Wednesday, January 13, 2016

Athari za Muda Mrefu za Mapinduzi ya Zanzibar

Athari za Muda Mrefu za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

Chambi Chachage

"Kasha lililofungwa ni vyema lifunguliwe watu wajuwe kilichomo" - Ripoti ya 'Hali ya Kisiasa na Kijamii Tanzania na Uwezekano wa Kupatikana Amani ya kweli Zanzibar'
--- 

Nilipokuwa shule ya msingi Mlimani nilifundishwa kuhusu mapinduzi ya Zanzibar katika somo la Siasa. Mwalimu wangu, Mama Kihongo, alikuwa ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Hizo zilikuwa ni enzi za chama kimoja kushika hatamu.

Kwa muda mrefu sana nimekuwa 'muumini' wa historia hiyo ya mapinduzi. Lakini hiki kilichotokea jana katika maazimisho ya miaka 52 ya mapinduzi hayo kimenifanya nikumbuke kile ambacho kijana mmoja aliwahi kuniambia nilipokuwa Zanzibar. Alinishauri nifuatilie jinsi jamii ilivyogawanyika kuhusu athari za mapinduzi.

Alichokuwa anamaanisha ni kwamba hadi leo kuna watu ambao wana hofu kutokana na mapinduzi hayo kufanywa ni suala la 'weusi' wanaojiona wao ndiyo 'waafrika' dhidi ya wasio 'weusi' wanaoonwa - au kujiona - kuwa ni 'waarabu' ama 'waajemi'. Hapo katikati wanaangukia hao ambao eti leo wanaitwa 'machotara', yaani, wanaonekana kuwa siyo 'weusi' wa kutosha kuwa 'Waafrika' wala siyo 'weupe' wa kutosha kuwa 'Waarabu' na 'Waajemi'.

Wanahistoria wa uchumi wana kitu wanakiita 'matokeo au athari ya muda mrefu' ya tukio' fulani. Hutumia kanuni na mbinu mbalimbali za kitakwimu kupima jinsi athari/matokeo, kwa mfano ya ukoloni na utumwa au ubaguzi uliotokea zamani, yanavyoendelea tu kwa muda mrefu hadi leo katika jamii iliyokumbwa na matukio hayo.

Labda huu sasa ni wakati mwafaka wa kuangalia kwa kina matokeo/athari chanya na hasi za muda mrefu za mapinduzi. Hii itatusaidia kujua ni namna gani tunaweza kutatua 'mkwamo wa kisiasa (na kiuchumi)' visiwani Zanzibar. La sivyo tutaendelea kubaki kwenye mataruma hayo hayo ya reli pale tulipokwamia.

Jambo mojawapo muhimu lililotokea mwaka 1964 ni kuundwa kwa 'Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.'  Lakini hii haikuwa jamhuri ya kawaida tu kama ile ya Tanganyika iliyopatikana mwaka 1962. Hii Ilikuwa ni ya kimapinduzi kama ile iliyoundwa nchini Cuba baada ya mwaka 1959. Ndiyo maana uongozi wake wa juu wa Serikali ulikuwa chini ya 'Baraza la Mapinduzi'. Hakukuwa na fursa kwa yeyote ambaye siyo 'mwanamapinduzi' kuwaongoza Wazanzibari.

Hivyo, vyama vilivyojulikana kama Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Pemba People's Party (ZPPP) havikuwa na nafasi ya wazi tena katika medani ya siasa. Kwa nini? Kwa sababu vyenyewe ndivyo ambavyo viliunda 'serikali' ilipinduliwa baada kuungana na kushinda uchaguzi wa mwaka 1963 ulioipa Zanzibar 'uhuru' ambao haukotofautiana sana na ule iliyoupata Tanganyika mwaka 1961. Angalau kulikuwa na mwanya kidogo kwa wanachama wa UMMA Party kujitutumia kisiasa. Lakini hata hiki chenyewe kililazimika kujivunja na 'kujiunga/kumezwa' na chama pekee, yaani Afro- Shirazi Party (ASP), katika mfumo mpya wa chama kimoja.
Uhalali wa iliyokuwa Serikali ya Zanzibar ya mwaka 1963 ni suala ambalo limewagawa wakazi wa Zanzibar japo haliongelewi sana kwa uwazi kutokana na hofu ya kuonekana unapinga 'Utukufu' wa Mapinduzi. Kitu kilichonishangaza hivi karibuni wakati natafiti historia ya kuundwa kwa iliyokuwa Jumuiya ya Kuiunganisha Afrika, yaani Organization of African Unity (OAU), mwaka 1963 ni uwepo wa Zanzibar kama mwanzilishi mmojawapo. Ilikuwaje (Serikali ya) Tanganyika ikalikubali hilo litokee wakati huo?

Inaonekana bado kuna uhusiano mkubwa kati ya Zanzibar ya mwaka 1963 na Zanzibar ya leo. Tatizo tunalolipata ni kudhani Zanzibar iliyoundwa ('upya') mwaka 1964 inaweza kuendelea leo bila mabadiliko makubwa ya mfumo wa serikali yatakayotatua kile ambacho kilijaribiwa kutatuliwa kwa mapinduzi. Kilichoundwa wakati huo kiliundwa (zaidi) kwa ajili ya 'waumini' wa mapinduzi.

 Zanzibar pia ina watu (wema) ambao siyo waumini wa mapinduzi. Hatuwezi kuwaita 'wahaini'. Wao wanachoamini ni kwamba labda kama mapinduzi hayo yasingetokea basi Zanzibar ingefuata nyayo kama za Tanganyika iliyopata uhuru ikiwa na Waziri Mkuu chini ya Malkia kisha baadaye ikapata Jamhuri yake chini ya Rais. Japo hatuwezi kujua kwa uhakika nini hasa kingetokea, kuna uwezekano kuwa Zanzibar iliyopata uhuru ikiwa na Waziri Mkuu chini ya Sultani nayo baadaye ingeweza kuwa Jamhuri chini ya Rais hasa ukizingatia zote mbili zilipata 'uhuru' wao kutoka kwa Uingereza.

Mapinduzi yalijaribu kuliharakisha hilo mwaka 1964. Mwisho wake ilichokiita 'Jamhuri ya Watu wa Zanzibar' ikawa chini ya 'Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)' badala ya 'Serikali ya Watu wa Zanzibar'. Sasa iweje leo tudhani kwamba itakuwa kazi rahisi tu kwa watu wasioonekana kuwa na 'mamlaka' ya 'kuyalinda' mapinduzi hayo japo nao ni Wazanzibari watoe Rais wa Zanzibar?
Tukubali kwamba hata muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) nao haujafanikiwa vilivyo kuondoa kiini hicho kikuu cha tatizo, yaani, ulazima wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mapinduzi. Ili kulielewa suala hili ni vyema mtu akajiuliza hivi huko Cuba kwa sasa kuna nafasi ya mwanasiasa au chama chochote ambacho sicho kilicholeta mapinduzi kutwaa madaraka na kuiongoza nchi hiyo?

Profesa Chachage na watafiti wenzake waliwahi kuichambua 'Hali ya Kisiasa na Kijamii Tanzania na Uwezekano wa Kupatikana Amani ya kweli Zanzibar' mwaka 2006. Baada ya kuirejea historia ya mapinduzi na matokeo yake ya baadaye, walizungumzia suala hili linalosaidia kuelewa kwa nini sakata la Chama Cha Wananchi (CUF) na CCM linatokana na tafsiri kinzani kuhusu Mapinduzi:

"Kwa mfano, kuna kundi linahusisha Mapinduzi ya Zanzibar na ukabila yaani kwamba yalihusu weusi kuuangusha utawala wa waarabu na marafiki zao. Kundi hili linahoji uhalali wa mapinduzi na kudai kwamba matatizo yote ya Zanzibar yanatokana na Mapinduzi ambapo kuna watu wa kabila fulani walinyang'anywa mali zao (ardhi, majumba, n.k.) na wengine kupoteza maisha. Kwa upande mwingine kuna kundi ambalo hupinga msimamo huu kwa kejeli kwamba wenzao wanataka kurejesha utawala wa Kiarabu ambao ulikuwa wa kinyonyaji na kibaguzi dhidi ya Waafrika na Washirazi wa Zanzibar. Hapa utengano mkubwa umetokea. Kuna wanaopinga Mapinduzi na wanaotetea Mapinduzi kwa kila hali. Wanaodaiwa kupinga mapinduzi wanaonekana hawana ajenda nyingine yeyote isipokuwa kuvunja muungano na kurudisha utawala wa kiarabu!"
Chachage na wenzake wanaendelea kuelezea hivi mgongano huo:

"Kwa hiyo pande hizo mbili ndizo zimekuwa zikipima ni nani ni mwenzetu na nani siyo mwenzetu. Hii imepelekea kubagua watu ambao wanaonekana siyo wenzetu wasishiriki katika mambo ya kitaifa yawe ya kiuchumi au ya kisiasa. Matokeo yake ni kwamba katika jamii ya Zanzibar sasa hivi kuna kiwango kikubwa sana cha kutoaminiana baina ya viongozi wa vyama vikubwa vya siasa nchini humo pamoja na wafuasi wao. CCM inaonekana ni ya Unguja na inajiona kuwa ni mlinzi wa Mapinduzi na Muungano bila kuthibitisha hilo kwa vitendo vinavyowaongezea wananchi maslahi; na CUF inaonekana ni ya Pemba na inajiona yenyewe inabaguliwa na ina jukumu la kurejesha demokrasia, haki na kuboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar."

Baada ya maelezo hayo ya kina akina Chachage wanakiri kwamba:

"Ni kweli, kwa mfano, kwamba uwiano wa kiuchumi kati ya Unguja na Pemba siyo mzuri. Pamoja na kwamba hali ya Unguja kiuchumi siyo nzuri pia lakini ni kweli kwamba hali ya Uchumi na maisha ya Pemba ni duni kuliko ile ya Unguja. Watu wametumia hili kuonesha kwamba Pemba inabaguliwa kwa makusudi na wale walio madarakani - CCM. Zimekuwepo hisia pia kwamba Wapemba wanabaguliwa eti kwa sababu hawakushiriki katika mapinduzi. Kwa kuwa CUF ina nguvu zaidi Pemba nao wamefanikiwa kutumia ukweli huu kama mtaji wa Kisiasa. Sababu za kutokuwa na uchumi mzuri na miundombinu pia inatajwa kwamba imewafanya wapemba wasiwekeze Pemba ndio maana wanakimbilia kuwekeza na kufanya biashara, Unguja, DSM [Dar es Salaam], Tanga, na kwingineko. Kuna kauli kwamba ni aibu kwa Mpemba kuwa mwanachama wa CCM. Mpasuko huu unawafanya wale ambao wanaona mapinduzi yalikuwa halali kuamua kuwatenga hawa kama kundi linalopinga mapinduzi."
Sasa inabidi tukubali kwamba mapinduzi yalishatokea. Hatuwezi kurudisha nyuma gurudumu la historia. Ila tunapaswa pia tukubali kwamba kile ambacho mapinduzi yalikiahidi kuhusu demokrasia pana hakikuweza kutimia (kikamilifu) wakati wa mfumo wa chama kimoja na hayawezi kukitimiza katika mfumo wa vyama vingi ambapo sivyo vyote ni vya '(ki)mapinduzi'. Ahadi hizi za kihistoria ambazo timu ya utafiti ya Chachage imeziainisha kwa hitimisho lifuatalo zinaweza kutusaidia kuelewa kwa kina kwa nini mfumo mzima wa SMZ inabidi ubadilike ili kutoa fursa kwa Wazanzibari wote kuwa na fursa sawa ya kuongoza dola bila misingi ya nafasi yao ama ya wazazi wao katika (historia ya) mapinduzi bali msingi mkuu wa uzalendo wao kwa Zanzibar kisiasa, kiuchumi na kijamii:

"Hakuna ubishi kwamba hatua zilizochukuliwa na serikali ya Zanzibar zilikuwa kwa maslahi ya Wazanzibari wote. Hata hivyo itakuwa makosa kukataa ukweli kwamba kulikuwa na matatizo ambayo ndiyo msingi wa kile kinachoitwa leo migogoro ndani ya jamii ya Wazanzibar.... Hali halisi ya Zanzibar inatupa picha tofauti kwani usawa na haki ambavyo vilikuwa vimelengwa na Mapinduzi ya Zanzbar bado ni ndoto. Tunapaswa kukubali kwamba Mapinduzi hayakukamilika au kuna mambo ambayo hayakufuatiliwa na yakapotosha nia nzuri ya mapinduzi ya kujenga jamii sawa na huru. Hali ya sasa ya kiuchumi na kisiasa nchini Zanzibar ni ushahidi tosha kwamba uhuru na usawa haupo na hicho ndicho kiini kikuu cha matatizo yanayoikabili Zanzibar sasa hivi."

Endapo tutakubaliana na pendekezo lifuatalo walilolitoa Chachage na timu yake miaka kumi iliyopita tutainusuru Zanzibar na kadhia isiyoisha ya kuwagawa Wazanzibari 'kwa mujibu wa mapinduzi':

"Katika kushughulikia suala na tafsiri ya Mapinduzi kusiwe na ulazima wa kuwalazimisha wale walioathirika vibaya na Mapinduzi au ambao hawakuunga mkono Mapinduzi kwamba ni maadui wa Mapinduzi na hivyo kuonekana kwamba wanakosa uzalendo na utaifa. Anayekubali Mapinduzi akubali na anayeyakataa ayakatae kwa sababu zake mwenyewe. Kama ilivyokuwa watu hawalazimishwi katika kuabudu na hili suala la kutukuza au kubeza Mapinduzi libakie katika uhuru wa mtu binafsi [Kwa mfano si busara kumlazimisha mtu aliyeuliwa baba yake asiyekuwa na hatia au aliyteswa wakati wa Mapinduzi na baadaye abadilike ayatambue Mapinduzi na kuyatukuza. Kufanya hivyo ni kuwalazimisha watu wawe wanafiki kusema kile wasichokiamini.]"
Dhana hiyo ya 'uhuru wa kuamini' itatekelezeka pia kama hili pendekezo lao lingine litatekelezwa na hata kutumika kama msingi wa kuwa na Serikali ya Mpito kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020:

"Kuundwe Tume ya Ukweli na Upatanishi (Truth and Reconcilliation Commission) kama ile ya Afrika Kusini ili watu waondoleane kinyongo kwa yale yaliyopita nyuma na waanze ukurusa mpya wa ushirikiano na upendo katika jamii. Katika muundo wake, Mwenyekiti na Katibu wa Tume wasiwe wanachama wa Chama chochote, Wawe ni watu wenye sifa za kitaalamu, wenye wasta na uadilifu wanaokubalika na pande zote zinazopingana katika jamii."

 Rohoni tujiulize: Je, kitu kitukufu ni kitakatifu, hivyo, hakiwezi kubadilishwa muundo wake na maana yake ili kiendane na wakati hata inapobidi kufanya hivyo haraka ili kunusuru roho za watu? 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP