Tuesday, October 16, 2018

Hoja Kinzani: Mke si Kahaba - Tusipoteze Mwelekeo

Mke si Kahaba; Tusipoteze Mwelekeo
Na Armstrong Matogwa[1]

Utangulizi
Lengo la makala haya ni kujibu hoja iliyotolewa na mwanasosholojia na mwanaharakati wa kutetea haki za Wanawake, Bi. Mwanahamisi Singano (Mishy) katika Makala yake yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa Udadisi blogspot tar. 13 october 2018, akidai kwamba wanawake wote ni makahaba kwa kuwa wote wanautumikia mfumo dume. Makala hayo yenye kichwa “We are all Prostitutes”yaani ‘Sisi wote ni Makahaba’ yanalenga zaidi kupinga kitendo cha askari polisi kuwakamata wanawake kadhaa na kuwaanika katika vyombo vya habari kwa tuhuma za kujihusisha na ukahaba (kibiashara). 

Kiini cha hoja ya mwandishi ni kuwa wanawake hao hawana hatia kwani kitendo cha ukahaba wanachofanya hakina tofauti na kitendo cha mwanamke mwingine ambaye yuko kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanaume (urafiki au ndoa), kwani wote wanauza penzi lao kwa wanaume; tofauti ni kwamba, Kahaba anauza “rejareja” na anachukua pesa baada ya tendo la ngono (postpaid) wakati wanawake walioolewa wanauza “jumla” kwa njia ya kutolewa mahari na wanachukua pesa yao kabla ya ngono (prepaid). Mwandishi anasisitiza kuwa aina zote mbili za ukahaba (wa jumla na wa rejareja), zinasukumwa na mfumo dume na kwamba jamii ione kuwa aina zote mbili ni tatizo. Kupambana kuuondoa ukahaba wa rejareja na kuuacha ule wa jumla ni kukosa maarifa. Hivyo tunapopambana na ukahaba kama jamii tulenge kuubomoa mfumo dume ambao ndio kiini cha aina zote mbili za ukahaba. 

Maoni yangu
Kwanza nampongeza mwandishi kwa kuweza kutoa mawazo yake na kujaribu kushawishi umma juu ya uhusiano wa ukahaba na mfumo dume. Ni katika mijadala kama hii ambapo watu huchangamsha akili zao na kukuza uelewa wa mambo mbalimbali. Hata hivyo, sikubaliani na mtazamo wake juu ya ukahaba hasa katika jamii ya Tanzania/Afrika. Hoja zangu nimeziweka katika mpangilio wa namba kamba ifuatavyo;

1.    Ukahaba ni nini? 
Kwa maelezo ya mwandishi, msomaji anaelewa kuwa ukahaba ni kitendo cha mwanamke kuwa na mahusiano ya mapenzi na mwanaume bila kujali mahusiano hayo ni ya siri au ya wazi, halali au si halali, ya muda mfupi au ya muda mrefu, yanalenga kupata pesa au kupata heshima n.k. Kwa mtazamo Wangu, mwandishi hayuko sahihi kwani kwanza, maana yake ya ukahaba haitofautishi aina za mahusiano ya mwanaume na mwanamke kwa kuzingatia thamani ya mahusiano hayo (kijamii) katika jamii husika na mchango wake katika historia ya maisha ya mwanadamu. Asili imeweka viumbe vyenye jinsi mbili yaani -me na -ke kwa ajili ya kuzaliana ili kuendeleza kizazi chao. 

Hivyo, mahusiano ya mwanamke na mwanaume katika jamii yanatakiwa kuakisi asili hiyo, yaani kuzaliana ili kuendeleza kizazi cha wanadamu hapa duniani. Bila hivyo, maana yake sisi tusingekuwepo wala hakutakuwa na wanadamu wengine baada yetu. Na hii ndio thamani pekee ya mahusiano ya mapenzi kati ya mwanaume na mwanamke inayotakiwa kulindwa na kuenziwa muda wote.

Katika kuratibu thamani hiyo (ya kuzaliana) wanadamu katika jamii mbalimbali waliweka na wanaendelea kuweka taratibu kadhaa. Taratibu hizo ambazo kwa pamoja zinaitwa ‘mila na desturi’ zinaakisi mazingira ya jamii husika. Neno mazingira hapa linamaanisha mfumo wa uzalishaji mali (mode of production) ambao nao umebeba mazingira ya asili (ecology) na mazingira/mahusiano ya kijamii (social relations). Kwa minajili hiyohiyo wakati binadamu anahama kutoka katika Ujima kwenda Ukabaila alijikuta analazimika kuzalisha na kumiliki mali peke yake (si kundi kama ilivyokuwa awali). 

Hivyo, akamiliki ardhi, akamiliki mifugo na zana za uzalishaji. Mazingira hayo hayo yakamlazimu kumiliki wanawake na watoto, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika uzalishaji mali na kuendeleza kizazi na urithi wa mali za kaya. Mazingira haya yakasababisha mgawanyo wa majukumu kulingana na jinsi na umri; na hivyo kwa kiasi kikubwa kazi za mwanaume hazikulingana na za mwanamke na za watoto. 
  
Mfano katika “jamii” ya Wagogo
Ninatoa mfano katika jamii ya wagogo kwa kuwa ndio jamii niliyoiishi na kushiriki katika kazi mbalimbali hasa katika kilimo na ufugaji, na pia nimeitafiti mara kadhaa. Kabla ya ujio wa wakoloni wagogo wote walikuwa ni wafugaji-wakulima. Hii ilitokana na maarifa waliyokuwa nayo juu ya ikolojia ya eneo lao kwamba ili kuweza kuishi katika eneo kame kama la Dodoma na Singida ni lazima kujihusisha na shughuli hizi mbili kwa pamoja. Ushahidi wa wapelelezi mbalimbali unaonesha kuwa kulingana na maarifa hayo katika karne ya 17 na 18, jamii ya wagogo ndiyo ilikuwa jamii “tajiri zaidi” kuliko jamii nyingine yoyote katika njia ya kati ya msafara wa watumwa, yaani kuanzia Bagamoyo, Mpwapwa, Tabora, mpaka Ujiji.  

Hayo yaliwezekana si kwa sababu walikuwa na matrekta au mashine lakini kwa kufanya kazi. Kwa mfano, kazi ya kuandaa shamba jipya (kufyeka pori), kutafuta zana za kuzalishia mali kama vile majembe, mapanga, shoka n.k., kulima mashamba ya mbali, kuchunga mifugo katika mapori ya mbali, na kuchimba visima hizi zilikuwa (na bado ni) kazi za mwanaume. Kupika, kuteka maji, kupalilia, kusaga, kuchunga ndama maeneo ya nyumbani, na kukamua maziwa hizi zilikuwa (na bado ni) kazi za mwanamke akisaidiwa na watoto. 

Katika mazingira haya watoto wa kiume walikuwa “wanapendwa” zaidi kuliko watoto wa kike kwani ukiwa na mtoto wa kiume kwanza atamsaidia mume (baba yake) kufyeka mapori zaidi hivyo familia inakuwa na mashamba mengi. Vilevile watoto wa kiume wataweza kuswaga mifugo na kwenda kutafuta malisho mbali zaidi (maporini) kwani ni rahisi kwao kupambana na hatari za huko. Tatu, watoto wa kiume wangesaidia kuzaa watoto wengi zaidi hivyo kuongeza nguvukazi katika kaya. Wapelelezi wanasema kuwa kaya za wagogo katika karne ya 17 na 18 zilikuwa na watu 100 mpaka 200. Wengine walisema kaya moja ilikuwa kama kijiji. Hao walisaidiana katika mgawanyo wa kazi kama ilivyoainishwa hapo juu. 

Katika mazingira hayo, mtoto wa kike “katika kaya” (sio katika jamii) fulani hakupewa kipaumbele kwani mara nyingi ilimpasa kuolewa na kwenda katika ukoo/kaya nyingine. Huku kulitafsiriwa kama kuhama ukoo. Uhamisho huu haufanyiki kienyeji, kulikuwa na utaratibu maalumu ujulikanao kama kuguma nitaueleza hapo baadaye. Mtoto wa kike anapoolewa kuna mambo mawili hutokea, kwanza ukoo/kaya ya binti inakuwa na hisia mchanganyiko. Kaya ina furaha kwa sababu binti yao anaolewa hivyo ni heshima kwa kaya (kumbuka kwamba binti anayepata mimba kabla ya ndoa anaitia aibu kaya), lakini pia ni furaha kwa kuwa kaya/ukoo unapata mahari. Huzuni huwa haikosi kwa sababu wanampeleka binti katika ukoo mwingine, wanakuwa hawana mamlaka naye tena, hata wakimhitaji ni lazima waombe ruhusa kwa mumewe. 

Hii inamaanisha kuwa si kweli kuwa mtoto wa kike alikuwa hapendwi au anaonekana ni mzigo katika kaya (kama wanaharakati wa kimagharibi wanavyojaribu kutuaminisha), la hasha bali ukiangalia mfumo wa uzalishaji mali uliopo katika ukoo wake anakosa thamani ya kiuchumi lakini anaongeza thamani ya kiuchumi katika ukoo mwingine. Hivyo, ukitizama mchakato huu kijamii bado unaona thamani ya mwanamke imezingatiwa. Na ndio maana siku ya kuolewa huyu binti ukoo ule unaomuoa unakuwa na furaha sana na kuimba;

“Chamsola chamsola, msaji wetu chamsola, wakunega malenga chamsola, wakuvuga ugali chamsola, wakulela wana chamsola, mkochi wetu chamsola.” 

Yaani, “tumemchukua tumemchukua, msagaji wetu (kumbuka kazi ya kusaga nafaka kwenye jiwe ili kuwa unga ilikuwa ya mwanamke), tumemchukua mchotaji wa maji tumemchukua, msongaji ugali (mpishi) tumemchukua mzaaji wa watoto tumemchukua, mlezi wetu tumemchukua.”

Kwa waoaji hii ni siku ya furaha sana kwa sababu kama wimbo unavyosema, mwanamke alithaminiwa kwa kuwa ndiye alitekeleza majukumu hayo sawa sawa kulingana na mfumo wa ukabaila ulivyo na sio mfumo dume. Hivyo, si kweli kwamba mtoto wa kike hana au hakuwa na thamani katika jamii za kiafrika. Wanaharakati wengi huangalia thamani ya mtoto wa kike “katika kaya” au familia tu lakini hawaioni thamani hii katika jamii ikihusianishwa na mfumo wa uzalishaji mali uliopo. Kuzaa na kulea watoto ni thamani ya mwanamke kimfumo na ndio maana katika ukabaila kama mwanamke hazai hurudishwa kwao au mwanaume huruhusiwa kuoa wanawake wengine (mitala). 

Nne, katika jamii ya kigogo mtoto wa kiume (hasa mkubwa) ndiye mrithi wa mali zote za baba yake. Mtoto huyo hupewa mamlaka yote ya kusimamia mali na kutunza wadogo zake. Watoto wa kiume ndiyo hugawiwa mali, kwa sababu ilisadikika kuwa watoto wa kike mali zao huzikuta kwa waume zao. Mali hizo kama ni mashamba au mifugo huwa ni mali za ukoo/kaya hata kama atapewa mwanaume azimiliki. Kumbuka dhana ya umiliki katika jamii ya wagogo (na jamii nyingi za waafrika) haimaanishi umiliki “binafsi” bali umiliki kwa niaba ya kaya/ukoo. 

Na ndio maana wanaume hawa hawakuruhusiwa kuuza au kuwapa watu wengine mali zao bila ukoo/kaya kuruhusu kwani wao ni wawakilishi tu, hawana mamlaka kamili. Mama (Mwanamke) alimiliki mali hizo kupitia mgongo wa mumewe na hata mumewe akifa mamlaka anapewa mtoto mkubwa wa kiume ili kuhakikisha kwamba mali hazipotei au haziendi katika ukoo mwingine kama mama ataamua kuolewa na mwanaume wa ukoo mwingine. Kwa mantiki hiyo hiyo wanawake walirithiwa na ndivyo kazi na majukumu yaligawanywa.
  
2.    Je, mwanamke anayeolewa ananunuliwa? Je, anafanya ukahaba wa Jumla/Kabla ya malipo?
Maswali haya yanahitaji maelezo kuhusu dhana nzima ya mahari. Kama tujuavyo, mahari ni utaratibu uliowekwa unaomwezesha mwanaume kumchukua mwanamke na kwenda kuishi naye pamoja (hasa kwa jamii zinazodaiwa kufuata mfumo dume). Kila jamii in utaratibu wake katika hili. Kama nilivyoeleza hapo juu, mchakato huu katika jamii ya wagogo hujulikana kama kuguma. Kuguma ni kitendo cha kutoa mahari (ndima) ambacho hujumuisha pande mbili za muoaji na muolewaji. 

Mchakato wa kuguma huanza kwa upande wa mwanaume, inawezekana wazazi/ndugu wakamchagulia kijana wao binti wa kuoa au kijana akachagua mwenyewe kisha akapeleka taarifa kwa wazazi/ndugu. Kama chaguo ni la kijana basi wazazi/ndugu hutuma wajumbe maalumu kuchunguza tabia za binti aliyependekezwa pamoja na tabia za jumla za ukoo wao. Binti mwenye tabia kama uasherati, uvivu, uchawi, au mwenye magonjwa ‘makubwa’ kama kifafa au kikohozi kisichoisha hawakupendekezwa kuolewa. 

Baada ya wazazi/ndugu wa mume kuridhishwa na tabia za binti aliyependekezwa kuolewa basi mchakato wa kuguma unaendelea. Kwa upande wa mwanamke pia wazazi/ndugu wana nafasi ya kushawishi au hata kulazimisha binti yao kuolewa. Huko zamani hii ilifanyika kwa sababu wazazi/ndugu waliona binti yao anakuwa mkubwa kiumri lakini hakuna waoaji. Hivyo, wazazi/ndugu walichukulia hiyo kama ni mkosi ambao licha ya kuwatia aibu kama ukoo lakini inachangia mabinti zao kuwa waasherati. 
 
Kikao cha kuguma huhusisha ndugu wa pande mbili. Wanaoguma ni upande wa mwanaume, hueleza nia yao ya kuja kuoa na kisha upande wa mwanamke wakikubali huwapangia kiwango cha ndima (mahari). Kiwango cha ndima hubadilika kulingana na mabadiliko (madogo na makubwa) ya mfumo wa uzalishaji mali. Kwa mfano, kabla ya karne ya 17 ndima/mahari katika jamii ya wagogo ilikuwa ni kipande cha nguo, karne ya 17 ndima ilikuwa ni jembe la mkono na kuanzia karne ya 18 ndima ilikuwa mifugo. Mambo haya yamedumu hadi hivi sasa ambapo wengine ndima hujumuisha vitu vyote vitatu, wengine viwili na wengine hubaki na mifugo pekee. 

Kwa hiyo mazungumzo ya ndima (mahari) hujikita hapo; upande wa mwanamke wanasema “tupeni ng’ombe kumi” upande wa mume wanasema “hatuna kumi tunazo sita”. Mjadala huendelea mpaka watakapoafikiana. Mazungumzo haya huwa hayahusishi wazazi wa binti au muoaji moja kwa moja bali ndugu wengine; wazazi wao huwa wasikilizaji tu. Kikao hiki hakimuuzi binti bali kazi yake ni kuhalalisha binti atoke kwa wazazi wake aende kwa mumewe kwa njia ya maridhiano na heshima. Kiwango cha ndima kitakachotolewa huafikiwa na wote katika mazungumzo ya urafiki/undugu na si mazungumzo baina ya muuzaji na mnunuzi. Kwa jinsi hiyo hakuna muoaji aliyeshindwa kuoa kwa sababu “hakuiweza bei” (japo siku hizi mambo hayo yameanza kujitokeza) kikao cha kuguma kilihakikisha ndoa inafanikiwa. 

Hivyo basi, tendo la kuguma na kutoa mahari lina maana zifuatazo. Kwanza, ni tendo la heshima la kuunganisha undugu. Ni kwa mara ya kwanza ndugu wa pande mbili wanakutana hapa na kufahamiana zaidi. Pili, ni mchakato unaotambua kuwa binti muolewaji ana kwao, ana wazazi na ndugu ambao wamemlea; hii huepusha waoaji kuoa “wanawake wasiojulikana au wanawake kuolewa na “wanaume wasiojulikana”. Tatu, kwa kuwa binti muolewaji ana ukoo wake ambao mume ameutambua na ameridhika nao, hivyo ndima ni kielelezo cha shukrani kwa wakwe zake na kutambua mchango wao katika kumlea vema binti yao. Nne, mchakato huu huashiria kuwa wazazi wa binti wamejivua rasmi mamlaka ya kumlea, kumtunza na kumlinda binti yao na kwamba mamlaka hayo sasa yanahamia kwa mumewe. Tano, kwa upande wa binti muolewaji wazazi/ndugu zake hawawezi kusema aolewe bila kutolewa ndima kwani hii hutafsiriwa kama binti yao hawampendi au wamemchoka. Vile vile waoaji nao hawawezi wakamchukua binti bila kutoa ndima kwani hutafsiriwa kama ni dharau, yaani ukoo wa binti wamewadharau waoaji kuwa ni masikini wa kutupwa. Na ndio maana mahari ikikubaliwa labda ngombe 8 muoaji huwa halazimiki kutoa zote, ni busara akatoa 6 au 7 ili hizo zinazobaki liwe deni lake la kudumu na hiyo inamaanisha anawaheshimu wakwe zake.  

Mambo yote hayo yamejengwa katika mfumo wa maisha yao ambapo tafsiri ya heshimana dharau ipo katika undugu, katika utu, na katika kutambua thamani ya mwanamke/mwanaume katika kuendeleza kizazi cha mwanadamu na hasa ukizingatia mfumo wa uzalishaji mali uliopo. 

Maelezo haya yote kwa ujumla yanatosha kujibu hoja kuwa katika jamii ya wagogo (na wengine wanaofanana) mwanamke hauzwi wala hanunuliwi bali anatambulishwa na kuchukuliwa kwa heshima kwa ajili ya kwenda kuendeleza kizazi cha ukoo wa mume wake na jamii kwa ujumla. Katika jamii nyingi za kiafrika pamoja na kupitia katika ukabaila (wa aina mbalimbali), ukoloni na hata sasa uliberali Mamboleo, bado zinajitahidi kutunza heshima hii ya mwanamke; kwamba mwanamke asifanyike bidhaa wala asiuze utu/uke wake ili tu kupata fedha. Hicho kinachoitwa mfumo dume huko nyuma kimejitahidi sana kuitetea heshima hii ya mwanamke na kamwe hakikutaka mwanamke atumike kama chombo cha starehe bali atimize wajibu wake wa kuendeleza kizazi cha wanadamu. Kama mfumo dume ndio unasababisha ukahaba wa rejareja basi huko zamani ukahaba huo ungekithiri zaidi kuliko sasa. 
  
3.    Ukahaba na mfumo wa uzalishaji mali
Katika jamii ya watanzania mahala pengi ukahaba hupambanuliwa kama ni tabia ya mwanamke kuwa na uhusiano wa kimapenzi usio rasmi/usiotambulika kijamii. Mara nyingi hushiriki mapenzi hayo na mume zaidi ya mmoja na pasipo kuwa na lengo la kuzaa mtoto/watoto. Katika siku za hivi karibuni mwanamke hufanya ukahaba ili kupata pesa (za kujikimu au kufanya starehe) hivyo hutafuta wanaume wenye pesa. Mwanaume anayeshiriki ngono na kahaba haitwi kahaba bali buzi, danga na majina mengine yafananayo. 

Kuna aina nyingi za ukahaba lakini zinazojulikana sana ni mbili; ile ya mwanamke kuuza penzi kwa mwanaume mwenye pesa ili apate kuishi, au mwanamke kununua penzi kutoka kwa mwanaume ili apate starehe. Makala ya mwandishi (Mwanahamisi Singano) ilijikita zaidi kwenye maana hii ya kwanza ambayo ndiyo maarufu. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba kwa nini aina hii ya ukahaba inaongezeka? Kwa nini wanawake hawa waishi kwa kuuza miili yao? Je, kwa nini wanawake wengine hawafanyi ukahaba?
 
Maswali haya yote yana lengo la kueleza chanzo cha ukahaba. Wanaharakati na wanazuoni hutoa majibu mbalimbali; wengine husema inasababishwa na mfumo dume, wengine husema ni utashi wa wanawake n.k. Hawa wote hueleza “uongo”. Majibu sahihi hutolewa na wanazuoni wa mrengo wa kushoto (kwa majina yao mbalimbali) ambao huona kuwa ukahaba ni tabia ambayo inatokana na mfumo wa uzalishaji mali uliopo. Katika historia ya mwanadamu hakuna mfumo wa uzalishaji mali uliokuza sana tabia ya ukahaba kama ubepari na hasa uliberali mamboleo. 

Kwa mfano, Marx(1844) anaonesha uhusiano uliopo kati ya ukahaba na mfumo wa ubepari na anasema;Hapo anamaanisha kuwa ukahaba wa mapenzi ni kielelezo tu cha ukahaba wa wafanyakazi wakihangaika huku na huku kutafuta kazi kwa maana ubepari ulitengeneza mazingira magumu kwa watu masikini kupata kazi. Katika mtazamo huo huo, Hunter (2002) kwenye makala yake ya The Materiality of Everyday Sex: Thinking Beyond Prostitution anaeleza jinsi gani ubepari ulivyosababisha kukua kwa biashara ya ukahaba huko Afrika Kusini. Van der Veen (2001) naye katika makala yake ya Rethinking Commodification and Prostitution anaeleza jinsi gani mfumo wa Uliberali Mamboleo ulivyofanya mapenzi kuwa bidhaa. 

Katika mfumo ambao unatukuza ukuaji wa soko kuliko utu makahaba wanafanyika kuwa watumwa kama vile wafanyakazi na wavujajasho wengine wanavyoteseka. Mfumo wa ubepari na hasa katika uliberali mamboleo umelenga kuwamasikinisha watu wanyonge kwa kupora rasilimali zao kijanja. Hivyo, wanyonge wengi hasa wanawake wanajikuta hawana rasilimali ya kutegemea isipokuwa miili yao. 

Japokuwa wapo baadhi ya wanaharakati wanaoona ni heri mwanamke kuwa kahaba kuliko kuolewa, ushahidi wa kisosholojia unapingana na hoja hii. Kwa mfano Linda Singer (1993) anaona kuwa makahaba wana unafuu wa maisha kwa kuwa wanajiamulia wenyewe namna ya kufanya mapenzi, wapi na wakati gani. Anasema, hii ni nzuri ukilinganisha na wanawake walio katika ndoa ambao hisia zao za kimapenzi zinatawaliwa na waume zao. Kwa maoni yangu mtazamo wa Linda ambao pia unaendana na mtazamo wa Mwanahamisi siyo sahihi. 

Wote hawa wanashindwa kuelewa ni jinsi gani nguvu ya soko inavyotawala maisha ya wanadamu bila kujali wameoa au makahaba. Na kimsingi kushabikia ukahaba (wa rejareja ambao ndio ukahaba kamili) ni kushabikia utukufu wa nguvu ya soko na jinsi inavyofanikiwa kuua taasisi kama kaya/familia. Swali la kujiuliza ni; je, wanawake wote wakiwa makahaba kizazi cha wanadamu kitaendelezwa na nani?

Hitimisho
Makala haya yalilenga kujibu hoja iliyotolewa na Mwanahamisi Singano kuwa “sisi wote ni makahaba” kwa kuwa wote tunatumikia mfumo dume. Kuwa wanawake walioolewa waliuza mapenzi yao kwa bei ya jumla wakati makahaba wengine wanauza rejareja. Na kwamba adui wa ukahaba kwa aina zote mbili ni mfumo dume na hivyo tuelekeze juhudi zetu zote katika kuubomoa mfumo dume. Ushahidi wa kisayansi umeonesha kuwa hoja ya Mwanahamisi si sahihi katika maeneo yafuatayo. 

Kwanza, anaona mfumo dume ndio chanzo cha matatizo kitu ambacho si kweli. Makala haya yameonesha kinagaubaga kuwa hicho kinachoitwa mfumo dume ni sehemu ya vimfumo vingi vidogo vidogo katika jamii ambavyo vyote huzalishwa na mfumo mkubwa wa uzalishaji mali kama vile ukabaila au ubepari. 

Pili, makala imeonesha ni makosa kuwaita wanawake walioolewa makahaba au kuwafananisha nao, kwa sababu mchakato wa kuguma ambao huhusisha kutoa mahari (ndima) ni mchakato unaolenga kutunza heshima ya mwanamke na kulinda thamani ya mwanamke kijamii. Mchakato wa kutoa mahari si mchakato wa kibiashara baina ya muuzaji na mnunuaji bali ni mchakato wa kindugu unaozingatia utu, heshima na usalama wa jamii na wanajamii wenyewe. Ukahaba halisi (ambao Mwanahamisi ameuita ni ukahaba wa rejereja) unahusisha muuzaji na mnunuaji na kamwe hautunzi heshima na utu wa mwanamke wala haulindi usalama wa jamii (haulengi kuzaliana).

Tatu, makala imeonesha kuwa ukahaba unakuzwa na kuchochewa na mfumo wa uzalishaji mali uliopo na siyo mfumo dume. Nimetoa mifano kutoka kwa wanazuoni mbalimbali kuonesha kwamba ubepari na hasa ubepari wa leo unawamasikinisha wanyonge na hivyo watu wengi hasa wanawake wanajikuta hawana namna yoyote ya kuishi isipokuwa kuuza miili yao. Hivyo, si sahihi kuwalaumu wanawake hawa kwa ukahaba wao bali mfumo huu kandamizi, na kwa namna yoyote ile ukahaba na mfumo wake ni lazima viondolewe. Swali linabaki; je, tunaviondoaje? Tunaanza na kipi? Hapa napo kuna mjadala mpana lakini kwa kifupi sikubaliani na Mwanahamisi anaposema “let women prostitutes live in peace”,kwamba tuwaache makahaba waishi kwa amani.

Mwisho, natoa rai kwamba tunapochambua mambo ya jamii zetu za kiafrika tujaribu kutumia mitazamo ya kisayansi. Mtazamo wa kisayansi huona jamii kwa hatua mbili; kwanza huona jamii kwa nje (yaani jamii kama kundi la watu wanaojihusisha na shughuli mbalimbali, wenye lugha na utamaduni mmoja) na pia huenda mbali zaidi kuangalia kiini cha jamii yenyewe (mahusiano ya jamii chini ya mfumo wa uzalishaji mali). 

Kwa kiasi kikubwa wanaharakati hutumia mtazamo usio wa kisayansi ambao huishia kuona jamii kwa nje tu. Hawa husikika wakitumia nguvu zao nyingi kupambana na vitu vinavyoonekana nje ya jamii kama vile, mimba za utotoni, ukatili wa wanawake, mfumo dume n.k. Lakini wangekuwa wanatumia mtazamo wa kisayansi wangejua kuwa hayo yote ni dalili za nje za tatizo kubwa la ndani ya jamii. Kwa namna hii wanaharakati hawa huishia kutoa maoni/mapendekezo potofu (fallible criticism/solutions) ambayo kama yatafanyiwa kazi basi jamii itaharibika zaidi. Tafadhali tusiwafuate, tutapoteza mwelekeo. 

Marejeo 
Hunter (2002) The Materiality of Everyday Sex, Thinking Beyond Prostitution. African Studies, 61, 1, 2002 pg. 99-120

Singer, L. 1993. Erotic welfare: Sexual theory and politics in the age of epidemic. New York:
University of Minnesota Press.

Van der Veen, M. 2000. Beyond Slavery And Capitalism: Producing Class Diffence In The Sex Industry. In Class and its others, ed. J. K. Gibson-Graham, 121–41. Minneapolis: Routledge.

Van Der Veen (2001) Rethinking Commodification And Prostitution; An Effort at Peacemaking in The Battles Over Prostitution, Rethinking Marxism Volume 13, Number 2 Pg. 30-51.

[1]Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Sosholojia na Anthropolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Email: armstrongmatogwa@gmail.com; mobile +255 717940841.
[2]Economic and Philosophic Manuscripts of 1844.

1 comments:

A. Massawe October 17, 2018 at 10:15 AM  


Nakubaliana na maoni ya wa mada hii kwa kiasi kikubwa, na ni hasa pale alipojitahidi kutuonyesha ukweli usiopingika kwamba kuolewa au kuoa sio kuuza au kununua penzi la mwanamke kijumla bali ni kutaka kuendeleza, kukuza na kuboresha uwezo na maendeleo ya kizazi cha binadamu kuanzia ngazi ya familia na koo zilizotofautiana kwa mengi yakuzingatiwa na anayechagua pa kuolewa au kuoa kwa umakini mkubwa uliolenga kupata ule ukoo na familia bora na wezeshi uendelezaji, ukuzaji na uboreshji wa kizazi cha binadamu kupitia anayeoa na anayeolewa zaidi.

Kwa mfano aliye makini vya kutosha kamwe hatakubali kuoa au kuolewa kwenye ukoo na/au famili ya walevi, wezi, vichaa, wavivu au makahaba, au ya walio na kasoro nyingine nyingi za kiokoo; au asiyekuwa na kumbukumbu ya historia kamilifu ya koo na familia zilizomzaa na kumlea, hasa ya yale ya kuzingatiwa wakati wa kuchagua pa kuolewa au kuolewa, hasa na wale wanaotaka kuolewa au kuoa ili kuendeleza vizazi vyao.

Na kwamba, kutofautiana kwa baadhi ya majukumu mengine mengi ya mwanamke na mwanamme kwenye jamii na familia yametokana zaidi na tofauti zao kimaumbile na kwenye kuzaliana na kulea mimba zao na wtoto wao.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP