Wednesday, February 10, 2016

Kutatua Migogoro ya Wakulima na Wafugaji

MAPENDEKEZO YA KUTATUA MIGOGORO YA BAINA YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

- Mipango ya matumizi bora ya ardhi izingatie mahitaji ya wazalishaji wote. Mathalani huwezi kutenga eneo au kijiji cha wafugaji halafu ukakitenga na maeneo yaliko maji kwa ajili ya mifugo. Katika hali kama hiyo mifugo itafuata maji tu na hapo ugomvi utatokea.

- Wapo waliopendekeza haja ya kukuza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kuwa na idadi ndogo ya mifugo lakini yenye ubora mkubwa; na haja ya kuwekeza katika miradi ya uboreshaji wa malisho ili kuhakikisha kuwa wakati wote kuna malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo.

- Kuhusu ranchi na mashamba yote yaliyobinafsishwa katika wilaya ya Kilosa lakini wale waliopewa hawajayaendeleza kwa muda mrefu, ulitolewa wito kwa serikali kuzitwaa ranchi na mashamba hayo na kuyagawa kwa vijiji ambavyo tayari vimeonyesha kuwa vina mahitaji, uwezo na utayari wa kuyaendeleza. Hii pia itasaidia kutatua baadhi ya migogoro inayotokana na uhaba wa ardhi kutokana na kuhodhiwa na wachache.

- Aidha, ilipendekezwa na kusisitizwa kuwa mazungumzo huru na ya wazi ni jambo muhimu sana. Na ndio baadhi ya misingi ambayo kwayo nchi yetu ilijengwa na waasisi wa Taifa letu. kutokana na umuhimu wa mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji wao kwa wao ilipendekezwa kuanzishwe kamati ya wilaya ya Usuluhishi na Maridhiano baina ya wakulima na wafugaji. Kamati hiyo itokane na iwe na uwakilishi toka pande zote za wazalishaji wadogo wadogo, yaani wakulima na wafugaji.

- Suala la kubaguana kikabila si jambo jema na lazima kwa pamoja lipingwe na kulaaniwa kwa nguvu zote. Aidha ikasisitizwa kuwa ni wajibu wa kila mshiriki katika mkusanyiko ule, na kila Mtanzania kupinga na kulaani hadharani pale anaposikia mtu au kiongozi yeyote analeta hoja za kuwabagua na kuwatenga watu kwa makabila au dini zao.

CHANZO:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP