Monday, March 4, 2019

Nini kimemrejesha Lowassa CCM?

Nini Kimemrejesha Edward Lowassa Chama Cha Mapinduzi?

Ronald B. Ndesanjo


Siku chache tu baada ya Ndugu Edward Ngoyai Lowassa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM), kumeibuka mjadala mkubwa miongoni mwa jamii ya Tanzania. Sehemu kubwa ya mjadala imekuwa ikihusishwa na kile kinachoelezwa kukata shauri kwa Lowassa na kukubali yaishe ili mambo yake ya kifamilia, biashara na mali yaende vizuri bila vikwazo toka kwa serikali ya CCM. Pamoja na kwamba sababu hii inaweza kuwa na mashiko, hasa kwa upande wa Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Serikali ya Tanzania, sioni CCM ina maslahi yapi kwa mambo binafsi ya Lowassa kunyooka. 
Hivyo basi, suala la msingi ninalotafakari katika makala haya ni kipi hasa kimepelekea CCM kumpokea Ndugu Lowassa chamani hasa baada ya kumnanga kuwa ndiye kinara wa ufisadi punde tu alipohamia upande wa upinzani. Inastaajabisha kidogo kuwa CCM wamefanya jambo lilelile walilofanya CHADEMA miaka mitatu iliyopita; kumpokea mtu waliyemtuhumu vikali kwa ufisadi. Je, ni nini hasa alichoondoka nacho Lowassa ambacho CCM bado wanakihitaji?

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, hasa kuelekea uchaguzi wa Raisi na Wabunge, ndipo jina la Edward Lowasa lilianza kuvuma katika siasa ndani ya CCM na Tanzania kwa ujumla. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliibuka kidedea katika mchakato wa kutafuta mgombea wa uraisi kwa tiketi ya CCM japo mwisho wa siku Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ndio aliyepewa nafasi hiyo. Nyuma ya ushawishi na hatimaye ushindi mkubwa wa Kikwete alikuwepo rafiki yake mkubwa (wakati ule), Lowassa. Ni katika kipindi hiki ndipo Lowassa alianza kuonesha uwezo na ushawishi mkubwa katika siasa za CCM na Uchaguzi kwa ujumla.

Kwa kipindi cha miaka 10 ambapo Mkapa alikuwa Rais, yaani kuanzia 1995 mpaka 2005, Lowassa na Kikwete waliendelea na harakati zao za kuutaafuta uraisi kama timu (maswahiba) mpaka kupelekea kubatizwa jina la kundi la Muziki wa Rhythm na Blues la Marekani, Boys II Men. Katika harakati hizi Lowassa alisemekana kuwa kinara wa kupanga na kutekeleza mkakati wa kumuwezesha swahiba wake Kikwete kupeperusha bendera ya uraisi kwa tiketi ya CCM na ikiwezekana kuwa Raisi wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo lilifanikishwa vizuri sana. 

Ni katika kipindi hiki vilevile ndipo ambapo Ndugu Rostam Abdulrasul Aziz, kinara mwingine katika siasa za CCM na swahiba wa Lowassa, anatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kumpeleka Kikwete Ikulu ya Magogoni. Pamoja na kuwa Rostam hakuwahi kutangaza hadharani kukihama CCM, ni ukweli usiopingika kwamba amekuwa kando sana na shughuli za chama hicho tangu mwaka 2015. Wakati wa tukio la juzi la kurejea kwa Lowassa pale Ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Rostam alionekana akiwa na shati lake la rangi ya manjano; na hii sio bahati/ajali.
Pamoja na mambo mengine, vyanzo vingi vimewahi kuripoti kuwa uswahiba wa ndugu Lowassa na Kiwete ulikuwa umejengwa juu ya makubaliano kuwa pale Kikwete atakapomaliza muda wake wa uongozi basi Lowassa atachukua nafasi yake. Mikakati na harakati zao ndani ya CCM zilikuwa zimepangwa kuwezesha hili kutokea. Ila kama ijulikanavyo kwa wengi, safari hii haikufika mwisho kama ilivyopangwa kutokana na Lowassa kujiuzulu wadhifa wa Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya umeme ya Richmond. 

Hata hivyo, harakati za Lowassa kuwania Uraisi wa Tanzania hazikukoma mpaka pale alipoenguliwa na Kamati Kuu ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015. Binafsi nadhani historia hii ya Lowassa katika siasa za Tanzania na nafasi yake ya kipekee katika siasa za uchaguzi za CCM kwa takribani miaka 20 ni sababu kubwa na ya msingi ya kurejea kwake katika chama hicho. Ukimuondoa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, nadhani Lowassa ni mmoja wa watu wachache ndani ya CCM ambao wametawala siasa za uchaguzi wa Tanzania tangu mwaka 1995. Na katika hili huwezi kuacha kumtaja Rostam Aziz, Right-Hand Man wa Edward Lowassa.
Ushawishi mkubwa wa kisiasa wa Lowassa nchini Tanzania ni jambo lingine linaloweza kuwa limepelekea kurejea kwake CCM. Pamoja na ukweli kuwa upinzani umedhoofika sana kwa sasa, mwanasiasa huyu bado ana kundi kubwa nyuma yake ambalo kwa namna moja ama nyingine linaweza kuikosesha CCM usingizi hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu tunakoelekea. Kurudi kwa Lowassa kutalirudisha kundi hili katika kambi ya CCM; jambo ambalo ni la manufaa kwa chama hicho kuliko kubaki upande wa upinzani. 

Sababu nyingine kubwa ya kurejea huku nazihusisha na siasa za ndani za CCM hasa baada ya Lowassa kukiacha chama hicho mnamo mwaka 2015. Itakumbukwa kuwa, baada ya Lowassa kutangaza kukihama CCM, kulitokea sintofahamu kubwa ndani ya chama hicho kiasi kwamba baadhi ya watu walitabiri tukio hilo kuwa mwanzo wa kusambaratika kwa CCM. Hili lilitokana hasa na nguvu na ushawishi mkubwa aliokuwa nao Lowassa ndani ya chama.
 Japokuwa CCM ilibaki salama bila kusambaratika, kuondoka kwa Lowassa kulikigawa chama katika makundi makubwa mawili; wale waliodhaniwa ni kundi la Lowassa na waliokuwa upande mwingine ndani ya chama. Mgawanyiko huu umekuwa mojawapo ya changamoto zinazokikabili CCM hata sasa hasa pale ambapo tumeshuhudia wale waliodhaniwa kuwa upande wa Lowassa kujikuta katika hali ngumu ndani ya chama. Pengine kurejea kwa Lowassa kunaweza kutibu donda hili.

Suala jingine linalofanana na hilo ni kwamba; kazi aliyokuwa ameifanya Lowassa kabla ya kuondoka CCM mwaka 2015 ilikuwa imemjengea nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya chama na alikuwa amejihakikishia kupita katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea uraisi kwa tikeki ya chama hicho. Kuondoka kwake ghafla kulikiacha chama katika mshangao na pengine hii ndio sababu baadhi wachambuzi wa mambo wanalihusisha na “uamuzi wa dharura” wa CCM kumnadi mgombea na si chama chenyewe hasa kutokana na kutokukubalika kwa chama hicho wakati ule.

 Wengi walijenga hoja kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2015, CCM kilibebwa na mgombea wake. Kwa hali ya mambo ilivyo sasa si rahisi kwa CCM kujihakikishia nguvu ya mtu mmoja kukibeba chama katika uchaguzi mkuu ujao. Hapa ndipo nguvu, uzoefu na ushawishi wa Lowassa katika siasa za uchaguzi unapohitajika ndani ya CCM.
Kufuatia uchaguzi mkuu wa 2015 kumefanyika mabadiliko makubwa ndani ya CCM. Kwa kiasi kikubwa mabadiliko haya yamebadili mfumo mzima wa uendeshanji wa shughuli za chama na hasa siasa za uchaguzi. Si rahisi kubaini mabadiliko haya yatakuwa na matokeo yapi kwa upande wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao. Katika kuweka mikakati ya ushindi suala la fedha linaweza lisiwe tatizo kwa CCM bali utengenezaji na uratibu wa mkakati wa ushindi. Hapa ndipo uzoefu na ushawishi wa Lowassa na swahiba wake Rostam Aziz ndani ya CCM unapohitajika.
Ni ukweli kuwa CCM inaweza tumia njia nyingine kushinda uchaguzi, kwa mfano, kupitia sheria na nguvu ya dola chini ya serikali inayoongozwa na chama hicho. Pamoja na hilo, nadhani CCM bado inaona umuhimu wa kujiandaa vema kwa kinyanga’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao. Ninajenga hoja kuwa ni katika muktadha wa masuala niliyoyaeleza hapo juu kuwa CCM kimebaini ni jambo la manufaa kwa Ndugu Edward Lowasa kuwa upande wao na si vinginevyo. 

Sioni ni kwa namna gani masuala binafsi ya kifamilia, biashara na mali za Lowassa inaweza kuwa sababu ya msingi kwa CCM kumpokea!

1 comments:

A. Massawe March 5, 2019 at 10:44 AM  

Let’s look at it from the big constructive point of view of it which means to agree with me that for the smart Opposition politician like Lowassa who has managed to understand that the only way he/she could accomplish the mission (s) of his/her political career is to operate from the inside of the ruling CCM dictatorship¸ is to relocate from the Opposition to the Ruling CCM?!

Me think this is what better explains the correct decision to relocate from the Opposition back to the ruling CCM dictatorship made by Lowassa.

My choice would also be to change the state of our political democracy from the too powerful to change or defeat from outside ruling CCM party dictatorship in place to a single or multiparty democracy from the inside rather than from the outside of the ruling CCM party dictatorship in place.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP