Wednesday, September 5, 2018

Tangulia Mama Zippora Shekilango (1938-2018)

Tangulia Mama Zippora: Taazia ya Kijana Mwenye Hisia za Majuto 

Seif Mwarizo Abalhassan 

Jijini Dar es salaam kuna barabara moja mashuhuri kwa jina la 'Shekilango Road', ikianzia maungio ya barabara ya Morogoro, eneo la Nyumba za NHC, mkabala na Kiwanda cha Urafiki, ikipitia mitaa yote ya Sinza na kuishia maungio ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi kituo cha Bamaga. Wengi wetu tunalijua hili.

Ambalo watu wengi hawalijui ni kuwa barabara hiyo ya Shekilango imepewa jina hilo kwa ajili ya heshima na kumuenzi ndugu Hussein Ramadhani Shekilango, aliyekuwa Mbunge wa Korogwe (1975 - 1980), Mkoani Tanga na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekufa kwa ajali ya Ndege Mei 11, 1980 wakati akiiongoza kwa muda nchi ya Uganda mara baada ya vita vya kung’olewa kwa nduli Iddi Amin Dada. Barabara hiyo imepewa jina hilo mara baada ya kifo chake pamoja na wenzake sita.

Asubuhi tulivu ya Desemba 15, 2013 ilinikuta Kinondoni Morocco, mtaa wa Bwawani, varandani kwa Mama Zippora, mjane wa mzee Shekilango. Mkono wangu wa kulia ukipokezana kikombe cha chai aliyonikirimu (watu wa Tanga ni wakarimu sana) na kalamu yangu, nikiandika kila linalonivutia kutoka mdomoni mwake. Tulifanya mahojiano juu ya maisha ya mumewe, aliyekuwa pia meneja wa shirika la taifa la usagishaji (NMC) kabla ya kuwa mbunge.

Ilitokea sadfa (‘koinsidensi’). Siku hiyo ya mazungumzo yangu na Mama Zippora pia ilikuwa ni siku ya mazishi ya mzee Nelson Mandela, Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini ya Kidemokrasia na isiyo ya Kibaguzi. Tulizungumza huku tukitazama luninga iliyokuwa ikionesha mazishi hayo. Mazungumzo yetu yakikatika kila mara tulipoona jambo lililotuvutia kwenye luninga iliyokuwa ikionyesha mubashara tukio hilo muhimu ulimwenguni.

Mara baada ya hotuba ya taazia ya Rais wa Malawi, mama Joyce Hilda Banda - aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC wa wakati huo, ukaja wasaa wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa fahari kabisa kuieleza dunia juu ya kila hatua za kiutu, za kujitolea ardhi, rasilimali na hata watu ambazo Tanzania ilizichukua kwa ajili ya Ukombozi wa Afrika Kusini. Muda huo tulisitisha mazungumzo. Tukamsikiliza Kikwete (akisoma hotuba bora katika miaka yake yote kumi ya Urais).

Mara baada ya Kikwete akapanda jukwaani Komredi  Kenneth Kaunda, Rais wa kwanza wa Zambia huru, na swahiba wa Mwalimu Nyerere katika Nchi za Mstari wa Mbele kwenye Ukombozi (Frontline States). Ikumbukwe kuwa Makambi ya mafunzo ya Kijeshi ya ANC yalikuwa Tanzania (Kongwa na Mazimbu), wakati makao makuu ya ‘Ughaibuni’ ya chama cha ANC yakiwa Lusaka, Zambia. Hivyo, wakati Rais Banda akizungumza kwa niaba ya SADC, Rais Kikwete na Mzee Kaunda walizungumza kwa sababu nchi zao ndizo hasa zilizokuwa mstari wa mbele kuikomboa Afrika Kusini.

Mzee Kaunda alianza hotuba yake na wimbo wa ukombozi, “Yamike Madiba 🎼🎼....” Hisia na kumbukumbu za Mama Shekilango zikamrudisha nyuma miaka ya ujana wake. Akajikuta naye kwa hisia kali anaimba kibwagizo cha wimbo ule wa kuhamasisha Ukombozi uliokuwa unaimbwa na Kaunda. Ilikuwa raha, furaha na hisia kali mno za Msiba.

Baada ya hotuba ile ya Kaunda ikatubidi kuzima luninga ili tuendelee na mazungumzo yetu. Lakini muda huo sasa tukiwa hatujadili tena juu ya maisha ya mumewe, bali akajikita kunielezea juu ya historia ya ukombozi wa Taifa letu. Mama Zippora alikuwa mtu mzima tayari, akiwa amezaliwa mwaka 1938, hivyo ameyashuhudia mengi ya Taifa letu.

Katika mazungumzo yetu hayo ndipo kwa mara ya kwanza nilipolisikia jina George Magombe, Mwanadiplomasia mbobezi wa Tanzania, na Katibu Mkuu wa 2 wa Kamati ya Ukombozi (Liberation Committee) ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Nikivutiwa zaidi na simulizi za Mama Zippora juu ya namna Balozi Magombe alivyoshawishi ‘Azimio la Mulungushi’ pamoja na lile ‘Azimio la Mogadishu’, yaliyoacha mapambano ya Diplomasia kwenye kupinga Ukoloni na kuruhusu mapambano ya Kijeshi. Ni maazimio mawili hayo ndiyo yaliyomfanya Magombe ampishe Brigedia Jenerali Hashim Iddi Mbita katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Kamati ya Ukombozi.

Ilikuwa siku ya bahati kwangu. Nilijifunza kuhusu mumewe, ndugu Ramadhani Hussein Shekilango, pamoja na wenzake sita aliofariki nao ajalini, Balozi wetu nchini Uganda, Balozi A. Faraji Kilumanga, mwanadiplomasia wetu, FSO Iddi Msechu, pamoja na Wanajeshi wetu, Luteni Mallya, Luteni Luoga, Koplo Petro Kalegi Magunda na Private Stephen Mtawa. Mola awalaze pema mashujaa hawa wa Taifa letu.

Mama Zippora alikuwa mpambanaji wa usawa wa jinsia nchini. Mimi ni shuhuda wa jambo hilo. Mara baada ya mahojiano yetu juu ya mumewe, naye akanihoji kwa utani:

 “Unaniuliza kuhusu mume wangu tu? Hutaki kujua mimi ni nani? Au huamini kuwa mwanamke anaweza kuwa na ‘role’ kubwa kama mumewe?” 

Nikahemewa!

Tukaanza upya mahojiano. Sasa ikawa ni juu ya maisha ya Mwalimu, Mama, Mkuu wa Shule, Mpambanaji wa Haki za Wanawake na Mwanachama Mwandamizi wa Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP). Ni maisha yenye changamoto na mapambano ya kupigania haki za wanawake, kupigania nafasi ya mtoto wa kike kielimu na kuhimiza haja na wajibu wa kufanya mabadiliko ya kisera na kiutamaduni katika kuhakikisha ushiriki wa wanawake kwenye maamuzi, kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa. 

Mama Zippora ni Mwalimu Kitaaluma, aliyeanzia ngazi ya chini kabisa, na kisha kupanda mpaka kuwa mkuu wa shule za Wasichana za Zanaki, Msalato, Kisutu, Jangwani, Iringa pamoja na shule ya mchanganyiko ya Forodhani. Amewahi pia kuwa Afisa wa Elimu wa Mkoa wa Dar pamoja na Makao Makuu ya Wizara. Ana stori ndefu ya maisha inayohitaji wasaa wake kuielezea.

Kwa hiyo, kwa nini nimeandika haya? Hisia za kujutia, naam ‘guilty conscious’. Miaka mitano baada ya mahojiano yetu yale, Septemba 1, 2018 Mama Zippora Lukuiya Shekilango alifariki dunia, akiwa na umri wa miaka 80. Ni huzuni kubwa.

 Lakini sikuandika kuhusu mahojiano yangu naye. Sikuandika kabisa kuhusu maisha yake, mapambano yake ya kutoa elimu kwa mtoto wa kike pamoja na kupigania haki za wanawake nchini. Amefariki bila mimi niliyemhoji kueleza stori ya maisha yake, kwa miaka mitano!

Sina sababu ya kwa nini sikuandika juu ya mahojiano yetu haya. Ni uzembe? Uvivu? Kutokujali? Kutingwa na kazi? Au labda ni kwa sababu ya mfumo dume tu? Kwa nini nimeandika juu ya maisha ya Balozi George Magombe, Hussein Ramadhani Shekilango na Balozi Faraji Kilumanga? Wote wanaume? Na sijaandika juu ya Zippora Lukuiya Shekilango, mwanamke P]pekee niliyomhoji? 

Sina utetezi!

Namuomba radhi mama Zippora. Sikumtendea haki kabisa. Nilimkosea. Kumuomba radhi kunaweza kusiwe na maana kwa kuwa hayuko hai tena, lakini itanipa amani ya moyo. Na siku moja, Inshaallah, nitaandika juu ya maisha yake.

Jumamosi, Septemba 8, 2018 Mama Zippora Shekilango atalazwa mahali alipolala mumewe miaka 38 iliyopita, Jitengeni, Mombo, Korogwe, Tanga. 

Mola ampe pumziko, na aipe subira familia yake kwa msiba huu mzito.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP