Saturday, February 20, 2016

Ranchi:Suluhu ya Migogoro ya Mfugaji & Mkulima?

Yafuatayo ni maoni yatokanayo na mjadala wa Wanazuoni wanaotafiti masuala ya ardhi kuhusu Tangazo la kujenga ranchi ili kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji. Maoni hayo yalitolewa kabla ya Tangazo kuhusu kupima ardhi yote nchini na Tangazo ;a kurudishwa kwa ardhi ambayo haijaendelezwa. Licha ya hayo, Udadisi inaamini maoni haya bado yana umuhimu.
---


Tatizo solutions zinazotakiwa zipo political, kiasi kwamba utekelezaji wake uta-challenge na utabadili status quo. 

Na kwa upande mwingine, sidhani kama Tanzania ina uhaba wa mapendekezo ya wasomi/wanazuoni katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaendeleo. Tatizo lipo kwenye utekelezaji wa hayo mapendekezo; kama nilivyosema hapo juu, utekelezaji wake utaleta mtikisiko.

Kwa mfano, mara ngapi tumesoma pendekezo la upimaji wa ardhi kwa nchi nzima ili kuweka matumizi na mipango bora ya utumiaji wa ardhi? Kama nakumbuka sahihi, sidhani kama ardhi ya Tanzania imepimwa kwa zaidi ya asilimia 20. Tibaijuka alipokuwa ardhi walianzisha mpango wa upimaji wa kutumia GIS/Remote sensing, sijui uliishia wapi? Lakini pengine kisingizio kinaweza kuwa uhaba wa pesa. Uhaba wa pesa nayo ni moja ya hizo simplistic narratives. 

Benjaminsen, Maganga na Abdallah katika andiko lao la mwaka 2009 wameeleza kwa hali ya juu kuhusu tatizo la mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Wameeleza kile nilichokisema juu ya namna gani wafugaji wanaonekana 'wakorofi' na 'waharibifu wa mazingira' hivyo kuwekwa 'pembeni' kinamna fulani huku wakulima wakiwekwa 'juu' zaidi. Vile vile wameongelea juu ya tatizo la rushwa na utawala bora, kiasi kwamba wafugaji pamoja na wakulima wanakuwa hawana imani na vyombo vya kisheria na haki, na kupelekea kuchochea migogoro zaidi, kwani kupigana ndiyo inakuwa njia wanayoiona inafaa. Wameeleza jinsi uongozi wa kiserikali unavyoshindwa kukabiliana na tatizo husika. 

Wakaenda mbele na kutoa baadhi ya namna ya kusuluhisha: kuboresha taasisi za usimamizi wa maliasili katika ngazi za vijiji. Hizi taasisi lazima ziwezeshwe kifedha na rasilimali watu na serikali ili ziweze kuwa na uwezo wa kutatua migogoro. Wamesema pia juu ya ulazima wa kubadili mtazamo hasi juu ya wafugaji, kwani mitazamo huchangia sana namna sera zinavyotungwa na matatizo yanavyosuluhishwa. Sasa ukiwa na mtazamo hasi juu ya wafugaji, ina maana hata sera na masuluhisho hayataleta manufaa bali yataleta matatizo zaidi, haswa kwa wafugaji. N.K.

Hilo ni andiko la mwaka 2009, lakini mpaka kesho migogoro Kilosa haijaisha. Sasa sijui hata kama watu wa wizarani wamesoma hilo andiko! 

Kwa hiyo... mimi kwa upande wangu sidhani kama kuna uhaba wa mapendekezo ya kutatua matatizo haya. Shida ipo kwa mtekelezaji: wasomi-watafiti ni kama marefa, wanachezesha mchezo kati ya serikali na wananchi, lakini hawawezi kucheza wenyewe katika timu yoyote kati ya hizo mbili. Ni wajibu wa serikali ama wananchi kucheza kutokana na miongozo ya marefa. Unaweza kuwa siyo mfano wa moja kwa moja lakini unaweza kutoa picha ya kwamba wasomi-watafiti wana limit katika kile ambacho wanaweza kufanya katika kuhakikisha vile wanavyovipendekeza vinatekelezwa. Labda kama waamue kuwa wanaharakati, kama baadhi ya wasomi walivyoamua kuwa.

Ni hayo tu. Ingawa hili suala linahitaji mjadala wa kitaifa, kama mambo mengi ya nchi yetu yanavyohitaji mijadala ya kitaifa.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP