Tuesday, February 16, 2016

Wosia wa Mwalimu Nyerere kwa Ndugu Mengi


Dunia imegawanyika hivyo sehemu ya wakubwa wana nguvu za uchumi na wanaitumia kuendeleza nguvu hizo. Nilisema Ndugu Kaunda alijaribu kuacha Coca-Cola nikamwambia : ‘‘Sasa utafanyaje?’’ Alisema: ‘‘Mwalimu, tunaanza mtambo wetu pale wa vinywaji vya nyumbani, unaweza kufanikiwa.’’ Nikamwambia: ‘‘Ken, huwezi… huwezi kwa sababu wako Wazambia pale watakuletea taabu kwelikweli.’’ Nimeambiwa jana kwamba nadhani sasa Coca-Cola watarudi. Wamesharudi kwa sababu sasa mapambano hayo dhidi ya ukoloni mamboleo si rahisi. Ndugu Mengi, ni magumu zaidi kuliko mapambano dhidi ya ukoloni kwa sababu tulipokuwa tukipambana na ukoloni ilikuwa ni rahisi zaidi kuunganisha nguvu za ndani. Ilikuwa rahisi vilevile kwa nchi changa kushirikiana. Kwa Tanzania kushirikiana na India; TANU kushirikiana na KANU, kushirikiana na Indian Congress, kushirikiana na UNIP, kushirikiana na African Congress. Tulikuwa tunaweza kufanya kazi pamoja na marafiki bila tatizo, lakini sio sasa.

...

Kwa hiyo, sisi hapa Tanzania tutakaposema tunataka kiwanda cha Tanzania kiwe cha Tanzania lazima wote tuseme hivyo. Mimi niseme hivyo, Mengi useme hivyo, Patel aseme hivyo, Shomari aseme hivyo. Wote. Lazima iwe ni biashara yetu, lazima … lazima tujenge biashara ya Tanzania. Sisi si watoto wadogo, dunia inabadilika hii bwana. Tumesomesha watu bwana. Kulikuwa kuna wakati tunaweza kusema kijingajinga, lakini sasa tumesomesha watu wote, yani watu wote hawa tumewasomesha. Kazi yetu nyinyi mtujengee tegemezi[?] Sasa nyinyi mtukwamue. Ndio hamuwezi kwenda mnakwenda kwenye Benki ya Taifa tumekupanga kwenye Benki ya Taifa mnakwenda kuomba fedha katika Benki ya Taifa kusudi kutusaidia kujenga uchumi tegemezi, haiwezekani. Mtusaidie kutukwamua. Katika hiyo lazima tuungane wote. Ujumbe namba moja; Somaia unanisikia? … Ndio ujumbe namba moja, hili halina itikadi; Waingereza wanafanya hivyo, wamekuwa wakifanya hivyo. 

...

Tutazidi kuongeza sekta ya umma na kuifanya imara. Sio dhaifu hata kidogo. Lakini sekta ya binafsi ipo tangu 1967 na kabla, sasa fanyeni kazi nzuri lakini tukabiliane na watu wa nje kwa pamoja. Mtu ambaye tutamkataa sisi ni yule ambaye kazi yake yeye ni kutufanya sisi tu ni wafanyakazi wa nchi za Kaskazini. Huyo si mwenzetu hata kidogo. Si mwenzetu, Mengi. Jifanye bepari mzalendo, tutakuunga mkono asilimia mia moja kama bepari mzalendo. Hatutakusaidia, tutapambana nawe kama utajaribu kuifanya nchi hii koloni mamboleo kwa ajili ya mtu mwingine nje ya Tanzania. Tuelewane hivyo. Kuwa bepari, tengeneza fedha, lakini fedha hizo kwa ajili ya Tanzania – kwa ajili ya kujitegemea kwa nchi yetu – lakini tukupe uwanja wa nchi yetu uutumie kutufanya wafanyakazi wa watu wengine, hatukubali hata kidogo. Tutapambana na nyinyi mkiwa namna hiyo. Ndio maana sasa hivi tunasema waziwazi. Tujenge nchi yetu. Hatutaji, katika hali ya kujaribu kuutoa uchumi wetu katika hali hii ya ovyo, tutatumia uwezo wetu wa ndani kwa ajili ya maendeleo, ubepari na ujamaa. Tutazichanganya zote hizi kwa nguvu kabisa kabisa kujenga uchumi wa nchi yetu.

...

Sasa ninasema katika hilo uwezo tunao. Ingawa bado uwezo wa kutengeneza viwanda vyetu wenyewe hatuna, lakini viwanda hivyo tulivyonavyo tuvitumie basi angalau tujitosheleze kwa nguo – kwa mavazi – kwa maana ya mavazi, yaani nguo zenyewe na viatu. Sisi tuna ng’ombe, tuna mbuzi; tunaendelea, watu wazima tunauza ngozi nje, ngozi hasa… tufanye hivyo, maana uwezo tunao, sio wa kutafuta, rasilimali ipo tayari… Mengi, hilo tunaweza tukafanya. 

...

Vifaa vya elimu… vifaa vya elimu. Mengi, si ulianza na kalamu? Sasa tuanze, tutengeneze karatasi. Leo tunatengeneza vifaa vya elimu vinatupa taabu tuna watoto wengi wanaosoma. Tuna watoto wanasoma kama milioni nne. Mimi nadhani kusema kweli tunaweza tukawa na viwanda maalum tu kwa shughuli za vifaa vya elimu. Tunaposema kwamba tunataka watoto wa shule wavae viatu, tunajua viatu vyenyewe vinapatikana wapi? Eh! hivi viatu tu, kusema viatu, sijui watu wana viwanda vyao wenyewe, sijui maduka yao wenyewe? Angalao tuseme, kwa shughuli za shule, tunatengeneza. Hivi yunifomu zinatengenezwa mahali fulani, hizi kalamu madaftari yanatengenezwa mahali fulani. Tufanye hivyo, maana kubwa jambo hili, ni kubwa kwetu; kusomesha watu wetu ni kubwa, na uwezo tunao, sio kwamba hilo nalo tena ni kazi ya kuweza kutegemea Kaskazini. Hivi sasa ni balaa kupata madaftari katika shule zetu. Watoto hawana daftari, walimu hawana ile chaki ya kuandika.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP