Monday, October 26, 2015

Jukumu la Kwanza la Rais Ajaye

Jukumu la Kwanza la Rais Ajaye

Chambi Chachage

Uchaguzi wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza jana tarehe 25 Oktoba 2015 sasa unafikia tamati. Tume ya Uchaguzi imeshaanza kutangaza baadhi ya matokeo. Wafuatiliaji wameshaanza kuona mwelekeo wa nani atakuwa Rais Mteule.

Rais huyo ajaye hakika atakuwa na vipaumbele vyake kichwani. Vipo vitakavyotokana na Ilani ya chama chake. Lakini tunaamini vipo ambavyo angalau vitatokana na maono yake ya uongozi.

Kama raia wa nchi hii nami nina maono yangu ninayotamani yaendane na ya Rais Mtarajiwa. Naamini jukumu la kwanza la Rais huyo linapaswa kuwa ni jibu kwa vijana waliochoka na hali ilivyo.

Baada ya kupiga kura, Jumapili jioni nilibahatika kutembelea vituo kadhaa Jijini Dar es Salaam nikiongozana na baadhi ya marafiki zangu ambao wana matumaini sana kwamba kama Mgombea wa Chama Tawala atashinda basi atalete mabadiliko makubwa, siyo kwenye Serikali tu bali pia katika chama. Hali tuliyoikuta vituoni ilituacha tukijiuliza maswali mengi kuhusu vijana hasa wa mijini.

Katika kituo kimojawapo kijana mmoja aliponiona tu (na nahisi) kupima kuwa mimi ni kijana mwenzake ukilinganisha na wenzangu akanisalimia: "Kijana, Mambo Mazuri!" Alichokuwa anamaanisha tuliweza kukiona katika vituo vya eneo hilo ambalo Mgombea wa Chama Tawala alipata kura chache ukilinganisha na yule Mgombea nguli aliyewahi kudai kuwa vijana ni 'Bomu linalosubiri Kulipuka'.

Swali kubwa ambalo limepelekea niandike makala haya na ambalo naamini ndilo hasa (linalopaswa kuwa) jukumu la kwanza la Rais Mteule ni: Je, ni namna gani Serikali ya Awamu ya Tano itarudisha (kwa maneno na vitendo) imani na matumaini ya vijana - hasa wa mijini - waliokatishwa tamaa na mfumo wa utawala wa nchi hii? 

Jibu la swali hili ni la kiuchumi na kiusalama. Ili vijana hao waone Serikali yao inafanya kitu lazima waone uchumi wenye ajira ukikua na siyo huu tulionao ambao wachumi kadhaa wanauita 'uchumi usio na ajira'. Na usalama wa nchi utategemea sana hili la vijana kuishi katika nchi ambayo ina uchumi unaokua huku ukileta ajira.

Ndiyo maana nakubaliana kabisa na mmoja wa marafiki zangu tuliokuwa nao vituoni hiyo jana ambaye anaamini kuwa ukuaji wa viwanda utasaidia suala hilo la uchumi na anayeamini kuwa suala hilo - na la usalama - linatakiwa kuwa kipaumbele cha Rais ajaye.

Lakini viwanda hivi vinapaswa kuzingatia uhusiano kati ya miji na vijiji pamoja na miji na majiji. Kama vijana wengi wamejazana mijini kutokana na sekta ya kilimo kutokuwa na tija basi ni heri viwanda vyenye mahusiano na kilimo vikajengwa katika namna ambayo vitaifanya miji mikubwa kama Dar es Salaam ambayo ina idadi kubwa sana ya vijana kupumua na kutoa nafasi kwa mingine.

Viwanda visijikite Dar es Salaam tu. Bali na Tanga, Mtwara na kwingineko. Ifike mahali kijana wa Kisosora asione ni lazima aje Kinondoni na 'kubanana hapa hapa' jijini tu ili aweze kuendelea. 

Pia tukumbuke kuwa watafiti mbalimbali - toka enzi za Profesa Justinian Rweyemamu - wametafiti sana suala la viwanda nchini Tanzania. Hivyo, ni vyema kuyarejea makabrasha na mapendekezo yao mengi ambayo mengine bado yana 'mashiko' hata hivi leo. 

Japokuwa nimehoji ni Ilani ya Chama gani inatumika kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017-2020/2021) utakaojikita katika 'Uchumi wa Viwanda' nchini Tanzania ambao tayari ulianza kuandaliwa hata kabla ya Uchaguzi huu wa mwaka 2015, naamini ni muhimu mchakato huo ukazingatia sana madai ya vijana wengi waliopiga kura zinazosemekana kuwa ni za 'hasira'.

Katika dunia ya teknolojia, unaweza kuzalisha viwanda vingi lakini vikazidi tu kujenga jamii yenye matabaka ya 'wavuja jasho' na 'wavuna jasho'. Kama viwanda havitazalisha ajira za 'kutosha' na zenye ujira wa 'kiheshima' basi Rais ajaye atakuwa anaendelea tu kuchochea kemikali za moto kwenye hilo bomu tulilotishiwa kuwa linasubiri tu kulipuka. Hivyo, wataalamu wetu wa viwanda - kina Profesa Samuel Wangwe na Dakta Blandina Kilama wa REPOA - wanaoshirikiana na Tume ya Mipango katika Ofisi ya Rais kuandaa huo Mpango wa Maendeleo wasisahau makabrasha yao ya zamani yaliyozingatia nafasi ya ajira na ujira katika mapinduzi ya viwanda.

Lakini viwanda siyo mwarubaini au mugyariga wa Babu wa Loliondo. Hauwezi kuponya kila tatizo letu nchini. Kuna njia nyingine nyingi tu za kujibu hilo 'Suala' na 'Swali la Vijana.' Wapo wanaotumia ujasiriamali. Hilo nalo lina utata na utete wake lakini ni muhimu sana hasa katika nchi ambayo haijaweza kikamilifu kutekeleza Sera ya Mgombea mmojawapo wa Urais iliyojikita katika kaulimbiu tamu ya 'Elimu, Elimu, Elimu' mpaka kupelekea 'wanailm' kudai tulichonacho ni 'Bora Elimu' na siyo 'Elimu Bora'.

Vijana wengi wana uwezo/akili. Lakini wengi hawakuchaguliwa kuendelea na 'Elimu ya Juu' n.k. Na kama Mwalimu Nyerere alivyosisitiza, siyo wote waliofeli - hawakuchaguliwa tu kwa kuwa hakukuwa na nafasi za kutosha. Na wengine hawakuweza 'kufaulu' kutokana tu na sababu za kijamii/kifamilia na kiuchumi/kifedha.

Hadi leo nakumbuka tukio moja lililonitokea enzi zangu za 'utoro' nilipokuwa mwanafunzi katika Shule ya Msingi Mlimani. Wakati wa likizo nilienda Gonja Maore, kijijini kwa Bibi yangu Mkunde Kitunga, ambapo kulikuwa na shule ambayo ilikuwa haijawahi 'kufaulisha' mwanafunzi yeyote toka enzi za Mama yangu Demere na nduguze. Basi kukatokea ubishani mkubwa sana kati yangu na watoto wa kijijini hapo kuhusu ubora wa shule zao na zetu za mijini. Nikajitapa na kujitapa kwa vigezo vya 'ufaulu' wetu n.k.

Mtoto mmoja akainama na kuchora maumbo kadhaa kwenye mchanga. Akaniambia tafuta basi 'mzingo'. Kilichofuata ni mimi 'kupotezea' kwa kuwa, kiukweli, sikuwa najua namna ya kuzifanya hizo Hesabu. Mtoto akalalama "hawa watoto wa mjini wanaringa tu kwa kuwa wana hali nzuri lakini hawajatuzidi maarifa". Pamoja na hayo nilifaulu Darasa la 7 na kwenda shule ya Sekondari Azania.

Mwenzangu hakufaulu kwa kuwa hakukuwa na shule ya sekondari hata ya Kata hapo kijijini. Za wilaya na mkoa zilikuwepo ila ndizo hilo walizokuwa wanashindania kuzipata na sisi watoto wa mjini. 

Kha, leo eti mimi ndiye nipo kwenye Chuo Kikuu maarufu duniani! Je, najua mwenzangu ambaye labda anastahili kuliko mimi kuwa hapo yuko wapi leo? Hata sijui. Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa ni miongoni mwa vijana wanaotaka mabadiliko kwa 'udi na uvumba', yaani kwa namna yoyote ile hata kwa kutumia 'daraja' la 'ufisadi'! Hawa ndiyo vijana ambao Rais ajaye anapaswa kuwajibu ni kwa nini pamoja na uwezo walionao na rasilimali tulizonazo, wagombanie tu kuchuuza karanga na kashata kwenye vituo vya mabasi n.k. ilhali wanaweza kufanya shughuli zenye tija zaidi?

Rafiki yangu mmoja sasa anafanya utafiti ambao umeonesha, kwa kufanya 'jaribio' halisi kabisa, kwamba hata  baadhi ya vijana ambao hawakufanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wakipewa mafunzo kidogo ya ujasiriamali na mtaji mdogo tu wanaweza kufanya biashara zenye tija na wengine hata kuweza kuajiri wenzao. Badala ya kijana kukaa nyumbani au mtaani akiwa hana matumaini kisa eti 'amefeli' kumbe anaweza 'kuwezeshwa' na 'akaweza' kufanya kitu chenye tija kwa kwa familia na Taifa lao.

Ni kweli siyo vijana wote wanaweza kuwa wajasiriamali. Pia ni kweli siyo vijana wote wanaweza kufanya kazi viwandani. Ila ni muhimu kuwa na namna ya kuwaandaa vijana waweze kufanya kile wanachokiweza na, zaidi ya yote, kile wanachokipenda maishani.

Isitoshe ukikipenda kitu ni rahisi kukimudu. Na ukikimudu ni rahisi kuwa mchapakazi. Kama kweli Tanzania ya mwaka 2015-2020 ya Rais ajaye itakuwa ni ya "Hapa Kazi Tu" basi wafanyakazi hao, hasa vijana wetu, wanapaswa kwanza kuwa na kazi za kufanya.

Viwandani na mashambani. Dukani na sokoni. Mijini na vijijini. 

2 comments:

Kambogo October 27, 2015 at 12:06 AM  

Nimeipenda! Umefanya uchambuzi mzuri na kutoa mapendekezo yanayotekelezeka iwapo vipaumbele ulivyoviorodhesha vitapewa kipaumbele. Binafsi naona inabidi kwanza kuainisha nini kifanyike kwanza, nini kifuate, na utaratibu gani utumike, kwa maana ya vijana wepi waanze kuhusishwa katika mkakati huo. Nasema hivi kwasababu, elimu, kilimo na ujenzi na/au ufufuaji wa viwanda vyote ni mipango ya muda mrefu. Hapa kati kati inabidi wataalamu wetu wabuni nini cha kufanya kuwainua vijana ili kuwawezesha kuendelea kusukuma maisha wakati wakisubiri mipango hiyo ya muda mrefu ikamilike. Imani ya vijana kwa Serikali yao itarudi tu pale watakapoona kwamba Serikali inawathamini wao na mchango wao katika ujenzi wa uchumi ya nchi na katika kuleta maendeleo ya nchi yao kwa ujumla.

lunogelo October 27, 2015 at 8:30 AM  

Ndugu Chachage,
Asante kwa mchango wako. Kuna maangalizo mengi katika mada hii lakini iliyonigusa mwanzo kabisa ni pale unaposema "kuna wachumi wachache wanasema tuna uchumi unaokuwa bila ajira". Nimeona labda nikurejeshe kwenye ukweli kuwa hitimisho la kuwa nchi nyingi za Kiafrika zina "jobless economic growth" imetokana na hali halisi na ukweli ambao kila mtu anaona na wasiokuwa na ajira ni mashuhuda. Ripoti ya United Nations Economic Commission for Africa (www.uneca.org) ya mwaka 2013 ilijikita katika kuangalia mapungufu hayo baada ya kufanya utafiti katika nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Mambo mawili yamechangia katika tatizo hili (a) ukuaji uchumi unatokana na uwekezaji katika sekta za maliasili (mafuta, gesi na madeni) bila kuwa na mikakati ya kuziongezea thamani nchini ambapo ajira zaidi ya zile za uchimbaji zingeongezeka (b) kutegemea wawekezaji wa kigeni ambao wanatumia teknolojia ya juu inayohitaji watu wachache; lakini pia wakipata faida wanaitoa kuipeleka kwao ambako inatumika kutenegeza ajira huko. Ilidaiwa kuwa kwa kiasi kikubwa wawekezaji wazawa, hata kama wanawekeza kwenye viwanda vidogo na vya kati, wana "impact" zaidi kwenye kutengeneza ajira za ndani kuliko wawekezaji wageni. Ripoti imehimiza nchi za Kiafrika kuliangalia upya swala la kuchakacha au kuongeza thamani bidhaa zake kabla ya kuziuza nchi za nje, na pia kuwaenzi wawekezaji wa ndani au wazalendo ambao wataendelea kuwepo nchini na faida wanaoipata huiwekeza ndani. nilifikiria ni bora nifafanue hilo baada ya kuona kama unadhani dhana ya "jobless growth" ni ya "wachumi wachache". Kwa vyovyote vile dhana hii haina maana kuwa hakuna ajira kabisa zinazoendana na kukuaji uchumi tunaoshuhudia, badi kasi yake ni ndogo kuliko mahitaji ya wananchi ambao wamefikia umri wa kuajiriwa. Mzee Lunogelo

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP