifisadi nchini haziwezi kufanikiwa chini ya uongozi wa CCM. Tukumbuke kuwa miongoni mwa mambo ambayo huyeyusha kabisa ule mshikanao na imani zinaotokana na "club au incumbency effect" ni rushwa na ufisadi uliopindukia. Ndiyo maana CCM nayo imekazania sana kwenye hiyo ajenda. Kufuatana na matokeo ya utafiti wa Twaweza inaelekea kuwa wengi wanaamini kuwa CCM/Magufuli atashughulikia kero hizo za ufisadi na rushwa.

Kwa kuhitimisha, naona kuwa kama utafiti wa Twaweza umefanyika kisayansi kweli basi uwezekano wa matokeo ya maoni kumpenda mgombea wa CCM kuteremka chini ya asilimia 55 ni mdogo sana. Hii ni kwa sababu, kufuatana na sayansi ya saikolojia ya wapiga kura, asilimia 90 ya wapiga kura huwa wanakuwa wameshaamua ni mgombea gani wanamtaka pindi tu kampeni zinapoanza (angalia somo kwenye http://study.com. somo la 5 na Ashley Dugger, dibaji ya 11). 

Nikiri kuwa mimi siyo mtaalamu wa sayansi ya siasa, hivyo nawaomba msahamaha kama nimekosea katika tafakari hii na kwa vyote vile nawakaribisha wataalamu watusaidie kutafakari zaidi ili tuweze kuelewa kwa nini tusione ajabu sana CCM ikiendelea kushinda hata kwenye uchaguzi huu. Naona ni muhimu kuelemishana kisayansi kwa vile kuna wengi ambao wanaamini kwa moyo mmoja kuwa haiwezekani kabisa CCM kushinda na ikishinda inakuwa imetumia "bao la mkono"! 

Mtizamo kama huo ni wa hatari maana unaweza kuashiria fujo na vurugu wananchi wanaounga mkono wataamini kuwa mgombea wao ndiye alistahili kushinda. Na huwezi kuwalaumu sana kwa kuamini hivyo maana mmoja wa viongozi wa juu wa Chama tawala alishatoa dokezo la "bao la mkono", kitu ambacho alistahili kuomba msamaha kwa umma. 

Aidha, viongozi wa CCM nao wana wajibu wa kuwaelemisha wanachama wao kuwa ushindi wa chama cha upinzani siyo mwisho wa CCM kwa kuzingatia kuwa maslahi ya NCHI na maamuzi ya wananchi wengi kupitia kura zao ndiyo yanapewa kipao mbele. Hakuna sababu kabisa kwenye hotuba za viongozi wa CCM au vyama vya upinzani kutabiri fujo. Inatakiwa wote waendelee kuhubiri "kura na amani" kama sehemu ya kujenga utamaduni wa demokrasia ya kweli katika nchi yetu. 

Nawasilisha: 

Ndugu H.Bohela Lunogelo, Mwanafunzi wa Political Economy.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP