Monday, June 20, 2016

Katiba Mpya Kuubadili Mfumo Dhalimu Uliopo?

Tuitazame Katiba Mpya kama Chombo cha kuubadili Mfumo Dhalimu uliopo

Richard Mbunda

(Makala haya yalitolewa katika gazeti la Mwananchi katika ulingo wa Siasa mwaka 2014 wakati mchakato wa uandishi wa katiba mpya unaendelea lakini haikuwekwa katika mtandao. Ni vyema sasa tukaiweka katika mtandao ili iwe rejea ya baadaye)

Mchakato wa kuandika katiba mpya katika nchi yoyote hugubikwa na mivutano inayoashiria kuwepo kwa maslahi ya makundi mbalimbali katika nchi husika. Kundi lolote lililo na maslahi linatambua kuwa, kulala wakati wa uandishi wa katiba ni sawa na ule usemi wa ‘cheka na nyani uvune mabua’. Tunapaswa kutambua kuwa, mivutano hii haina mantiki hasi, kwa kuwa uwepo wa maslahi yanayokinzana kutaifanya nchi kupata katiba nzuri kwa sababu mambo ya hovyo hovyo ni lazima yatapigiwa kelele na kuchujwa.
 Hata hivyo, hapana budi kuwepo kwa uwiano wa maslahi ya vikundi na maslahi ya taifa ili katiba isitumike kutetea maslahi binafsi ya watu wachache au vikundi fulani. Kwa mantiki hiyo basi, uandishi wa katiba unapaswa kuzingatia utaifa zaidi kuliko maslahi ya vikundi.

Matumaini ya Katiba Mpya kwa Makundi Mbalimbali

Wadau wa katiba ya muungano wamekuwa na matumaini mbalimbali. Kwa mfano, katika hotuba yake aliyoitoa kwenye uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba, Rais [Mstaafu]  Kikwete alitanabaisha kuwa kuna makundi yanayodhani katiba mpya, na hasa katika mapendekezo yake ya mabadiliko ya muundo wa Muungano, yangewarahishia kushinda uchaguzi na kushika madaraka ya nchi. Kwa vyama vya siasa, ambavyo malengo yake makuu ni kushika madaraka ya nchi hilo ni tumaini sahihi kwao na wanapaswa kulizingatia ili kulinda umuhimu na uhai wa vyama vyao. Kwa maana hiyo, vyama vya siasa vina haki ya kupigania kuwekwa kwa mifumo sahihi ya kiutawala na usimamizi ili pawepo na ushindani wa haki wakati wa uchaguzi.
Katika mijadala ya katiba, ndani ya Bunge Maalum na hata katika majukwaa tumesikia matumaini ya pande mbili za Muungano katika katiba mpya. Kwa upande wa Zanzibar, tumesikia matakwa yao, kuwa wanataka ushiriki katika medani za kimataifa kama vile kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam, kukopa kimataifa na kudhibiti biashara za kimataifa. Ingawa pia wapo wale wanaodai mamlaka kamili ya Zanzibar katika muungano wa mkataba, madai ambayo, kama yakizingatiwa, yatauweka muungano njia panda.

Katiba mpya imewapa pia watanganyika matumaini ya kufufuliwa kwa Tanganyika yao ili iweze kutetea maslahi yao ndani ya muungano. Wakati huohuo Wazanzibari wangependa Tanganyika ifufuliwe ili isiendelee kuvaa koti la serikali ya  Jamhuri ya Muungano na kujinufaisha na nafasi hiyo. Hivyo basi, kwa baadhi ya makundi, katiba mpya itakuwa na tija tu kama muundo wa serikali tatu kama ulivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba utazingatiwa. Kwa mtazamo wangu, tusijibane katika fikra hizo, bali tuangalie ni jinsi gani katiba itaweka mazingira ya kuubomoa mfumo dhalimu uliopo.
Matumaini ya Watanzania wa Kawaida

Matarajio ya wananchi wa kawaida, ambalo ndiyo kundi kubwa nchini yamekuwa tofauti na wanasiasa wetu. Takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba zinaonesha kuwa maoni ya wananchi wengi yalilenga zaidi masuala ya utawala bora, matumizi ya rasilimali na maisha yao ya kila siku kuliko hata miundo ya muungano ambayo wanasiasa wanaipigania. Wananchi wanakerwa na mfumo uliopo ambao hauna uwajibikaji kwa viongozi na raia. Badala ya kufanya kazi kwa bidii na kupata mapato halali, watu wengi wamekuwa wakiishi kwa ujanja ujanja tu! 
Wakati katika ngazi za juu kuna ufisadi wa kutisha, usemi wa ‘kila mbuzi hula kutokana na urefu wa kamba yake’ umekuwa halali kwa watumishi wa Serikali ambao wametumia nafasi zao kuomba rushwa ndogo ndogo kwa wananchi. Hizi rushwa ndogo ndogo zimekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa kuwa zinamkamua maskini huyu hata kile kidogo alichonacho.

Vivyo hivyo, wakati Tanzania imejaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali kama vile madini, misitu, mbuga za wanyama na gesi, rasilimali hizi zinaonekana kutokumsaidia mtanzania. Watu waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizo wametuangusha kwa kujali maslahi yao binafsi. Matokeo yake ni kuwa raia wa kawaida ameachwa katika maisha yasiyotabirika huku Serikali ikiendelea kuongeza kodi katika bidhaa anazozitumia.
 Tatizo ni Mfumo au Viongozi Wetu?

Mjadala umeibuka kwa muda mrefu sasa juu ya nini kikwazo kikubwa cha maendeleo yetu kama taifa. Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi mfumo uliopo ndio kikwazo kikubwa kwa nchi yetu kupiga hatua. Lakini kwa upande mwingine kuna wanaoamini kuwa tatizo letu kubwa ni uongozi.

Katika moja ya makala zake za wazi, M.M. Mwanakijiji anatuaminisha kuwa adui mkubwa wa maendeleo yetu ni mfumo haramu uliotengenezwa na utawala wa kifisadi. Kwa mujibu wa Mwanakijiji, “mfumo huu una mchanganyiko wa mifumo midogo midogo ya kisiasa, kiuchumi, na kisheria ambayo msingi wake ni ubinafsi, kutokuwajibika, kulindana, utawala wa hofu, kubebana na kuvumiliana kwa kadri ya kwamba wanufaikaji ni kikundi cha watu wachache walio katika utawala na wale wanaohusiana nao kwa karibu.” 
Kutokana na mrengo huu wa fikra, wakati tunatafuta mchawi wa maendeleo yetu tusianze kushughulika na mtu mmoja mmoja bali tuungalie mfumo huu. Kwa maneno mengine, kiongozi yeyote atakayeingia kufanya kazi katika mfumo huu, hawezi kuleta mabadiliko ya kweli.

Mrengo huu wa fikra kama unavyodadavuliwa na ndugu Mwanakijiji unashawishi kwa kiasi kikubwa. Lakini bado unaibua changamoto kadhaa za kifikra. Kwa mfano, je tumeshafanya udadisi wa kutosha kujua kuwa mfumo huu ulianzia wapi na umeota mzizi lini nchini Tanzania? Je, mfumo huu ulikuwepo hata wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere? Kwa ajili ya kuibua mjadala zaidi, ningependa kusema bayana kuwa ubinafsi, kutowajibika, kulindana, utawala wa hofu, na kubebana haukuzaliwa na Tanzania. Sidhani kama waasisi wetu walikuwa na utamaduni huu!
Hii ina maana kuwa, na ningependa kumuaminisha na ndugu Mwanakijiji, kuna uhusiano mkubwa kati ya uongozi na mfumo uliopo. Kwa mfano, katiba yetu imempa Rais wa nchi madaraka makubwa sana.  Katika kifungu cha 36 (1) kwa kuzingatia katiba, Rais ana mamlaka ya kuanzisha au kuifuta taasisi ambayo anaona itasaidia au kudhoofisha utendaji wa serikali yake.  Kifungu cha 36 (2) kinampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi wa viongozi waandamizi katika kuendesha taasisi mbalimbali ikiwemo zinazohusika na utungwaji wa sera. Wakati huo tukumbuke kuwa Rais anapoingia madarakani anaenda kutekeleza sera zake kama alivyopewa ridhaa na wapiga kura ambazo kimsingi zinaweza zikashabihiana na mfumo uliopo au zikaubomoa kabisa. Uanzishwaji au ufutwaji wa Taasisi pamoja na uteuzi ni baadhi ya silaha muhimu anazoweza kuzitumia Rais kuleta mabadiliko ya kimfumo.
Kwa mujibu wa Mwanakijiji chama kilichopo madarakani ndio chanzo cha kuendelea kwa mfumo huu dhalimu. Na kwa maoni yake, tunaweza kuondoa mfumo huu kwa kuking’oa chama hiki madarakani na kutoa nafasi kwa vyama vingine.  Kazi kubwa ya uchaguzi imekuwa kusaidia mabadiliko haya katika nchi nyingi. Uingereza inatupa mfano mzuri, ambapo, ingawa wao hawana katiba iliyoandikwa, lakini wamekuwa wakiuondoa utawala usiowafaa kupitia uchaguzi kwa ufanisi mkubwa. Lakini, je kama tatizo ni mfumo na sio viongozi, utasemaje ukikiondoa chama fulani utapata suluhisho? Hayawezi kutokea kama ya Rais Frederick Chiluba wa Zambia?
Kwa maoni yangu,vita hivi vinapaswa kupiganwa kila kona. Mosi, tunahitaji uwepo wa taasisi muhimu kikatiba. Tume ya Jaji Warioba walifanya kazi nzuri sana kutengeneza mifumo ya kiuwajibikaji ambayo wachambuzi wengi wanaziangalia kama chachu za kuondoa huu mfumo dhalimu. Hata hivyo, maswali mengi yameulizwa kuhusu kukosekana kwa TAKUKURU katika Rasimu ya katiba. Taasisi kama hizo zilitakiwa kupewa meno ili ziweze kudhibiti utamaduni huu wa rushwa ndogo ndogo zinazowakosesha haki raia.
Pili, viongozi wanaochaguliwa wanapaswa kuwa wenye nia thabiti ya kuliendeleza taifa na wanaouchukia  mfumo huu dhalimu. Viongozi ambao watakuwa wasikivu wa kilio cha wananchi na walio tayari kuleta mabadiliko katika jamii. Tatu, tunahitaji kuweka misingi ya uwajibikaji katika sheria zetu. Sheria hizo zizingatie pia mazingira ya kisiasa yanayoheshimu ushindani wa haki na zinazowajali wananchi kwa ujumla.
Hatuna budi pia kukubali kuwa sisi wenyewe kama raia wa Tanzania ni kikwazo kikubwa cha kupambana na mfumo huu dhalimu. Tumekuwa tukishabikia ufisadi bila aibu na pengine, kwa utamaduni wetu mbaya wa kuishi kiujanja ujanja, tumekuwa tukihamasisha uvunjaji wa sheria ili kukidhi maslahi yetu binafsi. Hivyo basi, nafasi ya wananchi ni kubwa sana katika kubomoa mfumo huu kwa kuwa ndio wanaochagua viongozi na ndio wanaoweza kushinikiza uwepo wa taasisi za kiuwajibikaji. Mjadala na kutokukubaliana kuhusu muundo wa muungano kisibeze jitihada ya kuundoa mfumo huu dhalimu.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP