Tuesday, September 29, 2015

Vyoo Vyuoni


Kapongola:

Ni kwanini hali ya vyoo (vingi) vilivyoko katika vyuo vikuu Tanzania si nzuri na vingi havina tofauti sana na vyoo vya sokoni, stendi za mabasi au baa za pombe (ambavyo vimekithiri kwa uchafu)? Pengine majibu ya swali hili yatatupa fursa ya kutoka kwenye kulalamika na kuanza kufanyia kazi vitu vidogo ambavyo havihitaji sayansi ya kurusha ndege. 

Chambi:

Labda nijibu kwa uzoefu wangu mdogo sana wa kuviona vyoo vya UDSM. Usafishaji wa vyoo kwa sasa Chuoni naona unaendeshwa na 'kampuni' ambayo (nahisi) imekodishwa na Chuo (Dakta Nandera saidia hapa). Ila vyoo vyenyewe ni vichache sana japo wanafunzi wameongozeka na havijaboreshwa kwa muda mrefu hasa ukizingatia vilijengwa zamani sana kukidhi mahitaji ya wanafunzi wachache wa enzi hizo. Naongelea maeneo ya pale Kampasi ya UDSM Mlimani.

Kitu kingine nilichogundua ni kwamba wahadhiri wao wana funguo kwa ajili ya vyoo vya wahadhiri/'mastafu' ambavyo vyenyewe vina afadhali tofauti na hivyo vya wanafunzi ambavyo mtu yoyote anaweza kuingia. Nadhani hili la ufunguo linasaidia walau kufanya usafi uwe bora zaidi. Pia kuna suala uhaba wa maji ambalo nalo linahitaji kutatuliwa kivyake.

Suluhisho ni la 'kimenejimenti', yaani, Chuo kuamua kujenga vyoo vingi zaidi kukidhi wingi wa wanafunzi na pia ni la kiuwanaharakati, yaani, wanafunzi wenyewe walipe suala la vyoo kipaumbele kama wanavyolipa lile la kupata 'bumu.'

Nadhani hoja hizo hapo juu pia zinahusu mabweni ya wanafunzi ambayo hayakujengwa kwa ajili ya wengi 'kubebana'.

Adolfo:

The toilets in question were built when there were about 600 students Ditto all around the campus !! Yes it is disgusting !! Who should be clamouring for change ??? .... Start with the Director of Estates .....

Begging is beginning to be part of the national ethos ..... parents begging the Government and the Donor Partners to dig pit latrines ... what does it take to build a VIP?

Kassala:

Watu wa Quality Assurance Unit/Department wanasemaje? Uwiano unapaswa kuwa choo kimoja kwa watuamiaji wangapi? Labda Tanzania Bureau of Standards wanaweza kusaidia!

Kamala:
.
Vyuo visivyo na uwiano mzuri wa vyoo vifungwe mara moja


Kapongola:

Kamala umenifurahisha sana. Umenikumbusha yule headmaster aliyefunga shule kwa kukosa chakula. Serikali ilikuja juu na kudai kwamba hakuwa na mamlaka ya kufunga shule. Sasa hii amri ya kufunga vyuo kwa kukosa vyoo itatoka kwa nani?

Kamala:

It sounds crazy kwa sababu vyuo vinavyolalamikiwa ni vya serikali. Si unajua serikali yetu huwa iko makini sana kwa taasisi zisizokuwa zake ila za kwake kila kitu hovyo.

Kwa mfano kuna speed limit barabarani na Matrafiki wako Imara, Gari lenye STK/J likikupita speed unalifukuza hulioni, linapeta kwa matrafiki then wewe unaandikiwa faini kwa kuzidisha speed kama kumi hivi n.k n.k sasa najiuliza ni mbabe gani kwa mfano atakayefungua kinywa chake na kusema UDSM ifungwe, Mukandala achunguzwe na uchunguzi ufanyike akiwa "ndani"?

Vicensia:

Kuna tatizo la kitaifa la matumizi ya vyoo nchini Tanzania. Lazima tukubali wengi wetu tumekuja kuona vyoo vya kizungu na kiasia tukiwa na uzoefiu wa vyoo vya jembe na vya shimo. Ndio maana ukitembelea vyoo vingi utagunda vyoo vya kukaa watu wanapanda na kuchuchumaa juu kama wako porini.

Uhalifu huu wa matumizi ya vyoo unatisha zaidi katika maeneo ya vyuo vikuu kwa sababu huko ndio wanakusanyika wazoefu wa vyoo vya jembe, wa ndoo, wa barabarani na vyoo vya kiasia na vya kizungu.

Ukosefu wa maji ni tatizo ila nimeshuhudia watanzania sisi hata tukiingia hoteli za nyota 5 chooni tunapanda juu au kukojoa chini. Mbaya zaidi Shirika la Ndege la Afrika Kusini katika moja ya safari zake walitangaza na kuhamasisha watu wawe wastaarabu katika kutumia vyoo vilivyoko kwenye ndege. Nilihisi ni ubaguzi kwani kwenye safari nyingine ambazo si za kutoka Dar au kurudi Dar huwa hawatoi tangazo. Ila nilipenda kwa upande mwingine maana tulipewa za uso.

Tunahitaji mkakati wa kitaifa wa kutatua tatizo la uchafu wa vyoo ili tusaidie kupunguza matumizi ya hela zinazotumika kutibu magonjwa ya vyoo ambayo mengi yanaepukika.

Naomba nipate watu wachache tushirikiane katika kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi bora na sahihi ya vyoo.

Bituro:

Suala la vyoo kwa kweli ni tatizo, licha ya kuwepo na kampuni za usafi nadhani usimamizi wa karibu wa uongozi ili kuhakikisha kwamba vyoo vinakuwa safi ni mdogo na hii nadhani husababishwa na hali ya kuona kama kiongozi akishupalia masuala ya vyoo ataonekana kashuka cheo au kudharauliwa hivi kitu ambacho siyo kweli kwa hivyo watu wa usafi wa makampuni husika hutumia fursa hiyo kutofanya kazi yao vizuri na matokeo yake ni hali mbaya ya harufu kali n.k mfano choo cha maktaba ya UDSM wakati mwingine huwa ni balaa harufu mbaya, kali ambayo huwa inahisiwa hadi ofisi ya UDSM GENDER CENTRE hivyo kuwa kero kubwa lakini cha ajabu utaona watu wapo kimya tu atakayejitahidi sana atasema tu du! leo choo kinatema ile mbaya sasa sijui hapo kasaidia kutatua tatizo au kakisifia tu kwamba siku hiyo kimefanya vizuri zaidi kwa kutoa harufu mbaya.

Suala lingine ni watumiaji wa vyoo hivyo wenyewe kwani wengi wao hususani wanafunzi wamekuwa wakitumia vyoo hivyo vibaya mfano mtu akikuta chooni hakuna maji atajisafishia makaratasi au vitu vigumu ambavyo huwa ni tatizo la kusababisha mifumo ya maji kuziba na kwenye vyoo vya vyuo vingi hususani UDSM pia ndiyo utakuta watu wameandika majina yao ukutani, wamechora picha n.k kitu ambacho pia ni uchafu maana yake siyo mahali pake.

Kazi bado ipo mimi nashauri elimu izidi kutolewa hususani kwa wanafunzi, namna ya kutumia vyoo ili kuwaepusha na magonjwa kama UTI n.k lakini kikubwa kwa UDSM ni muhimu vyoo vingine vipya vijengwe ili kuendana na wingi wa wanafunzi na wafanyakazi waliopo kwa sasa.

Mgune:

Binafsi naona tatizo ni moja tu: MENTALITY. Tukiweza kubadili mentality zetu, hiyo itakuwa hatua ya kwanza ya mabadiliko.

Nakumbuka enzi zetu pale UDSM mtu ulikuwa ukiingia maktaba kutafuta kitabu fulani, yes, mara nyingine utakipata, lakini utakuta karatasi kadhaa ZIMECHANWA. Ubinafsi at its best!

Mitaro ya kupitisha majitaka unakuta hata kama imejengwa "vizuri," haifanyi kazi iliyokusudiwa kutokana na kujaa takataka zilizotupwa humo kwa makusudi, au pengine nyingine zimetupwamo kutokana na kutokuwa na mahali sahihi pa kuzitupa. Nchini Japan, mathalan, suala la usafi na kutupa takataka linaanza kufundishwa nursery schools. Watoto hao wanafundishwa namna ya kutenganisha takataka (plastics, burnables, etc) na wanadeki vyoo wao wenyewe - I was so surprised! Na yote hayo yanakuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Jambo kubwa nililojifunza kutoka kwa wajapani ni kuweka maslahi ya umma kwanza kisha ndio maslahi binafsi yanafuata.

Jana nilibahatika kuingia kwenye maktaba moja ya ughaibuni - hakyamama sina maneno ya kuelezea! We will have a long way to go with our current mentality.

Hitimisho langu ni kwamba mambo yooooooote hayo ili yaweze kutekelezwa kwa usahihi wake it begins with our mentality change!

Kisinda:

Kwa kiasi kikubwa suala hili limenigusa kwa kuwa nimekuwa nikikereka nalo. Suala la Afya ya Jamii (Public Health) na mabadiliko ya kimtazamo (mentality changes) yanajikita kwa sehemu kubwa kwenye ELIMU, ELIMU, ELIMU.

Elimu ninayoongelea si ile ya darasani pekee kwa kuwa kama ingelikuwa hivyo basi tusingelitegemea kukuta vyoo vya kitovu cha elimu nchi hii, a.k.a Mlimani vina tatizo. Tusingelikuta hata vyoo vya baadhi ya ofisi za umma vikiwa na tatizo la usafi. Hivyo ni vizuri kuwa na elimu kwa upana wake na kama haki ya msingi basi iwafikie wote.


Pia kuna suala la malezi na makuzi. Ni aibu na fedheha kwa jamii kama yetu kuwa na magonjwa kama kipindupindu ambayo chanzo chake kikubwa ni uchafu ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya choo. Ulimwengu uliostaarabika katika karne ya 21, milennia ya 3 bado inasumbuliwa na magonjwa ambayo kwa kiwango cha maendeleo hayakupaswa kuwepo.

Nimependa jinsi Dr. Vicensia Shule alivyojiongeza na kwenda hatua moja mbele ya kufanya kitu. Nitakuwa tayari kushiriki katika kikosi kazi kwa kadiri muda utakavyoruhusu.

Hilo nalo tunahitaji mfadhili?

Bhuki:

Pamoja na kukubaliana na wewe [Vicensia] juu ya ustaarabu katika matumizi ya vyoo, ila nina mtazamo tofauti katika haya uliyoyasema hap[o] [juu].

Mimi naangalia hiyo tabia kwa mtazamo wa kiafya. Kwa vyoo vya umma [ambavyo hutumiwa na watu wengi] kama usafi ni wa mashaka, hakika kupanda juu ya choo cha kukaa ni bora zaidi kiafya kuliko kukikalia choo cha namna hiyo. Kuliko kukaa na kujipatia magonjwa ya ngozi na mengineyo ya kiafya, ni heri upande na kuchuchumaa kwa juu aisee. Yaani nikae kwenye choo ambacho watu hukojoa hovyo na kuchafua sehemu ya kukalia?

 Tena vingine unakuta hadi masalia ya kinyesi, halafu mtu ufike na kukalia choo cha namna hiyo kwa sababu unazingatia ustaarabu katika matumizi ya choo cha kukaa?! Hili laweza kuwa ni njia mojawapo ya kuishi kutokana na mazingira halisi ya vyoo vya umma, haswa pale UDSM-Mlimani.

Masuluhisho ya kujenga vyoo vipya vingi, uwepo wa maji ya uhakika na elimu ya matumizi ya kistaarabu ya vyoo vya umma ndiyo ya muda mrefu. Ila kutokana na mazingira yetu, ni heri vyoo hivyo vipya visiwe vya kukaa, viwe vya kuchuchuma, vile vinasemwa kuwa vyoo vya Kihindi.

Vicensia:

Uzuri Wanazuoni tunazifahamu changamoto za matumizi ya vyoo. Nimeomba watu wenye nia ya kusaidia hili tatizo, hata mtu mmoja ajitolee tufanye kazi ya kuja na mkakati wa kuboresha matumizi sahihi ya vyoo nchini Tanzania.

Sio kazi ngumu bali ni moyo tu wa kuona vyoo vya Tanzania vinakuwa bora na salama na vinatumika katika ubora wake. 

Please join hand in this choo initiative, at least I have a plan of where we can start to address this problem/challenge. Wanazuoni naomba mtu/watu (w)ajitolee tufanye kazi pamoja. No serious cost implications, only your passion will be exploited.

Hildergada:

Mimi nina background yote ya miradi ya kuboresha Afya na ujenzi wa vyoo, manuals na designs na kulikuwa na mikakati ya kitaifa nchi nzima na mikopo ya vyoo, magari ya unyonyaji vyoo mpaka ya wapakuaji kwa mkono (Frogman) mijini. Muone Mutalewa wa Dawasa, Kirago na George Makanyadiko wakupe Historia na uzoefu. Nenda UNICEF na Wizara ya afya before you reinvent the wheel.

Charles:

Having seen my fair share of toilet horrors - oh, the nightmares- in the three years I spent at the Hill which contributed probably above everything else to my depression and my extreme low esteem of my fellow countrymen (I mean, if that is the cream of the nation then just imagine what is out there!), I feel that your call deserves some support. 

They say that you can learn a lot about people's manners by visiting their toilets. I am not sure what Kiwasila and colleagues attempted to do in the past, and probably we can benefit from their experiences (if she chooses to share), but this madness has to end at least at the University level. (Although I am not sure how this can be achieved without adequate and reliable water supply. This is a completely different but related issue.)

I am not sure how I can contribute to your initiative, but if you feel you need one extra person to have a voice, you can count on mine. 

NB: About 20 years ago I was travelling from Arusha to Dar using one private car. Along the way my stomach started to feel funny and a moment after leaving Korogwe we needed to stop. I went to the only nearby house to ask for their help and to my great surprise they didn't have a toilet! You only read about these things but witnessing them is something else. Needless to say those guys were greatly embarrassed. One can only hope that they built one afterwards. 20th century Tanzanians!

Malata:

This choo initiative campaign kimsingi ni wazo zuri sana. Sijajua plani ya utekelezaji wake itakaa vipi but kwa phase ya kwanza ni budi kuangalia kama inawezekana kwa UDSM na AU udom kuwa maeneo ya majaribio. Unahitajika utayari wa watu katika hilo.Hali ni mbaya sana kuliko vile tunavoweza kufikiri. For those who climbed the Hill wanaweza kuwa mashahidi. Binafsi ilikuwa nikikamatika nalazimika kutoka Hall 2 hadi Chemistry Dept ambako ni afadhali kidogo.

Wakati fulani nikiwa na dada Emmy [alipata kuwa makamu wa rais UDSM] tulienda ofisini kwa Prof. Kitila Mkumbo kubadilishana mawazo kuhusu namna DARUSO kupitia ofisi ya Makamu wa Rais inavyoweza kufanya kampeni ya kupunguza maambukizi ya VVU miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, Prof Kitila by that time alikuwa Dean of Falculty-Education. Pamoja na mambo mengine, moja ya mambo tuliyojadili ni kuhusu hali ya usafi wa mazingira ya chuo na vyoo. Nilipenda sana hoja ya Prof aliyoitoa kuhusu usafi.Yeye alipendekeza tuangalie ni kwa namna gani tutaweza kuwashirikisha wanafamilia ya UDSM kufanya usafi japo wa maeneo yanayowazunguka hasa vyooni. Kwa kufanya hivyo nadhani alitaka kuona familia ya UDSM inawajibika kwa usafi wa maeneo badala ya kukodi kampuni kufanya usafi.

Kuna haja ya familia za vyuo vikuu kuanza kufikiria ni kwa namna gani usafi wa maliwato/vyoo unaweza kufanywa na wao wenyewe[ wanachuo] hasa katika maeneo wanayoishi. Hii itasaidia kufanya watamani kuvitumia kuliko ilivyo sasa.

Aikande:

Naomba mni include kwenye hiyo initiative niko tayari kushiriki maana tatizo hili la vyoo ni kubwa lakini linaweza kutatuliwa.

Kapongola:

Nafurahi kwamba wengi wetu tumekubali kwamba hali ya vyoo katika vyuo vikuu si nzuri (nadhani UDSM imetajwa kama mfano tu, mada hii inavihusu vyuo vikuu vyote vya Tanzania ambavyo hali ya usafi si nzuri). Na wengine wamediriki kusema ni tatizo la kitaifa. Hii ni hatua njema. Hongera kwa Vicensia na Aikande kwa kuonyesha nia ya kuchukua hatua. Hata hivyo nadhani juhudi za kubadili hali ingeanza katika maeneo madogo kama baadhi ya vyuo vikuu, ili kujifunza na kuona kiwango cha juhudi na rasilimali zinazotakiwa. Ushauri wa Hildegarda wa kujifunza kutoka Unicef na Wizara ya Afya nao ni mzuri.

Hata hivyo, tunaelezwa kwamba kuna baadhi ya vyoo vina unafuu, kama vile vya ‘mastafu’ (Chambi) na vya ‘Chemistry department’ (Malata). Binafsi niliwahi ingia vyoo vya Nkrumah Hall, navyo vina unafuu (siku nimeingia mimi kulikuwa na maji kwenye mapipa, toilet papers na air fresheners). Je, nini kinafanya vyoo vya ‘mastafu’ kuwa afadhali? Je, ni uelewa mkubwa wa matumizi mazuri ya choo au sababu ya uwajibikaji unaoendana na kupewa ufunguo. Yaani, kwa kuwa ni rahisi kujua nani alikuwa mtu wa mwisho kuchukua funguo, inalazimu kuacha choo kisafi kwa hofu ya kutambulika ni nani kachafua choo. 

Tumeambiwa kuwa uduni wa vyoo unatoa changamoto katika usafi. Kuna majengo mapya pale Chuo kikuu Dodoma na UDSM (natumai kuna vyoo vipya vimejengwa pia). Je, hali ikoje huko?

Nimesoma mahali kwamba hadi mwaka 1900, USA walikuwa na tatizo la afya ya kinywa. Hali ilibadilika baada ya watengeneza dawa za meno kugundua kwamba idadi kubwa ya watumia miswaki ingeongeza mauzo ya dawa za meno. Hivyo, wakachukua jukumu la kuongeza ushawishi kuhusu faida za kupiga mswaki kwa kutumia dawa ya meno. Baada ya muda mfupi walifanikiwa kuongeza idadi ya wapiga mswaki na hivyo kuongeza mauzo ya dawa za meno. Kwa kutumia neno la Sabatho Nyamsenda, wamarekani walifanikiwa kwa sababu wali-bidhaisha tatizo la afya ya kinywa. Je, nasi tunahitaji kubidhaisha usafi wa vyoo vyetu? Ili kila anaetaka kutumia choo alipe ili apewe ufunguo kama anavyosema Chambi.

Ubidhaishaji una uhusiano mkubwa na menejimenti (Chambi na Donaldi), hivi karibuni kuna mtu alipata kulinganisha vyoo vya UDSM na vile vya Mlimani City (MC) huku akieleza kwamba hali ya usafi katika vyoo vya MC inaridhisha. Hata hivyo aliuliza kwamba inakuaje hali ya usafi wa vyoo vilivyoko katika ardhi ya mmiliki mmoja kuwa tofauti hiyo? 

Vicensia:

Nashukuru kwa wanazuoni waliojitokeza. Labda nimtoe hofu Hildegarda na wengine kuwa huenda tunataka kurudia yaliyoshafanywa. Ukweli wazo hili halipingani na mawazo mengine ya taasisi kubwa kubwa ya kuboresha vyoo ila huenda si la kujenga miundombinu wala kuandika ma project documents makubwa makubwa. Ni wazo la kujenga 'miundobongo' zaidi, and it's about transforming our problems into passion through creativity.

Wanazuoni we'll get back with the way forward for your support. 

It won't cost much, only your passion will be exploited.

Hildergada:

Tuangalie mazingira kwa ujumla sio vyoo peke yake. Kwani, unaweza ukawa na choo kizuri, bora na safi lakini mazingira ya nje ya nyumba na choo ni machafu, unanunua vyakula vilivyouzwa au kuwekwa ardhini ambako kuchafu au mezani havikufunikwa mainzi yanakilamba; maji machafu yanaingia katika bomba lako la maji masafi ambalo limetoboka au unakanyanga na kupita katika mazingira machafu maji ya kinyesi kibao mvua imenyesha au jua linawaka maji ya kinyesi kibao. Personal, Environmental and Food Hygiene is vital for good healthy life.

Mandalu:

Nadhani unazuoni unachukua mwelekeo sahihi. Kuweka nadharia katika vitendo.


Majiyd:

Hili suala la huduma za maliwato lilijitokeza wakati nakusanya data za thesis yangu ambayo nimeipa title ya "Students' Satisfaction with Service Quality in Higher Education Institutions: In the Perspective of Expectations and Perceptions of Students Affairs". In fact, apart from from academic and consultation services, participants were more dissatisfied with water supply services, blocked and stinking sewage systems, terrible washroom services n.k. Nadhani suala la Huduma ya maliwato kwa UDSM inaonesha picha isiyoridhisha kuhusu wasomi tunaozalisha. Ni hatari kwa jamii ya Wanazuoni kuzidiwa usafi hata na Madrasa zinazosimamiwa na watu wasio hata na Shahada moja. 

Tunazalisha jamii ya wasomi ambayo baadaye ndiyo mamaneja kwenye mashirika makubwa ya uwekezaji kutoka nje. Picha inayojitokeza katika mazingira ya mashirika na taasisi za Umma inaakisi tabia na mienendo ya Vyuo vyetu Vikuu. Kwa mfano kuna tofauti kubwa moja kati ya maliwato ya UDSM NA UDOM ingawaje kote huko kuna shida ya maji. Ukiingia kwenye vyoo vya wanafunzi wa UDSM unakutana na maandishi yanayoonesha aina fulani ya uncivilized community, kuna matusi na maneno ambayo hayastahili kuandikwa na mkurufunzi wa kiwango cha Shahada ya awali au hata shule ya msingi. Hali hii ya kuandika matusi na maneno ya ovyo bado haijawa mila na desturi za wanafunzi wa UDOM, labda miaka ijayo wanaweza kubeba desturi hizi. 

Kwa ujumla niwape pongezi walioanzisha hiyo initiative.....Tasnifu yangu ikiwa tayari tunaweza kutumia kama sehemu ya kuanzia ustaarabu huu.

BeeJay:

Hongereni nyote kwa mawazo mazuri na moyo wa kutaka kuboresha hali ya vyoo vyuoni. Mimi binafsi nakubaliana na Vicensia kwamba suala hili halihitaji miundombinu bali miundobongo na naomba niipakue hiyo miundobongo kwa kuongeza kipengele ambacho ni muhimu sana - kuvunja mazoea ya matumizi mabaya ya choo. Hii inahitaji elimu inayolenga kujenga moyo wa kujali. 

We can have the best toilet facilities with reliable water supply, proper sewage, air freshners and the like, but if we have users who don't have and/or value proper hygiene habits no amount of uboreshaji will make a difference. Iwapo tabia ya kuacha mahali pasafi itatokana na woga wa kugundulika kwamba aliyekuwa wa mwisho ndio aliyechafua bado tutakuwa hatujapata ufumbuzi endelevu. 

Tutakapofanikiwa kujenga chuki ya dhati dhidi ya uchafu miongoni mwa walengwa wa initiative hii tutaweza kusababisha mabadiliko ya kudumu. And this goes for uchafu wa aina zote including kutupa taka hovyo, kutema mate hovyo na kujisaidia hovyo! My two cents...

Kapongola:

Nakubaliana nawe [Beejay] kabisa kwamba sehemu kubwa ya suluhisho (tena la muda mrefu) ni kubadili ‘mentality’ na wajibu wa kila mmoja wetu katika matumizi ya vyoo. Hii itasaidia 'kuvunja mazoea ya matumizi mabaya ya choo'. 

Nitoe mfano wa kubadili tabia bila ya kutumia gharama kubwa au kutumia mabango kama vile 'Usikojoe Hapa', 'Tafadhali Flashi. By Utawala' ambayo wengi wetu hatuyatilii maanani. Mwanzoni mwa miaka ya tisini, uwanja wa ndege wa Schiphol uliboresha usafi vyoo hasa vya wanaume kwa kutumia gharama ndogo sana. Kwa kutumia maarifa ya saikolojia ya mwanaume, waliweza kuweka picha ya nzi kwenye urinals na hivyo kila mwanaume aliekojoa alijitahidi kulenga picha ya nzi na matokeo yake walipunguza watu wanaokoja nje ya mabeseni ya mkojo kwa 80%. Hii inaitwa Nudging – kubadili tabia ya watu bila kushurutishwa, onyo/adhabu au ahadi ya zawadi/kichocheo.

‘Guys are simple-minded and love to play with their urine stream, so you put something in the toilet bowl and they’ll aim at that,’ says Reichardt. ‘It could be anything. I’ve seen a golf flag, a bee, a little tree. It just happens that at Schiphol it’s a fly.’ Source: Hapa

Sina taarifa kama kuna mifano inayofanana na huu kwa ajili ya wanawake. Natumai dhana ya 'nudging' inaweza kutumia kwa vyoo vya wanawake pia. Hata hivyo naamni matatizo ya vyoo vya wanawake yako tofauti na vile vya wanaume. 


Hildergada:

Mimi ninachosema, TZ imekuwa na miradi ya mingi ya vyoo mpaka kukawa na karakana ya vyoo Buguruni jirani na kituo cha polisi iliyokuwa chini ya wizara ya ardhi sewerage and drainage department-low cost sanitation unit; kulijengwa vyoo vya mfano 100 DSM low income areas na mkopo wa vyoo chini ya uhisani wa World Bank. Mkopo wa World Bank wa Squatter upgrading, construction of sewerage and drainage system na construction ya waste stabilization ponds za Dar uliingiza ujenzi wa Vyoo bora (VIPL) ambavyo design yao ilikubaliwa na W. Bank ibadilike isiwe ile standard design waliogharimia Botswana, Lesotho, Malawi etc yetu ikaitwa TANVIPL-Tanzania Ventilated Improved Pit latrine au DARVIPL. Ilikuwa 1.5 square meter sio skwea mita moja kama hiyo standard design ya World Bank kwani sisi huoga ndani na watu bonge na wababa shooting akiwa nje-ikakubalika. 

Mwanzoni kulijaribiwa compost latrine (Wen Kilama na Krisno Nimpuno initiative) ya sanitation without water (kitabu chake kipo) hivi havikufaa TZ waislamu kutumia kutawadha maji mengi na densely populated houses za dar; hakuna mashamba ya kutumia hiyo mbolea kutoka compost latrines. Hizo 54 zilizojengwa mfano Manzese ziliishia kubomolewa. Miradi ya vyoo mingi, vitini/manuals zipo kibao. 

Tatizo letu ni tabia yetu ya uchafu, hatuambiliki, hatubadiliki, sugu, ujuaji na kutokujipenda/kujijali kiusafi. Hata ukute mama/baba ntilie anauza samaki za kukaanga zipo wazi, vumbi, inzi, moshi mbaya wa gari-unanunua!! Samaki wabishi zinauzwa wazi barabarani viongozi wanapita wanaangalia nao wanasimama wananunua hapo Survey au Africana, Tegeta na Maji Machafu jirani yake na taka kibao.

Wizara ya Ardhi yard ya vyoo Buguruni in 1980s-1990 walisomesha mafundi ujenzi wakaweka na choo mtu ananunua anavyotaka chote au parts. Vikijengwa sites and services surveyed areas kama Kiwalani, Kipawa, Sinza, na squatter areas kama Buguruni, maeneo ya Mtoni. Kukatolewa mikopo ya vyoo chini ya mradi wa World Bank chini ya Wizara ya Ardhi-DSD Mkurugenzi Fredrick Njau Public Health Engineer wa kwanza TZ idara ilianzishwa wakati wa clean water and sanitation decade (1981-1991) and health for all by year 2000. Wakati huo mji wa Dar ulikuwa mchafu baada ya Ujamaa kuvunja City Council ikarejeshwa. DSD ikaunda DSSD City Council kama watekelezaji wa sera ya ujenzi wa nyumba bora (wizara ya ardhi) na vyoo Bora (City Council na Wizara ya afya). 

Hivyo, team ya Wizara ya Afya, ikaja Ardhi DSD kufanya kazi na wataalamu ambao consultants walitoka India, London School of Hygiene and Tropical Medicine, WEDC Leics UK na baadhi wakawekwa City Council kuboresha karakana ya vyoo, ujenzi wake, design na mfumo wa underground sewerage system ya Dar, stormwater drainage system na waste disposal sites (Solid and liquid waste). Waholanzi wakasaidia uanzishaji wa Centre for Housing Studies na Course ya Diploma ya Public Health Engineering ambao first batch walipelekwa DSSD ambayo kwa sasa ni DAWASA na DAWASCO (muone Archard Mutalemwa, Kirango watakupa background) baada ya sera na mikakati ya structural adjustment na kupunguza size ya public sekta na sera ya PPP. 

Mikopo ya vyoo haikulipwa hadi leo, vyoo vya mashuleni ukarabati hakuna hata kama walijengewa bure. Vya majumbani wamebomoa au kutoboa kuta maji yanamwagika nje wasiite gari kunyonya walipie. Waste stabilization pond wamevamia na kujenga nyumba katika kinyesi daima huzitoa picha humu mtandaoni. Dampo solid waste ndio wamehamia wamejenga huko, kukusanya nyanya, nyama wanauzina mama ntilie kumbe zimetupwa ni mbaya.

Hata gari za kunyonya kinyesi Tanzania zilitengenezewa za kumudu vyoo vyake vizee visibomoke wanavyoweka pressure yale makubwa ya UK yalisitishwa. Ikatengenezwa ndogo ya kuweza kupita squatter area njia nyembamba huko na kampuni za South Africa zikaja DSM na mpakua choo akatengenezewa kitoroli na kampuni ya Waste ya Holland kama consultants, wapakua vyoo wakapewa mafunzo, working gear kunyonya vyoo kwa usafi na kumwaga substation mojawapo hapo Makumbusho darajani njia ya kwenda Tandale jirani na COSTEC. 

Mikoani VIPL vilikwenda na Wizara ya Afya-Mtu ni Afya campaigns na donors (Rukwa-RUDED), Kagera, Mara, Mwanza-HESAWA program ya SIDA; Iringa, Mbeya-DANIDA (UNICEF-Waging'ombe); Tanga (TIRDEP) mhisani GTZ; Lindi, Mtwara -FINNIDA; Morogoro -Waholanzi-DHV, na Ireland (Irish Aid) integrated project za maji ya visima vya dando na gravity fed piped water supply with health education na mafunzo kwa village health workers, extension staff walipewa pikipiki na katibu kata, tarafa. Kukagua vyoo vyumba hadi nyumba huna-faini na utajenga. Wengine wakaweka kinyesi eti ukitumia na mkweo au mwanao kinyesi kikigusana sawa kama mmelala na kutenda uovu (kuzini). Design za vyoo zilizingatia mila na matakwa ya kaya mradi tu utagharimia gharama kiwe bora-ventilated.

BRU-Building Research Unit now an agency (BRU ni ya Wizara ya Ardhi) imejenga nyumba bora za mfano mpaka modern gogo tembe and modern Maasai Manyata. Juhudi zote hizi hazijazaa matunda sana. Kule Sinza ni sehemu low ina maji sana wakaweka underground sewerage system kuunganisha nyumba na vyoo na nyumba za mfano za low cost zilijengwa. Mifuniko ya sewerlines wametoa, kunafurika kinyesi, matambara, taka kibao yanaziba; pia kijiji cha Nyerere cha Mwenge-mifuniko wametoa kuna viroba vya taka, kinyesi kinafurika na overload kubwa, nyumba za lowcost za design moja wameuza wanajenga maghorofa makubwa-sinza pia, bar kibao overload ya mzigo wa sewage na waste water ambapo haikutegemewa kwa makisio ya 20 years badala yake mijengo imekuwa kutoka makisio ya 20% kwenda over 200% kwa miaka hiyo. 

Miji mingine Arusha, Morogoro iliingizwa katika Low cost sanitation project ktk low income areas kujenga Low cost durable toilets. Dodoma ulikuwa katika capital dev na ujenzi wa vyoo hivi na sasa Swiss support inaendeleza vibaya sana masuala ya sanitation ni mradi mkubwa. UNICEF Wanging'ombe sanitation project iliunganishwa na Nutrition Project na maji kutokana na malnutrition kipindi kile 1980-1990 Iringa ilikuwa balaa. Kukawa na forest protection na protection of catchment forest (maji ya mabwawa ya umeme); soil and moisture conservation projects; tree planting (agro-forestry) terracing na kupanda nyasi za mbolea na za kukinga mmomonyoko; vyoo visichafue chemchem za maji hivyo kila mtu kujenga vyoo-Iringa, Njombe, Makete, Kilombero na visima vya dando. Visima vya dando utakuta alama tu-wamebomoa kuuza chuma chakafu. Huko Mara na Mwanza bomba la handpump wanafungia mikokoteni ya ng'ombe na punda-kunya ziwani na kuoga na kuchota maji!

Ukifika vyuoni ambako kunasomeshwa sanitation engineers kwanza unakaribishwa na harufu ya kinyesi. hao wasomi wanaosoma waste water andsewage disposal, design za mifumo yake na vyoo na health education yake ndio hao wanaoingiza modess chooni, plastic ambazo ni condom na chupa za plastic wanazonawia zinakwama, vinafurika kutoka ghorofani hadi chini na ni university hiyo. Medical school haina usafi wa kufurahisha na vyoo vinakuwa vibovu.

Usishangae ukifika hata universities ambako kuna wasomi ukakuta mazingira machafu takataka kila kona, kuna dustbins lakini hawatupi humo. Ukiingia material testing lab ya construction engineers utakuta madirisha mabovu, ceilingboard imeanguka. hawana ufahamu wa kutest materials wakaweka au kujenga ceiling board. Teaching practice au practical training yao sio hapo mjengoni kwao au nje ya jengo within campus ila ni nje ya mji au mkoa na eti hakuna allowance hivyo hawaendi fungu hakuna! 

Nje jirani ya chuo cha usafirishaji kuna soko ambapo magari huleta ndizi kaangalie hali yake. Jirani ya TGNP-Mtandao kuna soko la Mabibo lipo hoi linavuja, chafu na jirani pia kuna watu wanaishi kinyesini wamevamia bwawa la kinyesi la Mabibo. Kunywa dawa za mabusha na matende hawataki. Taasisi za kuelimisha zipo jirani-

Tupo tupo tu. Kwani hata vyuo vya ujenzi mbona kuna ngazi za concrete hapo campus zimebomoka na hao technician wanaosomea ujenzi au mainjinia na maprofesa wao
hawaoni?? Harufu ya kinyesi wanaisikia.

Hebu mwambie jirani yako kuwa karo lake au choo kinamwaga maji yanakuja kwako kama hamtagombana na ametoboa makusudi. Kaweka bati dirishani kwake kuzuia maji ya mvua lakini yanapiga kwao na kuingia dirishani kwako na kuharibu vifaa vyako ndani ya nyumba yako kama ataliondoa au kuliweka lisikudhuru. Weka lako liingize maji kwake kama kutakalika. Mtenda atende yeye. 

Mitaro ya barabara mpya yote kwa sasa wametoboa na kuunganisha vyoo vyao. Angalia mitaro ya Ubungo Mwenge na hasa ya Mwenge Tegeta ujionee malundo ya taka na maji ya kinyesi na matundu ya kuunganisha vyoo vyao. Ukibomoa na kuziba uchukue hatua-serikali inaonea. Waliojenga kwenye barabara (road reserve) bomoa nyumba na biashara zao maana ni mkopo wa world bank survey ya plots huko Tangi Bovu to Tegeta. wameziba feeder roads huko, Sinza etc gari la fire la kunyonya vyoo litapita wapi. 

Sasa waste collection na disposal pamoja na kunyonya vyoo/septic tanks ni privatised na ni sekta ya kujiajiri kwa wale watakao kuunda CBO za kufagia na kuwa na magari ya kuzoa taka ngumu na takamaji. Polluter pay principle ndio donors wetu wanatulazimisha tuzingatie. Hakuna kuzolewa taka na kunyonyewa vyoo kwa hela ya kodi ya mzungu ulaya au Mchina na Mrusi.

Tuna tabia za uchafu, hatubadiliki. Kabla hatujaanzisha mradi muhimu kufanya review ya past efforts, kulifanyika nini kwa mfumo gani, kulitokea nini positive na negative, lesson learnt na utabadili nini kivipi.Tembelea miradi ya vyoo inayoendelea kama vyoo vya mbolea, vya gas vya shimo direct or off-set latrines; vyoo vya design kwa vilema na wazee. Boresha pale wengine walipokosea au kuwa na mapungufu. 

Tatizo TZ ni kurudiarudia yaliyokwisha kufanyika kufanya as if hakujafanyika kitu, kurudia makosa yale yale na watu wapo kusubiri msaada sio kubadilika kujidai as if nothing happened. DSM kumepimwa sasa hata kulikopimwa ni squatters. NHC houses hazikujengwa barabarani, wameuziwa-wanajenga frame mpaka barabarani. 

Vipi vya pombe mpaka njiani; footpaths za kupita watu kwa miguu wamepanga magari wananchi wanapita njia ya gari wagongwe wao wapo barabarani bar wanakunywa pombe. Naomba siku moja lije lori la mafuta likose break liingie barabarani ligonge hayo magari ya wanywao pombe bar barabarani yawake moto yateketee ndio tutajifunza kuheshimu sheria za nchi. Kwa mfano tu angalia magari hayo baraba ya ya Sinza na Lufungira/Kakobe-Mwenge

WRDP NGO tunahitaji partner wa kufanya kazi hii ya kupita nyumba hadi nyumba kuelimisha watu/kaya na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa usafi, tabia ya usafi, sera ilivyo sasa ya decentralization ya uzoaji taka na usafi wa mazingira na kuwasaidia kuunda CBOs za kufagia, kupata protective gear za kazi ambapo uzoaji taka Mtaa unaingia mkataba na mkandarasi mwenye magari wakisimamiwa na Municipality. Kuwapa training Mitaa ya usimamizi mzuri wa hela za usafi wakusanyazo na kuwafanyia auditing kuona efficiency na effectiveness ya kazi yao maana hata water user associations ni walaji raia hawapati maji. Kuhamasisha kaya ktk mtaa wachangie kupiga mitaro ya kuondoa maji yanayotuama kwa kuwa wapo bondeni na maji yanatuama lakini kila mtu anayaangalia tu na kuchuruzisha yao tena kuzalisha wadudu wa madhara. 

Kila mtu awe mlinzi wa mwenzake. Pia kutoa mafunzo ya wazoa taka binafsi wanaozoa taka majumbani kwa kujiajiri lakini huzitupa barabarani au nyumba zinazojengwa
mpya na public places. Pia, kufuatilia public sites ambazo watu binafsi wameweka karakana za furnitures, magari watoto hawana mahala pa kuchezea wapo kwenye maduka ya video na music kutwa wanaangalia picha. 

Tupinge na uwepo wa bar kila baada ya nyumba 3 viti mpaka barabarani wanapapasana na kukojoa hovyo watoto wanaona hapo mibaba iliyolewa inakojoa. Ni wazazi hasa wa kuzingatia maadili sisi wakati tunaweka baa kila nje ya nyumba; tunajali afya za binadamu sisi ambapo maji ya kemikali ya saluni za nywele yanamwagwa barabarani watoto na watu wasio na viatu wanayakanyaga yanawaletea madhara kimwili. 

Extension staff wapo, NGO za watoto, jinsia, mazingira, afya zipo lakini haya yote tunayatazama. Hata nje ya NGO kubwa za kitaifa malundo ya taka, bar za pombe viti mpaka barabarani vipo, music sauti kubwa kuathiri watoto lakini hakuna tufanyacho tunamsubiri Rais ajaye mwaka huu, ujao na mpaka sasa CCM na Ukawa kulumbana. Wape NGO masuala ya siasa-utaona maandamano, lakini nje ya mijengo yao mtaani-panafurika maji nao wanaogelea lakini hakuna hatua inayochukuliwa. 

Bado miradi ya SUDPF na baadae CIUP (donor funded ya kuboresha makazi na kurasimisha makazi). Walikoboresha tena kwa wananchi kuchangia 20% ya capital cost-wameuza plots na kuhamia maeneo hatarishi na kuishi kinyesini. Evaluation za miradi hiyo zipo uone utata na ukifika huko kulikoboreshwa na kurasimishwa Dar utaona ama kweli sisi ni zaidi ya manyani!! Gharama za GVt na za donor na michango yao wanasahau wanajali hela wanauza na kuwa masikini wala hawasongi mbele na kuishi katika uduni maisha wenzao wanajenga mijumba na mighorofa kuta ndefu.

TUBADILIKE SOTE VICENSIA-hili unalolisema hapa tuungane maana nasi tulikuwa tunaliandaa na ndio maana nimeandika kwa kirefu hapa.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP