Wednesday, May 15, 2019

Spika na Naibu Spika: Uhusiano wenye Utata

Tatizo si Dakta Tulia, Tatizo ni Naibu Spika

HIVI karibuni, wabunge wawili wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Msigwa wa Iringa Mjini na Godbless Lema wa Arusha Mjini, walihoji kupitia mitandao ya kijamii kuhusu nini hasa kinamfanya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuonekana kwenye ziara ya Rais John Magufuli iliyokuwa inaendelea mkoani Mbeya.
Ni swali ambalo limejengwa kutokana na misingi miwili; wa kwanza wa kikatiba, kwamba ziara ya Rais Magufuli ni ya kiserikali na Tulia kama mmoja wa viongozi wa Bunge hahusiki na, pili, ukweli kwamba Naibu Spika huyo hata si mbunge au mwakilishi wa watu wa Mbeya. Anafuata nini huko? Labda ndilo swali linaloulizwa.
Kabla sijaingia kwa undani kueleza mtazamo wangu kuhusu jambo hili, ningependa kidogo kuweka muktadha (context) wa jambo lenyewe. Na muktadha wenyewe uko hivi.
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mnamo mwaka 1992, Tulia ndiye Naibu Spika mwenye uzoefu mdogo wa kisiasa kuliko mwingine yeyote katika historia ya Bunge hilo.
Naibu Spika wa Bunge la 1990 hadi 1994 alikuwa ni Pius Msekwa. Wakati anakuwa Naibu Spika, Msekwa tayari alikuwa kiongozi kwa takribani miaka 20. Mwaka 1977 wakati TANU ikiungana na ASP kuunda CCM yeye ndiye aliyekuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa chama tawala wakati huo. 
Na Msekwa tayari alishakuwa mbobezi wa masuala ya Bunge, akiwa amejifunza kupitia utendaji wa Bunge la Mkoloni hadi Bunge la kwanza la Tanzania huru. Uzoefu huu ulimsaidia sana katika utendaji wa shughuli zake.
Kati ya mwaka 1994 hadi mwaka 2005, Msekwa alikuwa Spika akihudumiwa na manaibu wawili; kwanza Philip Marmo na halafu Juma Jamaldini Akukweti (RIP). Wakati Akukweti anakuwa Naibu Spika, tayari alikuwa Mbunge wa Tunduru tangu mwaka 1990. Kwa hiyo, aliipata nafasi hiyo wakati tayari akiwa na miaka 10 ndani ya Bunge.
Katika Bunge la mwaka 2005 hadi mwaka 2010, Naibu Spika alikuwa ni Anne Makinda. Mama huyu tayari alikuwa na uzoefu bungeni wa zaidi ya miaka 25 wakati akipata nafasi hii.
Jambo moja ambalo watu wengi hawalijui ni kwamba Makinda ndiye mwanasiasa pekee hapa nchini ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) au Mnadhimu Mkuu wa Serikali bungeni chini ya mawaziri wakuu watatu tofauti; Edward Sokoine, Salim Ahmed Salim na Cleopa Msuya.
Huyu sasa ndiye mtu aliyekuwa Naibu Spika wakati wa Bunge la Tisa lililoongozwa na Samuel John Sitta (RIP).
 
Kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2015, Naibu Spika alikuwa ni Job Ndugai ambaye naye alikuwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 10 bungeni lakini pia akiwa amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi na Mazingira. 
Tulia, kwa upande wake, amekuwa Naibu Spika akiwa ametoka kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba kwa kipindi kifupi akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Uzoefu wake huu kwa ujumla unaweza kuwa na kipindi kisichozidi mwaka mmoja. Hivyo, alikuwa hajawahi kushika wadhifa wowote wa uongozi wa kitaifa kabla ya hapo au wa kuchaguliwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. 

Kwa maana nyingine, huyu ndiye Naibu Spika aliyeingia bungeni akiwa ‘mwanafunzi’ ama 'mwanagenzi' na hana uzoefu wala 'uzeefu' wa aina yoyote  wa Kibunge kulinganisha na watangulizi wake.

Lakini kuna jambo moja ambalo pia ni lazima nilieleze ili kukamilisha muktadha huo niliousema. Tulia pia ndiye Naibu Spika aliyeingia kwenye wadhifa huo katika mazingira tofauti na watangulizi wake.
Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na baada ya Ndugai kuapishwa uspika, Spika alipata matatizo ya kiafya yaliyosababisha aende nje ya nchi kutibiwa. Kwa maana hiyo, Tulia hakuanza majukumu yake kama Naibu Spika. Kimantiki alianza kama Spika kwa sababu ya kutokuwepo nchini kwa Ndugai.
Mimi ni mmoja wa watu walioshangazwa baada ya kumuona Tulia akihudhuria mkutano wa Kamati Kuu ya CCM katika siku za awali za utawala wa Rais Magufuli. Kwa kawaida, Spika ni mjumbe wa Kamati Kuu lakini haikuwahi kutokea Naibu Spika kuhudhuria. Lakini Tulia alipata nafasi hiyo.
Hivyo, kwa hali yoyote ile, Dk. Tulia Ackson, ndiye aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania kwa walau mwaka wa kwanza wa Bunge hili la 10. Uzoefu huu wa Tulia ni mojawapo ya matatizo ambayo nitakuja kuyaeleza huko mbele.
Mjadala huu wa Tulia ulinirudisha nyuma hadi mwaka 2004 wakati nikiwa mwandishi anayechipukia wa gazeti la Mtanzania. Siku moja nilipata bahati ya kuzungumza na marehemu Akukweti katika Ofisi Ndogo ya Bunge hapa Dar es Salaam. 
Nilimsikia Akukweti akilalama kupitia mazungumzo ya simu kwamba hatakiwi kuzunguka na gari la Naibu Spika wakati akiwa katika shughuli zisizo za kumwakilisha Spika.
Picha niliyoipata wakati natoka katika mazungumzo yangu na Akukweti ilikuwa kwamba Msekwa alikuwa akiamini kwamba cheo cha Naibu Spika kinaishia ndani ya Bunge na hakitoki nje. Kwake yeye, Bunge lina kiongozi mmoja tu ambaye ni Spika na, hivyo, Naibu wake majukumu yake yanaishia ndani ya ofisi za Bunge na si nje. 
Kuna kipindi nilikuwa napata michapo kutoka kwa wafanyakazi wa Bunge. Walidai Akukweti alikuwa amepania kuwania nafasi hiyo mara baada ya uchaguzi wa 2005 hata kama Msekwa mwenyewe angewania. Eti kwamba alikuwa tayari kuwania nafasi hiyo na bosi wake huyo.
Kwa bahati mbaya, sarakasi na mitandao ya uchaguzi wa mwaka 2015 ulimweka Sitta katika Uspika. Akukweti akaishia kupata cheo cha Mnadhimu Mkuu wa Serikali Bungeni; bila shaka ikizingatiwa uzoefu wake kama Naibu Spika wakati wa Bunge lililotangulia. Msekwa aliamua kustaafu moja kwa moja.
Katika Bunge la Sitta, kwa sababu ya uzoefu wa wawili hao; yeye na Makinda, misuguano haikukosekana. Lakini mbunge huyo wa zamani wa Urambo alimweka Makinda ‘bize’ na shughuli za kibunge za nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki (EAC) kiasi kwamba hakuwa na ushawishi sana bungeni.
Kimsingi, ili kuepuka kuwa na nguzo mbili za utawala bungeni; Sitta aliamua kwamba Makinda asitulie sana bungeni na awe mbali kwa kadri itakavyowezekana. Leo hii, wakati tukizungumzia ‘utukufu’ wa Bunge la Tisa, sote tunamzungumzia Sitta na Makinda huwa hayupo katika ngano za taasisi hiyo. Anaibuka kwenye ngano za Bunge la 10.
Wakati Makinda akiwa Spika, uhusiano pia na Ndugai haukuwa wa kuvutia. Kuna wakati Ndugai alishangazwa baada ya kupanga kwenda kumsalimia Makinda ofisini kwake na kuambiwa kwamba amesafiri kwenda nje ya nchi kwa siku kadhaa nyuma pasipo yeye kujua.
Na nakumbuka kuna wakati kulikuwa na maneno kwamba kulikuwa na maelekezo kutoka Ofisi ya Spika kwamba endapo kutakuwa na hoja nzito dhidi ya serikali, Ndugai asiruhusiwe kukalia kiti kwa maelezo kuwa hakuwa na simile na serikali. Ikitokea kuna hoja nzito dhidi ya serikali, kiti angekalia Makinda mwenyewe au mmoja wa wenyeviti wa Bunge ambaye Spika angekuwa anamuona anafaa kwa jukumu hilo.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya Bunge, watakumbuka kwamba miaka miwili iliyopita, kulikuwa na maneno maneno kwamba hali si shwari baina ya Ndugai na Tulia. Watonyaji walikuwa wakieleza kwamba Ndugai hakuwa chaguo la Magufuli na kuwa Tulia ndiye hasa mwana mpendwa wa Ikulu. Maneno hayo sasa hayapo.
Lakini hiyo ni 'stori' ya siku nyingine, si leo.
Maoni yangu ni kwamba Tulia ameingia bungeni akiwa kijana na mwenye matamanio ya kufanya makubwa. Bahati mbaya ni kwamba nafasi ya Naibu Spika haimpi fursa ya kutimiza yale aliyoyapanga au anayoona yanafaa kufanyika. Kwa nini?
Hii ni kwa sababu Bunge lina upungufu mmoja mkubwa; hakuna majukumu ya kipekee ya Naibu Spika yaliyoainishwa kisheria. Tatizo hili linasababisha Naibu Spika awe ni mtu wa kukaa tu kutegemea huruma ya bosi wake kumpangia majukumu au kutokuwepo kwa bosi huyo. Kama bosi hatampa cha kumfanya, Naibu Spika anabaki na cheo chake tu pasipo majukumu.
Sasa, kwa bahati nzuri, huko nyuma, manaibu walikuwa ni watu waliokuwa na majukumu mengine ya kuwafanya wawe na shughuli za mara kwa mara. Msekwa alikuwa tayari amejijengea jina katika dunia ya kibunge na alikuwa pia mjumbe wa bodi mbalimbali za mashirika ya umma. Akukweti na Ndugai walikuwa na majimbo na hivyo walikuwa na watu wa kuwashughulisha.
Tulia hana jimbo. Yeye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais. Nikimnukuu mmoja wa wabunge waandamizi; “Jimbo la Tulia ni Ikulu”. Huyu ni kijana, msomi na mwenye matamanio makubwa ya kisiasa baada ya kuwa ameonja mojawapo ya madaraka ya juu kabisa hapa nchini. Ukweli huu kwamba kwa nafasi yake anatakiwa kukaa tu na kusubiri apangiwe kazi na bosi haukai vizuri na yeye. 
Damu inamchemka. Anataka kufanya kazi. Anataka sasa kutimiza ndoto zake.
Nadhani Tulia ana misheni mbili kwa sasa; moja ni kuweka jimbo lake la Ikulu salama na pili ni kutafuta jimbo la uchaguzi ili katika Bunge lijalo asipate taabu hii ya kukaa bila kazi.
 Si siri kwamba anataka ubunge katika mojawapo ya majimbo ya mkoa wa Mbeya. Na kuwepo kwake mkoani humo wakati wa ziara ya Rais kumeua ndege wawili kwa jiwe moja;  ameweka jimbo lake salama lakini pia kapata nafasi ya kuzidi kujitambulisha kwa Rais. 
Mtazamo wangu ni kwamba suluhisho la kudumu la migogoro na sintofahamu  zinazojitokeza mara kwa mara katika ofisi hii ya Bunge zinaweza kuondolewa tu kwa walau kutengeneza majukumu yanayoeleweka na ya kipekee ya ofisi ya Naibu Spika.
Utaratibu huu wa Naibu Spika kutegemea tu fadhila za Spika kuendesha ofisi yake unaweza kuja kuleta shida kubwa zaidi huko baadaye. Spika atabaki kuwa Mkuu wa Mhimili wa Bunge. Lakini itapendeza kama kutakuwa walau na kifungu kidogo cha sheria za kibunge kinachoeleza kuhusu majukumu ya kipekee kabisa ya Naibu Spika.
Yale ambayo kila anapoamka asubuhi kwenda ofisini, anajua kabisa kwamba hayo ndiyo ya kwake na si ya mwingine. Kama Spika, kwa hisani yake, akiona kuna umuhimu wa kumuongezea mengine ya hapa na pale, hilo litakuwa jambo zuri.
Lakini, la kwanza kabisa, ni kwamba ni lazima ‘Tulia’ mwingine atakayekuja huko baadaye, aikute ofisi ina kazi za kufanya ili atulie ofisini.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP