Thursday, September 24, 2015

Sayansi au Siasa ya Utafiti wa Twaweza?

Sayansi au Siasa ya Utafiti wa Twaweza?
Chambi Chachage

Kila tafiti ina sayansi na siasa zake. Sayansi huhusisha mbinu za kitakwimu na kiuchambuzi. Siasa huhusisha mbinu za kimaamuzi na kiusambazaji. Je, ni nini sayansi na siasa ya utafiti wa Twaweza kuhusu 'Sauti ya Wananchi' katika Uchaguzi ujao wa Oktoba 25, 2015 ambao umeibua mjadala mkali vijiweni, vyuoni na vyamani.

Maadam Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa anayeonekana kuwa  msemaji wake 'mpya', January Makamba, imetoa tamko linalodai wameshangazwa "na taharuki, hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati, kuhusu matokeo ya utafiti huu" ni vyema tukarejea dhana (tete na tata) ya sayansi na siasa za utafiti huo.

Nianze kwa kusema kwamba mimi ni muumini wa somo la Takwimu (Statistics) hasa pale linapozingatia viashiria (variables) mbali mbali na nadharia (theories) zinazokubalika kisayansi. Japo sikuwa mwanafunzi mahiri wa somo hilo nikiwa chuoni, lilinivutia sana hasa nadharia yake ijulikanayo kama Central Limit Theorem (CLT) ambayo ndiyo msingi mkuu wa tafiti za maoni (opinion polls). Pia kama afisa wa uchambuzi wa sera na tafiti, nilibahatika kuona kwa ukaribu jinsi taasisi ya HakiElimu ilivyokuwa inajaribu sana kushirikiana na taasisi kama REDET kuendeleza utamaduni huu wa tafiti hizi nchini enzi za Ukurugenzi wa Rakesh Rajani. 

Ikumbukwe Rakesh ndiye alikuwa Mkurugenzi mwanzilishi wa Twaweza kabla ya kumkabidhi mikoba Aidan Eyakuze. Usuli huu ni muhimu maana kabrasha ambalo ni msingi mkuu wa tafiti za Twaweza lilitolewa tarehe 14 mwezi wa Februari mwaka 2013 wakati wa Ukurugenzi wa Rakesh. Kabrasha hilo linajulikana kama Sauti za Wananchi: Collecting national data using mobile phones na limehifadhiwa katika faili lenye jina hili: SwZ Approach Paper.

Sasa kabla hatujalichambua kabrasha hilo hebu tujaribu kutoa tafsiri nyepesi ya CLT ambayo kwa Kiswahili tunaweza kuiita 'Nadharia ya Kiwango cha Wastani'. Kwa ufupi, tunaweza kusema nadharia hiii inasema kwamba kama ukichukua watu wachache, tuseme 2,000, kwa bahati nasibu kutoka katika jamii yenye watu wengi na wakakupa matokeo fulani - tuseme asilimia 70 wakasema wanapenda ugali na maharage  - basi ukirudia rudia bahati nasibu hiyo hata mara 100 kwa kuchukua watu wengine 2,000 katika jamii hiyo hiyo basi watakupa matokeo yanayofanana fanana na hayo. 

Hivyo, kwa maana nyingine, ni kwamba kadri unavyorudia ndivyo matokeo yanapojikita hapo kwenye Kiwango cha Wastani - Central Limit - ambapo kwenye huo mfano wetu tumesema ni asilimia 70 ya Watanzania wanaopenda ugali na maharage. Na kwa maana hiyo mtafiti hana haja ya kuchukua sampuli kubwa kwa ajili ya ukubwa tu ilhali kuna kujirudia huko. Kwa msingi wa kanuni hii tunaweza kusema kabisa kwamba Twaweza wako sahihi kuchukua sampuli ndogo ya 1,848 ambayo baadhi ya wapinzani wa utafiti wao - kama vile Malisa Godlisten - wanaiona ni ndogo sana na eti haiwakilishi wapiga kura milioni 24. Kama Twaweza wamezingatia sayansi yote inayohusiana na kanuni hiyo ya kitakwimu basi wako sahihi kabisa.

Tatizo langu binafsi na utafiti huu wa Twaweza ni kwamba, japo wametupa data zote, hawajatupa andiko mahususi na la kina la jinsi ambavyo wametumia mbinu/methodolojia yao kupata hizo data na hivyo kufikia kutoa tafsiri waliyoitoa katika utafiti huu wa mwaka 2015. Nimejaribu kuwauliza mara mbili mbili baadhi ya wahusika lakini wamenielekeza kwenye hilo kabrasha lao la mwaka 2013. 

Ukweli ni kwamba kabrasha hilo la mwaka 2013 linaelezea namna ambavyo mbinu/methodolojia inavyotumika lakini kamwe haliwezi kusema ni jinsi gani mbinu/methodolojia imetumika mwaka 2015. Ni sawa na kusema 'unatakiwa kufanya hivi' ila ili mtu mwingine ajue umefanya hivyo kweli inabidi umweleze kwa kina ni jinsi gani uliufanya utafiti wako - hatua kwa hatua, mwanzo hadi mwisho. 

Methodolojia/Mbinu ya Twaweza, kama ilivyobainishwa katika ukurasa wa 4 wa kabrasha la 2013, imejikita katika kutumia simu kufanya utafiti za kaya (household surveys) ili kupunguza gharama na muda pamoja na kuwezesha kupata taarifa/data kiurahisi katika zama hizi za kiteknolojia/tehama. Mbinu hii mahiri inazidi kupata umaarufu duniani kadri matumizi ya simu yanavyoongezeka katika nchi zinazoendelea. Kwa kuitumia Twaweza wanastahili pongezi.

Lakini kwa kuwa siyo kila mtu katika sampuli yao ya bahati nasibu (random sample) anakuwa na simu na ili kuhakikisha sampuli ni ya nasibu basi mwaka 2013 Twaweza iliona utatuzi wa changamoto hiyo ni kuwapa simu watu wote walio kwenye sampuli na vocha ya shilingi 1,000. Kuna wanaohoji kama kitendo hiki hakiathiri taarifa zilizokusanywa. Pia wapo wanaohoji kwamba kuitumia sampuli hiyo hiyo kwa muda mrefu hakuwafanyi watafitiwa wajenge mazoea fulani ya namna ya kujibu. Hapa tena kuna sayansi na siasa. Kama sayansi imezingatiwa - yaani watu hao kutopatiwa taarifa zozote za ziada ambazo zinaweza kuwafanya watoe majibu ya aina fulani - basi hakuna tatizo. Pia ni sawa tu kama ni kweli sampuli ya safari hii ni mpya kabisa. Ila kama kuna siasa basi tatizo ni kubwa hasa ukizingatia katika dunia ya utandawazi kuna mbinu za kutumia watu ujumbe kwenye simu/mtandao bila wao kutaka. 

Kwa mfano, mimi sikuandikisha anuani zangu mbili za barua pepe ziweze kupata matangazo/matamko ya CCM lakini nayapata tu na eti kama siyataki ninachopaswa kufanya ni kujitoa kwa kubonyeza tkitufe kidogo kwenye ujumbe huo. Tunajua pia kwamba kampuni mbalimbali, hasa za simu, zina uwezo wa kutuma ujumbe wa simu kwenye namba/simu zetu bila hata kuwaomba wafanye hivyo - kwa Kiingereza ujumbe wa aina hiyo unaitwa 'unsolicited message'. Je, tutajuaje kuwa mambo kama haya hayajatokea kama hakuna taarifa mahusisi ya jinsi utafiti wa mwaka 2015 ulivyofanyika kisayansi?

Cha kutia moyo ni kwamba mwaka huo 2013 Twaweza waliona kuna changamoto kubwa katika hilo la mwingiliano wa siasa na sayansi hivyo walitoa maelezo haya ya kiutatuzi katika ukurasa wa 23 ambayo nimejaribu kuyatafsiri hapo chini kwenye mabano: 

It was noted that once the community leaders identified that mobile phones were distributed they tried as much as possible to ensure that the selection goes to their favour. It is advised to inform them as well as to involve them in the random selection of participating households (Tuligundua kwamba viongozi wa jamii wanapotambua kwamba simu za mkononi zimesambazwa huwa wanajaribu kadri ya uwezo wao ili kuhakikisha kwamba uamuzi wa nani achaguliwe humo unafanyika kwa matakwa yao. Hivyo, inashauriwa kwamba wanapaswa kueleweshwa na kushirikishwa katika mchakato huo wa kuchagua sampuli ya kaya za kutafitiwa kwa bahati nasibu).

Ndiyo maana, kwa mfano, baadhi ya wasomi katika mtandao wa wazi wa Wanazuoni wanataka kuiona ripoti kamili ya utafiti wa Twaweza ili waweze kujua kwa kina jinsi utafiti ulivyofanyika safari hii maana hilo ndilo  litakalojibu maswali kama hayo kuhusu changamoto na mabadiliko yaliyojitokeza. Toleo lao fupi la kurasa 16 halimsaidii sana mtu kujua ni namna gani utafiti wao ulifanyika, changamoto gani mpya au za zamani zilitokea na zilidhibitwa vipi ili kuhakikisha utafiti haungii dosari. Na data siyo methodolojia, hivyo hazijielezi zilivyotokea. Kwa namna fulani toleo hilo fupi linaonekana limejikita tu katika mbinu hii ya usambazaji wa taarifa iliyoeelezwa katika ukurasa 21 wa hilo kabrasha la mwaka 2013:

Once the data has been quality checked and validated by Uwazi, they will use the information to prepare brief reports (2-4 pages), which will be put out for use by journalists, parliamentarians, decisions makers, researchers, and other interested parties (Mara tu taarifa zilizokusanywa zinapohakikiwa na kuthibitishwa na Uwazi, zinatumika kuandaa ripoti fupi (zenye kurasa 2 hadi 4) ambazo zitatumiwa na waandishi wa habari, wafanya maamuzi, watafiti na wengineo wanaozihitaji).

Alipoulizwa kuhusu hili kwenye mtandao wa wazi wa Wanazuoni, Profesa Kitila Mkumbo ambaye pia ni Mshauri wa chama kipya cha kisiasa cha ACT-Wazalendo na Mshauri Mtaalamu Mwandamizi (Senior Consultant) wa Twaweza katika kipindi hiki ambacho yuko likizo (Sabbatical) kutoka chuoni kwake pale DUCE/UDSM, alijibu hivi baada ya kutoa maelezo kwamba taarifa zinazojibu mengi ya maswali yanayoulizwa na taarifa zipo kwenye tovuti ya Twaweza: "Nadhani hawa bwana wanajitahidi sana kuwa wazi katika tafiti zao kwa kiwango cha kuweka hadharani hata raw data. Sijaona taasisi nyingine hapa nchini ikifanya hivyo."

Zitto Kabwe, ambaye naye amewahi kukiri (katika taarifa yake ya mali zake kwa umma) kuwa na mkataba wa kufanya kazi kama Mshauri Mtaalamu wa Twaweza kwa ujira wa dola elfu 2 kila mwezi kwa miezi 6, alitoa utetezi huu kuhusu taasisi hiyo japo matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa chama chao cha ACT-Wazalendo kimepata asilimia sifuri:"Our party believe in research and accept results whether positive to us or not. Our trust in @Twaweza_NiSisi work is unshakable" (Chama chetu kinaaminia tafiti na kinakubali matokeo ya utafiti, yawe hasi au chanya kwetu. Imani yetu kwa kazi ya @Twaweza_NiSisi haitetereki).

Lakini kwao ni rahisi sana kukubali utafiti huu kwa kutumia tu madai ya kisayansi na kisiasa kwamba ulifanyika kabla chama chao hakijamtangaza Anna Mghwira kuwa mgombea Urais na kuzindua kampeni. Hali inakuwa ngumu kwa vyama vinavyounda UKAWA ambavyo baadhi ya vijana wao, kama Malisa Godlisten, wanatoa sababu kama hiyo hapo juu ambayo haizingatii kiundani nafasi ya Nadharia ya Kiwango cha Wastani (CLT) katika tafiti za maoni.

CCM wao wanachekelea tu na kudiriki kuitaja hii ifuatayo kama moja ya sababu (kuu) tano zilizowafanya wasishangazwe na matokeo ya utafiti huo wa Twaweza: "Katika uchaguzi wa mwaka huu CCM tunafanya utafiti wetu wa ndani wa kisanyansi [sic] kila wiki kujua mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji nguvu mahsusi. Tangu tuanze utafiti wetu mwishoni mwa mwezi Agosti, karibu kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi kushuka chini ya asilimia 60 na zimekuwa zinapanda."

Pengine jambo lisiloshangaza ni kwamba hata CCM hawajatupa andiko la kina kuhusu methodolojia yao (labda) kwa kisingizio kuwa ni 'utatifi wao wa ndani'. Tamko lao awali lililotoka juma moja kabla ya utafiti wa Twaweza na kuwasilishwa na huyo huyo mtaalamu wao wa mitandao ya jamii, January Makamba, lilitupa tu dondoo kuhusu mbinu/methodolojia yao: "Utafiti wetu wa ndani, tulioufanya kwa kipindi cha siku kumi zilizopita katika majimbo 246 kati ya majimbo 269, unaonyesha kwamba Dr. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3. Tunaamini kwamba asilimia hizi zitaongezek[a] kadri Watanzania wengi zaidi wanavyopata fursa ya kumsikiliza Dr. Magufuli na kusikiliza Ilani na sera za CCM." 

La kushangaza ni kwamba katika tamko la sasa January Makamba anawashangaa wanatafakuri tunduizi na kusisitiza kwamba: "CCM ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini ili siku zijazo tujikite katika kurekebishana kwenye kanuni za utafiti na ithibati na uhakiki wa ubora. Tunasikitika kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa (atmosphere of intimidation) kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa nchini. Utafiti ni sayansi. Matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine, sio kwa kuponda tu au kwa matusi na vitisho. Ni vyema tukajifunza kupokea habari mbaya bila taharuki."

Nani alisema ili utafiti upingwe lazima utafiti mwingine ufanyike kwanza? Katika medani ya utafiti watafiti husisitiziwa kuweka wazi mbinu/methodolojia zao na jinsi walivyozitumia ili watafiti wenzao wachambue ni jinsi gani utafiti husika ulizingatia kile ambacho ulisema utakifanya. Na inapobidi watafiti wengine huenda kufanya utafiti kama huo kwa methodolojia hiyo hiyo ili kuona kama na wao watapata majibu hayo hayo. CCM hawajatupa methodolojia, wametoa tu matokeo. Twaweza hawajaeleza kwa uwazi kabisa jinsi ambavyo hiyo methodolojia yao ya mwaka 2013 imetekelezwa mwaka huu wa 2015 na kwa kiwango gani. Nilipomuuliza mtafiti wao mmoja nilichoambulia ni kujibiwa kwamba methodolojia ni ile ile tu. Hata kama ni ile ile, je, waliitumia vile vile kwa kiasi gani?

Hili la kutokuwa wawazi kuhusu jinsi matumizi ya methodolojia hiyo ndilo linalopelekea watu, wakiwamo wale ambao hata hawana mapenzi/mahaba na UKAWA, wahoji kuna nini nyuma ya pazia? Ndio maana sijashangazwa kuona mwananchi ambaye hamkubali kabisa mgombea Urais wa CHADEMA akisema maneno haya katika mtandao wa wazi wa Wanazuoni: "Miaka yote nimekuwa siamini kabisa hizi tafiti lakini kumbe kweli zinafanyika. Kimsingi Twaweza waliajiri kampuni moja ya kushauri kiuchumi ndiyo iliyoendesha utafiti huu tena kwa njia ya simu na Mke wangu alikuwa ni sehemu ya timu hiyo. Kweli ilifanyika mengine sijui, ila sample yenyewe ilikuwa na usumbufu wa kutisha." 

Sishangazwi kwa kuwa unapoacha kutoa taarifa muhimu kuhusu nani hasa alitafiti, kuchambua na kuandika taarifa ya utafiti unatoa mwanya wa kila mtu kuja na lake. Hakika nakubali kabisa katika masuala yenye joto kali la kisiasa ni vyema kuwalinda watafiti na wachambuzi kwa kuficha majina yao halisi kama nilivyodokezwa na mshauri mtaalamu mmojawapo wa Twaweza japo sina uhakika kwamba ni kweli huo ndiyo utaratibu duniani kote. Kama hilo la majina haliwezekani basi angalau hilo la methodolojia lifanyike.

Vinginevyo sayansi ya utafiti itaingiliwa sana na siasa za uchaguzi.

1 comments:

Baba Tegemea September 24, 2015 at 9:47 PM  

Asante sana ndugu Chachage kwa uchambuzi huu. Binafsi nimefuatilia maelezo ya Twaweza kwenye mtandao wao hasa lile andiko lao la methodolojia. Ni kama vile utafiti huo wa uchaguzi -- pamoja na tafiti zingine za Sauti za Wananchi -- ulitumia sampuli ile ile ya mwaka 2013. Najiuliza kama ni watu hao hao wamekuwa wakishiriki katika matoleo mbalimbali ya Sauti za Wananchi kwa kupigiwa simu --walau kila mwezi-- Je ni lini sampuli hiyo inapoacha kuwa ya nasibu na kuwa kundi la washiriki kwenye mradi wa Twaweza, na ukizingatia wameendelea kupokea vocha za simu n.k?

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP