Saturday, September 5, 2015

Mbali na Nyumbani

MAPITIO YA KITABU NILICHOKISOMA MWAKA 2015

Mpitiaji: Godfrey Eliseus Massay


Mwandishi: Adam Shafi Adam

Mchapishaji: Sasa Sema Publishers chapa ya Longhorn Publishers

Uchapishaji: 2013

Utangulizi

Mbali na Nyumbani ni tawasifu ya Adam Shafi Adam, mmoja wa waandishi mahiri wa kazi za fasihi kutoka Zanzibar. Maudhui yake hueleza maisha ugenini, jasira ya ujana, kiu ya kutafuta elimu na mikasa ya safari. Mwandishi anaeleza kwa utaalamu mkubwa misukosuko aliyoyapata katika safari iliyomchukua mwaka mmoja kuimaliza kutoka kwao Zanzibar hadi Kairo-Misri. Matukio yaliyoandikwa katika kitabu hiki ni yale ambayo yalitokea kati ya mwaka 1957 na 1961, kipindi ambacho nchi nyingi za Afrika zilikuwa chini ya ukoloni. Ni kipindi ambacho kulikuwa na harakati za kudai uhuru katika nchi hizi. Hata hivyo, hii si tawasifu ya kwanza kuandikwa na waandishi wa fasihi hapa nchini. Shaaban Robert aliwahi kuandika tawafisu ya Wasifu wa Siti Binti Saad na tawasifu yake ya Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Pamoja na tawasifu hii, Shafi ameandika riwaya nne ambazo ni; Haini, Kuli, Kasri ya Mwinyi Fuad na Vuta N’Kuvute. Ni mara yangu ya kwanza kusoma kitabu cha Shafi, lakini hii haitakuwa mara ya mwisho. Makala haya yanaeleza kwa ufupi yaliyomo katika tawasifu hii. 

Muundo na Maudhui

Mbali na Nyumbani imegawanyika katika sehemu Tatu. Japo sehemu hizi hazijawekwa bayana, ni dhahiri kuwa kitabu kina “Utangulizi”, Sura ya 1 hadi 44” na “Sherehe”. Katika Utangulizi mwandishi anamweleza msomaji kwa nini ameamua kuandika tawasifu yake, changamoto alizokumbana nazo wakati anaandika, utofauti uliopo kati ya tawasifu hii na riwaya zingine, na anawashukuru watu muhimu ambao walimsaidia katika safari yake- walio hai na waliotangulia mbele ya haki. Aidha, kwa sababu matukio aliliyoyaandika ni ya muda mrefu sana, mwandishi anawaomba radhi wote ambao ameshindwa kuwataja kwa sababu ya kushindwa kukumbuka majina yao. 

Sura ya 1 hadi 44 inaelezea matukio yote yaliyoteka katika safari ya Shafi. Kila sura ina kichwa cha habari. Sura mbili zina upekee na ni fotauti za sura zinginezo. Sura hizo ni sura ya 1 na sura ya 44. Katika sura ya 1 ya “naongea na watoto wangu”, mwandishi anasimulia tukio lililotokea tarehe 18 Oktoba 2001 ambalo liliifanya familia yake yote iwe nyumbani. Ilikuwa ni siku ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa mwanae wa tatu. Mwanae alikuwa anatimiza miaka 2. Mezani kulikuwa na picha ya mwandishi akiwa na umri wa miaka 21 wakati akiwa masomoni Ujerumani. Mwandishi akamwonyesha mwanae picha hiyo ambayo ilimfanya mwanae aiangalie kwa muda na kumwulize baba yake kwa nini afya yake ailikuwa dhoofu katika picha ile. Swali hilo ndilo lililomfanya mwandishi atoe ahadi kwa wanae ya kuwaandikia kitabu ambacho kitaelezea kwa kina maisha aliyoyapitia hadi kufanya aonekane hivyo katika picha ile. Katika sura ya 44 ya “tamati” mwandishi anajaribu kurejea baadhi ya matukio na wahusika ambao hakuhitimisha hekaya zao. Ni katika sura hii mwandishi anaeleza yaliyojiri zaidi ya miaka 40 tangu alipoimaliza safari yake, wahusika aliowapoteza na wale alioonana nao au kuzungumza nao baada ya kupotezana kwa zaidi ya miaka 40. Mwandishi anajihoji na kujijibu kwa nini aliamua kufanya safari ile kama namna ya kuihitimisha sura ya 44. 

Binafsi nilivutiwa sana na uandishi wa mwandishi hasa namna alivyotumia ndoto kuelezea matukio mbalimbali. Ndoto yake ya kwanza aliota akitokewa na binti aliyeonana naye jioni wakati alipomtembelea jirani yake ambaye alimkaribisha kwa chai. Kidosho huyo alimtokea katika ndoto na kumtaka waende mbali mahali watakapokuwa wao wawili tu. Ndoto ya pili aliota akiwa katika jumba la kifahari sana wakati kiuhalisia yeye alikuwa amelala nje pembeni mwa stesheni ya treni. Ndoto ya tatu aliota akiwa amezamia kwenye meli iliyokuwa ikienda Ulaya. Alikamatwa na mabaharia na kutupwa baharini ambako alijikuta yuko kwenye meno ya papa. Ni ndoto ya kwanza tu ndiyo niliyoijua kuwa ni ndoto wakati ninaanza kuisoma. Ndoto zingine nilizijua kuwa ni ndoto wakati ninamalizia kuzisoma na hivyo kunifanya nipigwe na butwaa na kuusifu uandishi wa mwandishi. 

Mwandishi alielezea matukio yote kwa ufundi unaomwezesha msomaji kuona picha halisi ya matukio yale. Uwezo wake wa kueleza kwa kina haiba ya wahusika, mandhari, na undani wa matukio ulinifanya nijione kama naangalia sinema nzuri ya kusisimua. Shafi aliweza kunifanya nicheke na kufurahi, nihuzunike na kulia, na kutamani kujua nini kitafuata baada ya kumaliza kusoma sura moja baada ya nyingine. 

Mbali na Nyumbani imesheheni matukio na visa vya kusikitisha sana. Kumwona mhusika mkuu akizuiwa kuingia Aden na Sudan, akiwekwa rumande mara mbili hata akaugua homa kali na kudhalilishwa utu wake kwa kuvuliwa nguo zote, kuishi kwa kutangatanga mtaani na kulala nje, kufanya kazi za shuruba, kuibiwa, kupata mafunzo ya kijeshi badala ya kusoma chuo kikuu, kurudi kwao Zanzibar na kushindwa kutumia mafunzo ya kijeshi kwani uhuru ulikuwa umekaribia kupatikana. Hata hivyo, ni kitabu kinachoonesha ujasiri wa hali ya juu wa mhusika mkuu, moyo wa kutokata tamaa, marafiki wa kweli na uhalisia wa maisha ya ujana. Katika matukio mawili mwandishi anatuonyesha uhalisia wa maisha ya kijana rijali aliyekumbwa na mikasa mingi lakini aliyeweza kupenda na kujiingiza kwenye mapenzi.

Sehemu ya mwisho ya kitabu ni “sherehe” ambayo inaeleza maana ya misamiati aliyoyatumia mwandishi. Nakiri kuwa Shafi ni mwandishi anayetumia maneno magumu ya Kiswahili. Mara nyingi ilinilazimu kutafuta kamusi ya Kiswahili ili kuelewa misamiati aliyoyatumia. Ni mwandishi anayepaswa kutunukiwa nishani ya kuchangia katika kuikuza lugha ya Kiswahili.

Mwisho

Tawasifu hii ni hadithi ya vijana wengi waliotafuta elimu ya vyuo vikuu ambayo ilikuwa haipatikani kwa urahisi kipindi cha ukoloni. Tunamwona Shafi akiwa na marafiki zake ambao wote walikuwa wakitafuta elimu na maisha mazuri mbali na nyumbani. Ni tawasifu ambayo inashawishi waandishi na watu maarufu kuandika tawasifu zao katika namna ambayo inakuza kazi ya fasihi andishi. Rai yangu kwa serikali ni kuhakikisha kuwa kitabu hiki kinakuwa cha lazima kwa wanafunzi wanaosoma fasihi ya Kiswahili hasa kidato cha tano na sita au vyuoni kwa sababu ya lugha yake ngumu. 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP