Monday, August 1, 2016

Magufuli Atamuunga Mkono Kikwete Kugombea AU?

Makala yaliyoandikwa kwenye Gazeti mmoja nchini Botswana na kuwasilishwa kwetu na rafiki kutoka Uganda yamechochea mjadala kuhusu hatma ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya 'Umoja wa Afrika (AU)' uliosogezwa hadi mwakani kufuatia 'kura kutotosha'. Tukumbuke kwamba Botswana ni nchi mojawapo iliyokuwa na mgombea wa nafasi hiyo, Pelonomi Venson-Moitoi, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Nkosazana Dlamini-Zuma wa Afrika Kusini. Lakini tukumbuke kwamba uhusiano wa Rais wa Botswana, Ian Khama, na AU umekuwa unatiliwa mashaka na baadhi ya wadadisi wa mambo. Uganda nayo ilikuwa na mgombea wake, Specioza Wandira Kazibwe, ambaye (alikuwa) 'anaungwa mkono' na Serikali ya Tanzania. Blogu ya Udadisi inauwasilisha uchambuzi ufuatao wa kimuktadha uliofanywa na Mwanazuoni Dastan Kweka ili kutusaidia kuelewa nafasi ya Jakaya Mrisho Kikwete kukikwaa kiti hicho na hatma ya Diplomasia ya Tanzania katika Nchi za Maziwa Makuu, Afrika Ya Mashariki na Kusini:

Ili tuelewe chimbuko la huu wasiwasi wa kama Rais (Magufuli) atamuunga mkono Rais Mstaafu (Kikwete) katika kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, AU, (kama itatokea), ni vema tukaangalia ni namna gani Rais (Magufuli) ameshirikiana na Rais Mwingine Mstaafu (Mkapa) katika jukumu lake la usuluhishi (facilitator) wa mgogoro wa Burundi. 

Baada ya Rais Mstaafu (Mkapa) kuteuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuwa 'muwezeshaji' wa juhudi za kutatua mgogoro wa Burundi, alianza kuzunguka katika ukanda huu kuonana na wadau mbalimbali ambao aliona ni muhimu katika kufanikisha mkutano wa kwanza (Tukumbuke kuwa ule uliokua umepangwa Desemba (2015) kule Uganda ulikuwa wa 'uzinduzi wa mazungumzo', na uliopangwa mwezi wa Februari na baadaey Machi (2016) haukufanyika. Hivyo basi, baada ya mzunguko, Rais Mkapa alimalizia kwa kuonana na Rais Magufuli na baada ya mazungumzo yao aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuhusu 'kuruhusiwa' kufanya mkutano wa kwanza, kama inavyoonekana hapa chini:


Ni vema kukumbuka kuwa  kipindi Rais Mkapa anasema alikuwa amepata ruhusa (na uungwaji mkono?), Rais Magufuli alikuwa ametoka Rwanda mapema mwezi huo ambako alishiriki katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda (Tarehe 07/04/2016). Pia ni vema kukumbuka kuwa, wiki moja tu baada ya Rais Magufuli kutoka Rwanda, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alituma ujumbe maalumu kwa Rais Magufuli. Mjumbe maalumu "alimueleza Rais Magufuli kwamba ametumwa kuleta barua hiyo pamoja na shukrani za dhati kwa Tanzania ambayo ni rafiki, jirani na ndugu wa kweli wa Burundi kwa ushirikiano mzuri inaoupata" (msisitizo wangu). 

Jambo ambalo lilikuwa la wazi katika ujumbe maalumu uliotumwa na Rais Nkurunziza na ambalo halikuandikwa na gazeti nililolinukuu hapo juu ni kuwa Rais Nkurunziza alikua na hofu na hatua ya Rais Magufuli kufanya safari yake ya kwanza nje ya nchi kwa kwenda Rwanda, ukizingatia uhasimu wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili. Hivyo lengo hasa lilikuwa ni kuikumbusha Tanzania kuhusu uhusiano wake na Burundi na hasa kwa Burundi/Nkurunziza kuonesha nia yake ya kuendelea kuimarisha mahusiano hayo. Mbali na ujumbe huo maalumu, uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umezidi kuimarika na matokeo yake, kwa upande mwingine, uhusiano baina ya Tanzania na Burundi umeendelea kudorora. Rais Magufuli amenukuliwa katika vyanzo mbalimbali akimuita Rais Kagame 'ndugu yangu, kaka yangu' n.k. 

Pia, ni vema kuweka wazi kuwa, mazungumzo ya kwanza yahusuyo mgogoro wa Burundi yaliyofanyika mwezi wa 5 mwaka huu, yalifanyika katika muktadha huu wa kuimarika kwa mahusiano baina ya Rwanda na Tanzania na 'kutelekezwa' kwa mahusiano baina ya Tanzania na Burundi. Athari ya hatua hii, kwa mtazamo wangu ni kuwa Rais Mkapa, ambaye anaitwa 'muwezeshaji' (facilitator), huku Rais Museveni akiwa 'mpatanishi' (Mediator), ni kuwa ingawa Rais Mkapa amefanikiwa kufanya mikutano miwili mpaka sasa (Mmoja Mei na Mwingine Julai), amefanya hivyo katika wakati ambao Tanzania ina ushawishi mdogo sana kwa Burundi na haishangazi kuwa inamuwia vigumu sana kupiga hatua maana, kuna mantiki kufikiri kuwa, Nkurunziza siyo msikivu kwa Tanzania kama ilivyokuwa kabla ya mabadiliko niliyoyaeleza kwenye aya zilizotangulia. Kuna taarifa za kichambuzi kuwa Burundi ilipoona Tanzania 'imeitelekeza', ilizigeukia Angola, Afrika ya Kusini na China na Urusi (kwenye Umoja wa Mataifa-UN), katika mkakati wa kusukuma ajenda zake katika ngazi mbalimbali. 

Maswali ya msingi ya kujiuliza na ambayo yanaweza kutusaidia kuelewa chimbuko la fununu za kama Rais (Magufuli) 'atamuunga' mkono Rais Mstaafu (Kikwete), ni je, kama Rais (Magufuli) alimruhusu muwezeshaji wa utatuzi wa mgogoro wa Burundi (Mkapa) kuendelea na hatua za kuandaa mikutano, hakujua kuwa kuendelea na juhudi zake za kuimarisha mahusiano yake na Rwanda tena kwa kasi ya ajabu, kungekuwa na madhara fulani, hasa hasi, dhidi ya juhudi za 'muwezeshaji'? Na je, kama alijua hivyo, ile ya 'green light' ambayo Rais Mkapa aliipata, ilikuwa ni uungwaji mkono wa roho moja au ilikua ni 'kafanye unavyoweza'? Nafikiri uzoefu huu unaweza kuwa ndio chimbuko la msingi sana la wasiwasi iwapo Rais (Magufuli) atamuunga mkono Rais mstaafu (Kikwete) iwapo atawania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC). Na hivyo basi, kutokumuunga huko mkono, kama kukitokea, kimantiki, hakutatokea waziwazi bali katika mazingira kama haya niliyoyaeleza. 

Jambo jingine ambalo siyo la kusahau ni kuwa, tangu Rais (Magufuli) aingie madarakani, ameonekana kuweka mkazo zaidi katika diplomasia ya kiuchumi katika ukanda huu. Hata hivyo, zaidi zaidi anaonekana kuwa Rais ambaye anaangalia zaidi ndani (inward looking) kuliko kuangalia kote kote. Mpaka sasa hajahudhuria kikao chochote cha SADC, AU au cha ICGLR. kuna maswali mengi iwapo anaipa diplomasia ya bara zima (continent-wide diplomacy) umuhimu katika kufanikisha ajenda zake. Kwa mantiki hii, inawezekana pia asione umuhimu mkubwa sana katika 'kumuunga' mkono Rais Kikwete. 

Rais Magufuli anaonekana kuwa na nakisi ya uelewa wa mambo ya diplomasia. Ukaribu wake na Rwanda unaibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa diplomasia ya nchi yetu dhidi ya Burundi, DRC na Kenya. Kikwete ni mjuzi katika hili. Tayari Rais Kikwete anaonekana kupata majukumu mengi kimataifa kuliko hata Rais Mkapa alipostaafu. Kwa Rais anayeonekana kupenda umaarufu kama Magufuli, kumuunga mkono Kikwete katika adhma hiyo ni kuchagua (na kukubali) kuendelea kuishi katika kivuli cha umahiri wa diplomasia ya mtangulizi wake kwa kipindi cha miaka 4/5 ijayo - mpaka 2020/2021, na hata baada ya hapo. 

Ngoja tuone. 

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP