Tuesday, October 24, 2017

Uteuzi wa Gavana na Njozi ya Rais kuhusu Benki Kuu

Uteuzi wa Gavana na Njozi ya Rais kuhusu Benki Kuu


Chambi Chachage

Uteuzi wa 'kushtukiza' wa Profesa Florens Luoga kuwa Gavana Mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) umeibua mjadala mkali nchini. Wapo wanaoona kuwa uamuzi huo ni wa ghafla na ni ishara kwamba Gavana wa sasa, Professa Benno Ndulu, ametumbuliwa. 

Pia wapo wanaoona kuwa kumteua Mwanasheria badala ya Mchumi kama ilivyozoeleka ni tatizo. Hali kadhalika wapo wanaoukubali uteuzi huo japo hawakubaliana na ulivyofanyika.

Uchambuzi ufuatao umejikita katika hoja ya kwamba Rais amechanganya majukumu ya BOT na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo alishamteua Profesa Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi yake. Hoja hii, inayoshadadiwa na wachumi na wanamabenki, inatokana na uelewa wa Benki Kuu kama chombo kilichojikita zaidi katika sera pana za kiuchumi na kifedha.

Hivyo, kwa mujibu wa hoja hii, viatu vya ugavana havimtoshi Profesa wa Sheria za Kodi. Hata kifungu cha sheria kinachoonesha kwamba Gavana anaweza kuwa mwanasheria hakitoshi kutuliza mtima wa wabobezi hawa wa sekta ya kiuchumi na kibenki. Pia maelezo haya ya Rais John Magufuli hayatoshi kukidhi kiu yao:


Ni rahisi kutafsiri maneno hayo ya Rais kama ishara kwamba malengo ya uteuzi huo ni kuchanganya masuala ya TRA na ya BOT. Lakini katika hotuba hiyo hiyo Rais anatoa maelezo haya:


Swali la kujiuliza ni: Je, nani hasa anapaswa kutekeleza hiyo sheria anayoizungumia Rais? BOT? TRA? Jibu lipo katika kipengele cha  'Usimamizi wa Benki' cha tovuti ya BOT ambacho kimeipachika Sheria ya Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992 inayoitaja Benki Kuu ya Tanzania kama mhusika muhimu katika udhibiti huo kisheria.

Lakini ili kupata muktadha zaidi wa kihistoria wa kwa nini Rais ameamua kumteua Mwanasheria aliyebobea katika udhibiti wa fedha, kwa mujibu wa wasifu wake uliopo mtandaoni, hebu tuirejee hotuba yake ya mwaka 2016 katika Jubilee ya Miaka 50 ya BOT:

"Hivi sasa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu kubwa moja nalo ni kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo thabiti wa fedha kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa letu. Benki Kuu, na hata taasisi zingine za fedha, hazijihusishi moja kwa moja kwenye masuala ya ukuzaji uchumi. Lakini ukiangalia historia katika nchi zilizoendelea, kama Marekani, Uingereza, Japani, Korea Kusini utaona Benki Kuu zilitoa mchango mkubwa katika shughuli za uchumi hususan kwenye kilimo, miundombindu, viwanda na kadhalika. Ingefaa basi nieleweke kuwa ninaposema Benki Kuu kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi sina maana ni lazima Benki Kuu ishiriki moja kwa moja. Benki Kuu inaweza kubuni mkakati na kutengeneza mazingira mazuri yanayoweza kuwezesha taasisi za kifedha nchini kama mabenki binafsi na [mifuko] ya hifadhi ya jamii kuona umuhimu wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi." 

Wigo wa BOT kwa maono ya Rais pia unaonekana katika nukuu hii:

"Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya fedha, ikiwemo huduma za kielektroniki kama vile mashine za kutoa fedha, ATM, na huduma za kibenki kwa ajili ya simu za viganjani, kwa mfano TIGO-Pesa, M-Pesa na kadhalika. Matumaini yangu..Benki Kuu mmejipanga vizuri katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa huduma hizo. Lakini...pia si usalama tu, lakini pia Serikali ni lazima ipate mapato yake stahiki. Ninafahamu katika transaction iliyofanyika kwenye mwezi wa tatu, kwenye fedha zilizotumwa katika nchi hii kwa kutumia mitandao ya simu, transaction iliyofanyika, kwa rekodi niliyonayo, ilikuwa na thamani ya trilioni 5.5. TSh. Je, Serikali imefaidika na nini na transaction hiyo? Kwa hiyo Benki Kuu mnatakiwa mjipange vizuri  katika masuala haya. Bila hivyo, Serikali haitapata fedha lakini patakuwa na business ambazo Benki Kuu haizijui na kuiletea hasara kubwa - na kuleta matatizo mengine makubwa ya kiuchumi. Kwa mfano, Benki Kuu mkishirikiana vizuri na TCRA ambapo hata ule mtambo wa Revenue Assurance bado haujafungwa mpaka leo, ambapo hata wale wanaohusika na simu sana sana wana-declare kwamba kila siku ni hasara. Kujua mapato yanayopatikana kule ni lazima wao waseme. Benki Kuu mnatakiwa mjipange....Bila hivyo, tutaendelea sisi kuwa wasindikizaji wakati Benki Kuu ndicho chombo kikubwa ambacho tunakitegemea. Na ninaposema Benki Kuu maana yake na Hazina lazima mjipange. Katibu Mkuu wa Hazina unafahamu mchezo ambao umekuwa ukifanyika kule ambao umetufanya sisi hata tushindwe kuingia ndani ya East African Community kwa umoja wetu kwa sababu ya hilo suala tumechelewa, katika masuala ya revenue assurance, kwamba palikuwa na utapeli wa ajabu."

Uteuzi wa Mwanasheria Nguli wa Biashara za Kimataifa pia inawezekana umelenga kutekeleza hili suala alilolisitiza Rais:

"Suala lingine ni kuhusu usimamizi wa vyombo vingine vya fedha, mfano, maduka ya kuuza fedha za kigeni, Bureau de Change. Ni vyema BOT ikaimarisha usimamizi wake. Ni lazima tujue kila fedha inayobadilishwa kule - uhalali wake na matumizi yake. Ili zisije zikatumika hizi Bureau de Change kama eneo lingine la kutoroshea fedha na kufanya uchumi wa nchi yetu uharibike. Ili hizi Bureau de Change pia zisitumike kuingizia fedha za madawa ya kulevya na fedha zingine ambazo si halali. BOT ni lazima mjipange vizuri."

Njozi ya Rais Magufuli, walau kwa kupima na maneno yafuatayo katika hotuba hiyo kwa BOT, ni kuhakikisha nadharia za kiuchumi zinatekelezeka katika uhalisia wa maisha ya kawaida ya Mtanzania:

"BOT ni lazima mjipange vizuri. Tunapozungumzia juu ya inflation kwamba iko single digit, imetoka asilimia 30 - 28 hadi asilimia 5.2, ni kitu kizuri, tunashangalia. Kwa ninyi wasomi wa BOT na baadhi ya wataalamu wengine tunaelewa maana yake. Lakini ni kweli hii inflation ya kutoka asilimia 30 mpaka 5.2 imekuwa reflected kwa wananchi wa kawaida? Je, ukizungumza kwa mwananchi wa kawaida kule kijijini kwenu, Profesa, ukasema sasa inflation imetoka asilimia 30 mpaka 5.2, imekuwa reflected kwa maisha yake? Hilo ndilo suala la kujiuliza. Hii inflation kwamba imerudi kwenye single digit iwe reflected kwa wananchi maskini! Na hapo ndipo tutakuwa tumejibu hoja za wananchi tunaowaongoza. Bila hivyo tutabaki na data zinazokaa kwenye matakwimu mazuri, tunashangilia inflation imeshuka from 30 to 5.2 lakini in the reality wananchi wanaona inflation kama imepanda kwa asilimia 70. Ni lazima iwe reflected hata kwenye bidhaa wanazozinunua. Kwamba kwenye miaka ya 90 inflation ilikuwa 30 percent na sasa hivi tunazungumzia is 5.2 percent, je, bidhaa wananchi wa kawaida walizokuwa wakizinunua mwaka 90 uki-compare na bidhaa wanazozinunua sasa hivi zina-reflect  hiyo calculation ambayo tunaitumia sisi wanauchumi kwamba kuna inflation imerudi kwenye single digit?"

Hivyo, hoja kuu ya Rais inaonekana ni hitaji la kuwa na uwezo wa kujenga  mifumo ya kisheria na kiutaratibu ya kulinda maslahi ya nchi katika ulimwengu unaohitaji sheria na akili. Na, kwake, BOT inaonekana ni sehemu muhimu ya kusimika hilo ikishirikiana na TRA na taasisi zingine. Na hata sheria inalitambua hilo, ndiyo maana kisheria Gavana wa BOT ni mjumbe wa Bodi ya TRA

Mwanamuziki mmoja wa enzi za 'Zilipendwa' aliwahi kuimba: "naelewa mazoea yana taabu." Pengine uwoga uliotukumba kutokana na uteuzi wa Profu Luoga unatokana na mazoea tu. 

Mabadiliko tuliyoyalilia sana mwaka 2015 si ndiyo haya 'jomoni'

3 comments:

Keyyula Kashaija October 24, 2017 at 5:13 PM  

Very observant! A great analysis!

Noverty Deograthias October 24, 2017 at 9:16 PM  

Kiongozi nimependa uchambuzi wako.

Noverty Deograthias October 24, 2017 at 9:16 PM  

kiongozi, nimependa uchambuzi wako.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP