Sunday, October 9, 2016

Taharuki ya Walimu: Mitandao ya Jamii Ipongezwe?

Jamhuri ya Mitandao ya Kijamii na Sakata la Walimu Mbeya

Richard Mbunda


Hali imekuwa tofauti sana na kipindi sisi tunakua kule Utiri, Mbinga ambapo taarifa yoyote utaipata kwa kusimuliwa. Kuona picha ilikuwa nadra, na sijui ni lini nilianza kuongea kwa simu tena zile za mkonge! Sasa mambo yamebadilika sana. Unapata taarifa kutoka sehemu yoyote ya dunia kiganjani kwako na unaweza kusambaza taarifa kwa kasi ya mwanga, ili mradi tu umetandaa. Haya si ndiyo maendeleo ndugu zangu?

Miaka kadhaa iliyopita mwandishi wa habari alinipigia simu kuuliza maoni yangu wakati muswada wa sheria ya mitandao ya kijamii ulipokuwa unaandaliwa. Kwa maoni yake yeye [naamini pia ni maoni ya nchi za magharibi], sheria hii ingekandamiza maoni ya wananchi. Mimi nikamjibu, kwa kasi hii ya kutandaa kwenye mitandao ya kijamii, naamini tungehitaji taratibu za kutuongoza. Nilimwambia; ‘pale ambapo uonevu utakuwepo tutapaza sauti kwenye mitandao ya kijamii’. Ndugu msomaji, nataka utambue kuwa upekee wa mitandao ya kijamii ni uwezo wake wa kujitetea. Na huwezi kuuondoa upekee huu.

Ingawa sheria hii imeshawatia hatiani watu kadhaa kwa uchochezi na wengine bado wanahitajika mahakamani [huenda sisi wote ni watuhumiwa watarajiwa], lakini mitandao ya kijamii haijaacha kuiteka nchi. Naam, ingawa siyo nchini kwetu tu, ni dhahiri sasa Tanzania tumekuwa Jamhuri ya Mitandao ya Kijamii.

Ukiachana na hizo mbwembwe za hapo juu, dhumuni la andiko hili ni kutoa maoni yangu kuhusu sakata la walimu kumpiga mwanafunzi Mbeya. Naam, nimesononeshwa na mambo mengi katika sakata hili kwa mantiki ya uzito wa jambo lenyewe, uwajibikaji, uongozi na taathira ya muda mrefu ya maamuzi yaliyochukuliwa na taasisi mbalimbali za kiserikali.

Uzito wa Makosa kama yanavyoonekana kwaye Video

Hakuna maswali, na mimi nataka kusisitiza, wakati video hii ikisambaa, sikuwahi kumuona mtu yeyote akikubaliana na kilichoonekana kwenye video. Walimu walikuwa wanapiga kwa kukomesha kama majambazi na sio kufundisha kama kanuni zao za kazi zinavyowataka. Mimi nataka nimpongeze mchukuaji wa video kwa jinsi alivyo mahiri kwani amefanikiwa kutuonesha sehemu muhimu zaidi ambayo ndiyo msingi wa mihemko yetu na maamuzi yaliyochukuliwa. Kitendo cha walimu hawa hakiwezi kufumbiwa macho na kwa namna yoyote lazima vyombo vya dola vichukue hatua stahiki. 

Maamuzi ya Viongozi wa Serikali

Mara baada ya video kusambaa, na kwa bahati nzuri viongozi wetu ni sehemu ya mitandao hii, hatua mbalimbali zilichukuliwa. Napenda kupongeza hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Kwanza kabisa aliutaarifu umma kuhusu tukio: wapi limetokea, nani wanahusika tathmini ya awali za chanzo cha tukio. Pili, alilaani kitendo hiki ili kuonesha kutokukubaliana nacho. Tatu, aliliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka kuwatafuta watuhumiwa hawa na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Nampongeza pia kwa kuwa alitumia mitandao ya kijamii ili kufikisha taarifa hizi haraka iwezekanavyo. Katika nchi inayofuata msingi ya sheria, hatua hii ya Waziri wa Mambo ya Ndani ndiyo haswa iliyotakiwa kuchukuliwa, na Mheshimiwa huyu alitumia madaraka yake vizuri sana.

Lakini, baada ya hatua hizi zilizochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, palifuata hatua zingine lukuki ambazo zimenichanganya sana, na huenda ndizo zilizonifanya nichukue kalamu. Kila Mtanzania alilaani vitendo hivi kwa nafasi yake, na hata kwenye mitandao ya kijamii kuna waliohukumu na hata kutekeleza hukumu zao mara tu baada ya kuona video. Hata hivyo, katika Habari za Mikoani TBC, iliripotiwa kuwa WAZIRI wa ELIMU na MAFUNZO ya UFUNDI alitamka kuwafukuza chuo walimu (wanafunzi wa chuo) waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi kama ilivyoonekana kwenye video. Hii ilinishangaza sana. Waziri kaona video tu amehemka na kufukuza watu chuo hata bila taratibu zingine kufuatwa! 

Ingawa wanastahili kuwa jela, na kufukuzwa lakini tunazungumzia walimu watatu, ambao tayari Serikali imeshawekeza pesa na ni nguvukazi ya taifa, hivyo basi, lazima Waziri huyu awe amejiridhisha siyo tu kuchukua maamuzi ya papo kwa hapo. Hoja yangu ni kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa na hao Walimu-Wanafunzi walikuwa bado ni watuhumiwa tu. Kama vile wanavyotoa vifungu vya kisheria kuhalalisha mamlaka zao za uteuzi, Waziri pia alipaswa kutuambia anatumia vifungu vipi vya kisheria vinavyompa mamlaka hiyo ya kufukuza wanafunzi chuo ili umma utambue kazingatia taratibu na sheria za nchi. Vinginevyo hatua hii aliyochukua haina tofauti na mama mmoja kwenye Basi la Mwendokasi aliyetaka wanafunzi hawa wafungwe moja kwa moja bila mahakama kuwasikiliza kwa kuwa alipoona video tumbo la uzazi lilimcheza.

WAZIRI WA NCHI- TAMISEMI aliandika barua akaisaini na ikatufikia kwenye mitandao ya kijamii. Waziri huyu anaandika barua yake kuwa amemtuma Mkuu wa Mkoa kufuatilia na mahojiano yanendelea. Lakini cha kushangaza anamhukumu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuwa hakutoa taarifa ya tukio, na bila hata kumsikiliza au kupokea/kudai maelezo yake anaagiza avuliwe madaraka yake ya ualimu mkuu! Hii imenishangaza sana. Mwalimu huyu alipaswa kusikilizwa na Waziri huyu ajiridhishe bila wasiwasi kuwa mwalimu alificha tukio hili ndipo hatua kama hii ingechukuliwa. Je, kama tukio hili halikufika ofisini kwa Mwalimu Mkuu ma liliishia 'staff room' tu? Halafu, huwezi kuagiza uchunguzi wakati huo huo unatoa hukumu, nadhani hukumu hii ilizingatia mihemuko ya jamii kwenye mitandao na siyo uongozi bora unaohitaji uvumilivu na utulivu kabla ya kuamua.
Mwisho katika mlolongo huu wa viongozi na Taasisi ni Bodi ya Mikopo. Ikiwa imevutwa katika mhemko wa tukio hili, Bodi hiyo iliandika barua tarehe 7/10/2016, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Abdul-Razaq Badru ,kuutarifu umma kuwa Bodi imesitisha mikopo kwa wanafunzi wanne waliohusika katika sakata hili, kitu ambacho sioni msingi wake. Je, bodi ya mikopo ilitaka kujitangazia tu mamlaka yake kupitia mgogoro huu wa video? Cha kushangaza zaidi ni pale wanapowataka wanafunzi hawa kurejesha mikopo waliyokopa mara moja, kana kwamba walikuwa wana uwezo wa kujilipa na wana pesa ila Bodi ilikuwa inawapa motisha tu ili wasome! Bodi ya Mikopo ilikuwa na uhalali gani wa kutoa tamko hili? Au ndiyo maana imeweza kuagiza makato ya wafanyakazi wa umma hasa katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) katika mishahara yao na kuwaongezea madeni hata kama walishamaliza tangu 2012! 

Kupost Video zinazoleta Taharuki

Pamoja na pongezi alizomiminiwa mtu aliyechukua tukio hili na kuposti video yake, lakini binafsi naona limeleta taharuki. Mchukua video hii, anayesadikiwa kuwa ni Mwalimu pia [na Mh. Mwigulu Nchemba amemtaja mpaka jina], alisononeshwa na tukio hili ndipo akaamua kulirekodi. Mwalimu huyu alipaswa kwanza kuipeleka video hii polisi ili sheria ichukue mkondo wake na labda hilo likishindikana ndiyo atumie mbinu hiyo ya 'ulipuaji' mitandaoni.

Madhara ya video hii yamekuwa makubwa. Kuna mama mmoja anasikikika akiongea na mtoto wake kuhusu video hii ambayo ilimtia hasira sana mtoto huyo wa takribani miaka sita au saba hivi. Mama huyu alirekodi mazungumzo hayo kwenye video ikionesha akilia kwa hasira na kutishia kwenda kuwaua walimu. Je, tunatengeneza kizazi cha aina gani na kiwe na uhusiano gani na walimu?
Pia naamini, pamoja na kuwa walimu hawakupendezwa na tukio hili la walimu-wanafunzi kumpiga mwanfunzi pasipo utaratibu, lakini huenda wametatanishwa na hatua zilizochukuliwa na kejeli walizozipata kutoka kwa jamii mara tu baada ya video hiyo kuwekwa hadharani. Nimeona video nyingine walimu wakiwarekodi wanafunzi waliowakuta na pombe kwenye viroba na bangi ili tu kuonyesha aina ya wanafunzi wanaodili nao kila siku wakiwa kazini. Posti hii pia haikubaliki kabisa, kwa kuwa video hizi zitaendelea kubaki mitandaoni kwa muda mrefu sana. Najaribu tu kuwaza kama walimu wa zamani wangekuwa wanaturekodi na kuposti video kwa umma sijui ni viongozi wangapi tulionao leo hii wangeathirika na jambo hilo! Huenda wengine wao wasingepata hata uthubutu wa kugombea nafasi walizonazo sasa.

Vilevile naona video hii imehamasiha uhasama kati ya walimu na wanafunzi. Najaribu kufikiri, idadi kubwa ya wanafunzi wapo shule za serikali na walimu wao wamekuwa walalamikaji wakubwa wa mazingira magumu ya kazi na hata mafao yao kutokuridhisha. Tukiwaongezea mzigo wa wanafunzi wakorofi kwa kuwa wakiadhibiwa watarekodi na kuwafukuzisha kazi walimu tunaweza kutengeneza kada ya walimu ambao watasusia kazi muhimu ya kuandaa nguvukazi hii ya baadaye. Wapo watoto wa siku hizi wanaovuta bangi, unga, walevi na wavivu. Hatupaswi kuwakatisha tamaa walimu wetu hata kidogo.

Mwisho, video hii ningependa iwe mwanzo wa mfumo mpya. Natamani video zinazoleta taharuki kama hizi zisiwekwe mitandaoni (kwanza) ila kupelekwa katika vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake. Pale hili linaposhindikana ndipo tuziweke mitandaoni ili kushinikiza vyombo vya dola vichukue hatua. Nataka utaratibu wa kutoa adhabu kwa wanafunzi ambao upo, uhimizwe ili kuhakikisha kuwa unafuatwa na pale ambapo mwalimu anakuwa amekosea hatua stahiki zichukuliwe. Video hii pia itufundishe kuwa watulivu na kujizuia kuchukua maamuzi ya haraka huku tukiziacha taaratibu husika kufuata mkondo. Tukichukua hatua kwa mihemko hatutakuwa na tofauti na wale wanaoua vibaka kwa kuwachoma moto au wale wanakijiji waliowachoma watafiti kwa kuwa tu walidhani ni wanyonya damu waliotishia maisha yao. Haya ni maoni yangu yenye nia ya kuleta utengamano wa kijamii. Maoni yangu siyo sheria na ninawajibika kuyatetea.

2 comments:

Mendes April 15, 2017 at 10:44 AM  

Hii ni kampuni ya Canada na sisi kuwa na kusoma maelezo mafupi ya nchi yako, kuelewa sasa uchumi kuvunjika fedha. Tumeamua kusaidia kwa kutoa msaada wa kifedha, huduma ya mkopo, ruzuku na paket nyingine za kifedha. Tunatoa 2% kwa ajili ya mkopo mipango malipo ya kila mwezi. Kwa maelezo zaidi barua pepe:

Nilceia Teofilo
+1 (774-234-8947)
Barua pepe: nilceiateofiloinvestments@gmail.com

Mendes April 15, 2017 at 10:44 AM  

Hii ni kampuni ya Canada na sisi kuwa na kusoma maelezo mafupi ya nchi yako, kuelewa sasa uchumi kuvunjika fedha. Tumeamua kusaidia kwa kutoa msaada wa kifedha, huduma ya mkopo, ruzuku na paket nyingine za kifedha. Tunatoa 2% kwa ajili ya mkopo mipango malipo ya kila mwezi. Kwa maelezo zaidi barua pepe:

Nilceia Teofilo
+1 (774-234-8947)
Barua pepe: nilceiateofiloinvestments@gmail.com

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP