Monday, November 2, 2015

Ningekuwa Magufuli

Ningekuwa Magufuli

Chambi Chachage

Rais-Mteule, Dakta John Pombe Magufuli, anajiandaa kuapishwa juma hili. Gumzo katika vyombo vya habari na vijiwe vya magazeti mijini na vijijini ni kuhusu nani atakuwa Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri litakuwaje. Mwanaudadisi nami nimeona nisipitwe.

Kwanza, najua kabisa mimi siyo Magufuli. Pili, Kikatiba Rais ndiye mwenye mamlaka na utashi, kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ya kuunda Baraza la Mawaziri. Tatu, mimi siyo msaidizi.

Lakini kama raia wa kawaida, jukumu langu la kwanza ni kufuatilia ahadi za Rais ajaye. Na ahadi ambayo pengine inapaswa kupewa kipaumbele sasa ni hii ahadi ambayo, kwa mujibu wa Mbunge Mteule wa Kigamboni Dakta Faustine Ndugulile, Magufuli aliitoa:Kwenye hilo tunaweza kuongeza ahadi ya 'Mpigaji Kampeni Wake Mkuu', January Makamba, aliyoitoa wakati na yeye alipokuwa anakiwania kiti hicho cha Urais: "....nitaunda serikali ya mawaziri .... ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake..." Kama naye atakuwa miongoni wa washauri waku , heri alishauri hili na 'vigezo vyote vizingatiwe'.

Nami ningekuwa Magufuli ningeuzingatia na kuutekeleza ushauri huo . Naamini unatekelezeka maana wahenga wetu walinena kuwa "Waarabu wa Pemba wanajuana kwa vilemba." Ndiyo. Wanasiasa wanajuana. Hasa tuliokuwa pamoja katika Baraza la Mawaziri.

Sisi wengine ambayo siyo wanasiasa tunawajua kwa mbali tu - kwa kusikiliza wanachosema na kuona wanachofanya. Hivyo, kwa lensi hiyo, ningekuwa mimi Magufuli ningehakikisha nalijibu lile swali la 'Jukumu la Kwanza la Rais Ajaye' ambalo Mwanaudadisi amedai kuwa ni 'Suala/Swali la Vijana' hasa wale wanaoyalilia mabadiliko.
Nitaanza kwa kuwateulia 'mawaziri vijana' wenzao ila ambao ni wachapakazi na siyo 'wapiga dili'. Safari yangu itaanzia Kigamboni ambapo nitamwomba Dokta Ndugulile atinge Wizara ya Afya.

Kwa nini? Kwanza kabisa kwa ushujaa wake wa kutoniogopa wakati wa lile sakata la Feri ya Kigamboni lililopelekea nitoe ile kauli tete/tata kuhusu 'Kupiga Mbizi'. Nahitaji Waziri jasiri ambaye yuko tayari kusimama upande wa 'watu wake' na, kwa heshima na taadhima, kuniambia, Mheshimiwa Rais hapa 'ndivyo sivyo'.

Baada ya kutoka hapo nitaelekea kule kwenye Wizara ya Sheria na kumwomba Angellah Kairuki awe Waziri kamili. Pamoja na ujana na ugeni wake (kiasi) wakati wa sakata zito la Escrow Bungeni, alihakikisha anaitetea Serikali yake na kuhakikisha Maazimio ya Bunge yanapata 'fomulesheni' inayoweza kutekelezeka haraka na kuridhisha pande zote. Ndiyo, pia nahitaji mtu ambaye haogopi hata kuchukiwa na wapinzani pale anapoitetea Serikali yangu kwa kile ambacho (tu)anaamini kiko - ama kinapaswa kuwa - sahihi.

Ila pia nitakumbuka kwamba kule vyuoni nilipokuwa kuna 'vijana' mahiri wasiotaka mchezo mchezo. Nitamfikiria Dakta Elinami Minja wa pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Kwa kuwa siyo Mbunge itabidi nitumie zile nafasi zangu 10 kumteua awe Mbunge. Kisha nitamwomba aingie Wizara ya Fedha, kwanza kama Naibu Waziri ajifunze siasa kidogo kabla sijampa madaraka makubwa zaidi. Pia kwa kuwa Taifa limepasuka kikanda, hii itakuwa vile vile ni jitihada ya kutoitenga inayosemekana eti kwamba ni Kanda ya Kaskazini ilhali hakuna eneo lolote lile la kiutendaji Bara liitwalo 'Kaskazini'. Tuna Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata na Mitaa/Vijiji tu. 

Wakati nafanya uteuzi huo nitakuwa nimezingatia sana huu ushauri wake: "Pia [Dakta Elinami Minja] alisema kuna haja ya kuwa na nidhamu katika bajeti hiyo kwa kuonyesha mahali ambako fedha zinatakiwa kuelekezwa. 'Kama ukisema fedha hizo zinakwenda kwenye Wizara ya Elimu lakini hujasema zinakwenda kufanya nini unakuwa hujaeleweka', alisema." Kwa kuwa huyu ana nidhamu na umakini wa hali ya juu, nahitaji aende kudhibiti bajeti na matumizi ya Serikali. Sitaki kusikia habari za upotevu wa fedha za Umma.
Itabidi pia nitoke kidogo nje ya mipaka ya nchi yetu na kwenda kumtafuta Rakesh Rajani kule Marekani na kumwambie, Ndugu, hebu rudi nyumbani. Wewe si ndiye ulikuwa mstari wa mbele pale HakiElimu kuhusu kupiga vita 'bora elimu' ili iwe 'bora elimu' huku ukitumia vile vigezo mnavyoviita 'SMART'. Sasa bado nina nafasi 9 za kuteua Mbunge hivyo nakuteua na naomba uende pale Wizara ya Elimu ukitekeleze ulichokuwa unakihubiri. Na hatutaki kusikia habari za eti wewe ni 'Mhindi,' mbona Mwalimu Nyerere alikuwa na kina Amir Jamal na Al Noor Kassum waliofanya kazi kizalendo.

Pia kwa kuwa ninaamini wapo ambao wanastahili 'nafasi ya pili' hata baada ya kujikwaa kidogo ama kukosea kabisa, nitamwomba Profesa Sospeter Muhongo arudi tena kwenye Baraza la Mawaziri. Nahitaji pia watu wenye hulka/tabia kama yangu - wanakuwa kama kioo cha kuakisi taswira yangu. Huyu nitamwomba arudi kwenye Wizara ya Nishati na Madini asimamie vitalu ili visigawiwe hovyo hovyo na atumie utalaamu wake kwenye sekta ya gesi na mafuta.
Najua Mbunge-Mteule wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, anaweza kuja juu. Lakini nitamkumbusha haya maneno yake: "Nimepata taarifa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Ndugu Sospeter Muhongo amechukuwa hatua ya kujiuzulu katika nafasi hiyo. Napenda kuchukua nafasi hii kutambua busara aliyochukua ambayo naamini itasaidia harakati za kujenga demokrasia yenye uwajibikaji. Naamini uamuzi wa Ndugu Muhongo umewezesha kulinda heshima ya Bunge na maazimio yake. Kwa muda mfupi alioongoza Wizara hiyo, Ndugu Muhongo ameweza kuongoza mabadiliko kadhaa muhimu ya kiutendaji katika wizara hiyo na taasisi zake. Hata hivyo, nafasi ya Wizara aliyokuwa anaongoza katika suala la Tegeta Escrow imemtia doa kubwa ambalo ilikuwa lazima awajibike. Naamini Rais Kikwete atamteua mtu mchapakazi na makini zaidi atakayeweza kuendeleza yale mazuri ya Ndugu Muhongo na kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza."

Na kwa kuzingatia mantiki hiyo hiyo nitajaribu kumfikiria Lazaro Nyalandu. Baada ya lawama nyingi tu alizotupiwa Rais aondokaye, Ndugu Jakaya Kikwete, kuhusu ujangili naona siku za hivi karibuni kumekuwa na matokeo mazuri katika masuala yanayohusiana na Wizara ya 'kijana' huyo. Kwanza vyombo vya dola vilianza na kumkamata Jangili Yang Feng Glan ajulikanaye kama 'Malkia wa Pembe za Ndovu.'  Kisha majuzi kakamatwa Jangili Bingwa, Boniface Matthew Mariango, aliyepachikwa jina la 'Shetani.'


Hakuna aliye malaika duniani. Pamoja na mapungufu yake ya hapa na pale, nitakubaliana na Dakta Aikande Kwayu kwamba kitendo cha Nyalandu kuunda tume ya kuchunguza idadi ya tembo/ndovu nchini na kuitoa kwa uwazi ni kitendo cha ujasiri hasa ukizingatia kuna viongozi na Serikali nyingi tu zinazopenda kuuficha 'ukweli'.
Vile vile kwa kuwa naamini ili Serikali yangu iwe makini zaidi na zaidi inahitaji Wabunge machachari wa upinzani - na kwa kuwa kuna uwezekano kwamba aliyekuwa Mgombea Urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, anaweza asitinge 'Mjengoni' kwa viti maalum basi nitatumia nafasi mojawapo kumteua awe Mbunge. Huyu 'vipande' alivyonipa - pamoja na Ilani ya chama chake inayogusia ajenda yangu ya kujenga viwanda - vinaonesha ana ujasiri wa kutosha kuisimamia vilivyo Serikali yangu Bungeni.
Hiyo ndiyo 'sampuli' ya 'majembe' ambayo ningeyateua. Ila kwa bahati nzuri/mbaya mimi siyo Magufuli. Hivyo, namwachia uwanja wake wa Kikatiba atimize ahadi yake ya kuja na timu kabambe.

Ahadi ni deni. "Sitawaangusha," ulituambia. Usituangushe.

2 comments:

Myanguzi Wakisa November 2, 2015 at 3:36 PM  

Ha ha ha chambi. haya maoni yako yanachekesha kweli. umecheza kuzunguka watu unaowajua wewe DSM, ukifikiri Tanzania ni DSM tu na UDSM. Wapo Watanzania wengi wanaofaa kuiongoza nchi hii, siyo lazima turudishe watu maarufu. Nani aliyekuwa anamjua mhongo kabla JK hajamteua? Magufuli ANAHITAJI KUVUKA MIPAKA TULIYOIZOEA KUHUSU SIASA ZA UTEUZI

Chambi Chachage November 2, 2015 at 5:08 PM  

Asante Myangusi Wakisa. Hiyo ni sampuli tu. Muhongo mimi nilikuwa namjua kabla. Alianza hapo hapo UDSM - Idara ya Jiolojia.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP