Wednesday, September 30, 2015

Tujikumbushe: Jinsi ya Kuhadaa kwa Takwimu

JINSI YA KUHADAA KWA TAKWIMU: UTALII NA UKUAJI UCHUMI TANZANIA

Profesa. Chachage Seithy L. Chachage

22 Oktoba 2005

Napenda kukiri wazi kuwa wengi wetu si wataalamu wa uchumi, na wala hatuna utalaamu wala ujuzi walionao wa kuyaanisha masuala hayo. Lakini kwa kuwa kila kuchapo sisi sote ni waathirika wa takwimu zitolewazo na wachumi, na hasa wanasiasa wetu katika kipindi hiki wakati kura zikitafutwa kwa udi na uvumba, yabidi kuyasaili baadhi ya mambo ambayo wanatuambia. 

Swali ambalo wengi tumekuwa tunajiuliza ni: hivi tunapoambiwa kuwa uchumi umekuwa ukikua kwa kutumia vigezo vya pato la taifa, mbona ufukara umekuwa ukiongezeka siku hadi siku miongoni mwa makabwela ambao ni asilimia 90 ya watu wa nchi hii? Huo uchumi ambao umekuwa ukiongezeka umekuwa ukienda wapi au ukimfaidisha nani? 

Je, hizi ahadi za kujenga uchumi kakamavu ambazo wanaopigania kinyang’anyiro cha kututawala katika miaka mitano ijayo zinazingatia kiasi gani matatizo ambayo yamekuwa yakiwapata wanyonge?

 Si masuala mepesi, lakini inabidi tuyatafakari kwa faida yetu.

            Waziri Mkuu wa Uingereza wa mwishoni mwa karne ya 19, Bwana Disraeli aliwahi kutamka kuwa kuna aina tatu ya uongo: uongo, uongo laanifu na takwimu. Kama tutakubaliana na mwanasiasa huyu, basi takwimu ambazo zimekuwa zikitangazwa kuhusu baadhi ya sekta za uchumi ni kidhihirisho cha maneno haya. Mfano wa sekta mojawapo ni ile ya utalii. 

Kwa miaka kadhaa sasa Watanzania na watu wa dunia nzima wamekuwa wakiambiwa na vyombo vya habari  kuwa kutokana na kulegeza masharti ya uchumi na kuingia katika mfumo wa soko huria (utandawazi), kumekuwa na ongezeko kubwa la vitega uchumi katika sekta ya utalii kutokana na kuuza mashirika na makampuni ya kitalii yaliyokuwepo, kuyakodisha na uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya nchi.

            Hakuna ubishi kuhusu kuongezeka kwa vitega uchumi, kama inavyojidhihirisha wazi kutokana na ongezeko la mahoteli na shughuli zingine ambazo zinahusiana  na mambo ya kitalii. Vyombo vya habari vimekuwa vikiyaainisha yale ambayo yamekuwa yakitamkwa na wanasiasa, watawala serikalini, watunga sera na hata baadhi ya wasomi ambao wamefanya utafiti katika nyanja hiyo. Hawa wote wamekuwa wakionyesha jinsi sekta ya utalii inavyochangia katika pato la taifa, ongezeko la ajira, “kupunguza umasikini” na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa mfano ilidaiwa kwamba utalii uliingiza kiasi cha dola milioni 725 kutokana na nchi kupata watalii 525,122 mwaka 2001, na pato hili likaongezeka hadi dola milioni 731 kutokana na kupata watalii 576,000 mwaka 2003. Imedaiwa kwamba sekta ya utalii imekuwa ikiiingizia nchi fedha nyingi za kigeni—asilimia 25, na kuchangia katika pato la taifa kiasi cha asilimia 16. Kutokana na mchango huo, utalii umefikia kiasi cha kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa nchi. 

Kwa wale ambao wamewahi kuziangalia takwimu za nchi ya jirani—Kenya, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikivuma kwa miaka mingi na kuongoza katika shughuli za utalii  Afrika Mashariki nzima, watagundua mara moja kwamba takwimu hizi zina mushkeli! Kenya ilitembelewa na watalii 750,000 mwaka 2002. Hawa ni zaidi ya wale waliotembelea Tanzania. Lakini mapato ya fedha za kigeni kutokana na idadi hiyo yalikuwa dola milioni 285!

Iweje kwamba Kenya iliyopata watalii wengi zaidi ipate theluthi moja ya fedha za kigeni ya zile ambazo Tanzania ambayo ilikuwa na watalii wachache? Miujiza gani hii ya kiuchumi na ni baraka gani ambazo Tanzania inazo mabazo Kenya haina? 

Kila aliyemdadisi inabidi ajiulize maswali zaidi kuhusu mchango wa sekta hii: inabidi aziangalie upya takwimu za sekta hii na kulinganisha na mchango wa sekta zingine za uchumi hapa nchini. Kwa kufanya hivyo, itagundulika wazi kwamba hizi takwimu ni sehemu ya siasa za kimataifa za ulipaji na upunguziwaji wa kulipa madeni. Inabidi nchi zetu ziuonyeshe ulimwengu kwamba uchumi unakua kutokana na kufuata sera za magharibi na kukaribisha wawekezaji, ili zisamehewe madeni. Kuonyesha kuwa kuna matatizo ni kufru katika muktadha wa sera za kiuchumi za dunia ya leo.

Kama ni kweli kwamba sekta ya utalii iliiingizia nchi dola milioni 731 mwaka 2003, ambazo ni asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni, inamaanisha kwamba mapato ya fedha za kigeni mwaka huo yalikuwa dola milioni 2,924 (au bilioni 2.9 kwa kifupi). Lakini takwimu za hali ya uchumi wa taifa za mwaka huo zinaonyesha tofauti: mapato ya fedha za kigeni mwaka huo yalikuwa dola milioni 1,142 (au dola bilioni 1.1 kwa kifupi)! 

Hizo takwimu za serikali za hali ya uchumi kwa mwaka huo zinaonyesha kuwa mauzo ya mazao ya kilimo (kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku, karafuu na korosho) yalichangia dola milioni 222.7 au asilimia 19.5. Kadhalika, mauzo ya bidhaa zingine (madini, bidhaa za viwandani, samaki na mazao ya baharini (marine products), maua na mboga na utalii) yalichangia dola milioni 919.7 au asilimia 80.5 ya mauzo yote ya nje.

Katika hizi dola milioni 919.7, sekta ya madini peke yake ilichangia dola milioni 548.3 au asilimia 48 ya mauzo yote ya nje. Dhahabu peke yake ilichangia dola milioni 499 au asilimia 43.7 ya mapato yote. Bidhaa za viwandani zilichangia dola milioni 99.9 au asilimia 8.8 na mauzo ya samaki na mazao megine ya baharini yalichangia dola milioni 136.2 au asilimia 12. Uuzaji wa maua na mboga ulichangia dola milioni 13.7 au asilimia 1.2 za mauzo yote ya nje. Katika hizi ripoti za hali ya uchumi wa taifa, hakuna takwimu za utalii na mchango wake katika upatikanaji wa fedha za kigeni haujaanishwa hata kidogo! 

Ikumbukwe kuwa sekta ya utalii iko chini ya Wizara ya Mali Asili na Utalii na takwimu za mauzo ya samaki zimeanishwa wazi, lakini si za utalii. Na takwimu za hali ya uchumi wa taifa ndizo zitumikazo katika upangaji wa mipango ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kupanga bajeti ambayo ni sehemu ya maamuzi ya kupanga kama sekta ipi ipewe kipaumbele au ipi ni muhimu.

Hadi kufikia hapo, yabidi tujiulize kama kweli utalii unachangia hicho kiasi kinachodaiwa na wanasiasa wetu. Cha kwanza kinachojitokeza wazi ni kwamba hizo takwimu za watalii na mchango halisi wa sekta hii katika uchumi ni za kubunia, na zinaficha mambo mengi sana, ikiwa ni pamoja na unyonywaji na ufukarishwaji wa nchi na watu wake. Fedha nyingi zinatumika kuutangaza utalii na vivutio vyake; na inadaiwa kuwa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka. 

Lakini kihalisia watalii ambao wamekuwa wakija nchini kwa ajili ya vivutio hivyo si wengi kwa kiasi kinachodaiwa, kwani, kwa mfano, Tourism Master Plan inaonyesha kuwa kati ya watalii 502,000  wanaodaiwa kuingia nchini mwaka 2000, wale waliokuja kwa ajili ya mapumziko au kutembelea vivutio hawafiki hata nusu. Asilimia 25 ya hao wanaodaiwa kuwa ni watalii walikuwa wafanyabiashara, asilimia 12 ni watu waliokuja kutembelea ndugu zao au marafiki, asilimia 12 walikuja kuhudhuria mikutano na makongamano na waliobakia ni watu walikuja kwa shughuli zao wenyewe.

Waafrika, ikiwa ni pamoja na Watanzania walioko nje walikuwa asilimia 40.5 ya wageni waliotembelea nchi, Wazungu walikuwa asilimia 30 na Wamarekani walikuwa asilimia 9. Idadi halisi ya watalii waliotoka Ulaya ilikuwa 118,000 na wale waliotoka Marekani ya Kaskazini ilikuwa 31,000. Mamlaka ya hifadhi za wanyama Tanzania (TANAPA) inaonyesha kuwa idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama mwaka 2001 haikuzidi 120,000 nayo ilipata kiasi cha dola 19,791,765. Kadhalika inakadiriwa kuwa mamlaka ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) ilipata dola milioni 7, na ile ya Ngorongoro ilipata dola milioni 6.79. Mapato kutokana na uwindaji wa wanyama pori wa kitalii yalikuwa dola 9,021,960. 

Hii inamaanisha kwamba Tanzania, kihalisia ilipata dola milioni 42.6 tu kutokana na utalii!

Hili linawezekana kuwa kweli kabisa, kwani hotuba zote za bajeti za Waziri wa Maliasili na Utalii, katika nyongeza zake zinaonyesha kwamba chanzo cha takwimu zake ni Idara ya Takwimu ya Taifa na si Wizara yenyewe! Lakini takwimu za mauzo ya samaki na mali asili zingine chanzo chake ni wizara yenyewe. Iweje Wizara husika isiwe chanzo cha takwimu, badala yake zitoke kwenye idara ya takwimu? 

Ni kwa sababu Wizara haina njia ya kupata takwimu za sekta hii: huu ndiyo ukweli. Na kitu ambacho Idara ya Takwimu inafanya ili kupata makadirio haya ya mchango wa sekta ya utalii ni kuchukua hesabu ya wageni wote wajao nchini, pamoja na ile ya wale ambao si watalii, ikajumlisha na hela zilizobadilishwa katika mabenki na maduka ya kubadilisha fedha ambazo watu wanaletewa na ndugu au marafiki zao au zile za “wataalamu” wa kutoka nje waliopo nchini na ndipo inapokadiriwa kuwa nchi imepata dola milioni 750 na kwamba utalii una mchango mkubwa katika uchumi wa taifa!


Kwa mfano, wageni walioingia nchini mwaka 2003 walikuwa 576,000, na mahesabu ya kukadiria ya Idara ya Takwimu yanadai kwamba mmapato ya wastani ya mahoteli kwa siku ambazo mtalii mmjoja alikaa nchini yalikuwa ni dola 1,169 (au dola 173 kwa siku). Kwa hiyo, kwa makadidirio hayo, mahoteli yalipata dola milioni 673. Hivyo basi, hizo zilizoongezeka zaidi ya hapo (dola milioni 58) yawezekana kuwa zilikuwa zile za kununulia vinyago, za kunywea kwenye mabaa, kula kwenye migahawa, n.k. 

Hiyo ndiyo njia pekee ya kufanya makadirio ya mchango wa utalii, kwani, tofauti na bidhaa zingine ambazo huuzwa nje ya nchi, utalii ni bidhaa ambayo haipelekwi nje. Kwa hiyo basi, kuna uwezekano mkubwa kabisa kuwa mapato halisi ambayo nchi inayapata na kiasi halisi cha mapato ya biashara ya utalii ni tofauti kabisa.

Lakini makadirio haya hayasemi ukweli wa mambo, kwani watalii hulipia gharama zote za safari zao, ikiwa ni pamoja na zile za vinywaji, huko huko nchini kwao wanakotoka. Hivyo basi, pesa kidogo wanazokuja nazo nchini ni zile za kununulia vinyago tu.

 Kadhalika, makampuni mengi ni ya kigeni na hivyo ni hela kidogo sana ambazo zinabakia nchini kwa ajili ya kulipia gharama za uendeshaji, kuwalipa wafanyakazi wa Kitanzania mishahara ya kitumwa kutoka na ajira za msimu, n.k. Kadhalika, sehemu kubwa ya vinywaji na baadhi ya mahitaji ya mahoteli na makampuni haya yanaagizwa kutoka nchi za nje. 

Utalii ni sekta ambayo imehodhiwa na makampuni ya Magharibi, na makampuni madogo yaliyopo nchini ambayo yanadaiwa kuwa ni ya “wazalendo”, kazi yake kubwa ni udalali.  

Sehemu kubwa ya mapato yatokanayo na sekta hii yanabakia nchi za nje na nchi haifadiki kiasi kinachodaiwa kutokana na biashara hiyo. Ikumbukwe kwamba, katika dunia hii, utalii ni biashara inayoshikilia nambari mbili duniani baada ya ile ya mafuta na makampuni makubwa kama vile TUI (Ulaya, zamani likiitwa Thomson), JTB na Kinki Nippon Tourist  Agency (Japan), American Express, Transat A.T. Inc, Thomas Cook, Abercrombie, Fitch, First Choice na My Travel, ndiyo yanayotalawala na kuhodhi biashara yote.

Ni kwa sababu hiyo, Mashirika ya Biashara ya Dunia kama vile WTO yamekuwa yakijishughulisha sana na uwekaji wa masharti ya kunufaisha makampuni ya nchi za magharibi katika sekta ya utalii. Imefikia hatua ambapo hata mabenki na taasisi za fedha za dunia, ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Goldman Sachs au hata Meril Lynch na mengine kama makampuni ya kidunia—Gulf and Western au Castle and Cook, yanachukua maeneo makubwa ya ardhi duniani na kuyageuza kuwa vivutio vya utalii. 


Katika nchi kadhaa, vivutio na hata hizo mbuga za wanyama zimebinafsishwa. Katika nchi zetu, wafugaji, wavuvi na wakulima wanaondolewa katika maeneo yao kwa nguvu ili yatumike na wawekezezaji. Wale walio katika maeneo yanayozunguka vivutio au ya uwindaji wanaishia kufanyiwa viini macho vya kujengewa madarasa au zahanati au kupewa madawati ya shule. 

Na huku ndiko kunaitwa kupunguza umaskini, baaada ya kufukarishwa kutokana na kunyang’anywa maeneo yao au kuzuiwa kufanya shughuli zao.

Unyonyaji mkubwa uliomo katika sekta ya utalii ndio unaopelekea kutoa takwimu ambazo hazitoi hali halisi. Na ni takwimu hizo hizo ambazo zinapelekea nchi zetu kuwekeza fedha nyingi za kodi katika ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya kuijenga sekta hiyo, kiasi cha kutusahaulisha kuwa muhimu kwa nchi kama za kwetu na msingi wa maendeleo ya kweli ni uwekezaji katika sekta ya kilimo, viwanda, madini, elimu, afya na huduma zingingine za kijamii na kiuchumi kwa ujumla. 

Kibaya kuliko vyote ni ukweli kwamba ukuaji wa sekta hii unaambatana na udhalilishaji wa wananchi, kwa kutumia raslimali zinazozalishwa na sekta zingine ambazo ni muhimu kwa maisha ya wananchi.

Kadhalika, kwa visingizio vya kuendeleza utalii wa kitamaduni na kimazingira (cultural tourism na eco-tourism), kwa madai kuwa ni njia mojawapo ya kupunguza umaskini, inabidi Wasonjo, Wamasai, Wazaramo waonyeshwe mbele ya watalii katika hali yao ya udhalili, kwani watalii wanataka kuona Waafrika katika mazingira yao ya “asili”. Hata umasikini unakuwa ni kivutio kwa wawekezaji. 

Haya ndiyo yanayodhihirishwa na matangazo yanayoitangaza sekta ya utalii ambayo yamegubikwa na ubaguzi wa rangi, udhalilishaji wa kijinsia na hata kuutukuza ukoloni kwa kutumia majina kama ya akina Livingstone, Speke, Rebman, Selous, n.k. katika matangazo ya vivutio vya nchi.


Inabidi tutafakari na kujiuliza mengi!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP