Wednesday, October 17, 2018

Ubepari ni Zao La Mfume Dume - Na Ukahaba Pia

Ubepari ni Zao la Mfume Dume - Na Ukahaba pia

Chambi Chachage

Leo nimeyasoma kwa tuo majibu ya Armstrong Matogwa kwa Mwanahamisi 'Mishy' Singano yaliyochapishwa katika blogu hii. Kwa hakika nimejifunza mengi kutokana na majibizano yao. Mjadala huo uliochochewa na makala ya 'Sisi Sote ni Makahaba' unagusa nyanja nyingi za maisha yetu binafsi na ya kijamii.

Hivyo, nami nimeona nichangie masuala machache. Mosi, nampongeza Mishy kwa kuibua mjadala. Kama tunavyosema mitaani, ameliamsha dude. Na dude la Mfumo Dume limeamka.

Pili, nampongeza Matogwa kwa kujikunja na kujibu kwa kirefu hoja za Mishy. Lakini pongezi hizo zinaishia hapa maana kwa kiasi kikubwa makala hayo yanadhihirisha ni jinsi gani hilo dude liitwalo Mfumo Dume limejikita hata katika fikra mahiri za Kiuwanazuoni.

Matogwa anadai kuwa Wanazuoni tunaodai kuwa "chanzo cha ukahaba" ni mfumo dume "hueleza 'uongo.'" Anachomaanisha ni kuwa hatuelezi ukweli kwa sababu hatutumii lensi anayoitumia yeye na anayoiona kuwa ni kisayansi. "Majibu sahihi", eti anadai, "hutolewa na wanazuoni wa mrengo wa kushoto (kwa majina yao mbalimbali) ambao huona kuwa ukahaba ni tabia ambayo inatokana na mfumo wa uzalishaji mali uliopo." Anasahau kuwa wapo Wanazuoni wa mrengo wa kushoto, kama vile Marjorie Mbilinyi, wanaouona huo Mfumo Dume ukibebana na ubepari.
Kwa mtazamo wa kisayansi wa Matogwa, hiki kimfumo kidume ni kimfumo tu kidogo kwa maana eti "mfumo dume ni sehemu ya vimfumo vingi vidogo vidogo katika jamii ambavyo vyote huzalishwa na mfumo mkubwa wa uzalishaji mali kama vile ukabaila au ubepari." Madhara ya uono huu ni kuwa unamfanya mwandishi atumie historia na utamaduni wa ndoa na uzalishaji mali wa jamii ya Wagogo kutetea Mfumo Dume kwa kujua ama kutojua.

Anahitimisha utetezi huo kwa kusema hivi: "Hicho kinachoitwa mfumo dume huko nyuma kimejitahidi sana kuitetea heshima hii ya mwanamke na kamwe hakikutaka mwanamke atumike kama chombo cha starehe bali atimize wajibu wake wa kuendeleza kizazi cha wanadamu." Kana kwamba haitoshi anadai kama "mfumo dume ndio unasababisha ukahaba wa rejareja basi huko zamani ukahaba huo ungekithiri zaidi kuliko sasa." Lakini historia yake inaanzia na ukabaila kana kwamba ujima ulikuwa sawia kabisa.

Sote tunajua kuwa ukabaila, kama ulivyo ubepari, ni mifumo ya hivi karibuni tu katika historia ndefu ya jamii za wanadamu. Lakini ukahaba ulianza zamani sana. Kilichozalisha yote haya ni Mfumo Dume. Mfumo Babe wa kuwaridhisha na kuwaridhia wanaume - na hasa wakina baba - katika kuzalisha mali na kuzaliana/kuzalishana.

Ukabaila kwenye jamii ya Wagogo wa karne ya 17 na ya 18 anaouongelea Matogwa kwa umahiri mkubwa  ulikuwa ni mfumo wa uzalishaji mali ndani ya Mfumo Dume. Ni kweli kwa namna fulani jamii hiyo, kama ya Wapare ambayo ndiyo naijua zaidi, zilitumia tamaduni zao kujaribu kulinda haki na thamani ya mwanamke. Lakini zilifanya hivyo ndani ya muktadha wa Mfumo Dume. Ilikuwa ni kama kupunguza makali tu ya ukandamizwaji wa mwanamke na si kuyaondoa au kuleta haki na usawa wa kijinsia. 

Ndiyo maana hata wimbo wa harusi alioutafsiri Matogwa kwa maneno haya unaashiria hilo: “tumemchukua tumemchukua, msagaji wetu (kumbuka kazi ya kusaga nafaka kwenye jiwe ili kuwa unga ilikuwa ya mwanamke), tumemchukua mchotaji wa maji tumemchukua, msongaji ugali (mpishi) tumemchukua mzaaji wa watoto tumemchukua, mlezi wetu tumemchukua.”
Cha kusikitisha ni kuwa lensi ya Matogwa inachoona kwenye wimbo huo ni uzalishaji mali tu katika mfumo wa kikabaila. Haioni kuwa huu nao pia ni uzalishaji mali katika huo Mfumo Dume - wa 'kumchukua' mwanamke kwenda kufanya kazi za kuzalisha mali na kuzaa wana/watoto kwa ajili ya kukuza utawala wa koo ya kibaba.

Badala yake jicho linalodaiwa kuwa ni la kisayansi linachoona ni kuwa kwa "waoaji hii ni siku ya furaha sana kwa sababu kama wimbo unavyosema, mwanamke alithaminiwa kwa kuwa ndiye alitekeleza majukumu hayo sawa sawa kulingana na mfumo wa ukabaila ulivyo na sio mfumo dume." Matogwa wala hajiulizi kwa nini anatumia neno "waoaji" na neno "ukoo ule unaomuoa." Lensi yake inamfanya aone kuwa hayo ni maneno tu yasiyotakana na jinsi Mfumo Dume ulivyojikita hadi kwenye misamiati ya kijinsia.

Inashangaza zaidi pale ambapo Matogwa anapohitimisha kuwa wanaharakati wanaotumia Mfumo Dume kuchambua jamii wana "maoni/mapendekezo potofu." Eti mfumo huo ni dalili za nje tu. Tukitumie sayansi ndiyo tutaona tatizo la ndani (ya jamii). Sayansi gani hiyo isiyoona kuwa kabla ya mifumo ya uzalishaji mali ya kitumwa, kikabaila, na kibeberu kuwepo, ukahaba ulikuwepo?

Yaani sayansi ya mrengo wa kushoto ndiyo inasema uzalishaji mali ndiyo ulizalisha ukahaba mwanzoni? Matogwa anaposisitiza, na hapa tunakubaliana naye, kuwa katika "historia ya mwanadamu hakuna mfumo wa uzalishaji mali uliokuza sana tabia ya ukahaba kama ubepari na hasa uliberali mamboleo" haoni kwamba huko kukuza kunaaminisha kuna mfumo - au utawala wa nguvu - mwingine uliopo na uliokuwepo kabla? Kigawe au Kigawo Kikubwa Kishiriki katika mifumo yote kandamizi ya uzalishaji mali katika historia ya mwanadamu ni nini kama si Mfumo Dume?
Je, siyo huo Mfumo Dume ambao hushiriki kuzalisha na/au kubadili mfumo wa uzalishaji mali? Kwa mfano, je, ushindi wa jumla wa Mfumo wa Kibepari dhidi ya Mfumo wa Kikabaila kati ya takribani Karne ya 15 hadi ya 19 ulitokea kwenye ombwe tu? Wakati Mabepari wanachukua nafasi ya Makabaila, makahaba si walikuwepo? Na, je, mfumo wa uzalishaji mali wa Ujamaa (wa kisayansi) unaoshadadiwa sana na Wanazuoni wenye mrengo wa kushoto utakaposhinda, ukahaba utapotea katika sura ya dunia?

Ole wetu siku hiyo ikifika bila kufanya kile ambacho Mishy amekipendekeza - kuutokomeza Mfumo Dume. Ndiyo baba lao!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP