Monday, January 18, 2016

Ngoswe Hatunaye? Kwaheri Ndugu Edwin Semzaba

Hivi karibuni nilikutana na jirani yetu wa zamani wa Ubungo Flats, Ndugu Edwin Semzaba. Nikajiuliza mara mbili mbili nimsalimie au 'nimpotezee' maana alikuwa hanifahamu kwa sura kwa kuwa aliniona ningali nikiwa mdogo. Moyoni nikajiambia ni vyema kuwashukuru waandishi ambao uandishi wao umetugusa. Hivyo, nikamkumbusha na kumjulisha kwamba nilipokuwa sekondari nilisoma kitabu chake cha 'Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe'
Lo, kumbe ilikuwa ndiyo buriani. Mwandishi huyo mahiri sasa ametutoka. Tutamkumbuka kwa kuweza kutufundisha, kwa namna yake, kuhusu umuhimu wa 'hapa kazi tu' hata pale ambapo penzi limekolea na hata kutishia kutupofusha. Kitabu hicho cha Ngoswe kiliwahi pia kujulikana kama 'Hesabu Iliyoharibika' kwa kuwa kijana huyo msomi alipoteza madodoso aliyoyatumia kukusanya takwimu za wakazi mbali mbali wakati wa Sensa ya Taifa. Sakata hili ilitokea alipojaribu kutoroka na Binti wa Mzee mmoja (kama sikosei Mwenyekiti) wa kijiji alichofikia. Hakika alifanya kosa la kuvunja maadili ya utendaji, yaani, kuchanganya 'penzi' na 'kazi'.
Lakini pia kitabu hicho kilitufundisha umuhimu wa wazazi (wenye upendo mkubwa) kutoyaingilia kati mapenzi ya watoto wao kwa jazba na ukali. Busara ingetumika zaidi inawezekana takwimu za sensa zingesalimika. Pengine ingepatikana namna ya kuipatanisha 'kazi' na 'penzi' ili angalau Serikali yetu isipoteze taarifa muhimu za kuwasaidia wananchi wake na nguvukazi ya kulijenga taifa letu. Hilo hakika lilikuwa fundisho tosha kwetu kuhusu uadilifu kazini na uhakika wa takwimu tunazozikusanya ambazo siku za hivi karibuni zimehojiwa kwa kina na mtafiti aitwaye Morten Jerven.
Tuwashukuru waandishi wetu wangali hai. Wakitutoka tuendelee kuzienzi kazi zao. Asante Edwin Semzaba. Ngoswe atasomeka.

1 comments:

Moderator January 18, 2016 at 10:46 AM  

Inasikitisha kuona jinsi wakiwa hai thamani yao isivyotambulika, magwiji wa fasihi andishi kama hawa, na wasanii wengine nguli. Tumuombee kwa Mungu, na tuzidi kuenzi na kuthamini kazi zake.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP