Saturday, January 2, 2016

‘Mateknokrati’ na ‘Fomesheni’ ya ‘Timu Magufuli’


Uteuzi wa ‘Mateknokrati’ na ‘Fomesheni’ ya ‘TimuMagufuli’

Chambi Chachage


Timu kabambe ya Makatibu Wakuu wa Wizara imetangazwa. Hawa watasaidiana na Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli. Wadadisi wa mambo wanakiri kwamba hii ni Serikali iliyojaa ‘mateknokrati’ kuliko ya awamu zote katika historia ya nchi yetu. 

Kwa tafsiri nyepesi ya kikamusi, tunaweza kusema ‘mateknokrati’ ni kundi la watu wachache waliobobea sana kitaaluma ama kiufundi. Hivyo, utawala au utendaji wa Serikali unaosimamiwa vilivyo na ‘wateule’ hao huitwa ‘teknokrasia.’ Vinara hao inasemekana huwa wanajikita zaidi katika vitendo kuliko nadharia na tafakuri.

Profesa Issa Shivji anatakumbusha kwamba wanaotekeleza majukumu ‘kiteknokrati’ hawafanyi kazi wakiwa kwenye ombwe la kiitikadi na kinadharia. Anachomaanisha ni kwamba hata maprofesa, madaktari na wahandisi waliosheheni katika Serikali ya Awamu ya Tano wana fikra na mitazamo inayowaongoza katika yale wayatendayo.
Hii ina maana watakapokuwa wanatekeleza kaulimbiu ya Rais Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”, watafanya hivyo kwa kufuata mwelekeo fulani. Hata ‘mashine’ hufuata mwelekeo au maelekezo. Swali la kujiuliza ni, je, (watakuwa) wanafuata mwelekeo upi hasa? Wao binafsi au wa mkuu wao wa kazi ama mchanganyiko wa yote mawili? 

Na, je, ni nini utakuwa msingi mkuu wa mwelekeo huo? Je, ni ilani ya chama tawala na sera pamoja na sheria za nchi? Hizo nazo huwa zinatungwa kwa mtazamo gani? 
Tuitazame, kwa mfano, migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji inayoibuka mara kwa mara kama ilivyotokea Mvomero hivi karibuni. Tunaona Rais amemteua aliyekuwa mwanaharakati wa ‘HakiArdhi’, Mwanasheria William Ole Nasha, kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi. Msimamo wake kuhusu haki za za ardhi kwa wazalishaji wadogo wadogo iko wazi kwenye majadiliano na makabrasha yake.

Lakini pia, labda awe amebadilika sasa, Mbunge huyo wa Jimbo la Ngorongoro ni muumini wa uwepo wa ‘maeneo ya umma’ (The Commons), kama malisho, ambayo waumini wa ‘mali binafsi’ wanadai yakibinafsishwa, hasa kwa wawekezaji wakubwa, kunakuwa na uzalishaji wenye tija. Hivyo, azma ya Serikali ya kutaka fukwe ziwe wazi kwa watu wote inaendana na mtazamo wake kuhusu ‘rasilimali za pamoja’.
Mbobezi mwingine wa masuala hayo ni Profesa Sifuni Mchome. Tasnifu yake ya Uzamivu (PhD) ilijikita katika kutazama nafasi ya sheria katika kusababisha na/au kutatua migogoro ya ardhi. Utafiti huo ulijikita katika migongano mbugani Mkomazi.

Alipoteuliwa na Serikali ya Awamu ya Nne kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu tupo tuliojuliza kwa nini hakupelekwa Wizara ya Ardhi. Lakini tukajiambia, maadam uprofesa unahusiana na elimu, hewala tu. Safari hii walau amesogezwa karibu zaidi kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Hapo kuna fursa ya kuhakikisha kuwa Ardhi inakuwa suala la Kikatiba ili kudhibiti ukiukwaji wa haki.

Changamoto kubwa ni kwamba Ardhi ni suala mtambuka, yaani, linalogusa Wizara zaidi ya moja. Na miingiliano hiyo huweza kuchochea migogoro hasa pale Serikali inapokuwa imejikita katika mwelekeo wa uwekezaji na ujenzi wa viwanda. Hivyo, kuna kazi ya ziada ya kuoanisha mitazamo ya ‘mateknokrati’ wa Wizara kadhaa.
Ili kulielewa hili suala kwa undani tuanze na mfano unaohusu wakulima wanaodaiwa kusababisha kupungua kwa maji kwenye mabwawa ya kuzalishia umeme. Tunakuta Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na wenzake, yaani, Dakta Medard Kalemani (Naibu Waziri), Profesa Justus Ntalikwa (Katibu Mkuu),
Profesa James Mdoe (Naibu Katibu Mkuu) na
Dakta Paulina Pallangyo (Naibu Katibu Mkuu). Hawa wanajua mgawo wa umeme usipoisha wataonekana hawajafanya kazi vilivyo.

Uhakika huo ndiyo ambao Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na wenzake – Dakta Adelhem Meru (Katibu Mkuu - Viwanda),
 Profesa Adolf Mkenda (Katibu Mkuu - Biashara na Uwekezaji)
 na Mhandisi Joel Malongo (Naibu Katibu Mkuu) – wanautaka ili kuleta ‘mapinduzi ya viwanda’ aliyoahidi bosi wao. Bila hilo si wawekezaji watalazimika kubwaga manyanga ama kuutafuta kwa taabu kama anavyohaha Aliko Dangote nakiwanda chake cha saruji cha Mtwara?
Viwanda, hasa visivyo vya ‘kijani’, huharibu mazingira na hewa ya ozoni. Ila ufugaji wa mifugo mingi na ukulima kama huo wa kwenye vyanzo vya maji huleta huo uharibifu na kuchochea mabadiliko hasi ya tabia nchi. Hivyo, itawalazimu Waziri January Makamba na Naibu Waziri Luhaga Mpina kwenye ‘Ofisi ya Makamu wa Rais: Wizara ya Muungano na Mazingira’, pamoja na Mbaraka Wakili (Katibu Mkuu) na
 Mhandisi Ngosi Mwihava (Naibu Katibu Mkuu), wajitokeze na hoja zao.

Bado kuna Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge pamoja na wenzake – Mhandisi Isack Kamwela (Naibu Waziri), Mhandisi Mbogo Futakamba (Katibu Mkuu)
na Mhandisi Kalobero Emmanuel (Naibu Katibu Mkuu) – ambao nao watahitajika kuhakikisha kuwa wakulima wanapata maji ya kumwagilia ili wazalishe chakula cha kutosha kuwalisha watakaokuwa wamekimbilia kufanya kazi viwandani. 
Sasa itakapobidi kuwapunguza au kuwasogeza wafugaji na wakulima kutoka kwenye vyanzo vya maji ili umeme uzalishwe, wawekezaji wafanikiwe na kuwe na mazingira mazuri hapo ndipo Ole Nasha na wenzake – kina Mwigulu Nchemba (Waziri), Dakta Florence Turuka (Katibu Mkuu - Kilimo), Dakta Mashingo (Katibu Mkuu - Mifugo) na Dakta Budeba (Katibu Mkuu - Uvuvi) – watafute namna ya kuzuia migogoro.

Je, ardhi mbadala ya kuwasitiri itatoka wapi? Kwenye mbuga za wanyama, vitalu vya uwindaji, hifadhi za taifa na maeneo mengi yalihodhiwa na dola kwa ajili ya masuala ya namna hiyo? Wenzao kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo inasemekana kuwa sasa inaiingizia sana Serikali mapato – wakina Profesa Jumanne Maghembe (Waziri), Mhandisi Ramo Makani (Naibu Waziri), Meja Jenerali Gaudence Milanzi (Katibu Mkuu)
na Angelina Madete (Naibu Katibu Mkuu) – wataridhia yamegwe?

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya William Lukuvi (Waziri), Angelina Mabula (Naibu Waziri), Dakta Yamungu Kayandabira (Katibu Mkuu) na
 Dakta Moses Kusiluka (Naibu Katibu Mkuu), italichukuliaje suala hilo? Kama lile sakata la kubomoa nyumba na makazi ya watu wanaoishi mabondeni n.k? 
Orodha ni ndefu lakini mfano huo wa ‘maji’ unatusaidia angalau kujua kwamba ‘uteknoktrati’ wa ‘Timu Magufuli’ utahitajika kuchekecha na kuchuja vipaumbele na vigezo vingi vya kinadharia na kimtazamo, achilia mbali kiutendaji na kiusimamizi, ili kuhakikisha kuwa kuna uwiano na ufanisi. Timu yoyote ikiwa na mikingamo au miingiliano mingi ya ‘kiteknokrati’ ni rahisi kupata tu ‘mafanikio ya kutofanikiwa’.

Dawa ya kuhakikisha kuwa ‘hatufanikiwi kutofanikiwa’, yaani ‘kupiga hatua moja mbele na mbili nyuma’, ni kuwa na ‘falsafa’ na ‘mfumo’ thabiti ya kitimu. Kwenye mchezo wa mpira wa miguu, kwa mfano, huwa kuna ‘fomesheni’ kadhaa za kupanga wachezaji 11 uwanjani. Hizo zinaangalia uwian wa mabeki wa pembeni, mabeki wa kati, viungo wakabaji, viungo washambuliaji na washambuliaji wa mbele wangapi. 

Zinatosha kuleta ushindi? La hasha! Ni ‘tekniki’ tu. Ili zifanikiwe lazima ziendane na mfumo mzima za timu husika. Kama mfumo ni kujihami basi mbinu ya ‘kujaza basi’ la mabeki watano golini kumlinfs kipa wao asifungwe kwa kutumika ‘fomesheni’ ya 5-3-2 inafaa. Lakini kama mfumo ni kujilinda kwa kushambulia bila simile basi 3-4-3 itafaa au hata 4-4-2 kama ina viungo washambuliaji. Mfumo fulani unaposimikwa ndipo timu inapojulikana kwa falsafa au itikadi yake ya kiuchezaji na kiushindani.
Florentino Perez aliyekuwa Rais wa timu ya soka ya Real Madrid alisajili kikosi cha ‘mafundi’ wa ‘mitindo’ anuwai ya kusakata kabumbu. Mashabiki walikibatiza jina la ‘Galacticos’ wakimaanisha kiwango chao si cha hili anga letu. Kilikuwa na bingwa wa kupiga chenga ya kuwazunguka mabeki iliyobodi ijulikane kama ‘La Roulette de Zidane’. Pia kilikuwa kinara wa kupiga mabao aliyefananishwa na tukio la ajabu na hivyo kupachikwa jina la ‘Il Fenemono Ronaldo’. Ila kilipata taabu kucheza kwa mfumo wa pamoja ukilinganisha na wapinzani wao wa jadi, Barcelona, watumiao mtindo wa ‘Tiki Taka’ uliojikita katika ushirikiano wa kitimu kuliko umahiri binafsi.

Gundi ya kuwaunganisha pamoja ‘Galacticos’ wa ‘Timu Magufuli’ inapatikana(je)?

2 comments:

Pascal Bacuez January 2, 2016 at 11:09 AM  

Naomba kuchangia hapo kwa machache tu kwa kuwa mimi ni mgeni wa ugenini. Makala yako imenipendeza sana kwa kuwa imesisitiza tatizo kubwa mojawapo ambalo litawakumba Watanzania katika enzi hizo za usoni, yaani migogoro baina ya watu wenye maslahi tofauti. Mapaparazi wa Tanzania wangekuwa na upeo wa fikra wa kusoma kinachoendelea duniani, wangejua kwamba balaa kubwa imeshaanza kupiga hodi kwenye milango ya Tanzania. Asia na Uarabani kote balaa hizo — ukame, uchafuzi wa vyanzo vyote vya maji, ukosefu wa maji safi, utele wa tindikali katika mazingira, moshi wa kila wakati katika miji mikubwa, kufyekwa kwa misitu yote, kutoweka kwa viumbe wote, na kadhalika… Sijasikia tangu zamani sana mwana siasa yeyote Afrika (isipokuwa hivi karibuni rais wa Rwanda mheshimiwa Kagame) ambaye amekubali kulisakata ishu hilo la Uzazi wa mpangilio !! au ishu hilo lilikuwepo katika kampeni ya Mheshimiwa Pombe ?… lakini hayo ni maoni ya kizungu, kwa hivyo napita na zangu ! Wa salaam.

Anonymous January 4, 2016 at 12:54 AM  

Tatizo la Nchi hii ni viongozi kukosa Vipaumbele vyenye maono au mlengo mmoja. Ngoja tuone kama uchakataji wa awamu hii utakua sawasawa

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP