Wednesday, October 31, 2018

Barua ya Wazi kwa Rais: GMO ni Sera ya Serikali?

Barua ya Wazi kwa Rais wa Tanzania: Je, GMOs ni Sera ya Serikali?


Mheshimiwa Rais;

Heri ya siku ya kuzaliwa! 

Kwa heshima na taadhima, niruhusu mimi mtoto wa mkulima mdogo na mwananchi wa nchi yetu tukufu nikusalimu. Hali yangu mimi na wanafamilia wenzangu, ambao ni wakulima wadogo nchini, si njema kabisa. Mheshimiwa Rais, kama ujuavyo, sisi ni takribani asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wote, na naamini kuna ndugu zako wa damu ambao ni sehemu ya jamii hii ya watanzania. 

Ukulima mdogo ndiyo uhalisia wetu. Hatuwezi kuukataa kwa sasa, japo wengi tuna matumaini ya kupiga hatua, kama serikali itatuwekea misingi thabiti. Lakini hali yetu ni ile Waswahili wanasema ‘bora ya jana kuliko leo.’ Mikakati ya kumkwamua mkulima mdogo nitaieleza katika kitabu changu, lakini kwa leo niruhusu tu nikuulize swali la kisera. 

Mheshimiwa Rais, tarehe 28  Septemba, 2018 Jijini Geneva, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilipitisha Azimio la Haki za Wakulima Wadogo. Azimio hili ni ushindi kwa wakulima wadogo duniani dhidi ya Makampuni hodhi katika sekta ya kilimo katika mapambano yaliyochukua zaidi ya miaka 17. Azimio hili linazungumzia haki za ARDHI, MBEGU, BAIOANUAI (Biodiversity) na SOKO LA NDANI LISINAJISIWE NA BIDHAA KUTOKA NJE.  

Kimsingi haki hizi zinaendana na Uhuru wa Chakula (Food Sovereignty) kwa nchi maskini, ambao ndiyo uhuru pekee tuliobaki nao. Kinachonishangaza Mheshimiwa Rais ni kuwa, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wakulima wadogo nchini, Tanzania haikuwakilishwa katika Azimio hili muhimu. Jumla ya nchi 34 zilikubali Azimio, nchi 11 zilikaa pembeni (abstain) na kama ilivyotegemewa, nchi zilizoendelea zilipinga Azimio hili. Mheshimiwa Rais, tulipitwa au hatujali? Namshukuru Mungu wa wanyonge Azimio limepita.

Lakini Mheshimiwa Rais, mienendo ya Serikali inatupa mashaka makubwa zaidi sisi familia ya wakulima wadogo. Naliongea hili kwa ujasiri kwa kuwa nimekulia kilimo na naishi na wakulima wadogo. Hata utafiti wangu wa uzamivu uliwalenga wakulima wadogo na unahusu Uhuru wa Chakula Tanzania. 

Mheshimiwa Rais, serikali imekuwa ikipigia chapuo teknolojia ya uhandisijini wa mazao ya GMOs nchini. Tumeliona hilo katika Programu ya ASDP II uliyoizindua hivi karibuni, ambayo inatamka wazi mwelekeo wa kilimo chetu kwa matumizi ya GMOs, siyo tu katika mimea, bali hata wanyama (ikanifanya niwaze majaliwa ya ng’ombe za rafiki zangu Wamasai). Angalau basi tukusikie kwa maneno yako, je, wewe ni shabiki wa teknolojia hiyo na kwamba ni mdau wa mradi ya GMOs katika utafiti unaoendelea Makutupora, ambayo sasa inahalalishwa hapa nchini kupitia vyombo vya habari?

Barua yafaa iwe fupi ili isomeke kwa haraka na kueleweka kirahisi. Hivyo, Mheshimiwa Rais, nitaandika kwa uchache kuhusu sababu kwa nini Tanzania haihitaji GMOs. Lakini ninazo makala ndefu za kitaaluma zinazohusu jambo hili. 

Sababu mojawapo ya kukataliwa GMOs inatokana na athari zake katika mazingira. Kwa mfano, katika utafiti uliofanywa na Mwanazuoni John Paul na kuchapishwa mwaka huu wa 2018, ikiwa na kichwa Genetically Modified Organisms (GMOs) as Invasive Species unaonesha kuwa GMOs ni viumbe vamizi. Huharibu mazao asilia, mimea mingine, wanyama na kuleta athari katika mazingira ya viumbe hai.

Hata katika elimu ndogo ya Kilimo tuliyojifunza sekondari, Mheshimiwa Rais, mahindi huzaa kwa uchavushaji. Kama mahindi ya GMOs na ya kawaida yatapandwa pamoja tutegemee nini? Kimsingi mahindi ya mbegu zisizo za GMOs yakiingiliana na ya GMOs yatapotea na kutuletea balaa kubwa la utegemezi huko mbeleni. Izingatiwe kuwa mbegu za GMOs hazirudiwi kupandwa zikatoa mazao. 

Mheshimiwa Rais, napenda kujua kama hayo majaribio ya Makutupora yanajibu wasiwasi huu. Kwamba mbegu zao za GMOs hazitaathiri mbegu zetu, mimea mingine na mazingira kwa ujumla! Au ni utafiti unaoonesha tu kuwa GMOs zitastawi nchini? Mheshimiwa Rais unisamehe kwa kusema hili, hata bangi, ule mmea tunaoupiga vita, bado unastawi katika nchi yetu tukufu, tena vizuri mno.

Kupotea kwa mbegu zetu [kutokana na kuingiliana na mbegu za GMOs] kutatufanya tuwe watumwa wa makampuni ya mbegu. Mheshimiwa Rais, naamini umefuatilia habari kuhusu kampuni ya Monsanto, ambayo sasa imenunuliwa na kampuni ya Bayer ya Ujerumani kwa zaidi ya shilingi trilion 120 (USD 62 bn). Monsanto imekuwa ikipigwa vita hasa Amerika ya Kusini kwa namna ilivyotaka kuwafanya watu wake watumwa wa chakula. Pale ambapo tutapoteza mbegu zetu za asili, au tulizoziendeleza muda mrefu kupitia taasisi zetu za utafiti, tutakuwa tumekubali kuwa mateka. 

Mheshimiwa Rais, wewe umekuwa ukipinga ubeberu kwa nguvu zako zote, na nisingependa hili la utumwa wa mbegu litokee katika utawala wako. Afrika Kusini, ambako waliruhusu GMOs tangu miaka ya 90, sasa zaidi ya asilimia 90 ya mahindi ni GMOs na wakulima wanalazimika kulipa ziada ya ada ya teknolojia kwa Monsanto. Pamoja na kubeparisha kilimo chao, bado Afrika Kusini hawajaweza kutokomeza njaa.

Suala la utamaduni wa chakula ni muhimu pia liongelewe katika muktadha huu. Kuna ladha, harufu nzuri na uasili wa chakula. Kama ujuavyo, Mheshimiwa Rais, hizi ni sifa pekee zinazotofautisha chakula chetu. Na tunapaswa kuvitunza vyakula hivi kwa choyo kubwa - hasa kwa kuwa sisi ni kitovu cha utalii Afrika. 

Tukisoma baadhi ya makabrasha na shuhuda za wageni, tunaona watalii wanakizungumzia chakula chetu katika namna ya sifa ya pekee. Mheshimiwa Rais, pengine unakumbuka kuwa, mmoja kati ya watetezi wa GMOs Robert Paarlberg aliwahi kusema mwaka 2009 kuwa “chakula kilichozalishwa kiasili (organically) kina ladha na harufu ya kuvutia zaidi kuliko vyakula vya GMOs ndiyo maana nchi za Ulaya hazitaki GMOs" lakini "masikini wa Afrika hawapaswi kuwa na uchaguzi” Je, ni kweli tumefika sehemu ambayo hatupaswi kuwa na uchaguzi kwa kuwa sisi ni maskini? 

Mheshimiwa Rais, katika makala yenye kichwa No Scientific Consensus on GMO Safety iliyochapisha wa wanasayansi 15 kwa pamoja katika Jarida la Environmental Sciences Europe mwaka 2015, tunaelezwa kwamba japo kumekuwa na jitihada za kuuaminisha ulimwengu kuwa GMOs ni salama kwa afya, lakini kimsingi hakujawa na muafaka wa usalama wa GMOs. Na kuna baadhi ya tafiti zilizoenda mbele kueleza kuwa GMOs zina madhara kiafya. Baadhi ya madhara ya afya yanayotajwa ni pamoja na uzio na saratani. Je, utafiti unaofanyika Makutupora unalenga kuleta majibu ya wasiwasi wa madhara ya afya yatokanayo na GMOs?

Monsanto imeshtakiwa zaidi ya mara hamsini huko Marekani na hivi karibuni ilipatikana na hatia, wananchi wakiilalamikia bidhaa zao kuwaleatea saratani. Kuhusu chakula cha GMO jibu la kampuni hiyo limekuwa hilo hilo kuwa hawalazimiki kisheria kudhibitisha kuwa vyakula vyao havina madhara. Wanaojiita wanasayansi wetu nchini hawatuambii ukweli, labda kwa maslahi yao binafsi. Lakini katika majadiliano tuliyofanya HakiArdhi hivi karibuni, mmoja wa wanasayansi hao, baada ya kubanwa na wakulima, alikiri kuwa uangalifu unahitajika hasa katika mimea iliyobadilishwa kuzalisha sumu ili kuua wadudu. 

Mheshimiwa Rais, Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa Tanzania bado hatujafikia hata asilimia 30 ya matumizi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu. Bado tumekuwa tukizalisha zaidi ya asilimia 120 ya chakula kinachohitajika nchini. Wiki tatu zilizopita nilikuwa Mkoa wa Rukwa (Sumbawanga) na nilikutana na Wazalishaji wanaolalamikia soko la mahindi na siyo changamoto za uzalishaji. Tena kuna waliovuna mahindi ya kutosha bila hata kutumia mbolea. 

Lakini watu wa GMOs wanatuletea taarifa kuwa kuna uzalishaji mdogo sana na mahindi yanashambuliwa sana na wadudu. Kimsingi wanatangaza Hali ya Hatari (National Emergency) kwa jinsi wanavyotuonesha wadudu wala mahindi katika video zao. Mheshimiwa Rais, ni kweli tumefikia huko? Kama ni kweli mbona hujatutangazia hali ya hatari ili basi GMOs tuipokee kama hatua yetu ya kupunguza kifo cha haraka? Na kama siyo kweli, kwa nini tunalazimishwa kuruka kutoka kutumia mbegu za asili kwa asilimia 80 za sasa hadi GMOs, teknolojia ya juu kabisa wakati hatujaweza kuvuna tija itokanayo na mbegu bora za OPVs na Hybrid? 

Kuna agenda gani hapo? Tunakimbilia wapi? Tunapitwa na nini?

Mheshimiwa Rais, sipendi nikuchose sana. Naomba niulize swali moja la mwisho. Ubora tulio nao kama nchi ukilinganisha na nchi zingine (Comparative Advantage) wanaouongelea wachumi au kile wasomi wa fani ya Biashara wanachokiiita eneo la ubora (niche) wetu lipo katika nini? Sidhani kama tunaweza kushindana na Marekani katika kuzalisha mahindi ya GMOs, chakula chenye unyanyapaa duniani kote. Sisi tunapaswa kuwa msingi wa chakula salama Afrika Mashariki na kwingineko duniani. Wakulima wetu wanapaswa kuwa msingi wa kuzalisha chakula hiki na kunufaika kama ilivyo sasa, ambapo soko bado si la uhakika.

  Katika utafiti wangu  nilitembelea vituo vya utafiti wa kilimo. Nikiri kuwa ni taasisi nyeti na zina wataalam (japo wametelekezwa) wanaoweza kutusaidia katika kuboresha mbegu zetu za asili kama wakiwezeshwa. Sote tunajua mbegu bora siyo lazima iwe ya GMOs.

Mheshimiwa Rais, tukumbuke kuwa wakati wa Utawala wa Rais Dkt. Jakaya Kikwete, mradi wa GMOs wa WEMA haukuanza nchini  japo ulipaswa kuanza 2008. Hii ilitokana na kifungu kinachohusiana na dhamana ya uharibifu kijulikanacho kwa Kiingereza kama ‘strict liability’ kilichopo katika kanuni zetu za usalama wa viumbe na uhai (Biosafety). Kifungu hiki kilisema mtu atakeyeingiza GMOs nchini atawajibika moja kwa moja kwa madhara yoyote yatakayotokana na GMOs kiafya, kimazingira na kiuchumi.

Hiki kifungu kiliwachelewesha watu hawa wa WEMA kuanza utafiti mpaka mwaka 2016 Serikali ilipolegeza masharti na kuweka kifungu kinachosema ‘strict liability’haitatumika katika utafiti. Kama GMOs ni kitu chema kama WEMA unavyodai na ni ukombozi wetu, waliogopa nini kuanza 2008 hadi wakashawishi kanuni zibadilike? Hata sasa wanadai sheria zetu zinawabana wanataka tulegeze zaidi watuletee balaa tushindwe pa kuwabana.

 Walaji wa chakula kinacholimwa na wakulima wadogo hawapo salama pia. Muda si mrefu tutaanza kuona maduka makubwa (supermarkets) za vyakula vya asili (organic food) ambavyo watu wa kada ya juu tu ndio pekee watamudu kununua.  Wameshaanza na madogo madogo. Tunaendelea kutengeneza matabaka kwa maslahi ya mwekezaji.

Mheshimiwa Rais, huenda barua hii haitakupendeza. Najua pia barua hii haitawapendeza wadau na watunga sera wanaopigania GMOs izidi kutamalaki nchini. Hakika itaichukiza kampuni husika inayowekeza katika mradi wa WEMA huko Makutupora.

Wanatudhihaki kuwa sisi tunapinga sayansi. Lakini ni sayansi zipi tumezipinga hapa nchini? Kama alivyowahi kusema mwanazuoni nguli Karl Polanyi  mwaka 1944, hatuwezi kuiruhusu teknolojia ya kinyonyaji na inayokusudia kunufaika na majanga ya watu itamalaki.

Mheshimiwa Rais, nakushukuru kwa kusoma hii barua. Hatimaye nimetimiza wajibu wangu. Nimesema ukweli na sina haja ya kujificha.

5 comments:

A. Massawe October 31, 2018 at 1:23 PM  

Natarajia jibu la Mheshimiwa Rais litakuwa ni lile linalotutaka tuunde kampuni itayokuwa ikishindanisha mbegu zetu za asili na GMOs zao kwenye soko la mbegu duniani, na tukishindwa/kama haiwezekani tushirikiane na wanaozizalisha GMOs kisayansi na kiteknolojia.
Yaani badala ya kulilia kinga ya Mh. Rais dhidi ya uwepo GMOs shindani hapa nchini, tuupe ushirikiano ili tuwe sehemu ya wanaofaidi uwepo wa GMOs duniani.

Ni jibu la Mh. Rais litakalokuwa limezingatia kwamba madhara yatokanayo na matumizi ya GMOs yatakuwa sawa tu na yale yanayokabilika kisayansi na kiteknolojia yatokanayo na utokomezwaji wa mbu wanaosambaza gonjwa la malaria, au binadamu kuwekewa kinga dhidi ya gonjwa la malaria.

Ni jibu Litakalokuwa pia limezingatia kwamba binadamu ni tofauti na wanyama wengine kwa mnyama pekee anayedumisha uwepo wa anavyovitegemea hapa duniani kwa njia ya kuviboresha kiendelevu kwenye mazingara yanayobadilika badilika kiendelevu.

NeyK November 1, 2018 at 11:17 PM  

Barua hii imenigusa Sana. Siku hizi nchi zilizoendelea zinarudi kwenye vyakula vya asili Kwa ajili ya Kia na afya Nora, ila Sisi ndio Kwanzaa tunalaghaika na Luanda kuiga njia ambazo wanazitupa. Had Monsanto wanajenga soko jipya LA watumwa WA mbegi, na Susi tunaingia kichwa kichwa kisa misaada Kwa hisani ya wary Fulani. Ni vizuri kuhoji na kuamka. Asante mwanazuoni Kwa makala hii.

Unknown November 2, 2018 at 9:20 AM  

Hakika Tanzania na Africa tunapaswa kuwa makini na mapokezi na matumizi ya GMO! Ni bora tukahimiza selective breedi, matumizi bora ya mbolea, na kufuata kanuni bora za kilimo! Kukubali GMO ni kukubali kubadili asili na kwa uchumi na teknolojia yetu ndogo ni ngumu kukabiliana na madhara GMO kama vile kansa! J karoti za njano/ orange ni GMO?

Unknown November 4, 2018 at 10:25 AM  

Niseme tu huu ni uzalendo namba moja, afya, uhai, uchumi,brain sovereignty, uanazuoni wako ni wenye tija sana, thank you very much, the real sense of education has truly manifested!Asubisye, E

Unknown November 5, 2018 at 7:56 PM  

Wanazuoni tusome Machapisho na tufanye tafiti za kutosha ili unapopingana kwa Hoja basi hoja zijae na zisheheni takwimu za Kitafiti kama hivi. Tukibishana kwa maneno na fikra zetu tuliangamiza Taifa letu badala ya kulisaidia. Nimependa Mwandishi ameweka na Uchumi ndani yake alipotaja Compartive Advantages. Tukijikita hapa kwenye Comparative and Absolute Advantage kwa upana wake bila shaka tutawasaidia Watunga Sera na Watoa Maamuzi wetu kufanya maamuzi yenye uweledi yanayoakisi takwimu halisi zilizopo. Hakika Barua hii inapasa iwe iumechokoza Mjadala Mkali wa Kitaaluma na Kijamii pia maana imejaa Maswali ya Msingi sana ndani yake. Haya Wanazuoni shime tuisome na kuijadili kwa pamoja. Tusibaki Nyuma halafu watoa Maamuzi wakishaamua tunaanza kulalamika. Wakati wa Kuwapa Takwimu ni sasa ili wanapofanya Maamuzi wawe wanazifahamu Takwimu hizo.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP