Saturday, November 3, 2018

Kongamano la Kirais na Hatima ya Uwanazuoni

Kongamano la Kirais na Hatima ya Uwanazuoni Tunduizi

Chambi Chachage

Juma hili wanazuoni nguli walijumuika katika ukumbi adhimu wa kiuwanazuoni wa Nkrumah. Jukumu lao lilikuwa ni kutathmini hali ya kisiasa na kiuchumi katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano. Jumuiko hilo lilihudhuriwa pia na viongozi wengi wa juu.

Busara inasema ni vyema kuanza tathmini ya kongamano hilo kwa pongezi. Kama alivyosema mhudhuriaji mmojawapo, Profesa Issa Shivji, lilikuwa ni jambo la kupendeza kumwona Mkuu wa Nchi akijumuika kama mhudhuriaji. Hili lilimkumbusha mwanazuoni huyo na wengineo enzi za Rais wa Awamu ya Kwanza aliyependa kujihudhurisha hapo katika Chuo Kikuu cha Dar e Salaam. Ahadi ya Rais ya kujihudhurisha mara kwa mara nayo inastahili pongezi na pengine akipatembelea tena atajibu maswali papo kwa papo.

Pongezi pia zinapaswa kuelekezwa kwa waandaaji wa kongamano hilo, hasa kwa kumwongeza mtoa mada mwanamke mmoja baada ya wanaharakati wa haki na usawa wa kijinsia kuja juu na kupaza sauti mitandaoni. Na wahudhuriaji walioweza kuuliza maswali magumu mbele ya vyombo vya dola wanastahili pongezi. Baada ya pongezi hizo, sasa tujikite kwenye suala la uwanazuoni tunduizi.

Uwanazuoni tunduizi, kama jina hilo linavyoashiria, ni aina ya uwanafikra uliojikita katika kutafiti, kudadisi, na kuhoji pasipo hofu. Ni hali ya kuwa mtundu mno katika kutafuta na kuona yale ambayo hayaonekani kwa urahisi tu au yanayofumbiwa macho ama kutofuatiliwa kwa undani kutokana na sababu mbalimbali. Azma kubwa ni kuweka wazi masuala muhimu ambayo yakifanyiwa kazi yanaweza kusaidia kubadilisha kabisa au kuboresha hali iliyopo.

Kabla ya kongamano hilo mijadala mbalimbali mitandaoni ilitabiri kuwa litakuwa ni tukio la kupongezana tu na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano. Hoja hii ilitokana na ukweli kuwa watoa mada wakuu walikuwa ni pamoja na watendaji wa serikali na maprofesa ambao wanaojulikana kuwa wanaunga mkono chama tawala na dola. Lakini tupo tulioamini kuwa uwanazuoni tunduizi utajitokeza tu kutokana na historia ya ukumbi huo wa Nkrumah.

Profesa Martha Qorro, kwa mfano, aliweza kutumia fursa hiyo kuwasilisha suala ambalo amekuwa akilipigania kwa muda mrefu.  Hii ni hoja ya kutumia Kiswahili kufundishia masomo ili tuweze kupata maarifa kwa urahisi zaidi na kuyatumia kujiletea maendeleo ya kiuchumi n.k. Kwa upande wake tunaweza kusema alitimiza wajibu wake wa uwanazuoni tunduizi kwa kuwa bado hoja yake iko pembezoni katika sera za nchi hii ambazo, japo zinakitambua Kiswahili, kwa kiasi kikubwa zinakipa upendeleo Kiingereza. Ila bado na yeye alionekana anapongeza zaidi kuliko kuhoji kwa nini serikali ya sasa yenye kiongozi mkuu anayekithamini Kiswahili haichukui hatua za dhati na madhubuti kubadilisha hali hiyo.

Labda uteuzi wa Profesa Humphrey Moshi siku chache zilizopita kuwa mwenyekiti mpya wa Bodi ya Tume ya Ushindani ulichangia kupunguza uwanazuoni tunduizi wake katika kongamano hilo. Kwa ambao tumeshawahi kumsikiliza kwenye makongamano mengine, tumeona utayari wa kuhoji hata yale yasiyotupendeza. Ujasiri huo uliwahi hata kupelekea profesa mmoja katika kongamano fulani la  Kiingereza kumwambia kwa Kiswahili mbele ya kadamnasi kuwa mambo mengine siyo ya kuyaongelea mbele ya wageni kutoka nje.

Hapo ukumbini Nkrumah, lakini, Profesa Moshi wala hakutoa tathmini ya uzalishaji na utendaji wa viwanda zaidi ya 3,000 hivi ambavyo huwa tunaambiwa kuwa vimeanzishwa katika awamu hii. Profesa huyo, ambaye amewahi hapo kabla kutoa tathmini ya jinsi ambavyo maeneo maalum yaliyotengwa ili kuchakata nchini kwa kiasi kikubwa hayana uzalishaji, alibakia anatoa pongezi tu kuhusu 'uviwandanishaji.' Hakukuwa na mjadala kati ya wazungumzaji na wahudhuriaji, hivyo, hata 'swali-hoja' la Profesa Shivji kwa Profesa Moshi kuhusu umuhimu wa kilimo na wakulima katika ujenzi wa viwanda katika nchi zetu tofauti na zile za magharibi halikujibiwa. Na hata profesa nguli wa uchumi, Ibrahim Lipumba, hakupata fursa ya kutoa zile hoja zake mbadala kuhusu hali ya siasa na uchumi wa viwanda bali aliambulia kusifiwa tu na Mtoa Hotuba wa mwisho.

Vivyo hivyo, Profesa Hudson Nkotagu aliitumia nafasi yake kusifia miradi yetu mikubwa kama ya Stiegler's Gorge bila, kwa mfano, kutueleza kwa nini wanazuoni wengi wa mazingira wanaipinga. Ni kana kwamba alijua kuwa mwisho wa mjadala huo wanazuoni hao watasimangwa kwamba siyo wazalendo n.k. Katika mazingira hayo tulikosa mjadala tunduizi kuhusu uhasi na uchanya wa mradi huo. Hii ni kutokana na kile ambacho mwanazuoni tunduizi, Ronald Ndesanjo, anakitanabahisha kuwa ni kutumika kwa uzalendo "kama karatasi ya litimasi ya kupima wale wanaounga mkono watawala/wanasiasa hasa wa chama tawala na wale wanaokaidi."

Zamani hapo ukumbuni mada kama hiyo ingemjumuisha profesa nguli wa sheria za mazingira, Palamagamba Kabudi, ambaye angejibizana kwa hoja na wenzake. Ila safari hii Profesa Kabudi alikuwa ni msemaji maalum wa serikali akimwakilisha Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako. Kwa umahiri mkubwa, Profesa Kabudi aliwanukuu wanazuoni wa kushoto na kulia - Vladimir Lenin na Joseph Schumpeter - kuonesha umuhimu wa kusambaza umeme kwa ubunifu nchi nzima n.k. Lakini hatukusikia hoja za kitunduizi za upande mwingine kuhusu namna mbadala ya kufanya hivyo pia. Tulichopatiwa ni mhadhara au hubiri la kiuwanazuoni.

Cha kutoshangaza, japo kinastaajabisha, ni pale tulipomuona Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliutumia ukumbi huo kuongoza mijadala ya kiuwanazuoni tunduizi enzi zake za uwenyekiti wake wa jumuiya ya wanataaluma wa chuoni hapo, UDASA, akiutumia kivingine kabisa. Wakati muasisi mwenzake wa chama cha ACT Wazalendo, Mh. Zitto Kabwe, akiwa  korokoroni, Profesa Mkumbo alikuwa kibwetani akihubiri tu mafanikio ya serikali. Inasemekana muasisi huyo mwenzake naye alipanga kuhudhuria hapo na, kama angepewa nafasi, angehoji kiuwanazuoni tunduizi takwimu na hoja za mshauri mtaalamu huyo wa zamani wa chama chao. Wadadisi wa mambo wanaamini kutopewa dhamana siku hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuhakikisha mjadala huo tunduizi hautokei ukumbini.

Tuanze kumalizia tathmini kwa kurejea wasilisho la Profesa Rwekaza Mukandala. Kama kawaida yake, aliweza kuitumia fursa hiyo kutoa uchambuzi 'unaouma na kupuliza'. Badala ya kuinyonga serikali aliipa kamba ya kujinyonga yenyewe kwa kutoa vigezo ambavyo kila mtu angeweza kuvitumia mwenyewe kuipima. Yeye alitumia vigezo hivyo kuonesha kuwa, kwa kiasi kikubwa, kuna mafanikio. Lakini ni wazi kwamba wapo wasikilizaji watundu waliovitumia kuona mengineyo hasa kwenye kigezo cha hisia za wananchi kuhusu hali ya siasa na uchumi ambacho hakukidadavua. Pengine ugwiji wake wa kiuwanazuoni ungemfanya asijizuie walau kuunukuu utafiti wa maoni wa Twaweza. Hitimisho lake kutoka kwa wahenga ndilo hasa lililobeba hisia za pande zote zilizotumia vigezo vyake vizuri. "Dalili ya mvua", alihitimisha, "ni mawingu."

Dalili ya hatima ya uwanazuoni tunduizi katika vyuo vyetu vya umma yalikuwa ni mawasilisho hayo ya maprofesa nguli. Lakini dalili kubwa kuliko yote ilikuwa ni hitimisho la mgeni maalum wa kongamano ambaye alitoa hotuba ya mwisho. Pamoja na masuala mengine, hotuba hiyo ndefu ilitofautisha maprofesa wasio wazalendo wachache na wengi walio wazalendo. Hakukuwa na mjadala kuhusu hotuba hiyo. Wanazuoni tunduizi waliohudhuria walitumika kutoa uhalali wa hoja za serikali kwa kujua au kutojua.

Sidhani kulikuwa na 'ukasuku' miongoni mwao. Lakini naamini kulikuwa na 'ustempu' hasa pale jina la mmojawapo liliposifiwa sana ili kuhalalisha tu yale yanayofanywa na serikali na vyombo vyake vya dola. Hata maswali magumu machache yalipoulizwa kitunduizi kuhusu uhuru wa maoni na utete wa demokrasia, watoa mada hawakuyajibu bali yalijibiwa kimamlaka kutoka ukumbini na mwakilishi wa watendaji vijana wa serikali ambao tumejulishwa kuwa eti 'damu zao zinachemka', hivyo, tuendelee kuwavumilia tu. 

Ama kweli, dalili za mvua nzito ya masika ni mawingu mazito.

5 comments:

Unknown November 4, 2018 at 9:23 AM  

Mzalendo umenena vyema na uchambuzi wako wa mjadala husika ni sahihi kwa kiasi kikubwa. Lakini katika hali ya kushangaza kama ulivyokuwa mjadala ule, nawe pia umetuacha katika hali ya sintofahamu. Kwa kuwa ni kama umesema matarajio ya wananchi hayakuweza kufikiwa, sasa wananchi tufanyaje ili kujinasua na mtanzuko huo wa kukosa watu wa kutusemea?

Unknown November 4, 2018 at 11:31 AM  

Haukuwa na Tija,mjadala ulienda chaka sijui kwa ubwege ama kwa kusudi sijui, it was worse to be retrieved in the near future, UDSM is no more!Edwin A

Gerson Janga November 4, 2018 at 5:45 PM  

Vijana ambao na sisi tumeambiwa damu yetu! Inachemka! Ni kweli inachemka imejawa na ghadhabu na hasira ya kifikra kutafakari mstakabali wetu kama wazalishaji na wachangiaji wakuu! Lakini ghadhabu zetu zilifinywa na referee ambaye alipuliza filimbi kila tulipogusa mpira. Tunahitaji mijadala ya kitaifa, itakayo changanya wasomi, wananchi wa kawaida na wafanyakazi wamulike kurunzi zao.

Gerson Janga November 4, 2018 at 5:46 PM  

Vijana ambao na sisi tumeambiwa damu yetu! Inachemka! Ni kweli inachemka imejawa na ghadhabu na hasira ya kifikra kutafakari mstakabali wetu kama wazalishaji na wachangiaji wakuu! Lakini ghadhabu zetu zilifinywa na referee ambaye alipuliza filimbi kila tulipogusa mpira. Tunahitaji mijadala ya kitaifa, itakayo changanya wasomi, wananchi wa kawaida na wafanyakazi wamulike kurunzi zao.

A. Massawe November 4, 2018 at 10:08 PM  

Ni kweli kwamba yaliyochangiwa na wanazuoni wetu viongozi waliotoa mada kwenye hili la Kirais ni pungufu ya yaliyotarajiwa kutoka kwao.
Mada zao zilipashwa kuchangia zaidi mapendekezo ya masahihisho na/au maboresho yatakayotuongezea ufanisi wa utendaji wa Rais dhidi ya vitendo vya rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za taifa, na wa miradi mikubwa inayoanzishwa na serikali yake ya awamu ya tano kama ule wa umeme wa maji huko Stiegler’s Gorge na ule wa ujenzi wa reli mpya ya kati iliyo ya kisasa zaidi.

Hata hivyo nyingi ya mada zao hizo ziliishia kusifia tu utendaji wa Rais na miradi mikubwa inayoanzishwa na serikali yake labda kutokana na wao kutotaka kuzingatia kwamba hakuna hata moja lifanywalo na binadamu lisilokuwa na kasoro au kushindwa kubaini kasoro kwenye utendaji wa Rais na miradi mikubwa inayoanzishwa na serikali yake.
Nilitaria wangezingatia kwamba mafanikio makubwa yaliyokwishaptikana haidi sasa kutokana na vita iliyoanzishwa na Mh. Rais dhidi ya uwepo wa rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za taifa hapa nchini hayatakuwa endelevu pasipo kupewa nguvu ya kiKatiba iliyokwisha pendekezwa na Tume ya Warioba iliyotutengenezea Rasimu ya Katiba mpya iliyokwama kwenye Bunge maalum la utunzi wa Katiba hiyo, na hivyo kupendekeza nguvu hivyo ijumuishwe kwenye Katiba iliyopo mara moja.

Nilitarajia pia kwamba wangebaini na kuzingatia pia kwamba chaguo la kujenga reli mpya ya kati inayotumia magari moshi yanayotumia nishati ya umeme, na ambayo husafirisha kwa gharama kubwa zaidi ya yale yanayotumia nishati ya diseli au gesi asilia sio chaguo sahihi kwa yetu ya kati inayotarajiwa kuweza kusafirisha abiria wote watakokuwepo na mizigo yote itakayokuwepo kwa kipindi kirefu cha miaka mingi ijayo ikitumia magari moshi ya diseli au gesi asilia yanayosafirisha kwa gharama ndogo zaidi, na hivyo kupendekeza chaguo la nishati itakayotumiwa na reli mpya ya kati inayojengwa lipitiwe upya kwa kuzingitia yaliyosemwa hapa:

https://www.msn.com/en-xl/africa/africa-top-stories/botched-chinese-railway-project-in-africa-is-a-warning-to-belt-and-road-investors/ar-BBP2R4J?li=BBKhQr3&ocid=mailsignout
hapa: https://www.google.com/url?sa=t&rct=j&q=&esrc=s&source=web&cd=12&cad=rja&uact=8&ved=2ahUKEwiNncPztK3eAhUHfxoKHae-CHEQFjALegQIBRAB&url=https%3A%2F%2Fwww.quora.com%2FWhy-dont-trains-in-the-US-have-electric-locomotive-engines-Arent-they-more-efficient-than-diesel-locomotives&usg=AOvVaw1vh9ZOLP9-4P0yhjKfwKbx

na hapa:

https://www.google.com/url?sa=t&rct=j&q=&esrc=s&source=web&cd=3&cad=rja&uact=8&ved=2ahUKEwiY4tvZsK3eAhW2gM4BHQr6AXsQFjACegQIBhAL&url=http%3A%2F%2Fwww.theeastafrican.co.ke%2Fbusiness%2FKenya-drops-bid-for-electric-SGR-trains%2F2560-4279596-g3fey3z%2Findex.html&usg=AOvVaw3zxSqK6iRgbYLeG3urFbOL

Kuhusu ule mradi mkubwa wa umeme wa maji huko Stiegler’s Gorge, nilitarajia kwamba mtoa mada kuuhusu angelilifahamisha kongamano kisomi na kwa kujiamini kwamba hakuna hata pingamizi moja la wanamazingira dhidi ya mradi huo lililo na mashiko na/au litakaloweza kuaminisha yeyote kwamba madhara ya kijumla ya kimazingira na kiuchumi ya mradi huo ni makubwa kuliko manufaa ya kijumla ya kimazingira na kiuchumi ya mradi huo yatokanayo na umeme utakaozalishwa, kilimo cha maji na samaki kinachoanzika kweye bonde la mto Rufiji kwa kutumia maji ya bwawa la maji la mradi huo yaliyoshazalishwa umeme, na yatakayotokana na mtumizi mengine ya maji ya bwawa la maji la mradi huo.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP