Friday, September 8, 2017

Wizi Mkuu Wa Kiingereza Afrika?

"Hii ni Insha inayonuia kuhimiza, kushangilia na kuendeleza mchango wa Ngũgĩ wa Thiong’o katika mjadala muhimu unaohusu swala la lugha barani Afrika. Lengo kuu hapa ni kusema kwamba hoja ya majadiliano kuhusu lugha ya Kiingereza katika akademia inabidi isibaki tu kwenye ubishi kati ya swala la umilikaji -aidha Kiingereza ni lugha ya Mwafrika au si lugha ya Mwafrika lakini isonge mbele na iangalie kwa makini swala la mizigo, gharama, na hasara za kuchukua Kiingereza tunavyokichukulia barani Afrika. Hatuna budi kujiuliza kwanini Kiingereza kinaendeleza ubaguzi, ubinafsi, na udanganyifu kuwa lugha za wenyeji Afrika hazihitajiki katika maswala ya elimu na maisha ya kisasa. Insha hii inajaribu kubainisha kati ya ‘Vertical English’ yaani ‘Kiingereza fasaha na cha kitaaluma’ ambacho ni Kiingereza maalum na tena teule ambacho ndicho kinatumika katika kazi za kisomi zikiwemo harakati za kujifunza, kufundishia, kutahini na kufanyia utafiti. Kwa upande mwingine ‘Horizontal English’ yaani ‘Kiingereza cha watu wa kawaida’ ambacho kimetanda kote Afrika ambako Kiingereza ni lugha rasmi. Kiingereza hiki pamoja na lugha zetu havithaminiwi. Hoja ni kwamba Kiingereza hicho fasaha (kimuundo na kimatamshi) ndicho pasipoti ya kupanda ngazi kielimu, kutambulikana kisomi, na kuwa mwanachama mheshimiwa katika klabu cha wanataaluma duniani. Kiingereza hicho kinatoa fursa hizo kwa Waafrika wachache mno na kuwanyima nafasi hizo wote wale ambao hawakimudu. Tamko ‘heist’ linamanisha ‘unyang’anyi’ na usemi ‘The great English heist’ una maana ya ‘wizi na unyang’anyi mkuu unaohusu Kiingereza’ katika masomo ya Kiafrika. Maana ya kutumia neno hili ‘heist’ unyang’anyi/wizi ni kushtaki jinsi ambavyo elimu na ujuzi wa mwafrika unavyokusanywa, kujadiliwa, na kuhimarishwa kwa lugha zetu za asilia na Kiingereza cha watu wa kawaida zikiwemo pijini, lakini kusahaulika makala zinapochapishwa. Kile kinachokosekana na kusahaulika katika mchakato huu ni mchango mkubwa wa lugha hizi katika akademia ihali wale walio wachache wakinufaika kwa tuzo, umashuhuri na kupanda ngazi. Basi wakati mwingi mchango wa mwafrika hauonekani wala kuchangamkiwa ila kupitia lenzi za wasomi walio wachache wanaomudu Kiingereza fasaha" - John Mugane

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP