Thursday, June 8, 2017

Kuvuna Viongozi wa Upinzani na Kisa cha Mtu Tajiri

Kuvuna Viongozi wa Upinzani na Kisa cha Mtu Tajiri

Chambi Chachage


Kwa mara nyingine uteuzi alioufanya Rais Magufuli umeibua mjadala mkali. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Mama Anna Mghwira, kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kumepokelewa kwa hisia tofauti: furaha, masikitiko, hasira n.k.

Mama huyo aliyobobea katika taaluma ya theolojia atakuwa anakijua kwa undani kisa ambacho Nabii Nathani alimsimulia Mfalme Daudi. “Palikuwa na watu wawili katika katika mji mmoja”, Nabii alimsimulia Mfalme, “mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.” Hivyo, yule “tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwanakondoo mmoja mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake…akawa kwake kama binti.”

Siku moja tajiri akapata ugeni. Lo, badala ya kutumia utajiri wake mkubwa kumkirimu mgeni “alimnyanganya yule maskini mwanakondoo wake.” Mfalme Daudi aliposikia hitimisho hili alikasirika sana na kusisitiza kwamba mtu huyo asiye na huruma anapaswa kumrudisha yule mwanakondoo mara nne.” Nabii Nathani akamjibu Mfalme: “Wewe ndiwe mtu huyo.”

Nimekumbuka kisa hiki usiku huu baada ya kusoma tamko la kumvua uwenyekiti wa ACT Wazalendo Mama Mghwira ambaye alikaribishwa katika chama hicho kichanga, akalelewa katika itikadi zake za Ujamaa wa Kidemokrasia hadi akagombea Urais mwaka 2015. Lepe la usingizi likanipotea ghafla, ikabidi nimwazime Bibi yangu Biblia yake ili ninukuu hicho kisa. 

Hakika ni tamko la kujitutumua mithili ya la Kijana Daudi dhidi ya Jitu Goliath. Kwa wachambuzi wa kisiasa, ni muhimu kuzoea na kukubali kwamba matamko ya vyama hasa vile visivyotaka ugomvi na Dola lazima yajaribu kuwa ya kidiplomasia. Hivyo, kama ilivyo ada, ACT Wazalendo wanatoa matamshi ya kuuma na kupuliza au kukejeli kwa tafsida.

Lakini unaposoma kwa jicho la tatu maneno kama haya yanayoelekezwa kwa Rais Magufuli ndipo unapokikumbuka kisa cha mtu tajiri na mtu maskini: Asichoke na asisite kuja kuvuna na wengine maana tumeonyesha uwezo wa kutengeneza wengi wa aina hiyo.” Unabaki unajiuliza si ni hivi majuzi tu Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alihojiwa na gazeti la The Citizen kwa barua pepe na kusema kwamba wao kama “chama kichanga” wako “hatarini” na “kwa kila mwanachama” wanayempoteza “ni pigo kubwa na hasa anapokuwa ni kiongozi”? 

Wakati unatafuta majibu unakutana na ujumbe wa leo wa Kiongozi wa Chama huyo uliokuwa kwenye ukurasa wake wa Facebook ukisema: “Unajua uimara wa vyama kwenye Mitihani kama hii inayotukuta sisi.” Hakika huu ni mtihani mkubwa hasa ukizingatia kwamba mmoja wa waasisi wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, amekitosa chama kama yule nahodha aliyejitosa baharini kwenye ile Zilipendwa ya wanamuziki wa Mlimani Park Orchestra. Hicho kilichokuwa kichwa cha chama sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Ujumbe huo wa Facebook wa Zitto Kabwe pia una maneno haya yanayoashiria kwamba teuzi hizi mbili ni mapigo makubwa: “Wanachama 400,032 wa ACT Wazalendo mliotapakaa nchi nzima msiingie kwenya malumbano na nyumbu.” Wanaofuatilia siasa za vyama vingi nchini wanajua kwamba wanaofananishwa na nyumbu ni wafuasi wa CHADEMA ambako Zitto Kabwe, Kitila Mkumbo – na hata Anna Mgwhira – ndiko walikotokea. “Asili ya kuanzishwa kwetu”, ujumbe huo unasisitiza kuhusu hao mahasimu wao wa kisiasa, “ni kuukataa unyumbu.”

Pamoja na kwamba ujumbe huo umekwishafutwa kwenye Facebook ya mhusika, kwa wachambuzi wa Saikolojia ya Siasa hiyo ni ishara ya taathira ya uteuzi alioufanya Rais Magufuli. Unabomoa nguvu ya chama pekee cha upinzani chenye itikadi mbadala kwa uliberali mamboleo na hivyo kufifisha demokrasia ya vyama vingi. Wapo wanaodai ni hatua ya aina yake na inalenga kuleta ‘mseto’ unaonesha utayari wake wa kufanya kazi na wapinzani. Lakini Wadadisi tunaona maneno yafuatayo ya Rais yanaashiria kwamba lengo lake ni kuwapa nafasi ambazo zitawafanya wawe chini ya mamlaka yake ya kidola:


Demokrasia ya Kibunge inayotenganisha mihimili ya Dola inafanya kazi kwa uthabiti pale ambapo Bunge lenye Meno linaisimamia Serikali kijasiri. Hivyo, Serikali inayopambana na ufisadi kwa dhati inapaswa kuwa tayari kuhakikisha kuna wapinzani mahiri watakaoisakama Bungeni kwa ukweli na uwazi ili itekeleze majukumu yake vilivyo. Na ndiyo maana Wadadisi wa Mambo tuliwahi kudai kama tungekuwa Rais Magufuli, tungesema na kutenda hivi wakati wa kuteua:


Ila Rais wetu hapangiwi. Anashauriwa tu. Na kama Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi alivyodadavua Bungeni: “Tutunze heshima ya Rais akiwa Mkuu wa Nchi. Tutunze heshima ya Rasi akiwa Amiri Jeshi. Lakini inapokuja kwenye nafasi ya Ukuu wa Serikali, serikali isimamiwe.”
Rais Magufuli katukumbusha kwamba Mama Mghwira alikuwa na dhamiri na utashi wa kuweza kukataa uteuzi. Tunaomfahamu tunajua ilikuwa ni vigumu kukataa. Na ndiyo maana wachambuzi wa siasa kama mgawanyo wa mamlaka na rasilimali tunasisitiza kwamba, kuna mstari mwembamba kati ya hiari na shurti. Je, kweli chama maskini kimeridhia tu kumpoteza Mwenyekiti wake? 

Chama tajiri nacho, je, kinataka kuua Upinzani ili kishike hatamu?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP